Friday, November 27, 2009

Elimu ya Kijijini

Makala hii ilichapishwa katika gazeti la KWANZA JAMII

Profesa Joseph L. Mbele

Mara kwa mara nakumbuka elimu niliyopata kijijini, kabla ya kuanza shule. Wengi wetu tulipitia njia hiyo. Ni elimu gani hiyo? Tangu utotoni, tulipata maelekezo kutoka kwa wazazi kuhusu mambo mbali mbali, kufuatana na umri, kuanzia namna ya kuvaa hadi namna ya kula kwa adabu na kuwasalimia watu.

Baadaye wavulana tulijifunza kuchunga mbuzi na ng’ombe, na kutandika nyasi kwenye zizi la ng’ommbe, na kukamua maziwa. Wasichana walifundishwa kazi za jikoni na kulea watoto.

Kama ilivyo kwa watoto wengine, baba na mama walikuwa wananituma kufanya shughuli hii au ile. Hata majirani walikuwa wanatutuma sisi watoto kuwasaidia shughuli mbali mbali. Yote hii ilikuwa ni sehemu ya elimu yetu.

Nilipokua kidogo nilianza kushiriki katika kilimo. Nilijifunza kulima, kupanda, kupalilia, na kuvuna mazao. Nilijifunza kuchuma kahawa na kuishughulikia baada ya hapo. Shughuli hizi ziliniwezesha kufahamu zaidi habari za udongo, nyasi, na magugu. Niliwafahamu wadudu wanaoishi mashambani, kama ni wadudu salama kwa mimea au ni adui wa mimea. Nilizijua tabia za wadudu mbali mbali, kuanzia siafu hadi sisimizi na mchwa. Nilijua kama wanauma au hawaumi. Tulijifunza namna ya kuwanasa kumbikumbi, ambao walikuwa ni chakula.

Katika kuchunga mbuzi na ng’ombe tulipata fursa ya kujifunza mambo mengi, sio tu kuhusu tabia za hao wanyama, bali pia elimu ya mimea na nyasi, zikiwemo nyasi ambazo ni chakula cha mbuzi au ngombe na kadhalika. Huko porini tulijifunza pia aina mbali mbali za mboga za porini, matunda, uyoga, na kadhalika. Tuliweza kutofautisha uyoga ambao unalika na binadamu na ule ambao ni sumu.

Katika kukua kwetu kijijini, tulisikiliza hadithi na nyimbo, tukaweza kusimulia hadithi hizi na kuimba nyimbo. Hadithi hizi zilisheheni falsafa, maarifa, na maadili. Tulishiriki katika ngoma, tukaweza kupiga ngoma na ala zingine za muziki, kucheza na kuimba. Mbali ya kwamba hii ilikuwa ni burudani, ilikuwa pia elimu ya sanaa. Ilikuwa ni elimu kuhusu namna ya kushirikiana na wengine, kwani ngoma inahitaji nidhamu na ushirikiano.

Kwa kuwa nilisoma shule ya msingi nikiwa bado naishi kijijijini, niliendelea kuipata elimu ya kijijini hata baada ya kuanza shule. Baada ya masomo shuleni, niliporudi nyumbani, niliendelea na shughuli ya kuchunga mbuzi na ng’ombe, na kusaidia shughuli mbali mbali za nyumbani ambazo ziliendelea kuimarisha elimu yangu ya kijijini.

Baada ya kumaliza darasa la nne, mambo yalibadilika sana. Nilikwenda shule ya bweni, mbali kabisa na nyumbani kwangu. Elimu niliyoipata kule ilikuwa ya vitabuni zaidi. Ingawa tulifanya pia shughuli za nje, kama vile shambani na bustanini, muda mwingi zaidi tulitumia katika kujifunza yaliyomo vitabuni. Elimu ya vitabuni ilishamiri kichwani mwangu nilivyozidi kuendelea na madarasa, hadi chuo kikuu Dar es Salaam, na hatimaye Marekani.

Kadiri nilivyoendelea na elimu ya shuleni, nilizidi kusahau elimu ya kijijini. Kusoma sana kuliendana na kufifia kwa elimu niliyoipata kijijini. Leo hii, sikumbuki majina ya mimea mingi, wala ya aina nyingi za majani niliyojifunza kijijini. Nimesahau majina na tabia za wadudu, wanyama, na ndege mbali mbali. Sina tena ufahamu mzuri wa miti na majani ambayo ni dawa, miti ambayo ni bora kwa kuni na ile ambayo si bora, kwa vile labda haishiki moto haraka au inatoa moshi mwingi. Hii ni hasara kubwa.

