Friday, November 27, 2009

Elimu ya Kijijini

Makala hii ilichapishwa katika gazeti la KWANZA JAMII

Profesa Joseph L. Mbele

Mara kwa mara nakumbuka elimu niliyopata kijijini, kabla ya kuanza shule. Wengi wetu tulipitia njia hiyo. Ni elimu gani hiyo? Tangu utotoni, tulipata maelekezo kutoka kwa wazazi kuhusu mambo mbali mbali, kufuatana na umri, kuanzia namna ya kuvaa hadi namna ya kula kwa adabu na kuwasalimia watu.

Baadaye wavulana tulijifunza kuchunga mbuzi na ng’ombe, na kutandika nyasi kwenye zizi la ng’ommbe, na kukamua maziwa. Wasichana walifundishwa kazi za jikoni na kulea watoto.

Kama ilivyo kwa watoto wengine, baba na mama walikuwa wananituma kufanya shughuli hii au ile. Hata majirani walikuwa wanatutuma sisi watoto kuwasaidia shughuli mbali mbali. Yote hii ilikuwa ni sehemu ya elimu yetu.

Nilipokua kidogo nilianza kushiriki katika kilimo. Nilijifunza kulima, kupanda, kupalilia, na kuvuna mazao. Nilijifunza kuchuma kahawa na kuishughulikia baada ya hapo. Shughuli hizi ziliniwezesha kufahamu zaidi habari za udongo, nyasi, na magugu. Niliwafahamu wadudu wanaoishi mashambani, kama ni wadudu salama kwa mimea au ni adui wa mimea. Nilizijua tabia za wadudu mbali mbali, kuanzia siafu hadi sisimizi na mchwa. Nilijua kama wanauma au hawaumi. Tulijifunza namna ya kuwanasa kumbikumbi, ambao walikuwa ni chakula.

Katika kuchunga mbuzi na ng’ombe tulipata fursa ya kujifunza mambo mengi, sio tu kuhusu tabia za hao wanyama, bali pia elimu ya mimea na nyasi, zikiwemo nyasi ambazo ni chakula cha mbuzi au ngombe na kadhalika. Huko porini tulijifunza pia aina mbali mbali za mboga za porini, matunda, uyoga, na kadhalika. Tuliweza kutofautisha uyoga ambao unalika na binadamu na ule ambao ni sumu.

Katika kukua kwetu kijijini, tulisikiliza hadithi na nyimbo, tukaweza kusimulia hadithi hizi na kuimba nyimbo. Hadithi hizi zilisheheni falsafa, maarifa, na maadili. Tulishiriki katika ngoma, tukaweza kupiga ngoma na ala zingine za muziki, kucheza na kuimba. Mbali ya kwamba hii ilikuwa ni burudani, ilikuwa pia elimu ya sanaa. Ilikuwa ni elimu kuhusu namna ya kushirikiana na wengine, kwani ngoma inahitaji nidhamu na ushirikiano.

Kwa kuwa nilisoma shule ya msingi nikiwa bado naishi kijijijini, niliendelea kuipata elimu ya kijijini hata baada ya kuanza shule. Baada ya masomo shuleni, niliporudi nyumbani, niliendelea na shughuli ya kuchunga mbuzi na ng’ombe, na kusaidia shughuli mbali mbali za nyumbani ambazo ziliendelea kuimarisha elimu yangu ya kijijini.

Baada ya kumaliza darasa la nne, mambo yalibadilika sana. Nilikwenda shule ya bweni, mbali kabisa na nyumbani kwangu. Elimu niliyoipata kule ilikuwa ya vitabuni zaidi. Ingawa tulifanya pia shughuli za nje, kama vile shambani na bustanini, muda mwingi zaidi tulitumia katika kujifunza yaliyomo vitabuni. Elimu ya vitabuni ilishamiri kichwani mwangu nilivyozidi kuendelea na madarasa, hadi chuo kikuu Dar es Salaam, na hatimaye Marekani.

Kadiri nilivyoendelea na elimu ya shuleni, nilizidi kusahau elimu ya kijijini. Kusoma sana kuliendana na kufifia kwa elimu niliyoipata kijijini. Leo hii, sikumbuki majina ya mimea mingi, wala ya aina nyingi za majani niliyojifunza kijijini. Nimesahau majina na tabia za wadudu, wanyama, na ndege mbali mbali. Sina tena ufahamu mzuri wa miti na majani ambayo ni dawa, miti ambayo ni bora kwa kuni na ile ambayo si bora, kwa vile labda haishiki moto haraka au inatoa moshi mwingi. Hii ni hasara kubwa.

