Showing posts with label Tungamalenga. Show all posts
Showing posts with label Tungamalenga. Show all posts

Saturday, January 24, 2015

Wanachuo wa Gustavus Adolphus Wako Tanzania

Wanachuo wa chuo cha Gustavus Adolphus, ambao niliongea nao kabla ya safari yao, walifika salama Tanzania. Wako Tanzania kwa ziara ya kimasomo kwa mwezi moja. Wamekuwa wakiandika kuhusu ziara yao katika tovuti ya chuo chao.

Walitua uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kilimanjaro wakatembelea sehemu kama hospitali ya KCMC na shule ya wasichana ya Maasae. Kisha walienda Iringa, ambako wameshatembelea sehemu kama vile Chuo Kikuu cha Iringa, soko kuu, na hospitali ya Ilula. Wamesafiri hadi Tungamalenga, pembeni mwa hifadhi ya Ruaha, ambapo wamepata fursa ya kutembelea hospitali na kuangalia utendaji kazi wake.

Kwa ujumla, wanachuo hao, kama ilivyo kwa wa-Marekani wengine wanaotembelea Tanzania, wanaifurahia nchi yetu na watu wake. Wanawasiliana na familia zao na marafiki huku Marekani, na kwa namna hii jina la Tanzania linasambaa kwa namna nzuri. Kwa kawaida, ziara za wanafunzi nazienzi kuliko zile za watalii. Kwa vile wanafunzi wanajumuika na wananchi katika mazingira mbali mbali, wanaondoka wakiwa na ufahamu fulani wa jamii yetu kuliko watalii, ambao wanakaa nchini mwetu siku chache tu, wakikimbizwa kutoka kivutio kimoja hadi kingine, hasa Mlima Kilimanjaro, mbuga za wanyama, na fukwe za bahari.

Kwangu ni heshima na furaha kuweza kuchangia maandalizi ya vijana hao, kama ninavyofanya mwaka hadi mwaka, kupunguza matatizo yanayoweza kutokea sababu ya tofauti za tamaduni. Haiwezekani mgeni aelewe kila anachoshudia katika utamaduni usio wake. Hata mimi ilinichukua miaka mingi hadi kuanza kuelewa misingi muhimu ya utamaduni wa Marekani, kama nilivyoelezea katika kitabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, na bado ninajifunza. Ndio maana, wanafunzi wanaporejea tena nchini kwao Marekani, tunajitahidi kuongea nao kuhusu yale waliyoyashuhudia kwenye nchi waliyoitembelea, ili wawe na ufahamu zaidi.

Tuesday, October 29, 2013

Nimepata Wageni Leo

Leo nimepata bahati ya kutembelewa na wageni wawili. Mmoja ni Mchungaji John Mhekwa kutoka Tungamalenga, Iringa. Mwingine ni Profesa Paula Swiggum wa chuo cha Gustavus Adolphus, St. Peter, Minnesota.

Mchungaji Mhekwa hatukuwa tunafahamiana, lakini Profesa Swiggum tumefahamiana kwa miaka kadhaa, kwani katika programu yake ya kupeleka wanafunzi Tanzania, alinialika kuongea nao kuhusu masuala ya tofauti za tamaduni, kama maandalizi ya safari.

Wanafunzi walikuwa wanasoma kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences. Huo ulikuwa ni uamuzi wake. Mazungumzo yangu na hao wanafunzi yalihusu mambo niliyoandika katika kitabu hiki. Baada ya Profesa Swiggum kustaafu, profesa aliyemrithi, katika kuendesha programu hiyo, Barbara Zust, aliendelea na utaratibu huo.

Kifupi ni kwamba Profesa Swiggum tumeanza zamani kiasi kushirikiana katika nyanja hizo. Leo ilikuwa fursa ya pekee ya kufahamiana na huyu mgeni mwingine, Mchungaji Mhekwa. Nimemwambia kuwa Tungamalenga nilipita, mwezi Agosti mwaka 2011, nikiwa na wanafunzi tukiwa tunaelekea hifadhi ya Ruaha.

