Sunday, April 26, 2009

Migogoro ya Kitamaduni Sehemu ya Kazi

Kadiri dunia inavyozidi kuwa kijiji, kwa maana kwamba umbali kutoka sehemu moja hadi nyingine unazidi kupoteza umuhimu, na mawasiliano baina ya watu yanazidi kuwa rahisi, na kukutana uso kwa uso inazidi kuwa rahisi, tutakuwa na kazi kubwa ya kujizatiti kukabiliana na tofauti za tamaduni duniani.

Watu wa kila utamaduni wana namna yao ya kufikiri, kuelewa, kufanya mambo, kuongea, na kadhalika. Wao kwa wao wanaelewana. Lakini dunia ya leo si ya watu kukaa na wenzao wanaoelewana tu, bali ni ya kukabiliana na watu wa tamaduni tofauti. Haijalishi kama uko Dar es Salaam, Tokyo, au Los Angeles. Mchanganyiko wa watu wa tamaduni mbali mbali unazidi kuziathiri sehemu zote za dunia.

Hapa Marekani, nimeona juhudi inayofanyika ya kujizatiti na hali hiyo. Sehemu za kazi, kwa mfano, kutokana na kuwa na wafanyakazi kutoka sehemu mbali mbali za dunia, wahusika wanaanza kuelewa umuhimu wa kujielimisha na kuelimishana kuhusu tofauti za tamaduni, ili kuzuia migogoro na kuboresha mahusiano kazini.

Mimi mwenyewe, kutokana na utafiti na uandishi wangu kuhusu masuala hayo, nimekuwa napata fursa za kwenda sehemu mbali mbali kuchangia mawazo na uzoefu wangu. Kwa mfano, tarehe 14 Februari, 2008, nilialikwa kwenye mji wa Minneapolis na kampuni ya RBC Wealth Management kutoa ushauri na uzoefu mbele ya timu ya uongozi wa kampuni hiyo.

Kampuni hii, kama kampuni zingine nyingi, ina mchanganyiko wa wafanyakazi kutoka sehemu mbali mbali duniani, wakiwemo waAfrika. Mazungumzo yangu yalihusu umuhimu wa kujifunza kuhusu tamaduni mbali mbali na mbinu za kukabiliana na hali hiyo, ili tuwe na maelewano na ufanisi mahali pa kazi na duniani kwa ujumla.

Pamoja na mazungumzo hayo, kampuni iliagiza nakala za kutosha za kitabu changu, Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, kwa watendaji waliohudhuria. Nilitambua kuwa kampuni hii inayo jadi ya kutafuta elimu kwa njia ya vitabu. Walinionyesha vitabu ambavyo walikuwa tayari wanavyo na wanavitumia, kwa lengo hilo hilo la kuelewa namna ya kushughulikia masuala yatokanayo na tofauti baina ya wafanyakazi. Kitabu kimoja walichonionyesha ni A Peacock in the Land of Penguins.

Hili ni fundisho kwetu waTanzania. Ni muhimu tuamke. Kama vile ilivyo Marekani na sehemu zingine duniani, waTanzania wanavyo vyuo, makampuni, na taasisi mbali mbali ambamo watu wa tamaduni mbali mbali wanashughulika. Kwa mfano, katika vyuo hivi na taasisi kuna watu wa kujitolea wanaotoka Marekani, Ulaya na sehemu zingine. Je, waTanzania wanaoendesha taasisi hizi wameshawahi kuwazia suala la elimu kwa wafanyakazi wote kuhusu tofauti za tamaduni? Mahusiano baina ya waTanzania na wageni katika sehemu hizo za kazi yakoje?

Kuna vile vile makampuni na taasisi za kigeni Tanzania, zenye wafanyakazi wananchi na wageni. Wahusika wana mkakati wowote wa kutoa elimu kuhusu tofauti za tamaduni?

Ukweli ni kuwa, mara kwa mara tunasikia taarifa za migogoro katika sehemu za kazi nchini Tanzania. Ninapoziangalia taarifa hizi, naona kuwa baadhi ya migogoro hii chanzo chake ni tofauti za tamaduni, au inachochewa na hizo tofauti za tamaduni. Tabia au kauli ya mgeni inaweza kuwaudhi waTanzania, ambao wanaichukulia kwa msingi wa utamaduni wa kiTanzania, na papo hapo, tabia au kauli ya mTanzania inaweza kumwudhi mgeni, kwa vile naye anaichukulia kwa misingi ya utamaduni wake. Shutuma zinatokea pande zote mbili. Nimeona, kwa mfano, waTanzania daima wanatoa malalamiko kuhusu ubaguzi. Sina hakika kama muda wote suala ni ubaguzi, bali nahisi kuwa wakati mwingine ni tofauti za tamaduni. Na wageni nao wanayo malalamiko mengi kuhusu waTanzania, ambayo msingi wake ni kutoelewa tofauti za tamaduni. Bila kuelimishana, magomvi hayo yataendelea na ufanisi sehemu za kazi utakuwa wa matatizo.