Elimu ya kijijini ni elimu thabiti. Ni elimu ambayo imekusanya ujuzi na maarifa kutoka enzi za zamani. Vizazi kwa vizazi vimechuja na kuhifadhi yale yaliyo muhimu tu. Kila kinachofundishwa kina maana katika maisha. Ndio elimu ya kijijini.

Hapakuwa na vitabu wala maktaba. Kila kitu kilihifadhiwa akilini na kurithishwa kutoka kizazi hadi kizazi kwa maneno ya mdomo na kwa vitendo. Elimu ya kijijini haikuwa inakaa maktabani, bali watu walitembea nayo vichwani. Kutokana na ulazima wa kuhifadhi kila kitu katika akili ya binadamu, hapakuwa na nafasi kubwa ya kuhifadhi lolote ambalo halikuwa na maana au umuhimu. Hii ni tofauti na leo, ambapo tunatumia zaidi vitabu. Tunao uwezo wa kuhifadhi vitabu kiasi chochote, hata kama havina maana.

Hakuna ubishi kuwa vitabu vingi ni muhimu, kwani vinabeba elimu ya aina aina. Lakini, kuna pia vitabu ambavyo havina uhusiano na maisha ya wale wanaosoma. Katika shule, kuanzia enzi za ukoloni hadi leo, tunawafundisha vijana mambo mengine ambayo hayana mantiki wala umuhimu katika hali na mahitaji ya jamii zetu. Wakoloni walianzisha mtindo wa kufundisha mambo ya kwao bila kuzingatia umuhimu au uhalali wake katika mazingira ya kwetu. Walizipotosha akili za vijana, na kwa bahati mbaya upotoshaji wa aina mbali mbali bado unaendelea, kama walivyoelezea watalaam kama Franz Fanon na Mwalimu Nyerere. Hii ni tofauti na elimu ya kijijini, ambayo ilienda sambamba na maisha na mahitaji ya wahusika.

Kwa vile elimu ya shuleni inadhihirishwa kwa vyeti, wako ambao wanatafuta njia za mkato, zisizo halali, kupata hivyo vyeti. Wengine wanaiba mitihani. Huu ni udhaifu wa mfumo wa elimu ya shule. Elimu ya kijijini haikuwa na mwanya wa namna hiyo. Hapakuwa na njia za mkato. Hapakuwa na mitihani ya kuiba. Kama ilikuwa ni kwenda kwenye unyago na jando, kila mhusika alitimiza yaliyohitajika.

Tujiulize suali moja: Je, kuna sababu yoyote ya kuendelea kuisahau au kuififisha elimu ya kijijini kwa vile tu mtu anaendelea na elimu ya shuleni? Je, haingekuwa bora kuiingiza elimu ya kijijini mashuleni ili kuhifadhi na kudumisha hazina hii ya urithi wetu?

Tuesday, November 24, 2009

Utamaduni na Utandawazi

Makala hii ilichapishwa katika KWANZA JAMII.

Profesa Joseph L. Mbele

Tangu mwaka jana, nimekuwa naendesha warsha hapa Tanzania kuhusu utamaduni na utandawazi. Mwaka jana nilifanya hivyo Arusha, na mwaka huu nimeendesha warsha Tanga na Dar es Salaam. Warsha hizi zimehudhuriwa na watu kutoka Tanzania, Kenya, Cameroon, Uingereza, Sweden, na Marekani. Hao wa nchi za nje ni watu waliokuwepo Tanzania kwa shughuli mbali mbali.

Niliamua kuanza kuendesha warsha hizi hapa Tanzania kutokana na kutambua kuwa ni muhimu katika dunia ya leo inayozidi kuwa kijiji. Watu wa tamaduni mbali mbali wanazidi kukutana kwa sababu mbali mbali, kama vile biashara, masomo, utalii, na uwekezaji. Watu wa tamaduni mbali mbali wanajikuta wakifanya kazi pamoja viwandani, maofisini, na kadhalika. Wanafunzi, watafiti, na walimu, wanajikuta wakishughulika na watu wa tamaduni mbali mbali.