Monday, November 19, 2012

Kwa wa-Luteri wa Tungamalenga, Iringa

Makanisa mengi ya ki-Luteri Marekani, ELCA, yana ushirikiano na makanisa ya ki-Luteri ya Tanzania na nchi zingine. Kanisa la Shepherd of the Valley, ambalo liko hapa Minnesota, lina uhusiano na kanisa la Tungamalenga, mkoani Iringa. Kwa taarifa zaidi, soma hapa.

Nimewahi kutembelea Shepherd of the Valley kuongea na wanafunzi wa Chuo cha Gustavus Adolphus ambao walikuwa hapo kufanya maandalizi ya safari ya Tanzania, kama nilivyoelezea hapa.

Kwa miaka mingi kiasi nilifahamu kuhusu uhusiano baina ya Shepherd of the Valley na Tungamalenga.  Kila ninapoliwazia kanisa la Shepherd of the Valley, au ninapoliona, naiwazia Tungamalenga, ingawa mimi si m-Luteri. Kwa vile liko pembeni mwa barabara, ninaliona kanisa hilo kila ninapoenda kutoa mihadhara katika Chuo cha Mazingira.

Sikuwahi kufika Tungamalenga, hadi mwaka jana, niliposafiri na wanafunzi wa ki-Marekani kutoka Iringa kwenda hifadhi ya Ruaha. Ghafla tulipita sehemu iitwayo Tungamalenga. Nilishtuka, kwa sababu sikuwa hata najua kama Tungamalenga iko katika njia hiyo, karibu kabisa na hifadhi ya Ruaha.

Picha inayoonekana hapa juu nilipiga tarehe 13 Novemba, nilipokuwa narudi kutoka kwenye Chuo cha Mazingira. Kwa miaka miwili au zaidi nilitaka niweke picha ya Shepherd of the Valley hapa katika blogu yangu, nikiwawazia wa-Luteri wa Tungamalenga.

Friday, November 11, 2011

Nitakutana na Mteja Maarufu

Mara kwa mara napata fursa ya kukutana na wateja. Hao ni watu waliosoma vitabu vyangu au wanapangia kufanya hivyo au wamehudhuria mihadhara yangu. Wengine, ambao hatupati fursa ya kukutana uso kwa uso, wanawasiliana nami kwa barua pepe. Kwangu ni jambo la kushukuru, kwamba Mungu kanijalia uwezo na fursa hizo.

Siku chache zilizopita, nilipata ujumbe kutoka kwa mama mmoja akisema kuwa alipata taarifa zangu kutoka kwa mama mwingine wa Shepherd of the Valley Lutheran Church. Nilivyoangalia mtandaoni, nimegundua kuwa huyu aliyeniandikia ni mtu maarufu.

Wakati anaulizia kama tungeweza kukutana, alisema kuwa amenunua kitabu changu cha Africans and Americans na atakisoma hima. Anapangia kuandika kitabu kingine, na anapenda kusikia mawaidha yangu kuhusu masuala ya utamaduni katika malezi ya watoto.

Huyu namhesabu kama mteja maarufu, kwa vile anafahamika sana kutokana na shughuli zake za kuandika na kuelimisha umma. Nangojea siku tuliyopanga kukutana, wiki ijayo, nikizingatia kuwa mteja ni mfalme.

Nimalizie tu kwa kusema kuwa niliwahi kwenda Shepherd of the Valley kuongelea suala la tofauti za tamadununi. Kanisa hili lina ushirikiano na waumini wa Tungamalenga, Iringa. Nilifanya hiyo shughuli, na sikutegemea kuwa ingezua hayo niliyoeleza hapa juu. Ndivyo mambo yanavyokwenda hapa duniani. Unaweza kufanya jambo, usijue litazua nini, litaishia wapi au vipi.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...