Je, waTanzania tunajizatiti vipi na masuala hayo ya dunia ya leo ambayo inazidi kuwa kijiji? Ninapenda sana kutafakari masuala hayo na kutoa mchango kwa kadiri niwezavyo. Nimeanza kuendesha semina nchini Tanzania. Ninajiandaa kufanya semina hizo mwaka huu pia. Kwa taarifa zaidi, yeyote anaweza kuwasiliana nami, kwa anwani hii: info@africonexion.com

Saturday, April 25, 2009

Mmarekani na Mswahili

Kwa miaka mingi nimekuwa katika utafiti wa tofauti baina ya utamaduni wa Mmarekani na ule wa Mswahili (yaani Mwafrika). Huwa najiuliza masuali mengi, kuhusu matatizo yanayoweza kutokea pale Mmarekani anapokutana na Mswahili. Nafahamu fika, na wengine wanafahamu pia, kuwa matatizo yanaweza kuwa mengi, kero, maudhi na kutoelewana. Lakini sikuwahi kuona kitabu kinachotoa mwanga kuhusu masuala hayo, kwa namna ya kuniridhisha.

Kwa vile kitabu cha aina hiyo niliyowazia hakikuwepo, niliamua kukiandika mimi mwenyewe. Niliona kuwa hakuna maana kukaa tu na kulalamika. Tatizo haliondoki kwa malalamiko, bali kwa vitendo.

Kitabu nilichoandika kinaitwa Africans and Americans: Embracing Cultural Differences. Napenda kuwashukuru wasomaji waliotoa maoni yao kuhusu kitabu hiki kwenye kumbi mbali mbali. Mmoja wa hao ni Dada Sophie ambaye ameandika maoni yake kwenye blogu mbali mbali.

Miaka ya karibuni, nimefahamiana na kikundi cha vijana wa Mto wa Mbu, Tanzania, wanaojishulisha na utalii. Hao vijana wananitia moyo kwa jinsi wanavyotambua umuhimu wa elimu, katika kufanikisha shughuli na miradi mbali mbali, na katika maisha kwa ujumla. Unaweza kusoma baadhi ya maelezo yao hapa na unaweza kusoma maelezo yangu hapa.

Sote tungefaidika iwapo wengine wangejitokeza na kuandika mawazo yao. Tunahitaji maandishi kuhusu tamaduni mbali mbali. Mimi niliandika kuhusu Wamarekani na Waswahili kwa vile hao ndio ninaowafahamu. Naendelea kuandika, hasa makala fupi fupi magazetini na katika majarida, kuhusu masuala hayo hayo. Panapo majaliwa, nitatoa kitabu kingine. Lengo ni kumsaidia Mmarekani na Mswahili kuepuka migongano isiyo ya lazima.

Kwa yeyote atakayependa, kitabu hiki na vingine vinapatikana Dar es Salaam, simu namba 0754 888 647 au 0717 413 073.

Tuesday, April 21, 2009

Maendeleo ni Nini?

(Makala hii imechapishwa katika gazeti la Kwanza Jamii, April 2009)

Dhana ya maendeleo iko kila mahali, katika maisha yetu binafsi, na katika maisha ya jamii na nchi kwa ujumla. Sote tunaamini kuwa tunahitaji maendeleo. Tusipofanya jitihada katika maendeleo, tunashinikizwa kwa namna moja au nyingine tufanye hiyo jitihada au tunaburuzwa tuendelee.

Katika kuziongelea nchi, watu hutumia dhana ya nchi zilizoendelea na nchi zinazoendelea au zisizoendelea. Kwa mujibu wa dhana hizo, nchi kama Marekani, Uingereza, Sweden, Ujerumani, na Japani zinahesabiwa kuwa zimeendelea. Lakini nchi kama Tanzania, Kenya, na Uganda zinahesabiwa kuwa nchi zinazoendelea. Dhana hizi zimejengeka vichwani mwa watu, tangu zamani. Je tunapotumia dhana hizi, tunaelewa tunachoongelea? Dhana hizi zina mantiki yoyote?

Binafsi, ingawa zamani nilikuwa na mawazo kama wengine, kwamba kuna jamii au nchi zilizoendelea na zile zisizoendelea au zinazoendelea, miaka hii nimegundua kuwa dhana hizi zina walakini au hazina mantiki bora. Nadiriki kusema kuwa dhana hizi zinadhihirisha kuwepo kwa kasumba vichwani mwetu, au elimu duni.

