Saturday, January 24, 2015

Wanachuo wa Gustavus Adolphus Wako Tanzania

Wanachuo wa chuo cha Gustavus Adolphus, ambao niliongea nao kabla ya safari yao, walifika salama Tanzania. Wako Tanzania kwa ziara ya kimasomo kwa mwezi moja. Wamekuwa wakiandika kuhusu ziara yao katika tovuti ya chuo chao.

Walitua uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kilimanjaro wakatembelea sehemu kama hospitali ya KCMC na shule ya wasichana ya Maasae. Kisha walienda Iringa, ambako wameshatembelea sehemu kama vile Chuo Kikuu cha Iringa, soko kuu, na hospitali ya Ilula. Wamesafiri hadi Tungamalenga, pembeni mwa hifadhi ya Ruaha, ambapo wamepata fursa ya kutembelea hospitali na kuangalia utendaji kazi wake.

Kwa ujumla, wanachuo hao, kama ilivyo kwa wa-Marekani wengine wanaotembelea Tanzania, wanaifurahia nchi yetu na watu wake. Wanawasiliana na familia zao na marafiki huku Marekani, na kwa namna hii jina la Tanzania linasambaa kwa namna nzuri. Kwa kawaida, ziara za wanafunzi nazienzi kuliko zile za watalii. Kwa vile wanafunzi wanajumuika na wananchi katika mazingira mbali mbali, wanaondoka wakiwa na ufahamu fulani wa jamii yetu kuliko watalii, ambao wanakaa nchini mwetu siku chache tu, wakikimbizwa kutoka kivutio kimoja hadi kingine, hasa Mlima Kilimanjaro, mbuga za wanyama, na fukwe za bahari.

Kwangu ni heshima na furaha kuweza kuchangia maandalizi ya vijana hao, kama ninavyofanya mwaka hadi mwaka, kupunguza matatizo yanayoweza kutokea sababu ya tofauti za tamaduni. Haiwezekani mgeni aelewe kila anachoshudia katika utamaduni usio wake. Hata mimi ilinichukua miaka mingi hadi kuanza kuelewa misingi muhimu ya utamaduni wa Marekani, kama nilivyoelezea katika kitabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, na bado ninajifunza. Ndio maana, wanafunzi wanaporejea tena nchini kwao Marekani, tunajitahidi kuongea nao kuhusu yale waliyoyashuhudia kwenye nchi waliyoitembelea, ili wawe na ufahamu zaidi.

No comments: