Tuesday, January 6, 2015

Mazungumzo ya Jana na Wanachuo wa Gustavus Adolphus Yalifana

Jana niliandika taarifa fupi kuhusu mazungumzo yangu na wanachuo wa chuo cha Gustavus Adolphus. Ningeweza kuandika kirefu na kuelezea, kwa mfano, masuali niliyulizwa kuhusu yaliyomo na yasiyokuwemo katika kitabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences. Ningeweza kuelezea jinsi wanachuo na wakufunzi wao walivyoyapenda mazungumzo yale, kama walivyoniambia wao wenyewe.

Lakini niliona ni bora ningoje watakavyoandika kuhusu mazungumzo yale, wakiwa peke yao bila mimi. Nimeona leo kuwa tayari mmoja wa wanachuo ameshaandika kwenye tovuti ya chuo chao.

Sishangai kusikia kauli kama ya mwanafunzi huyu, kwani ninapoalikwa popote kutoa mhadhara, ninalichukulia jukumu langu kwa umakini. Ni namna yangu ya kuwaheshimu wanaonialika na wale watakaohudhuria. Ni kudhihirisha jinsi ninavyoiheshimu taaluma na jinsi ninavyojiheshimu mwenyewe kama mwanataaluma.

Kwa jinsi ninavyowafahamu wanafunzi wa Marekani, kuna uwezekano mkubwa kuwa wengine wataandika pia, na nikiona taarifa zao, nitaziweka katika hii blogu yangu.

No comments: