Tuesday, November 24, 2009

Utamaduni na Utandawazi

Makala hii ilichapishwa katika KWANZA JAMII.

Profesa Joseph L. Mbele

Tangu mwaka jana, nimekuwa naendesha warsha hapa Tanzania kuhusu utamaduni na utandawazi. Mwaka jana nilifanya hivyo Arusha, na mwaka huu nimeendesha warsha Tanga na Dar es Salaam. Warsha hizi zimehudhuriwa na watu kutoka Tanzania, Kenya, Cameroon, Uingereza, Sweden, na Marekani. Hao wa nchi za nje ni watu waliokuwepo Tanzania kwa shughuli mbali mbali.

Niliamua kuanza kuendesha warsha hizi hapa Tanzania kutokana na kutambua kuwa ni muhimu katika dunia ya leo inayozidi kuwa kijiji. Watu wa tamaduni mbali mbali wanazidi kukutana kwa sababu mbali mbali, kama vile biashara, masomo, utalii, na uwekezaji. Watu wa tamaduni mbali mbali wanajikuta wakifanya kazi pamoja viwandani, maofisini, na kadhalika. Wanafunzi, watafiti, na walimu, wanajikuta wakishughulika na watu wa tamaduni mbali mbali.

Hali hii inaweza kusababisha migogoro ya aina aina, kwani kila mtu ana namna yake ya kuongea, kufikiri, kufanya mambo, ambayo inatokana na utamaduni wake. Bila kuelewa utamaduni wa wengine, matatizo lazima yatatokea, kama vile kutoelewana na kugombana.

Kwa miaka mingi katika kufundisha Marekani, nimehusika pia katika kutoa ushauri kwa waMarekani kuhusu utamaduni wa waAfrika. Wamarekani hao ni wale wanaokuja Afrika, iwe ni kwa masomo, utalii, shughuli za kidini, au za kujitolea. Nimehusika pia katika kutoa ushauri kwa waAfrika waishio Marekani, kuwasaidia kuulewa utamaduni wa Mmarekani.

Uzoefu huu umenifungua macho kuhusu umuhimu wa suala hili la kuelewa tamaduni mbali mbali, hasa kwa kuwa dunia inabadilika na kuwa kijiji. Hatutaweza kukwepa maingiliano baina ya tamaduni mbali mbali. Wafanya biashara watahitaji kutafuta masoko katika nchi za mbali, au watahitaji kutafuta washiriki kutoka nchi za mbali, au watahitaji kutafuta malighafi kutoka nchi za mbali. Makampuni yatahitaji kuwaajiri watu kufanya shughuli zake sehemu mbali mbali duniani, na katika kufanya hivyo, yatawajibika kuwaajiri watu wa tamaduni mbali mbali.

Kutokana na uzoefu huu nilioupata Marekani, niliona niko tayari kufanya warsha Tanzania. Nilikuwa na hamu ya kukutana na waTanzania na kuona nitafanikiwa vipi kuleta ujumbe wangu.

Jambo la kwanza nililofanya katika warsha hizi ni kuelezea maana ya utamaduni na maana ya utandawazi. Utamaduni, kama nilivyogusia, ni dhana inayojumlisha tabia, mwenendo, hisia na taratibu za maisha. Hata namna ya kuzungumza hutofautisha utamaduni mmoja na mwingine, kiasi kwamba, kwa mfano Mmarekani akisema jambo, linaweza kuonekana kuwa ni maudhi kwa Mwafrika au utovu wa heshima, wakati kwa utamaduni wa Mmarekani, ni usemi wa kawaida au wa heshima. Kadhalika, Mwafrika anaweza kusema jambo ambalo ni la kawaida au la heshima katika utamaduni wake, lakini likawa kero kwa Mmarekani.

Kuhusu utandawazi, dhana yangu ni kuwa utandawazi haukuanza miaka yetu hii, kama wengi wanavyofikiri. Ni jambo lililoanza zamani sana, tangu enzi za binadamu wa mwanzo kabisa. Utandawazi ulianza pale binadamu waliposambaa kutoka Afrika, ambako ndiko walikoanzia, na kuenea duniani. Kuenea huku kwa binadamu kuliandamana na kuenea kwa ujuzi, maarifa, lugha, na mambo mengine mengi.

Utandawazi ulichukua sura mbali mbali kadiri historia ilivyosonga mbele. Katika enzi zetu, utandawazi umetawaliwa na kuenea kwa ubepari, ambao umeathiri uchumi, siasa, utamaduni, na mambo mengine mengi.

Pamoja na hayo, bado tunazo tofauti za tamaduni ambazo zinaweza kuwa kipingamizi tunapokutana na watu wa nchi mbali mbali. Hapo ndipo ulipo umuhimu wa kujielimisha kuhusu tofauti hizi.

Baada ya kuongelea masuala haya ya jumla na kinadharia katika warsha hizi, niliingia katika kutoa mifano ya matatizo ambazo makampuni yamekumbana nayo wakati wa kujaribu kupeleka shughuli zao katika nchi za mbali, kwenye utamaduni tofauti. Makampuni ya Marekani, kwa mfano, yamewahi kupata matatizo katika nchi za Ulaya na Asia. Hata namna ya kutangaza biashara inaweza kuwa chanzo cha matatizo. Tangazo ambalo linavutia wateja katika utamaduni fulani linaweza kuwa kero kwa watu wa utamaduni tofauti. Hata rangi zinazotumika katika tangazo zinaweza kuwa na maana tofauti au kuleta hisia tofauti katika tamaduni mbali mbali.

Kwa bahati nzuri, washiriki wa warsha hizi wamevutiwa na wamesisitiza kuwa ni muhimu warsha hizi ziendelee siku za usoni, kwenye mashirika, vyuo, na taasisi mbali mbali. Kwa upande wangu, nimefurahi kupata fursa ya kuongea kwa undani na waTanzania ambao tulikuwa hatufahamiani. Nimefurahi kuanza kuamsha fikra za masuala haya muhimu miongoni mwa waTanzania. Nimefurahi kuanza kujenga mtandao wa watu ambao tutaweza kuchangia kwa namna fulani maendeleo katika jamii yetu.

Katika kuthibitisha zaidi hoja hizi, nimekuwa nikiongelea mifano hai ya jinsi utamaduni wa Mmarekani unavyotofautiana na utamaduni wa Mwafrika, kama nilivyojionea mimi mwenyewe katika kuishi kwangu na waMarekani. Katika kufanya hivyo, nimekuwa nikitumia kitabu ambacho nimeandika, na ambacho kinatumika na waMarekani wanaofika Afrika, na pia waAfrika wanaoishi Marekani. Ninaandika muda wote, na hii ni njia ya kuendelea kujifunza mimi mwenyewe na kuendelea kutoa mchango wangu katika masuala haya muhimu.

Kitu kimoja ambacho nimekuwa nikisisitiza ni kuwa hili ni suala la elimu, na elimu haina mwisho. Tunawajibika kuanza kujielimisha na kuendelea hivyo bila kuchoka. Warsha moja au mbili haitoshi, bali ni mwanzo. Ni mwanzo mzuri, na nangojea kuendelea kuendesha warsha hizi siku zijazo.

1 comment:

Yasinta Ngonyani said...

Nimefurahi sana kusoma mada hii. Na hasa jinsi ulivyokuwa na mayo wa kuhamashisha utamaduni wetu na pia utandawazi. Nadhani wengi tunahitaji kufuata nyayo zako Prof. Asante sana maana nimesoma na naimesoma na nimerudia tena safi sana.Upendo daima na tutafika tu.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...