Elimu ya kijijini ni elimu thabiti. Ni elimu ambayo imekusanya ujuzi na maarifa kutoka enzi za zamani. Vizazi kwa vizazi vimechuja na kuhifadhi yale yaliyo muhimu tu. Kila kinachofundishwa kina maana katika maisha. Ndio elimu ya kijijini.

Hapakuwa na vitabu wala maktaba. Kila kitu kilihifadhiwa akilini na kurithishwa kutoka kizazi hadi kizazi kwa maneno ya mdomo na kwa vitendo. Elimu ya kijijini haikuwa inakaa maktabani, bali watu walitembea nayo vichwani. Kutokana na ulazima wa kuhifadhi kila kitu katika akili ya binadamu, hapakuwa na nafasi kubwa ya kuhifadhi lolote ambalo halikuwa na maana au umuhimu. Hii ni tofauti na leo, ambapo tunatumia zaidi vitabu. Tunao uwezo wa kuhifadhi vitabu kiasi chochote, hata kama havina maana.

Hakuna ubishi kuwa vitabu vingi ni muhimu, kwani vinabeba elimu ya aina aina. Lakini, kuna pia vitabu ambavyo havina uhusiano na maisha ya wale wanaosoma. Katika shule, kuanzia enzi za ukoloni hadi leo, tunawafundisha vijana mambo mengine ambayo hayana mantiki wala umuhimu katika hali na mahitaji ya jamii zetu. Wakoloni walianzisha mtindo wa kufundisha mambo ya kwao bila kuzingatia umuhimu au uhalali wake katika mazingira ya kwetu. Walizipotosha akili za vijana, na kwa bahati mbaya upotoshaji wa aina mbali mbali bado unaendelea, kama walivyoelezea watalaam kama Franz Fanon na Mwalimu Nyerere. Hii ni tofauti na elimu ya kijijini, ambayo ilienda sambamba na maisha na mahitaji ya wahusika.

Kwa vile elimu ya shuleni inadhihirishwa kwa vyeti, wako ambao wanatafuta njia za mkato, zisizo halali, kupata hivyo vyeti. Wengine wanaiba mitihani. Huu ni udhaifu wa mfumo wa elimu ya shule. Elimu ya kijijini haikuwa na mwanya wa namna hiyo. Hapakuwa na njia za mkato. Hapakuwa na mitihani ya kuiba. Kama ilikuwa ni kwenda kwenye unyago na jando, kila mhusika alitimiza yaliyohitajika.

Tujiulize suali moja: Je, kuna sababu yoyote ya kuendelea kuisahau au kuififisha elimu ya kijijini kwa vile tu mtu anaendelea na elimu ya shuleni? Je, haingekuwa bora kuiingiza elimu ya kijijini mashuleni ili kuhifadhi na kudumisha hazina hii ya urithi wetu?

8 comments:

Albert Kissima said...

Elimu ya darasani imeshawaathiri vijana kweli kweli. Ugusia tu swala la kufanya kazi za nje, wanafunzi wanaona kama vile wako jela.
Kazi za nje ya masomo ya vitabuni yanaonekana kuwapotezea muda wanafunzi kwa kigezo cha kuwa wanakazi kubwa moja tu, ya kukiremba cheti ili wasipate shida kwenye "kuajiriwa". Sijui itakuwaje kwa wanafunzi wa vyuo kwa mfano waambiwe kuwa watatakiwa kupanda maua ktk maeneo ya chuo, kufanya usafi,kwenda shambani,n.k. Mbaya zaidi kuna shule za sekondary hususani za binafsi, watoto hawajishughulishi kabisa na kazi za nje, hawadeki, yani kazi yao ni kushangaa vitabu tu. Sijui vijana hawa wataijenga jamii gani hapo badae.

Mbele said...

Ndugu Kissima, umenipa changamoto ya kuongezea jambo moja.