Hali hii inaweza kusababisha migogoro ya aina aina, kwani kila mtu ana namna yake ya kuongea, kufikiri, kufanya mambo, ambayo inatokana na utamaduni wake. Bila kuelewa utamaduni wa wengine, matatizo lazima yatatokea, kama vile kutoelewana na kugombana.

Kwa miaka mingi katika kufundisha Marekani, nimehusika pia katika kutoa ushauri kwa waMarekani kuhusu utamaduni wa waAfrika. Wamarekani hao ni wale wanaokuja Afrika, iwe ni kwa masomo, utalii, shughuli za kidini, au za kujitolea. Nimehusika pia katika kutoa ushauri kwa waAfrika waishio Marekani, kuwasaidia kuulewa utamaduni wa Mmarekani.

Uzoefu huu umenifungua macho kuhusu umuhimu wa suala hili la kuelewa tamaduni mbali mbali, hasa kwa kuwa dunia inabadilika na kuwa kijiji. Hatutaweza kukwepa maingiliano baina ya tamaduni mbali mbali. Wafanya biashara watahitaji kutafuta masoko katika nchi za mbali, au watahitaji kutafuta washiriki kutoka nchi za mbali, au watahitaji kutafuta malighafi kutoka nchi za mbali. Makampuni yatahitaji kuwaajiri watu kufanya shughuli zake sehemu mbali mbali duniani, na katika kufanya hivyo, yatawajibika kuwaajiri watu wa tamaduni mbali mbali.

Kutokana na uzoefu huu nilioupata Marekani, niliona niko tayari kufanya warsha Tanzania. Nilikuwa na hamu ya kukutana na waTanzania na kuona nitafanikiwa vipi kuleta ujumbe wangu.

Jambo la kwanza nililofanya katika warsha hizi ni kuelezea maana ya utamaduni na maana ya utandawazi. Utamaduni, kama nilivyogusia, ni dhana inayojumlisha tabia, mwenendo, hisia na taratibu za maisha. Hata namna ya kuzungumza hutofautisha utamaduni mmoja na mwingine, kiasi kwamba, kwa mfano Mmarekani akisema jambo, linaweza kuonekana kuwa ni maudhi kwa Mwafrika au utovu wa heshima, wakati kwa utamaduni wa Mmarekani, ni usemi wa kawaida au wa heshima. Kadhalika, Mwafrika anaweza kusema jambo ambalo ni la kawaida au la heshima katika utamaduni wake, lakini likawa kero kwa Mmarekani.

Kuhusu utandawazi, dhana yangu ni kuwa utandawazi haukuanza miaka yetu hii, kama wengi wanavyofikiri. Ni jambo lililoanza zamani sana, tangu enzi za binadamu wa mwanzo kabisa. Utandawazi ulianza pale binadamu waliposambaa kutoka Afrika, ambako ndiko walikoanzia, na kuenea duniani. Kuenea huku kwa binadamu kuliandamana na kuenea kwa ujuzi, maarifa, lugha, na mambo mengine mengi.

Utandawazi ulichukua sura mbali mbali kadiri historia ilivyosonga mbele. Katika enzi zetu, utandawazi umetawaliwa na kuenea kwa ubepari, ambao umeathiri uchumi, siasa, utamaduni, na mambo mengine mengi.

Pamoja na hayo, bado tunazo tofauti za tamaduni ambazo zinaweza kuwa kipingamizi tunapokutana na watu wa nchi mbali mbali. Hapo ndipo ulipo umuhimu wa kujielimisha kuhusu tofauti hizi.

Baada ya kuongelea masuala haya ya jumla na kinadharia katika warsha hizi, niliingia katika kutoa mifano ya matatizo ambazo makampuni yamekumbana nayo wakati wa kujaribu kupeleka shughuli zao katika nchi za mbali, kwenye utamaduni tofauti. Makampuni ya Marekani, kwa mfano, yamewahi kupata matatizo katika nchi za Ulaya na Asia. Hata namna ya kutangaza biashara inaweza kuwa chanzo cha matatizo. Tangazo ambalo linavutia wateja katika utamaduni fulani linaweza kuwa kero kwa watu wa utamaduni tofauti. Hata rangi zinazotumika katika tangazo zinaweza kuwa na maana tofauti au kuleta hisia tofauti katika tamaduni mbali mbali.

