Friday, January 23, 2015

Kwa Anayewazia Kuchapisha Kitabu

Wazo la kuchapisha kitabu linawavutia watu wengi. Ni wazo lenye ndoto za mafanikio.Wako wanaoamini kuwa kuchapisha kitabu kutawapa umaarufu. Kuna wanaoamini kuwa kuchapisha kitabu kutawaletea fedha nyingi. Wengi, labda wote, wanaamini kuwa wakisha chapisha kitabu, kazi yao inakuwa imemalizika; kinachobaki ni kungojea matokeo, kama vile umaarufu na fedha.

Ni bora mtu anayewazia kuchapisha kitabu ajielimishe zaidi kuhusu jambo hili, nami hupenda kuchangia yale ninayoyafahamu, kwa kadiri ya uwezo wangu. Vipengele ni vingi, lakini hapa nitaongelea vichache tu.

Mtu uandike kitabu kutokana na kujua kuwa una jambo la kusema kimaandishi. Uwe una jambo ambalo linakuelemea akilini mwako na kukusukuma uandike. Msukumo utoke ndani ya nafsi yako. Ukishaandika kitabu kwa msingi huo, utajisikia una raha sawa na mtu aliyetua mzigo. Kuridhika kwako ndilo jambo mihimu. Mengine yanafuata baadaye.

Huenda kitabu chako kitawavutia watu wakakinunua na kukisoma, au huenda kisiwavutie. Lakini sidhani kama hili ni tatizo lako, maadam umeshakidhi haja ya kutua mzigo uliokuwemo akilini mwako, na sasa uko huru kuwazia mambo mengine. Uhuru huu ni jambo muhimu.

Katika miaka yangu ya kuandika, na hata kuchapisha vitabu, nimekuwa nikisoma kuhusu uandishi, uchapishaji na uuzaji wa vitabu. Kitu kimoja mihimu nilichojifunza ni kuwa kuandika na kuchapisha kitabu sio mwisho wa kazi yako kama mwandishi. Kuna kazi kubwa mbele yako, kazi ya kuutangazia ulimwengu kuhusu kuwepo kwa kitabu chako, na kazi ya kukiuza kitabu chako.

Watafiti na waandishi wa masuala hayo wanasisitiza kuwa wajibu wa kuuza kitabu ni yako wewe mwandishi. Kabla ya kuanza kusoma mawazo haya, niliamini, kama wengi wanavyoamini, kwamba kazi ya kutangaza na kuuza kitabu ni ya mchapishaji. Kumbe, hata kama mchapishaji anaweza kuchangia katika jukumu hilo, mwandishi unawajibika sana, na pengine zaidi kuliko mchapishaji.

Kwa upande wa Tanzania, kwa hali ilivyo, tatizo kubwa ni kwamba utamaduni wa kununua na kusoma vitabu ni hafifu sana. Watu wengi wanadhani kusoma vitabu ni shughuli ya wanafunzi, na hivi vitabu viwe vimo katika mitaala ya shule.

Kujisomea vitabu bila shinikizo la shule au mitihani ni utamaduni ambao unakosekana. Hii ni sababu moja inayonifanya nitoe angalizo kuwa mtu unaweza kuchapisha kitabu na kisiwe na wasomaji.

Masuala haya ya uandishi na uuzaji wa vitabu nimeyaelezea katika kitabu changu cha CHANGAMOTO: Insha za Jamii, na katika makala mbali mbali katika blogu hii. Ninaendelea kujielimisha kuhusu masuala hayo, na nitaendelea kuandika.

2 comments:

Rasto Liosi wa Nairobi Kenya said...

Ni jambo la kuvunja moyo kubaini kuwa uchapishaji wa vitabu ni mithili ya ndoto kwa waandishi wengi.Je umuhimu wa somo hili utakuwa nini iwapo hali hii itaendelea hivyo?

Mbele said...

Ndugu Rasto Liosi

Nashukuru umepita hapa kwangu na kuweka ujumbe. Makala hii isikuvunje moyo. Nimeandika makala zingine kabla kuhusu uchapishaji wa vitabu mtandaoni, ambao ni rahisi na ni fursa kwa yeyote kujichapishia vitabu, hata bila gharama. Makala mojawapo ni hii hapa.