Kwa nini nasema hivi? Kwanza, kusema kuwa jamii fulani au nchi fulani imeendelea inaleta dhana ya kwamba jamii au nchi hiyo imefikia kilele na imegota hapo. Ukweli ni kuwa hakuna jamii wala nchi duniani ambayo imesimama tu. Kila jamii na kila nchi inabadilika muda wote, katika nyanja na vipengele mbali mbali: uchumi, siasa, utamaduni, na kadhalika. Hata hizo jamii au nchi ambazo zinasemwa zimeendelea nazo zinabadilika muda wote. Marekani ya mwaka juzi ni tofauti na Marekani ya leo, na Marekani ya miaka mitano ijayo itakuwa tofauti na hii ya leo. Kwa mfano, tekinolojia inabadilika muda wote katika nchi kama Marekani. Utamaduni na elimu ni hivyo hivyo. Na ndivyo ilivyo kwa nchi zote. Mabadiliko hayaishi, iwe ni katika Tanzania, Uingereza, au Marekani.

Kama huu mchakato na mabadiliko ndio maendeleo, basi kila nchi duniani ni nchi inayoendelea. Kwa hivi, dhana ya kuwepo kwa nchi zilizoendelea na nchi zinazoendelea haina mantiki bora. Ni upuuzi kuziweka baadhi ya nchi katika kundi la nchi zilizoendelea, wakati nazo ziko katika kubadilika muda wote.

Lakini, jambo la msingi zaidi ni kuitafakari dhana ya maendeleo. Tunapaswa kujiuliza: maendeleo ni nini, na nani anayeweka vigezo vya kupima haya maendeleo? Hili ni suali la msingi.

Kwa ujumla, baadhi ya nchi, hasa zile zilizotutawala wakati wa ukoloni, na zile zenye nguvu katika dunia ya leo, ndizo zinazoweka vigezo vya maendeleo. Kwa vile Ulaya inajitapa kwamba imeendelea, Waafrika na wengine sehemu mbali mbali za dunia nao wanakubali hivyo na kuziona nchi zao kuwa ni nchi zinazoendelea au zisizoendelea. Hayo ni mawazo ya kikoloni mamboleo. Ni kasumba ambayo ilienezwa na inaendelea kuenezwa mashuleni, katika vyombo vya habari, na taasisi nyingine nyingi.

Tunao wajibu wa kujikomboa kimawazo ili tuweze kufikiri sisi wenyewe, badala ya kuwa kasuku. Tuwe na vichwa timamu vya kutuwezesha kuyatafakari masuala sisi wenyewe. Tunapaswa tujijengee huu msingi ili tuweze kuitathmini dhana ya maendeleo, tuweze kujiuliza maendeleo ni nini? Katika kufanya hivyo, tuweze kujiuliza iwapo dhana ya maendeleo iliyoko Ulaya ni sherti tuipokee na kuikubali. Katika kutathimini suala la maendeleo, tunapaswa kuchukua jukumu na wajibu wa kujitungia vigezo vyetu na kuvitumia. Lazima tujenge utashi wa kujiamini na kujiamulia mambo yetu wenyewe kwa manufaa yetu.

Bila kufanya hivyo, tutabaki kuwa kasuku. Chochote wanachofanya Ulaya au Marekani, chochote kilichopo Ulaya au Marekani, au chochote kinachotoka huko tunakiona ni maendeleo. Tunaamini kabisa kuwa kuwaiga watu wa Ulaya na Marekani ndio maendeleo. Wao wakianzisha kitu, nasi tunataka tufuate. Vigezo vya elimu, utawala bora, demokrasia, na kadhalika vinawekwa na wao. Sisi tumekuwa watu wa kufuata.

Papo hapo, watu wa Ulaya na Marekani hawaoni mambo yetu kuwa ni maendeleo. Ni pale tu tunapoiga mambo yao ndipo tunahesabiwa kuwa tunaendelea. Hata tukaanzisha jambo, hawaoni kuwa ni maendeleo. Na sisi wenyewe, kwa kuangalia Ulaya na Marekani, hatuamini kuwa tunachofanya ni maendeleo. Kitu hichi kingeanzia Ulaya au Marekani, tungekiona kuwa maendeleo.

Hata kama jambo halina maana, au lina madhara, maadam linatoka Ulaya au Marekani, watu katika nchi zetu wanaliona ni maendeleo. Hata kama ni mambo yasiyoendana na utu, maadam yametoka Ulaya, watu wetu wanayaona ni maendeleo.

Naweza kutoa mfano moja. Nchi zinazoitwa zimeendelea zimefanikiwa kujenga miji mikubwa, viwanda, na miundombinu ya aina aina, na hivi kuonekana zimeendelea. Pamoja na kuwa kuna uharibifu mkubwa wa mazingira katika haya maendeleo, dhana ya kuwa hizo ni nchi zilizoendelea inabaki pale pale, na sisi tunakazana kuiga waliyofanya wao. Tunahangaika kufuata mkondo ule ule na kuharibu mazingira kwa ujenzi wa viwanda na miundombinu mbali mbali. Hatujali kuwa haya yanayoitwa maendeleo yameharibu na yanazidi kuhatarisha mazingira. Tunataka viwanda, bila kuangalia athari zake katika maji tunayotumia, hewa tunayovuta, na mazingira kwa ujumla. Hatujali kuwa maendeleo ya Ulaya na Marekani yameharibu mahusiano ya jamii. Je, hayo ndio maendeleo?

