Thursday, October 29, 2015

Shairi la "Kimbunga" (Haji Gora Haji)

Kutafsiri kazi ya fasihi ni kazi ngumu ya kuchemsha bongo. Inahitaji ufahamu wa hali ya juu wa lugha husika, na pia hisia makini za kifasihi. Tofauti na inavyoeleweka katika jamii, kutafsiri ni suala pana kuliko kuwasilisha ujumbe kutoka lugha moja kwenda lugha nyingine, bali ni kutunga upya kazi ya fasihi inayotafsiriwa. Hili suala linajadiliwa sana na wataalam wa lugha, fasihi, na falsafa.

Pamoja na matatizo yote, ninapenda kuchemsha akili yangu kwa kutafsiri kazi za fasihi. Kwa mfano, nimetafsiri hadithi za ki-Matengo, na shairi la Mama Mkatoliki.

Hapa naleta shairi la Haji Gora Haji, mshairi maarufu wa Zanzibar, ambaye niliwahi kukutana naye. Shairi hilo ni "Kimbunga" ambalo limo katika kitabu chake kiitwacho Kimbunga. Jisomee shairi hilo na ujionee nilivyopambana na lugha katika kutafsiri. Ni mapambano, na kuna wakati unajikuta umepigwa butwaa au mwereka.
-----------------------------------------------------------------------------------------------------------------

                               Kimbunga

1.     Kimbunga mji wa Siyu, kilichowahi kufika
       Si kwa yule wala huyu, ilikuwa patashika
       Kimeing'owa mibuyu, minazi kunusurika
       Nyoyo zilifadhaika.

2.     Yalizuka majabali, yakabirukabiruka
       Zikadidimia meli, ngarawa zikaokoka
       Kimbunga hicho kikali, mavumbi hayakuruka
       Nyoyo zilifadhaika.

3.     Nyumba kubwa za ghorofa, siku hiyo zimeruka
       Zikenenda kwa masafa, kufikia kwa kufika
       Vibanda vyao malofa, vyote vikasalimika
       Nyoyo zikafadhaika.

4.     Chura kakausha mto, maji yakamalizika
       Pwani kulikuwa moto, mawimbi yaliyowaka
       Usufi nusu kipeto, rikwama limevunjika
       Nyoyo zikafadhaika.

5.     Kuna kikongwe ajuza, viumbe kimewateka
       Hicho kinamiujiza, kila rangi hugeuka
       Wataokiendekeza, hilaki zitawafika
       Nyoyo zikafadhaika.


                                 A Hurricane

1.     A hurricane once arrived in Siyu town
       Sparing neither that one nor this one, it was sheer mayhem
       It uprooted babobab trees, the coconut trees surviving
       Hearts went panicking.

2.     Big rocks turned up, tumbling over and over
       Ships were sinking, while mere boats survived
       Fearsome as the hurricane was, it raised no dust
       Hearts went panicking

3.     Great storied houses were blown away that day
       They flew quite a distance, landing wherever they landed
       The huts of the lowly, all survived intact
       And hearts went panicking

4.     The frog drained the river, the water all dried up
       On the shore was conflagration, of the waves flaming
       Half a container of kapok, broke the coolie's cart
       And hearts went panicking

5.     A wizened hag there was, who held beings captive
       She is given to magical powers, changing hues at will
       Those who let her be, perdition will be their lot
       And hearts will go panicking.

Wednesday, October 28, 2015

Maprofesa na Wajibu wa Kuandika

Profesa ni mtu aliyefikia kiwango cha juu cha ufanisi katika ufundishaji, utafiti, uandishi, na kutoa ushauri kwa jamii katika masuala mbali mbali yanayohusiana na utaalam wake. Siwezi kuongelea hapa vipengele vyote vya suala hili, kama vile vigezo vinavyotumika katika kupima ufanisi wa mhusika hadi kumfikisha kwenye hadhi ya uprofesa. Ninakumbushia tu suala la wajibu wa profesa wa kuandika.

Baadhi yetu wa-Tanzania tumeliwazia na kuliongelea suala hili kwa miaka mingi, kwa manufaa ya jamii, tukiliunganisha na masuala kama sera ya elimu, matatizo ya uchapishaji, na kukosekana kwa utamaduni wa kununua na kusoma vitabu.