Kwa bahati nzuri, washiriki wa warsha hizi wamevutiwa na wamesisitiza kuwa ni muhimu warsha hizi ziendelee siku za usoni, kwenye mashirika, vyuo, na taasisi mbali mbali. Kwa upande wangu, nimefurahi kupata fursa ya kuongea kwa undani na waTanzania ambao tulikuwa hatufahamiani. Nimefurahi kuanza kuamsha fikra za masuala haya muhimu miongoni mwa waTanzania. Nimefurahi kuanza kujenga mtandao wa watu ambao tutaweza kuchangia kwa namna fulani maendeleo katika jamii yetu.

Katika kuthibitisha zaidi hoja hizi, nimekuwa nikiongelea mifano hai ya jinsi utamaduni wa Mmarekani unavyotofautiana na utamaduni wa Mwafrika, kama nilivyojionea mimi mwenyewe katika kuishi kwangu na waMarekani. Katika kufanya hivyo, nimekuwa nikitumia kitabu ambacho nimeandika, na ambacho kinatumika na waMarekani wanaofika Afrika, na pia waAfrika wanaoishi Marekani. Ninaandika muda wote, na hii ni njia ya kuendelea kujifunza mimi mwenyewe na kuendelea kutoa mchango wangu katika masuala haya muhimu.

Kitu kimoja ambacho nimekuwa nikisisitiza ni kuwa hili ni suala la elimu, na elimu haina mwisho. Tunawajibika kuanza kujielimisha na kuendelea hivyo bila kuchoka. Warsha moja au mbili haitoshi, bali ni mwanzo. Ni mwanzo mzuri, na nangojea kuendelea kuendesha warsha hizi siku zijazo.

Tuesday, November 17, 2009

Maprofesa Hatuvunji Msitu, ni Mwalimu wa Shule ya Msingi

Picha hii ilichapishwa tarehe 15 Novemba katika blogu ya Haki Ngowi, pamoja na maelezo haya: Mwalimu, Albert Juakali wa shule ya msingi Iboma iliyopo kijiji cha Udinde Wilaya ya Chunya Mkoani Mbeya akifundisha wanafunzi wa darasa la kwanza chini ya Mti wa Mbuyu kama alivyokutwa na Mpigapicha wetu. Picha na Brandy Nelson
Nina mengi ya kusema kuhusu picha hii. Kwa leo napenda kumwongelea huyu mwalimu, kwa kuirejesha makala yangu iliyotokea katika gazeti la KWANZA JAMII.

Maprofesa hatuvunji msitu, ni Mwalimu wa Shule ya Msingi


Na Profesa Joseph L. Mbele

TUNAONGELEA sana mfumo wa elimu. Kitu kimoja ninachoona hatukizungumzii ipasavyo ni wadhifa wa mwalimu wa shule ya msingi. Jamii haimwoni mwalimu wa shule ya msingi kama mtu wa pekee sana. Lakini, akitokeza mwalimu wa chuo kikuu, kama mimi, jamii inafungua macho na kutega masikio. Jamii inamwona mwalimu wa chuo kikuu, profesa, kuwa mtu wa pekee sana, kumzidi mwalimu wa shule ya msingi.

Kwa miaka kadhaa sasa, nimejjijengea mtazamo tofauti kuhusu suala hilo. Hii ndio mada ya makala yangu hii. Hoja yangu ni kuwa, mwalimu wa shule ya msingi anastahili heshima ya pekee. Tunaposema shule ya msingi, tuzingatie neno msingi.

Neno msingi tunalitumia sana tunapoongelea ujenzi wa nyumba. Basi, tuchukulie mfumo wa elimu kama nyumba. Tunapowazia kujenga nyumba, tunazingatia sana msingi, kuhakikisha kuwa ni imara. Kila mtu anajua kuwa ukishafanya hivyo, nyumba yako itakuwa imara. Basi, na elimu ni hivyo hivyo. Ili iwe imara, ni lazima tuanzie kwenye msingi. Na hapo ndipo tunamkuta mwalimu wa shule ya msingi. Yeye ni kama yule fundi mjenzi tunayemtegemea kutujengea msingi imara. Hapo tunaanza kuelewa maana halisi ya dhana ya shule ya msingi.