Kama nilivyosema, hakuna nchi ambayo imesimama tu na haibadiliki. Kosa tunalofanya ni kutozingtia ukweli huo na badala yake kuziona nchi za Ulaya na Marekani kama nchi zilizoendelea. Kwa mtindo tulio nao, wa kufuata kila kinachotoka Ulaya na Marekani, tutabaki na hii dhana ya kujidunisha, ya kujiona sisi ndio nchi zinazoendelea au zisizoendelea.

Kwa mtazamo wetu huu, hatutafikia kuwa sambamba na nchi hizo tunazosema zimeendelea. Tutabaki tukiamini kuwa sisi ni nchi zinazoendelea au zisizoendelea. Watu wa Ulaya na Marekani wataendelea kuyaona yale wanayofanya kuwa ndio maendeleo, na wataendelea kutushinikiza katika njia wanayoona wao kuwa ya maendeleo. Sisi tutakuwa daima watu wa kufuata. Kuna mipango mingi katika nchi yetu, ambayo inaitwa mipango ya maendeleo, inayofuata msingi huu na kuna taasisi nyingi kutoka nje ambazo zinafanya shughuli hizo zinazoitwa za maendeleo katika nchi yetu. Kwa mtindo huu wa kujidhania tuko nyuma, tutabaki nyuma daima.

Tunawajibika kujikomboa kifikra, tuweze kujiwekea vigezo vyetu wenyewe. Pasipo kuwa na vigezo vinavyozingatia haki ya kila watu duniani kuchangia katika kutunga tafsiri na viwango vya maendeleo, si sahihi kuendelea kutumia dhana ya nchi zilizoendelea na nchi zinazoendelea au zisizoendelea. Inatubidi tubadili fikra; tukatae huu mkondo uliopo sasa wa kuitwa au kujiita nchi zinazoendelea. Ni fikra tegemezi, za kikasuku, na kikoloni mamboleo. Athari za hizi fikra tegemezi zinaonekana kila mahali.

Tunapoongelea mfumo wa uchumi, kwa mfano, tunajikuta tunahangaika kuiga mambo ya Ulaya au Marekani. Tunapoongelea elimu, ni hivyo hivyo. Tunahangaika kufuata viwango vya Ulaya au Marekani. Leo hii, mtu akianzisha shule na kuiita Cambridge Academy halafu mwingine aanzishe yake na kuiita Upogoro Academy, watu watavutiwa zaidi na Cambridge Academy, bila kutafakari. Tunapoongelea urembo, kwa mfano, ni hivyo hivyo. Vigezo tunaiga vya Ulaya na Marekani.

Kutokana na fikra zetu hizi, mitumba kutoka Ulaya na Marekani tunaiheshimu sana. Vyakula kutoka huko navyo tunavienzi sana, hata kama havina ubora kiafya. Watu wa Ulaya na Marekani wakija kwetu na kujinadi kama wataalam tunawashabikia sana, hata kama watu hao ni mbumbumbu. Kwa vile tunaamini Ulaya na Marekani wameendelea, hatuwazii kuwa kuna mbumbumbu huko. Lakini mtu kama mimi, ambaye nimefundisha sana huko Marekani, ninajua kuwa Marekani, kama ilivyo Tanzania, kuna wenye vichwa na mbumbumbu pia wako.

Kuhitimisha, turudi kwenye suali la awali: maendeleo ni nini? Maendeleo ni mabadiliko katika kitu au hali yoyote, katika nyanja mbali mbali za maisha, mabadiliko ya manufaa kwa mujibu wa mazingira husika. Katika jamii au nchi, maendeleo yanaboresha maisha ya binadamu, yanahifadhi au kuboresha mazingira, na yanaendana na heshima, utu, na haki. Maendeleo yanatokana na msukumo wa jamii au nchi husika, kwa mujibu wa mahitaji yake halisi, na kwa mujibu wa maamuzi na matakwa ya jamii hiyo, maamuzi yatokanayo na fikra huru na tambuzi, zenye mwelekeo wa ukombozi. Maendeleo hayaathiri mazingira bali yanadumisha muafaka na kuyaboresha. Maendeleo hayaleti matabaka miongoni mwa wanadamu. Kama kuna kuiga, uigaji huo unazingatia vigezo hivyo vyote, na umejengeka katika kuheshimiana, si kushinikizana.