Kilichonifanya nirejeshe mada hii leo ni kwamba nimejikumbusha tamko la Rais Kikwete, "Maprofesa Wananisikitisha," ambalo lilijadiliwa katika blogu yangu hii na blogu ya Profesa Matondo. Mambo yaliyosemwa katika majadiliano yale ni muhimu na yataendelea kuwa muhimu. Wajibu wa profesa wa kuandika, kama njia mojawapo ya kufundisha na kuchangia maendeleo ya taaluma ni jambo lililo wazi.

Hata hivi, kwa kuzingatia kuwa dunia inabadilika muda wote, kuna umuhimu wa kulitafakari suala hili kwa mtazamo unaozingatia mabadiliko haya. Fikra zilizokuwa sahihi miaka michache iliyopita, huenda zimepitwa na wakati. Wataalam katika nyanja mbali mbali, kama vile ujasiriamali, elimu, na biashara wanatufundisha kuwa mabadiliko yanatulazimisha kuwa wabunifu na wepesi wa kubadilisha fikra, mahusiano, mbinu na utendaji wetu. Ndio maana ni muhimu kusoma daima na kujielimisha kwa njia zingine.

Katika dunia ya utandawazi wa leo, ambamo tekinolojia mbali mbali zinastawi, zikiwemo tekinolojia za mawasiliano, tunawajibika kuwa na fikra mpya kuhusu usomaji, uchapishaji na uuzaji wa vitabu, na kadhalika. Shughuli nyingi sasa zinafanyika mtandaoni, ikiwemo ufundishaji, kama nilivyowahi kugusia katika blogu hii. Tunawajibika kufunguka akili na kuacha kujifungia katika hiki tunachokiita sera ya elimu ya Tanzania. Je, inawezekana kuandika kitabu chenye umuhimu kwa Tanzania lakini si kwa ulimwengu? Taaluma inaweza kufungiwa katika mipaka ya nchi? Kuna dhana katika ki-Ingereza tunayopaswa kuitafakari: "The local is global."

Naona ni jambo jema kuirejesha mada hii, tuendelee kuitafakari katika mazingira ya leo. Lakini, naona tusome kwanza mjadala uliofanyika katika blogu hii na blogu ya Profesa Matondo.

Monday, October 26, 2015

Shukrani kwa Wa-Tanzania Wadau wa Kitabu Changu

Blogu yangu ni mahali ninapojiandikia mambo yoyote kwa namna nipendayo. Siwajibiki kwa mtu yeyote, wala sina mgeni rasmi. Leo nimewazia mafanikio ya kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences. Nimejikumbusha kuwa mtu hufanikiwi kwa juhudi zako pekee, hata ungekuwa hodari namna gani. Kuna watu unaopaswa kuwashukuru.

Nami napenda kufanya hivyo, kama ilivyo jadi yangu. Nimewahi kuwaongelea na kuwashukuru wanablogu wa-Tanzania, na nimewahi kuwaongelea na kuwashukuru wa-Kenya. Ninapenda kuendelea kuwakumbuka wa-Tanzania.


Mwanzoni kabisa, nilipokuwa nimeandika mswada wa awali kabisa wa kitabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, rafiki yangu Profesa Joe Lugalla, wa Chuo Kikuu cha New Hampshire, alipata kuusoma, akapendezwa nao.

Yeye, kwa jinsi alivyoupokea mswada ule, alikuwa kati ya watu wa mwanzo kabisa kunitia hamasa ya kuuboresha. Tangu wakati ule hadi leo amekuwa mstari wa mbele kuwahamasisha watu wakisome kitabu hiki. Kwangu hili ni jambo la kushukuru sana, nikizingatia kuwa Profesa Lugalla sio tu ni m-Tanzania mwenzangu anayefahamu ninachosema kitabuni, bali pia yeye ni mtaalam wa kimataifa wa soshiolojia na anthropolojia.