Tunaweza kutoa mfano mwingine. Tukichukulia ualimu kama kazi ya ukulima, basi mwalimu wa shule ya msingi ni sawa na yule mkulima anayevunja msitu. Sisi walimu tunaokuja baadaye kwa mfano chuo kikuu, tunakuta shamba limeshatayarishwa. Kazi yetu ni nyepesi tukiichukulia kwa mtazamo huu wa kumkumbuka aliyevunja msitu. Ni lazima tumwenzi mvunja msitu, ambaye ni mwalimu wa shule ya msingi. Ni msitu gani huo anaovunja?

Mwalimu wa darasa la kwanza ana jukumu la kuleta mapinduzi katika akili ya mtoto. Anamtoa katika fikra na mazoea ya kucheza siku nzima na kuwinda ndege na kumwingiza katika ulimwengu wa ukurasa wa daftari na kitabu. Huu ni ulimwengu mwingine kabisa, na mapinduzi yanayofanyika hapa ni makubwa. Mtoto alikotoka anajua lugha ya kuongea na kusikia. Lakini mwalimu wa darasa la kwanza anambadilisha na kumfanya aifahamu lugha andishi. Maneno ambayo mtoto alizoea kuyasema tu na kuyasikia, sasa anapaswa ayaone na ayaelewe yanakuwaje kimaandishi. Ajifunze kuandika na kusoma, sio kusema tu na kusikia. Ajifunze namna ya kupanga kila herufi, neno, na sentensi kwenye mstari ulionyooka. Afahamu ukurasa unapangwaje: aanzie juu kwenda chini, si vinginevyo. Maneno ayaandike vipi, nukta na mkato aziweke wapi, na alama za kuuliza na kushangaa aziweke wapi. Haya ni mapinduzi makubwa ya akilini.

Katika mapinduzi hayo, mtoto anaanza kukiona kila kitu kwa mtazamo wa maandishi. Akiona kiti, anajua namna ya kuandika neno kiti. Akiona mnyama au mdudu, anajua namna ya kuandika mnyama au mdudu. Akili ya kuielewa lugha kama kitu cha kusema na kusikia tu inapanuliwa. Akili hiyo inakutana na lugha kwa kutumia macho. Hii ni lugha andishi.

Baada ya mwalimu wa shule ya msingi kufanya hayo mapinduzi akilini mwa mtoto, ndipo sisi walimu wa madarasa yanayofuata tunaletewa huyu mtoto. Sisi hatuleti mapinduzi. Hatuvunji msitu, wala kujenga msingi. Tunaingia darasani na kuongea sana, na wanafunzi wanaandika wanachosikia. Tunawaambia waende maktabani wakasome. Lakini hayo yanawezekana tu kwa vile mwalimu wa shule ya msingi alishawafundisha hao wanafunzi kuandika na kusoma. Bila hivyo, sisi tungekwama. Kwa bahati mbaya, tunasahau jambo hilo. Tunamsahau aliyevunja msitu na tunadhani kusoma na kuandika kuliwezekana au kulijitokeza kiurahisi tu.

Huwa najiuliza, je, nikiambiwa nikafundishe darasa la kwanza, nitaweza? Nina hakika nitaumia kichwa. Bahati nzuri, kwa miaka kadhaa nimekuwa nawatafuta walimu wa shule za msingi sehemu mbali mbali za Tanzania na kuongea nao. Wamenifungua macho kuhusu mambo kadhaa, kama vile saikolojia na tabia ya watoto. Wamenielimisha kuwa watoto wana saikolojia tofauti kufuatana na umri: watoto wa darasa la kwanza wana tabia hii na hii, na unapaswa unapowafundisha ufanye hivi au hivi. Ukifanya vile au vile, hutafanikiwa katika kuwafundisha. Mimi sikujua hayo, lakini walimu wa shule ya msingi wamenifundisha.

Walimu hao wameniambia kuwa unapowafundisha watoto wadogo, uangalie unatumia muda gani kwa kitu kimoja, ili ubadili na kufanya kitu kingine. Usijaribu kuwafundisha kitu kimoja kwa muda mrefu. Ukitoa maelezo kwa dakika kadhaa, unabadili; labda uwaimbishe wimbo. Baada ya dakika kadhaa, labda wachukue daftari na kuchora; baadaye wasome, na kadhalika. Usijaribu kutoa mhadhara kwa muda mrefu, kama tunavyofanya chuo kikuu. Elimu hii nimeipata kutoka kwa walimu wa shule za msingi. Kwa maana nyingine, ningekurupuka tu na kwenda kufundisha kule, ningeharibu mambo. Sijui maprofesa wangapi wanajua hayo.