Wednesday, April 15, 2009

Mhadhara kwa Wamarekani Waendao Afrika Mashariki

Jioni hii, nimetoa mhadhara kuhusu tofauti za utamaduni wa Mwafrika na ule wa Mmarekani, kwa walimu na wanafunzi wa vyuo vya St. Benedict/St. John's, kwenye mji wa St. Joseph, Minnesota. Nilialikwa na idara inayoshughulika na masomo ya amani. Mhadhara huo ulihudhuriwa pia na watu ambao hawako katika idara hii.

Walimu walionialika wamesoma na wanakitumia kitabu changu kinachoelezea tofauti za tamaduni hizi. Baadhi ya hao walimu na waliohudhuria wanajiandaa kwa safari ya kwenda Kenya na Tanzania wiki za karibuni.

Mhadhara wangu ulikuwa sehemu ya matayarisho ya safari. Nilifanya nilivyoweza kuwaeleza mambo muhimu ya kuzingatia, nikinukuu niliyoeleza katika kitabu changu. Jambo moja la msingi nililosisitiza ni kuwa tunapofanya uamuzi kushirikiana na watu wa utamaduni tofauti na wetu, tuzingatie sana suala la kujielimisha kuhusu tofauti za tamaduni zetu, tangu mwanzo na wakati wote wa mahusiano hayo, na baada ya hapo pia. Tusipofanya hivyo, tutajikuta katika matatizo yasiyo ya lazima.

Baada ya mhadhara wangu, kama kawaida, tulikuwa na kipindi cha masuali na majibu. Nilikuwa nimewaeleza kwa mfano, jinsi waMarekani wanavyotofautiana na waAfrika kuhusu suala la kuwahi. Nilisema wazi kuwa waMarekani, ambao kwao suala la kuwahi ni muhimu sana, wawe tayari kuona tofauti wanapokuwa Afrika. Mtu mmoja akaniuliza kama itakuwa ni sahihi kwake kuchelewa atakapokuwa Afrika Mashariki. Nilimjibu kuwa akiwahi ni sawa, ila asisumbue akili yake akiona watu wamechelewa. Atulie, maana watakuja tu, kwani wana majukumu mengi humo njiani, kama vile kusalimiana vizuri na watu wanaokutana nao.

Kama nilivyosema, baadhi ya watu hao wataenda Tanzania, sehemu za Dar es Salaam, Njombe na Songea. Nimevutiwa kwa namna ya pekee na kikundi hicho, kwani kule Songea wataishi kwa wiki moja mahali ambapo nilisoma shule ya kati, ambapo panaitwa Hanga. Wataenda pia Mbamba Bay. Niliposikia hivyo, nilikumbuka nilivyotembelea Mbamba Bay mwaka jana, nikaandika habari zake.

Hadithi za waMatengo Minnesota

Jana nilifika hapa mjini St. Joseph, Minnesota, nikiwa mgeni wa vyuo vya St Benedict/St. John's. Nilialikwa na Profesa Lisa Ohm, ambaye alihudhuria semina niliyoshiriki kuiendesha miaka michache iliyopita, kuhusu hadithi za waSomali. Katika semina ile, Profesa Ohm alipata fursa ya kununua kitabu changu cha hadithi za Wamatengo. Baada ya kukisoma, aliniandikia ujumbe akisema kuwa amekipenda sana na akanipa tafakari yake kuhusu yaliyomo katika baadhi ya hadithi zile. Tafakari yake ilinifungua macho, kwani alinionyesha mambo ambayo sikuwa nimeyawazia, ingawa mimi ni mMatengo.

Profesa Ohm alinieleza kuwa anatumia kitabu kile cha hadithi za waMatengo katika kozi yake ya hadithi. Alisema pia kuwa hapo mjini St. Joseph wana kikundi cha watu ambao wamekuwa wakizisoma na kuzijadili hadithi zile. Ziara yangu ilitazamiwa kuwa fursa ya wanafunzi wake na wanakikundi kujifunza zaidi kuhusu hadithi na utamaduni wa waMatengo na waAfrika kwa ujumla.

Jana tulijumuika katika huo mjadala, ambao ulidumu kiasi cha saa nzima. Nilijitambulisha kifupi, na nikatoa fursa ya wao kuuliza masuali. Walikuwa na masuali mengi kuhusu vipengele mbali mbali vya hadithi za kiMatengo na utamaduni wao, na pia masuala ya hadithi kwa ujumla, wakizingatia yale niliyoandika katika kitabu changu.

Baadhi ya masuala yaliyojitokeza ni athari za kurekodi katika maandishi hadithi ambazo kwa asili yake ni za masimulizi ya mdomo. Katika hali yake ya kawaida, ya masimulizi, hadithi hizi hubadilika muda wote, hata kama ni kwa kiasi kidogo sana, kwani wasimuliaji hawakariri maneno ya hadithi. Wakiambiwa kusimulia tena na tena hadithi ile ile moja, tofauti nyingi zinajitokeza. Ukirekodi mara moja hadithi hiyo, kama tunavyofanya, na kisha kuiweka kitabuni, unakuwa umeipa sura ambayo haibadiliki, wakati katika mazingira yake halisi, hadithi hii haina sura moja.

