Thursday, October 6, 2011

Mwalimu Nyerere Aliiogopa CCM

Makala hii nilishaichapisha katika blogu yangu hii mara mbili. Mara ya kwanza ilikuwa ni hapa.


------------------------------------------------


Ingawa alikuwa mwanzilishi wa CCM, kwa nia njema ya kuendeleza mapinduzi katika nchi yetu, miaka ilivyozidi kwenda Mwalimu Nyerere alishuhudia jinsi CCM ilivyobadilika na kuwa mzigo kwake na pia tishio kwa usalama wa Taifa.

Mwaka 1993 Mwalimu alichapisha kitabu kiitwacho Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania (Harare: Zimbabwe Publishing House, 1993). Pamoja na mambo mengine katika kitabu hiki, Mwalimu alisema kuwa kuna kansa katika uongozi wa CCM. Nanukuu baadhi ya maneno yake:

Chama cha Mapinduzi, kwa sababu ya uzito wa historia yake, hadhi ya jina lake, mfumo wa wavu wake, mazoea ya watu, na ubovu wa Vyama vya Upinzani, kinaweza kuchaguliwa na Watanzania, pamoja na kansa ya uongozi wake. Au watu wanaweza wakachoka, wakasema, "potelea mbali:" wakachagua Chama cho chote, ilimradi tu watokane na kansa ya uongozi wa CCM. Hainifurahishi kuyasema haya, lakini uhai wa Nchi yetu unataka yasemwe
. (Ukurasa 61)

Mwalimu hakuishia hapo, bali aliongezea namna hii:

Nilisema awali kwamba kansa ya uongozi ndani ya Chama cha Mapinduzi isingekuwa ni jambo la kutisha sana kama tungekuwa tumeanza kuona Chama kizuri cha upinzani kinachoweza kuiongoza Nchi yetu badala ya CCM. Ubovu wa uongozi ndani ya CCM ndio uliofanya nikapendekeza tuanzishe mfumo wa Vyama Vingi. Nilitumaini kuwa tunaweza kupata Chama kingine kizuri ambacho kingeweza kuiongoza Nchi yetu badala ya CCM; au ambacho kingekilazimisha Chama cha Mapinduzi kusafisha uongozi wake, kwa kuhofia kuwa bila kufanya hivyo kitashindwa katika uchaguzi ujao. Lakini bado sijakiona Chama makini cha upinzani; na wala dalili zo zote za kuondoa kansa ya uongozi ndani ya CCM. Bila upinzani mzuri wa nje, na bila demokrasia halisi ndani ya Chama cha Mapinduzi, Chama hiki kitazidi kudidimia chini ya uzito wa uongozi mbovu. Kwa hali yetu ya kisiasa ilivyo nchini hili si jambo la kutarajia bila hofu na wasi wasi!
(Ukurasa 66)

Ni wa-Tanzania wangapi wenye utamaduni wa kusoma vitabu? Ni wangapi wanaosoma vitabu vya Mwalimu Nyerere? Ni wazi kuwa umbumbumbu miongoni mwa wa-Tanzania ni neema kwa CCM.

3 comments:

tz biashara said...

Najua profesa unamkubali sana Nyerere lakini inawezekana hujamsoma upande wa pili alikuwa ni mtu wa aina gani.Sishangai wanachama wa CCM leo jinsi walivo na udini ni kutokana na Nyerere ndie hasa alie anzisha na mpaka leo waisilamu wenyekujua wengi hawamthamini Nyerere.

sijui kama uliwahi kusoma kitabu cha "LUDOVIC S MWIJAGE" ktk Google unaweza ipata hii makala ambayo ilipigwa marufuku nchini na inaitwa "The dark side of Nyerere legacy" Na pia isome makala inasema "Nyerere against Islam in Zanzibar" Na vilevile kama utaweza kuingia ktk web moja inaitwa "mzalendo.net ningeomba umsikilize shekhe anatoa hotuba ya kumhusu Nyerere na vita ya majimaji ukweli wake ambao historia za ukweli zilipigwa marufuku kwa amri ya Nyerere.

Kwakweli profesa ni masikitiko matupu na uonevu mtupu na wakati huo wa nyerere hakuna mtu anaweza kumkosoa na ukijaribu utayapata makubwa kama yaliyo mfika Ludovic mwijage au makubwa zaidi.Mimi binafsi wajomba zangu watatu walikamatwa na kufungwa zaidi ya miezi mitatu ktk uhujumu uchumi na baadae kuachiwa huru kwa kukosa ushahidi na kisa kwanini walikuwa na gunia la sukari na kwanini wanalory na walipata wapi???

Naomba utafute hizo video ktk hiyo web ya mzalendo.net ili uijue au uwajue hawa mashekhe ambao walikuwepo pamoja na Nyerere na ukipata nafasi ya kwenda TZ ukawatafute wapo Tabora kama sikosei na wakupe full issue.

Anonymous said...

kumkosoa Mwalimu kwa kutumia dini ni makosa makubwa kwa kuwa Mwalimu alikuwa ni mwanasiasa na sio kasisi hivyo kwa imani yake angeweza kutenda kama mkristo na pengine asifurahie uislam au waislam...Ila kama mwanasiasa tunashawishika kusema kuwa huyu ndiye kiongozi pekee aliyekuwa na maono juu ya mustakabali wa nchi yake na ilimlazimu wakati mwingine kufanya maamuzi magumu ili tu halaiki kubwa ya watanzania inufaike. Siuoni ubaya wa mtu kuwa na gari enzi zile hilo naliafiki ila siafiki kama mtu akiulizwa umepataje gari afu aanze kuwa mkali au alete jeuri. Ikumbukwe kuwa kama kiongozi wa nchi kuna maeneo lazima usimame na uoneshe kama unao uwezo wa kusimamia masuala muhimu na kuyatolea uamuzi.. hilo kwa sasa halipo kwa vile watu wameondsha utamaduni wa kuulizana nivipi umezipata mali zako... hamna utamaduni wa kuamua kutoka katika mapendeleo ya wengi(wananchi) badala yake viongozi wanatabiri matatizo ya watu... nguvu za kiserikali zimenyang'anywa toka ktk mamlaka za chini na kubakia juu tu..matokeo yake ni kuwa utawaona viongozi wa kijiji au kata wanafuatwa pale tu mtu anataka jambo lake fulani litimizwe.. Ni uozo tu umejaa sasa hivi. Mi nadhani tukichanganya changamoto za kisiasa na matukio ya kiimani ni rahisi kufikiri vibaya... na hivyo viongozi wabovu wataweza kujitafutia vichaka ktk dini zao.. Ila ikumbukwe kuwa hata siku moja dini haiwezi kuwa na urafikiwa kweli na siasa kwa vile siasa ni propaganda ambazo zinaweza kuwa ni ukweli au hata uwongo wakati dini ni ukweli mtupu... Tumlinganishe Mwalimu na viongozi wetu sasa au hata na wale wa enzi zke na tuseme nani anaweza kuiishi enzi yake sasa otherwise R.I.P Mwalimu.

Mbele said...

tz biashara shukrani kwa mawazo na mawaidha yako. Mimi hupenda kujielimisha muda wote, na sijiwekei mipaka. Maandishi ya Mwijage nimeyasikia siku zilizopita, na kiasi nimesoma, ila muhimu ni kuendelea kusoma. Hizo video nazo nitazifuatilia, Insha Allah. Sijiwekei mipaka katika kutafuta elimu.

Kwa msingi huo huo, suala la kupiga vitabu marufuku linanikera muda wote. Nilikerwa wakati kitabu cha Salman Rushdie cha "Satanic Verses" kilipopigwa marufuku. Nilikerwa wakati kitabu cha Hamza Njozi kuhusu mauaji ya Mwembechai kilipopigwa marufuku. Na kama kitabu cha Mwijage kilipigwa marufuku, inanikera.

Tabia za CCM ya leo haiendani na yale aliyotaka au kufundisha Mwalimu Nyerere. Mwalimu Nyerere mwenyewe alikuwa akiikosoa CCM kwa miaka mingi kabla ya kifo chake. CCM iliasi sera za mapinduzi aliyoyoaelezea Mwalimu katika Azimio la Arusha na kadhalika.