Kitu kimoja tunachohitaji ni kumtambua mwalimu wa shule ya msingi kwa kazi anayofanya na kumpa fursa kamili ya kufanya kazi yake. Katika Tanzania, tangu miaka ya mwanzo ya Uhuru, tuna jadi ya kuwatwisha walimu majukumu ambayo si ya lazima. Kwa mfano, kwenye sherehe za kitaifa au mapokezi ya viongozi, walimu wametegemewa kuwaandaa watoto wa shule katika gwaride, nyimbo, ngoma, au halaiki. Maofisa kilimo, wahasibu na watumishi wengine ambao wangeweza kabisa kufanya shughuli hizo, hawaguswi. Kwa nini hao wasifanye hizo shughuli za magwaride, ngoma, na halaiki, kama ni shughuli muhimu? Walimu wametumika katika shughuli nyingine pia, kama vile kusimamia kura na hata kuwapikia viongozi. Hizi ni kero zisizo na sababu. Walimu wana kazi nyingi: kuandaa masomo, kufundisha, na kusahihisha daftari za wanafunzi au mitihani..

Baadhi ya matatizo yanayoendelea kuwepo kutokana na walimu wa ngazi mbali mbali kutokuwa na mshikamano. Ingekuwa bora iwapo walimu wa shule za msingi na wale wa sekondari, hadi wa vyuo vikuu, wawe na mshikamano thabiti, na mawasiliano ya daima. Kama nilivyogusia hapo juu, mwalimu wa shule ya msingi ana mengi ya kutufundisha sisi wengine. Anao uwezo wa kutupa mwanga kuhusu njia waliyosafiri wanafunzi tunaowafundisha vyuoni.

Naamini, ingekuwa bora pia kwa walimu wa vyuo vikuu kujaribu kufundisha shule ya msingi. Ingekuwa njia nzuri ya kujielimisha. Ninafahamu kuwa profesa akienda kufundisha shule ya msingi, waTanzania watamshangaa, na huenda wakadhani amechanganyikiwa. Lakini kuna mengi muhimu ambayo profesa anaweza kujifunza kwa kufundisha shule ya msingi, angalau mara moja moja.

Monday, November 16, 2009

Ziara Katika Shule ya Sayansi ya Mazingira

Kwa miaka yapata kumi, nimekuwa nikialikwa kila mwaka kwenda kwenye shule ya sayansi ya mazingira mjini Apple Valley, Minnesota, kutoa mhadhara kwenye somo la falsafa za jadi na mazingira.Mimi kama mtafiti wa masomo yahusuyo masimulizi na falsafa za jadi na utamaduni kwa ujumla, nimetumia fursa hii kuwaeleza wanafunzi namna binadamu, tangu mwanzo wake hapa duniani, alivyoweza kuyatafakari, kuyatathmini na kuyaelezea mazingira. Tangu enzi za mwanzo binadamu aliunda lugha kama chombo mahsusi cha kumwezesha kufanya yote hayo. Uundaji wa lugha halikuwa jambo rahisi, tangu kuvipa majina viumbe na vitu vyote vilivyomzunguka hadi kusema na kuelewana na binadamu wengine.

Kila mwaka, mwalimu Todd Carlson, ambaye amekuwa akinialika, anawaelezea wanafunzi kuhusu utafiti wangu juu ya fasihi simulizi na falsafa za jadi, na anawasomesha kitabu changu cha Matengo Folktales. Hadithi, nyimbo na semi ni baadhi ya mikondo aliyotumia binadamu kuyaelezea mazingira yake na kukidhi duku duku ya akili yake kuhusu yote yaliyomzunguka. Historia ya binadamu imeenda sambamba na upanuaji na utajirishaji wa urithi huo. Hakuna kitu wala kiumbe ambacho binadamu hakukipa angalau jina. Jina ni simulizi ambalo linapambanua kitu au kiumbe kimoja na kingine. Kutoka kwenye kiwango cha majina, binadamu ametunga hadithi, nyimbo, na semi kuhusu misitu, wanyama, ndege, maporomoko ya maji, tufani, ukame, na kadhalika. Hadithi, nyimbo, na semi hizo zimeelezea pia mahusiano ya binadamu na yote hayo. Kuna pia maombezi na matambiko, na njia zingine za kumsaidia binadamu kukabiliana na mazingira na hali mbali mbali za maisha.Mwalimu Carlson anaonekana katika picha hapo juu upande wa kulia kabisa, akiwa ameweka mkono kiunoni. Wanafunzi wa shule hii wanajifunza mambo ya msingi yanayohusu mazingira na namna ya kuyahifadhi. Wanapata fursa ya kutembelea nchi za nje pia, kujifunza.
Katika kutembelea kwangu shule hii nimeona jinsi wanafunzi walivyo makini na wenye duku duku ya kujua mambo. Ni wanafunzi hodari kabisa. Kila ziara imekuwa ya kuridhisha sana. Taarifa na picha hizi zinatokana na ziara yangu ya tarehe 10 Novemba, 2009.