Hili ni tatizo moja, ambalo nimelielezea katika kitabu changu. Yako masuala mengi mengine. Kwa mfano, kuna dhana zilizomo katika hadithi, ambazo undani na maana yake sisi watu wa leo hatuzielewi. Ni dhana za kale mno, na hata lugha inayotumiwa aghalabu hatuielewi, kwani nayo ni ya kale mno. Suala hili linajitokeza zaidi kwenye nyimbo zilizomo katika hadithi, na msingi wa tatizo ni kuwa nyimbo huwa na muundo maalum ambao si rahisi kubadilika, na kila kizazi kinarithi nyimbo hizi na kuziimba kama zilivyo. Watafiti wanakubaliana kuwa nyimbo ni kati ya vipengele vya hadithi ambavyo ni vigumu kabisa kubadilika.

Suala jingine lililojitokeza ni vitendo vya kutisha vilivyomo katika hadithi, kama vile vifo visivyo vya kawaida na mapambano baina ya binadamu na majitu ya kutisha. Leo waMarekani wengi wanajiuliza kama mambo hayo yanastahili kusimuliwa kwa watoto au la. Kumekuwa na juhudi ya miaka mingi Ulaya na Marekani ya kujaribu kurekebisha hadithi ili kupunguza vipengele hivyo vya kutisha, kwa hoja kwamba vinaweza kuwa na athari mbaya kwa watoto.

Binafsi, ninazingatia kuwa tangu enzi za mababu na mabibi, kuanzia huko kwetu hadi Ulaya na sehemu zingine duniani, jamii asilia hazikuwa na tatizo lolote kuhusu suala hilo. Hadithi hizi ndizo walizokuwa wanasimuliwa watoto, na hazikuwaathiri. Hata hadithi za waJerumani wa zamani, ambazo hatimaye zilirekodiwa na watafiti kama akina Jacob Grimm na mdogo wake Wilhelm Grimm, ambao walianza kuzichapisha mwaka 1812, zilikuwa na mambo ya kutisha au "yasiyofaa." Kuna malumbano miongoni mwa watafiti kuhusu suala la kama hao jamaa walizirekebisha kabla ya kuzichapisha.

Wanasaikolojia wa Marekani wanahangaika na masuali hayo, lakini kwa mtazamo wangu na uzoefu wangu wa kusimulia hadithi hizi kwa watu wazima na pia watoto wa hapa Marekani, naona labda watu wazima hawawaelewi vizuri watoto. Kila nilipopata fursa ya kuwasilimua watoto wa kiMarekani hadithi, wameonyesha kuvutiwa nazo kwa namna mbali mbali, hata kama zina mambo ambayo watu wazima wangesema yanatisha. Naona kuwa saikolojia ya watoto ni fumbo ambalo sisi watu wazima wa leo bado hatujalifumbua. Ni suala linalohitaji utafiti zaidi. Hayo yote nilipata fursa ya kuyaeleza kwenye mazungumzo ya jana.

Baada ya mjadala huo wa darasani, nilipata fursa ya kuongea tena kwa undani na Profesa Ohm, nyumbani kwake. Tuliongea kirefu, yeye, mume wake, na mimi, na Profesa Ohm alieleza kwa undani zaidi uchambuzi na tafakari yake kuhusu vipengele mbali mbali vya hadithi za kiMatengo. Aliniuliza pia masuali ya kufikirisha. Niliona jinsi anavyozama katika uchambuzi na kufichua mambo ambayo sikutegemea, yanayoonyesha falsafa nzito katika hadithi hizo. Pamoja na kuwa nami ni mtafiti, na ni mzaliwa katika utamaduni wa kiMatengo, ninakiri kuwa ninayo mengi ya kujifunza kutoka kwa watafiti makini kama Profesa Ohm. Nimeamini kwa miaka mingi kuwa mtu wa utamaduni tofauti anaweza kukuonyesha mambo yaliyomo katika utamaduni wako ambayo wewe mwenye utamaduni yatakufungua macho na akili kwa namna ambayo hukutegemea.

Sitasahau jambo hili, la kukutana na wageni hao, waMarekani, ambao wanazama namna hii katika kutafakari hadithi na utamaduni wa kwetu. Ni fundisho kwetu pia, kwamba tujizatiti kujifunza mambo ya wenzetu. Tutatambua tunavyofanana au kutofautiana, na tutajenga heshima kwa tamaduni zote, kwani kila utamaduni umesheheni hazina kubwa ya sanaa, falsafa na maadili ambayo kwa ujumla wake ni hazina kwetu binadamu wote.