Suala la kukubaliana au kutokukubaliana na Mwalimu ni uhuru wa kila mtu. Wengi wanampinga Mwalimu, na hao ni wa-Islam, wa-Kristu, watu wa dini zingine, na wasio na dini. Wengi wanamwunga mkono Mwalimu. Na hao ni wa-Islam, wa-Kristu, wa dini zingine na wasio na dini.

Kwa hivi tusichukue mtazamo wa mkato wakati suala ni tata. Hata kama kuna waIslam wasiomthamini Nyerere, ukweli ni kuwa kuna waIslam wanaomthamini Nyerere. Mmoja wa hao ni Mzee Ruksa. Yeye alisema kuwa Mwalimu ni kama mlima na wengine ni vichuguu. Ni lazima tuheshimu mtazamo wa Mzee Ruksa, kwani yeye ni kati ya watu waliomfahamu sana Mwalimu, kwa miaka mingi ya kufanya naye kazi pamoja.

Tunasema kila siku kuwa tuheshimu taaluma za watu na uzoefu wao, na ni kwa msingi huu nasema msimamo wa watu kama Mzee Ruksa kuhusu Mwalimu una maana sana kwangu.

Hizi makala kama "Nyerere Against Islam in Zanzibar" zina kasoro moja kubwa kimtazamo. Kama Nyerere alipingana au kukorofishana na watu ambao ni waIslam, sio sahihi kusema kuwa yeye aliupinga au kuuchukia u-Islam. Nikigombana huko mitaani na akina Abdalla, Hussein, Salim, Rukia na Saida, mtu asiruke na kudai kuwa mimi nashambulia u-Islam.

Nyerere huyo huyo aliyewaweka kizuizini wa-Islam aliwaweka kizuini wa-Kristu. Kuna ndugu yangu mmoja, m-Katoliki kama mimi, ambaye naye alizuiliwa na Nyerere kwa namna hiyo. Je, niseme kuwa Nyerere alikuwa mpinzani wa u-Katoliki?

Nikipata fursa ya kukutana na hao mashehe, nitapanua uwigo wa mazungumzo ili tuwajumlishe pia hao waKristu ambao Nyerere aliwaweka kizuizini.

Ni muhimu kuangalia kwa undani na uyakinifu mambo yaliyosababisha tatizo, badala ya kurukia dini. Nimewasikia watu wakidai, kwa mfano, kuwa Nyerere alivunja jumuia ya wa-Islam iliyokuwa ikiitwa EAMWS na eti akawaanzishia BAKWATA badala yake.

Msimamo huu hauzingatii ukweli wa historia ambayo ilikuwa na masuala mengi. Suala mojawapo ni kuwa waIslam wengi waliokuwa wanaunga mkono sera za Mwalimu za utaifa na mapinduzi waliona EAMWS kuwa ni taasisi isiyoendana na malengo hayo, taasisi isiyoendana na misingi ya utaifa na ujamaa. Kwa hivi, hao walitaka kujitoa EAMWS na waliamua kuanzisha BAKWATA.

Kuna hoja zingine, lakini hiyo nayo inapaswa kuzingatiwa, badala ya kumpakazia Nyerere.

Wa-Islam wa Tanzania nawaona kama watu wenye akili na uwezo wa kujiamulia mambo yao, na ndivyo walivyofanya kwa kuanzisha BAKWATA.

Lakini utawasikia watu wameshikilia tu kuwa Nyerere alifanya hivi, mara hivi, mara vile, kama vile wa-Islam ni kondoo wasio na uwezo wa kufikiri na kujiamulia.

Mimi nawaheshimu wa-Islam kama watu waliokuwa wanajiamulia mambo yao, na wanaendelea kujiamulia. Sifa au lawama ni yao, kama ilivyo kwa wanadamu wengine.

Uthibitisho mojawapo wa kuwa wa-Islam ni watu wenye tafakari na uwezo wa kutoa maamuzi kwa maslahi yao na ya Taifa ni pale walipoamua kuwa Nyerere aongoze harakati za kudai Uhuru.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...