Sunday, November 8, 2009

Watanzania jitokezeni kwenye mijadala ya elimu

Habari hii imechapishwa katika gazeti la Habari Leo

Imeandikwa na Na Simon Nyalobi; Tarehe: 7th November 2009

WATANZANIA wametakiwa kujenga tabia ya kuandika machapisho ya utafiti wao na kujitokeza katika mijadala ya kimataifa kuhusu elimu badala ya kuogopa na kukaa pembeni.

Mwito huo ulitolewa jana Dar es Salaam na Ofisa Mipango ya Elimu wa Shirika la Oxfam tawi la Tanzania, Mary Soko wakati wa akifunga warsha ya siku tatu ya Jumuiya ya Utendaji wa Elimu nchini iliyokuwa na washiriki 40 kutoka maeneo mbalimbali nchini.

Soko alisema kuwa Wataznania wengi hawajitokezi katika makongamano ya kimataifa kuonesha utafiti wao ikilinganishwa na mataifa mengine hususani Nigeria ambayo raia wake hujitokeza kila kongamano la usomaji wa vitabu linapotokea.

Alisema kuwa hata makongamano yanayofanyika hapa nchini, hayana muamko kwa kuwa watanzania wengi wamekuwa nyuma kushiriki. Kutokana na hali hiyo, amewataka sasa kujitokeza kila yanapotokea makongamano ya usomaji wa vitabu ili kuiweka nchi katika ramani ya wasomi kwani uwezo wa kufanya hivyo wanao.

Hata hivyo aliasa tabia ya kusoma iboreshwe katika jamii hususani wadau wa elimu, ili waongeze maarifa ya kuandika utafiti wao kwa usahihi.

Pia aliwataka walimu kuacha kulala na badala yake waihamasishe serikali kuhusu mustakabali wa elimu ili kudumisha kiwango cha elimu nchini kwani wakishindwa wao taifa nalo litashindwa.

Katika hatua nyingine alilitaka Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA), Taasisi ya Ukuzaji wa Mitaala na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kushirikiana kwa pamoja ili kuboresha kiwango cha elimu nchini.

Vitabu Bila Karatasi

Kitu kimoja ambacho kinampambanua mwanadamu na viumbe wengine ni tekinolojia. Chimbuko la binadamu lilifungamana na uwezo wake wa kutengeneza na kutumia zana mbali mbali, kuanzia zana za miti na mawe, hadi chuma na leo zana zinazoendeshwa na umeme au nguvu za nyuklia. Katika maendeleo haya ya tekinolojia, binadamu amegundua na kuweza kutumia nishati mbali mbali, kama vile maji, upepo na jua.

Uandishi na uchapishaji vimefungamana na maendeleo ya tekinolojia. Tangu binadamu wa kwanza alivyoandika michoro kwenye miamba au kuta za mapango, kwenye ngozi za wanyama, vibao vya udongo, au karatasi, yote hayo ni matunda ya tekinolojia. Leo kuna mashine na mitambo ya aina aina ya kuchapisha magazeti na vitabu.

Maendeleo ya tekinolojia ya uchapishaji yametufikisha mahali ambapo uchapishaji sasa unaweza kufanyika bila karatasi. Vitabu vinaandikwa na kusomwa bila kutumia karatasi, bali kwa mtindo wa digitali. Kwa mtindo huu wa digitali, mtu anaandika kitabu chake kwa kutumia kompyuta, na anakihifadhi mtandaoni. Mwenye kutaka kukisoma kitabu hiki anatumia kifaa maalum kiitwacho "e-reader" au "e-book reader." Kuna vifaa vingine pia. Mtu huyu anaingiza kitabu kutoka mtandaoni katika kifaa chake na kukisoma kwenye skrini ya kifaa hicho. Anaweza kuhifadhi vitabu vingi katika kifaa hicho.