Friday, April 10, 2009

Watanzania Wanaoishi Bloguni

Hivi karibuni nilianzisha mada hii hapa kuhusu Watanzania wanaoishi baa. Katika mjadala, ndugu Bwaya alishauri kuwa tunapozungumia suala hilo, tukumbuke pia kuna Watanzania wanaoishi vijiweni.

Nafikiri hili ni wazo muafaka. Na wazo hilo limenifanya nifikirie hizi blogu zetu. Tunaweza kuzichukulia blogu zetu kuwa ni vijiwe. Zinatoa huduma ile ile kama vijiwe. Ndugu Kamala ni mkweli, maana blogu yake ameiita kijiwe. Tuko Watanzania wengi ambao tunaishi bloguni, kama vile wenzetu wanavyoishi baa au vijiweni.

Jumuia ya wanablogu inaongezeka. Tumeshaanza kuwa kama kabila. Tunajitambua, na tunao utamaduni wetu, kama vile Wapogoro, Wakwere, au Wasukuma wanavyojitambua na tamaduni zao.

Tofauti na kijiwe asilia, ambacho labda kiko Buguruni au Magomeni, na ambacho wateja wake kwa kawaida ni wakaaji wa hapo hapo mtaani, hivi vijiwe vya mtandaoni, yaani blogu, vinajumuisha wateja kutoka pande zote za dunia. Hii ni ajabu, kwamba mtu unaweza kuanzisha kijiwe chako, yaani blogu, popote ulipo na kompyuta yako, halafu wateja wa kijiwe chako wakawa wanatoka pande zote za dunia.

Tofauti na vijiwe asilia, ambavyo ukitaka kuhudhuria, ni lazima utoke nyumbani mwako na kwenda vilipo, mtu anahudhuria vijiwe vya mtandaoni bila kutoka nyumbani au ofisini. Anakaa hapo hapo na kutembelea vijiwe vingi apendavyo. Hii ndio mila na desturi ya hili kabila jipya linalojumuisha wanablogu na wateja wao. Wanapita kwenye blogu nyingi na kusikiliza yanayozunguzwa huko na kuchangia. Mimi mwenyewe natumia muda mwingi kuzungukia hivi vijiwe vya mtandaoni. Nimeshakuwa mmoja wa Watanzania wanaoishi bloguni.

Tuesday, April 7, 2009

Ninakuja Tanzania: Nisome Vitabu Gani?

Jana nimepata barua pepe kutoka kwa kijana mmoja Mmarekani ambaye alikuwa mwanafunzi wetu hapa St. Olaf College, Minnesota miaka michache iliyopita. Ameniambia kuwa anaenda kutembelea Tanzania na Kenya wiki chache zijazo. Anauliza kama ninaweza kumpa ushauri wowote kuhusu namna ya kujiandaa, ikiwa ni pamoja na vitabu vya kusoma au filamu za kuangalia kabla hajasafiri.

Kwa waMarekani, kuuliza masuali ya aina hii na kujiandaa namna hii ni kawaida. Nazungumzia suala hilo mara kwa mara, kama unavyoona hapa. Tatizo ni upande wetu waTanzania. Sijawahi kumwona Mtanzania ambaye, anapopata fursa ya kwenda nchi ya nje, anatafuta vitabu vya kusoma kama sehemu ya maandalizi ya safari. Mtanzania huyu inawezekana anakwenda kufanya ziara au biashara au kutembelea ndugu na marafiki, kusoma au kufanya kazi. Anaondoka nchini na kwenda, bila kujishughulisha kama hao waMarekani wanavyojishughulisha. Ubalozi wa Marekani katika Tanzania una programu za kuwapeleka waTanzania Marekani kwa masomo. Wanajitahidi kutoa semina pale Ubalozini kuhusu hali ya Marekani, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya safari. Lakini sisi wenyewe waTanzania hatuna utaratibu kama huo. Tunawapeleka watu wetu nje, kwa mtindo wa "bora liende," au waende wakitegemea kudra ya Mwenyezi Mungu.

Je, hii ni sahihi? Tutaweza kuwa na ufanisi katika shughuli zetu nchi za nje ikiwa tunaingia huko bila ufahamu wa hali ya huko, tabia za watu, mila, desturi, na kadhalika? Tunaishije na watu wa huko? Tunaongeaje na watu wa huko? Tunafanyaje madajiliano na watu wa huko? Wanatuelewaje, nasi tunawaelewaje? Tunawaelewa wanaposema au kufanya jambo au tunabahatisha? Isije ikawa tunashangaa pasipo sababu, au tunakerwa na vitu ambavyo, kama tungekuwa tunavielewa, havingetukera. Isije ikawa tunawaudhi wengine kwa kufanya mambo yanayokubalika katika utamaduni wa kiTanzania, wakati huko ugenini hayakubaliki, ila sisi hatujui. Isije ikawa tunajikwamisha kwa kutofahamu hili au lile.

Katika dunia ya leo, tutaweza kweli kufanikiwa kwa kiwango tunachotegemea iwapo hatuna tabia ya kusoma vitabu?

Sunday, April 5, 2009

Kujichapishia Vitabu

Tangu shughuli ya uchapishaji wa vitabu ilipoanza nchini mwetu, wakati wa ukoloni, kuchapishwa kwa kitabu kulitegemea uamuzi wa mchapishaji. Waandishi hawakuwa na madaraka juu ya mchapishaji bali walikuwa kama watumwa mbele ya mchapishaji. Hali hii haikuwa kwa upande wa vitabu tu, bali hata aina nyingine za maandishi. Watunzi wa mashairi, kwa mfano, au insha, walikuwa chini ya himaya ya wahariri na wachapishaji pia. Ilikuwa ni kawaida kwa waandishi wa mashairi kuanza shairi kwa kumbembeleza mhariri asiwatupe kapuni.

Ukifanya utafiti kuhusu yule mwandishi wetu maarufu, Shaaban Robert, kwa mfano, utaona kuwa pamoja na kipaji kikubwa alichokuwa nacho, hakuwa na madaraka juu ya wachapishaji wake. Hali hii ya waandishi kuwategemea wachapishaji bado haijabadilika nchini Tanzania. Wachapishaji wameendelea kuwa kama miungu, na waandishi wanalalamika sana kuhusu wachapishaji. Malalamiko ni ya namna nyingi, kama vile kucheleweshwa taarifa kuhusu miswada, kucheleweshwa kuchapishwa miswada, kucheleweshwa malipo ya ruzuku ya uandishi, au kutolipwa kabisa.

Sio jambo jema kwa waandishi wetu kubaki na mtazamo tegemezi, tuliorithi tangu zamani. Dunia inabadilika. Mabadiliko hayo yapo pia katika uwanja wa uchapishaji vitabu. Maendeleo ya tekinolojia yamefikia mahali ambapo mwandishi anaweza kujichapishia vitabu vyake bila kutegemea wachapishaji.

Niligundua hayo miaka kumi na kidogo iliyopita, nilipokuwa tayari kuchapisha kitabu changu cha hadithi za waMatengo. Nilikuwa nimesikia na kusoma kuhusu kuwepo kwa tekinolojia ya kuchapisha vitabu mtandaoni. Nilifanya utafiti, nikaona aina mbali mbali za uchapishaji huo. Hatimaye, niliamua kuchapisha kitabu changu kwenye kampuni mojawapo. Niliendelea kuandika, na papo hapo nikaendelea kufanya utafiti juu ya tekinolojia ya uchapishaji. Hatimaye, nikagundua kampuni iliyonivutia zaidi, na huko ndiko ninachapisha vitabu vyangu.

Ushauri wangu kwa waandishi wa Tanzania na kwingineko ni kuwa badala ya kukaa na kuendelea na jadi ya kuwalalamikia wachapishaji, watafakari suala la kujichapishia wenyewe vitabu vyao. Kitu cha msingi ni kuhakikisha mswada umeandikwa vizuri na kuhaririwa kikamilifu. Kwa kawaida, mswada unachapishwa mtandaoni kama ulivyoandikwa, hata kama una makosa. Hakuna huduma ya uhariri. Hii ndio tahadhari. Vinginevyo, kama mswada umeshakuwa tayari, uchapishaji unaweza kuchukua dakika chache tu, badala ya miezi au miaka, kama ilivyo sasa. Leo hii, kutokana na maendeleo ya tekinolojia, kila mtu anaweza kuchapisha kitabu chake.

Friday, April 3, 2009

Santa Claus Anafanya nini Tanzania?














Miaka hii, Santa Claus anaonekana Dar es Salaam na sehemu zingine Tanzania. Zamani, tukiwa wadogo, hatukuwahi kumwona babu huyu, labda vitabuni. Siku hizi wakati wa Krismasi, anaonekana, hasa kwenye maduka makubwa mijini.

Santa Claus ametokea Ulaya. Wakati wa Krismasi, huko Ulaya na Marekani ni majira ya baridi kali, na theluji hutanda kila mahali. Wenyeji wa huko huvaa mavazi mazito kutokana na hali hiyo. Santa Claus naye anavaa hivyo, kutokana na hiyo baridi kali.

Sijui hao waliomleta Santa Claus Tanzania walisahau kuwa Tanzania hakuna baridi ya aina hiyo? Nashangaa kumwona Santa Claus sehemu kama Dar es Salaam, kwenye joto sana majira ya Krismasi. Au labda ndio maendeleo yenyewe?
(Foto kutoka PDPhoto.org)

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...