Nimeshaalikwa mara kadhaa miaka iliyopita, kuongea na wanachuo wa Gustavus Adolphus, katika maandalizi ya kwenda Tanzania, kama nilivyoelezea katika blogu hii.
Nilikuwa nimeamua kuwa leo, baada kutoa utangulizi mfupi, nitumie muda karibu wote katika kujibu masuali ya hao wanachuo, kwani nilishafahamishwa kuwa watakuwa wamekisoma kitabu changu. Ilidhihirika wazi, kutokana na masuali yao, kuwa walikuwa wamekisoma kwa makini. Wote tuliyafurahia mazungumzo yetu, ambayo yalidumu kuanzia saa nne hadi saa sita. Baada ya hapo, tulikula chakula cha mchana, ambapo niliendelea na maongezi na Profesa Zust na mshiriki wake Mchungaji Todd Mattson, na wanachuo ambao tulikaa meza moja.
Katika picha ya mwanzo hapa juu, ninaonekana hapo mbele. Kule nyuma kabisa, upande wa kulia mwishoni, anaonekana Mchungaji Mattson, mwenye ndevu nyeupe, na mbele yake ni Profesa Zust. Pichani hapa kushoto, naonekana nikisaini kitabu cha mwanafunzi mojawapo.
No comments:
Post a Comment