Hapa Marekani, wanamtegemea mwanafunzi awe makini sio tu kwa masomo ya darasani, yaani vitabuni, bali pia kwa shughuli za nje, kama vile shughuli za kujitolea. Mwanafunzi anayefanya vizuri darasani na halafu yuko mstari wa mbele katika shughuli za nje, kama vile kuwatembelea wazee hospitalini na kuwasaidia, kwenda kusafisha miji iliyokumbwa na mafuriko, na kadhalika, huyu ndiye wanamwona mwanafunzi bora.

Watoto wa kiMarekani wanajengewa tabia hiyo na wanategemewa kuwa nayo maisha yote. Ndio maana utaona waMarekani wana mashirika mengi ya kujitolea, na wengi utawaona wanakuja kujitolea hata huko vijijini kwetu. Mashirika yao yaliyopo Tanzania ni mengi, kama vile "Peace Corps," "Global Service Corps," na "Cross Cultural Solutions."

Sisi wenyewe waTanzania utakuta tumekaa baa tunapiga ulabu hata kama hapo pembeni kuna shule ambayo kuta zake zimebomoka. Hatuwazii kupunguza ulabu tununue sementi ya kukarabatia ule ukuta. Kazi yetu ni kuilaani serikali huku tunaendelea na ulabu.

Watanzania ukisikia tunafanya shughuli za kujitolea, ni shughuli kama za vikao vya arusi. Hapo kweli tuko mstari wa mbele.

Rais Kennedy wa Marekani aliwaambia waMarekani "Usijiulize ni nini nchi yako inakufanyia wewe, bali uliza ni nini wewe unaifanyia nchi yako." Usemi huu unawasilisha vizuri mtazamo wa jamii ya kiMarekani, tofauti na wanaBongo ambao tunakaa vijiweni na kulaani serikali.

Mwalimu Nyerere alipoongelea mapinduzi katika elimu, aliingiza pia hii dhana ya umuhimu wa elimu ya darasani kuunganishwa na shughuli za nje. Lakini, kama unavyosema ndugu Kissima, wazo hilo tumelitupilia mbali.

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...

niliipenda hii makala na nikiwa kijijini huwa nakumbuka mengi pia. moja wapo ya mbinu za utandawazi ni kuhujumu utamaduni mzuri na wakipekee wa waafrika. kwa kweli elimu zetu zilikuwa ni za aina yake na mifumo ya maisha ilikuwa mizuri sana.

Unknown said...

Mbele kusema kuwa elimu ya marekani inawatayarisha wanafunzi wa jamii hiyo kujitolea si sahihi. Mimi nadhani watoto wa baadhi ya watu fulani hapo ni sawa kabisa na wale wa Tanzania ambao ndugu Kissima anawazungumzia. Naam kuna baadhi ya wale wanaofanya hivyo kama vile ilivyo Tanzania.

Mbele said...

Ndugu Hassan, ingetusaidia iwapo ungeeleza uzoefu wako wa elimu ya Marekani. Mimi uzoefu wangu wa elimu ya Marekani ni wa miaka yapata 25, nikijumlisha miaka niliyosoma huku zamani, na miaka niliyofundisha.

Unasema ninayosema si kweli, na badala ya kutueleza uzoefu wako, unaongelea unavyodhani. Bora utueleze unachojua.

Emmanuel Msangi said...

Kongole sana Prof.
Mwakyembe nduguyo katuvumbulia dhahabu

John Paul said...

Naamini mataifa Tajiri wametunza Elimu zao za Vijijini na kuzirithisha na wanaendelea hadi sasa,lakini wakiwa wameongezea Maarifa ya kisasa.

Ndiyo maana tunaweza kuona Wachina, Wajapan na mataifa mengine yaliyoendelea pasipo kuhusika katika Ukoloni, wakiendelea kuwa na vyakula vyao vya asili; Dawa zao za mitishamba zikiwa zimeboreshwa, Mavazi yao ya asili na mbinu nyingi mbali mbali ambazo huwezi kuzipata katika Vitabu vya Elimu iliyoletwa na mfumo wa Ukoloni hususan barani Afrika.

Profesa Joseph Mbele, naamini kwa ngazi yako ya Elimu na Ufahamu inatosha kutoa mwelekezo wa namna gani Elimu hii irudishwe na muongozo huo ukasikilozwa na wahusika.

Tumaini Geofrey Temu said...

Elimu ya kutawaliwa na mbinu za wakoloni wetu

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...