Hatua hii ni muhimu, kwani kati ya faida zake nyingi ni kuwa inachangia kuhifadhi miti na misitu ambayo ilikuwa inaharibiwa ili kutengeneza karatasi. Tekinolojia hii ya digitali ni baraka kwa waandishi na wasomaji. Waandishi hawalazimiki tena kuwategemea wachapishaji. Wasomaji hawalazimiki kwenda kwenye duka la vitabu, au kuagiza kitabu na kukingoja kisafirishwe. Wanakipata papo kwa papo mtandaoni. Baadhi ya vitabu vangu, sasa vinapatikana kwa mtindo huo, kama inavyoonekana hapo upande wa kulia.

Saturday, November 7, 2009

Tutajengaje Utamaduni wa Kusoma Vitabu?

Leo asubuhi nilienda kwenye mji wa Brooklyn Park, Minnesota, kuhudhuria kikao cha kamati inayojishughulisha na masuala ya kujenga na kuboresha mahusiano baina ya waAfrika na waMarekani Weusi. Baada ya kikao, wakati narudi kwenye mji ninapoishi, nilipita kwenye mji wa Apple Valley, nikaingia katika duka la vitabu la Half Price Books. Ni duka ambalo nimelitembelea mara nyingi. Half Price Books ni mtandao mkubwa wa maduka ya vitabu hapa Marekani, ambao una maduka katika miji mingi kama inavyoonekana hapa.

Kama kawaida, ninapoingia katika maduka ya vitabu hapa Marekani, nawakuta watu wa kila aina wakizungukazunguka kutafuta vitabu, wakivisoma, na wakivinunua. Kuna maduka mengi ya vitabu hapa Marekani ambamo watu wanaleta vitabu vyao kuviuza, na wengine wanakuja kununua. Unaweza kuja kuuza vitabu vyako na kununua vitabu vingine. Nimewahi kufanya hivyo. Maduka ya Half Price Books yanafuata mtindo huo. Kwa hivi, daima utawaona watu wakija na mifuko au makasha ya vitabu vya kuuza, wakati huo huo unawaona watu wakinunua vitabu.

Leo, kama ilivyo kila ninavyoingia katika maduka haya, niliona jinsi Wamarekani wanavyojali utamaduni wa kusoma vitabu. Niliwaona wazee, watu wazima, wake kwa waume, vijana, na watoto. Niliwaona wazazi wakiwa na wamekuja na watoto wao. Niliwasikia wakiongea na watoto kuhusu vitabu, wakiwasomea watoto vitabu, wakijibu masuali ya watoto, na kadhalika.

Nilijisikia vibaya kukumbuka hali ilivyo nchini mwetu Tanzania. Leo ni Jumamosi. Je, ni mzazi gani Mtanzania ambaye siku kama ya leo anaenda kwenye duka la vitabu? Ni mzazi gani ambaye anampeleka mtoto wake kwenye duka la vitabu?

Sasa, kama watoto wa wenzetu wanalelewa hivyo, je, tunaweza kutegemea kuwa Taifa letu litaweza kushindana na hao wenzetu katika ulimwengu huu wa leo na wa kesho ambao unategemea elimu na maarifa? Ni lini na vipi waTanzania tutajenga utamaduni wa kusoma vitabu? Hatima ya Taifa letu itakuwaje?

Tuesday, November 3, 2009

Kijitabu Kuhusu "Things Fall Apart"

Riwaya ya Chinua Achebe, Things Fall Apart, inafahamika duniani kote. Inatumika sana mashuleni. Mimi kama mwalimu wa fasihi nimefundisha riwaya hii kwa miaka mingi, hadi nikaandika mwongozo kwa wasomaji, wanafunzi, na walimu. Mwongozo huu ni kijitabu ambacho kinapatikana mtandaoni. Bofya hapa.

Lakini, kama watu wasemavyo, tunakwenda na wakati. Tarehe 1 Novemba, 2009 nimekichapisha kijitabu hiki kama "e-book." Yeyote mwenye kifaa kiitwacho "e-reader," au "e-book reader," anaweza kukiingiza katika kifaa hicho, akakisoma. Bofya hapa.