Katika Blogu, Sijui Ninamwandikia Nani Zaidi Yangu Mwenyewe
Je, mwandishi wa blogu anamwandikia nani? Kwa mtazamo wangu, hili ni suali gumu. Naliona gumu kulitafakari, achilia mbali kulijibu. Baada ya kuona ugumu wa suali hili, nimeamua kukiri kuwa ninajiandikia mwenyewe. Ndio maana makala ninazoandika aghalabu zinanihusu mimi mwenyewe, shughuli zangu, matatizo na mafanikio yangu, mategemeo yangu na kumbukumbu zangu. Sipendi sana kuwaongelea watu wengine, wala sipendi sana kuongelea mambo kinadharia, bila kujihusisha mwenyewe. Naweza kusema kuwa ndivyo nilivyoandika kitabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences . Sijajificha nyuma ya pazia la nadharia au taaluma. Nimejiweka wazi kwa namna nilivyoweza. Mwandishi Ernest Hemingway aliongelea suala hili vizuri alipofafanua dhana ya ukweli katika uandishi. Nilivyomwelewa, anasema kuwa ukweli katika uandishi ni kwa mwandishi kuifungua na kuiweka bayana nafsi yake. Ningependa sana niweze kuandika namna hii aliyoongelea Hemingway. Ni ndoto inayovutia, sawa na nyota inayong