Mtu mwingine aliyenihamasisha tangu miaka ya mwanzo ya kuwepo kwa kitabu changu ni Mhashamu Askofu Owdenburg Mdegella wa dayasisi ya Iringa ya Kanisa la ki-Luteri Tanzania. Nakumbuka tulivyokutana katika eneo la shule ya Peace House, Arusha, na hapo hapo akaanza kuongelea kitabu changu, akisema kuwa ni muhimu wazungu wakisome ili watufahamu sisi wa-Afrika. Siwezi kusahau kauli yake hiyo na namna alivyoongea kwa msisimko. Nilimwelewa vizuri kwa nini aliongea hivyo, kwani yeye anahusika moja kwa moja na mipango ya ushirikiano baina ya wa-Marekani na wa-Tanzania, hasa wa Iringa.


Dada Subi, mwanablogu maarufu miongoni mwa wa-Tanzania, ni mtu mwingine ambaye namkumbuka kwa namna ya pekee, kwa yote aliyofanya katika kunihamasisha na kukipigia debe kitabu changu. Nakumbuka aliwahi kuwasiliana nami juu ya kitabu hiki, lakini cha zaidi ni kuwa alikipigia debe katika blogu yake.

Dada Subi alinisaidia sana katika shughuli zangu za kublogu. Ingawa hatujawahi kuonana, ninamfahamu ni mkarimu sana.
Napenda nichukue fursa hii kumtaja na kumshukuru Bwana Muhiddin Issa Michuzi, mwanablogu maarufu wetu wa-Tanzania. Ingawa tumewahi kukutana mara moja tu, Michuzi amekuwa mstari wa mbele kutangaza shughuli zangu katika blogu yake, ikiwemo kitabu changu. Kutokana na hayo tumekuwa kama watu tuliozoeana. Kwangu hilo ni jambo la kushukuru.

Sitachoka kuwashukuru wachangiaji wa mafanikio yangu. Kama nilivyosema, hakuna mtu anayefanikiwa kwa uwezo wake peke yake. Ule usemi wa ki-Ingereza, "No man is an island," yaani hakuna mtu ambaye ni kisiwa, una ukweli usiopingika.

Kwa wanaotaka, walioko Tanzania, Kitabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences kinapatikana Burunge Visitor Centre, simu 0754 297 504.

Monday, October 19, 2015

Matamasha ya Vitabu: Tanzania na Marekani

Nimehudhuria matamasha ya vitabu Tanzania na Marekani. Kwa usahihi zaidi, niseme nimeshiriki matamasha hayo, kama mwandishi, nikiwa na meza ya vitabu vyangu. Nimeona tofauti baina ya Tanzania na Marekani katika uendeshaji wa matamasha haya. Hapa napenda kugusia kidogo suala hilo, nikizingatia kwamba ni suala linalowahusu waandishi, wasomaji, wachapishaji na wauza vitabu.

Tofauti moja ya wazi ni kuwa matamasha ya vitabu ni mengi zaidi, maradufu, Marekani kuliko Tanzania. Marekani kuna matamasha makubwa ya kitaifa na matamasha makubwa kiasi ya kiwango cha majimbo, na pia matamasha ya kiwango cha miji. Mtu ukitaka, unaweza kuzunguka nchini Marekani ukahudhuria matamasha ya vitabu kila wiki, kila mwezi, mwaka mzima. Angalia, kwa mfano, orodha hii hapa. na hii hapa.

Kwa upande wa Tanzania, hali ni tofauti. Matamasha ya vitabu hayafanyiki mara nyingi. Tunaweza kuwa na tamasha la vitabu la kitaifa mara moja kwa mwaka. Lakini hatuna utamaduni wa kuwa na matamasha ya sehemu mbali mbali za nchi, kwa mfano tamasha la vitabu mikoa ya Kusini, tamasha la vitabu mikoa ya Magharibi, mikoa ya Mashariki, na kadhalika.

Tofauti hizi zinatokana na tofauti za utamaduni wa kusoma vitabu. Utamaduni wa kusoma vitabu umejengeka miongoni mwa watu wa Marekani, tangu utotoni. Watoto, hata wanapokuwa wadogo sana, husomewa vitabu; vijana, watu wazima, na wazee husoma vitabu. Utawakuta katika matamasha ya vitabu, kama ninavyoeleza mara kwa mara katika blogu hii.

Katika matamasha ya vitabu ya Marekani, ni kawaida waandishi kuwepo. Wengine huja kuonesha na kuuza vitabu vyao. Wengine huwa wamealikwa kama wageni rasmi. Waandishi huongelea vitabu vyao. Nilivyoona Tanzania ni kwamba wachapishaji ndio huleta vitabu kwenye matamasha. Mtu ukihudhuria matamasha hayo, ukawa na hamu ya kujua kuhusu vitabu vya mwandishi fulani, utaongea na mchapishaji. Mwandishi humwoni.

Ninaona kuwa hii ni dosari. Ni jambo ambalo tunaloweza kujifunza kutoka kwa wa-Marekani. Kuwepo kwa waandishi ni kivutio kimojawapo katika matamasha ya vitabu. Hapa Marekani, ni kawaida kuona matangazo katika vyombo vya habari, au mabango kwenye meza za waandishi yameandikwa "MEET THE AUTHOR." Ni kivutio. Watu hupenda kuonana na waandishi, kuongea nao, kununua vitabu na kusainiwa, na pia kupiga nao picha.

Utaratibu huu ungeweza kufanyika Tanzania, ungesaidia. Ninafahamu, kwa mfano, kwamba wengi wanalijua jina la Ngoswe. Wamesikia, na wanatumia usemi "Ya Ngoswe mwachie mwenyewe Ngoswe." Lakini hawajui asili ya jina Ngoswe. Kumbe, hili ni jina la tamthilia ya Ngoswe: Penzi Kitovu cha Uzembe iliyotungwa na Edwin Semzaba.

Kutokana na umaarufu wa jina la Ngoswe, kama waandaaji wa tamasha la vitabu wangeweka tangazo kuwa mtunzi wa Ngoswe atakuwepo katika tamasha, naamini itakuwa ni kivutio kwa watu kuhudhuria tamasha. Ninaweza kutoa mifano mingine. Jina kama Kinjeketile ni maarufu. Ebrahim Hussein, mwandishi wa tamthilia ya Kinjeketile akijitokeza katika tamasha la vitabu, atakuwa kivutio. Kadhalika Euphrase Kezilahabi, mwandishi wa riwaya maarufu kama Rosa Mistika na Dunia Uwanja wa Fujo.

Waandishi, wachapishaji, na wadau wengine wa vitabu tunakubaliana kwamba kuna haja kubwa ya kujenga utamaduni wa kusoma vitabu katika nchi yetu ya Tanzania. Hilo wazo langu la kuboresha matamasha ya vitabu huenda likachangia mafanikio ya ndoto yetu.

Saturday, October 17, 2015

Kitabu Kinapouzwa Amazon

Nina jadi ya kuandika kuhusu vitabu katika blogu hii. Ninaandika kuhusu vitabu ninayonunua na ninavyosoma, uandishi, uchapishaji, na uuzaji wa vitabu. Ninaandika ili kujiwekea kumbukumbu na pia kwa ajili ya wengine wanaotaka kujua mambo hayo, iwe ni wasomaji na wadau wa vitabu, waandishi, au wanaotarajia kuwa waandishi. Leo napenda kuongelea kidogo juu ya vitabu vinavyouzwa katika tovuti ya Amazon.

Nimewahi kuandika kuhusu mada hii. Lakini nimeona si vibaya kuirudia, ili kuelezea kama yale niliyoyasema mwanzo yamebaki vile vile au kama kuna lolote jipya. Ninaongea kutokana hali halisi ya vitabu vyangu Amazon.

Kwanza kabisa, mambo ya msingi niliyosema mwanzo yamebaki vile vile. Vitabu vyangu viliingia Amazon bila mimi kuvipeleka kule. Vinauzwa kule kuliko sehemu nilipovichapisha au kwenye duka langu la mtandaoni. Ninajionea mwenyewe kuwa Amazon ni mtawala wa himaya ya uuzaji wa  vitabu mtandaoni.

Kila niendako, kwenye matamasha ya vitabu au katika kukutana na watu popote, likijitokeza suala la upatikanaji wa vitabu vyangu, watu wanaovitaka wanaulizia kama vinapatikana Amazon. Imefikia mahali sasa sioni hata umuhimu wa kuwatajia sehemu nyingine. Amazon imejengeka vichwani mwa watu sawa na nyumba ya ibada ilivyojengeka kichwani mwa muumini wa dini: mu-Islamu na msikiti, au m-Kristu na kanisa.

Mimi mwenyewe sina tofauti na hao watu. Ninapotaka kununua kitabu mtandaoni, ninakwenda moja kwa moja Amazon. Ninavutiwa na urahisi wa kuviagiza na kuletewa, na uhuru wa kuchagua bei unayotaka kulipia, kwani kitabu hicho hicho kinauzwa kwa bei mbali mbali.

Hiyo ndio hali halisi ya ununuaji wangu wa vitabu mtandaoni. Tofauti ni pale ninapotaka kununua vitabu vyangu. Hapo siendi Amazon, bali kwenye duka langu. Ninavipata kwa bei pungufu. Punguzo la bei linaongezeka kufuatana na uwingi wa vitabu ninavyonunua. Ninapenda kununua vingi, kwa sababu ninapenda pia kutoa nakala za bure kwa taasisi, vikundi, au watu binafsi wanaojishughulisha kama mimi mwenyewe katika kujenga mahusiano mema baina ya jamii mbali mbali.

Kama nilivyosema katika ujumbe wangu wa mwanzo na kurudia hapa juu, Amazon inauza vitabu kwa bei pungufu. Kwa upande mmoja, hii ni hasara kwa mwandishi. Ni hali halisi ya mfumo wa biashara, na hakuna sheria inayokiukwa. Kwa upande mwingine, hii ni baraka kwa mteja. Kama methali isemavyo, Kuvuja kwa pakacha, nafuu ya mchukuzi.

Tuesday, October 13, 2015

Michango ya Papa's Shadow Imekamilika

Kwa mwezi mzima kumekuwa na kampeni ya kuchangisha fedha kwa ajili ya filamu ya Papa's Shadow, kama nilivyoelezea katika blogu hii. Leo, shughuli imekamilika, masaa sita kabla ya kipindi cha michango kwisha.

Mafanikio haya yamefungua njia kwa mambo makubwa siku zijazo. Papa's Shadow sasa itapatikana kwa wadau, pindi taratibu za malipo zitakapokamilika. Kwangu ni furaha kubwa, kama mchangiaji mkuu wa filamu hiyo, sambamba na Mzee Patrick Hemingway, wa maelezo na uchambuzi juu ya mwandishi Ernest Hemingway. Ninafurahi pia kwamba filamu hii itaitangaza Tanzania kwa namna ya pekee, kama nilivyoelezea katika blogu hii.

Umaarufu wa Ernest Hemingway ulimwenguni ni wa pekee. Pamoja na kuelezea uhalisi wa maisha ya binadamu, kama walivyofanya waandishi wengine maarufu, pamoja na kuzipa umaarufu kwa maandishi yake sehemu alizotembelea hapa duniani, Hemingway alianzisha jadi mpya kimtindo katika uandishi wa ki-Ingereza. Hilo limesemwa tena na tena na wataalam wa fasihi. Ninaamini kuwa Papa's Shadow itahamasisha ari mpya ya kusoma maandishi ya Hemingway.

Ninafurahi kuwa, katika Papa's Shadow, nimechangia kuleta mtazamo mpya juu ya Hemingway, na kuelekeza mawazo ya wasomaji na wapenzi wa Hemingway upande wa Afrika Mashariki, na hasa Tanzania. Wote waliochangia mradi huu kwa namna moja au nyingine, kwa hali na mali, wana sababu na haki ya kujipongeza.

Monday, October 12, 2015

Kama Mwandishi, Ninawaenzi wa-Kenya

Mimi kama mwandishi, ninawaenzi wa-Kenya. Naandika kutokana na uzoefu wangu. Tena na tena, mwaka hadi mwaka, nimeshuhudia wa-Kenya wakifuatilia vitabu vyangu. Wamekuwa bega kwa bega nami kama wasomaji wangu.

Tangu nilipochapisha kitabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, wa-Kenya walikichangamkia. Ndugu Tom Gitaa, mmiliki wa gazeti la Mshale aliandaa mkutano kuniwezesha kukitambulisha kitabu hicho, kama ilivyoelezwa katika taarifa hii.

Kati ya watu waliohudhuria alikuwepo Julia Opoti, m-Kenya mwingine, ambaye alishajipambanua kama mpiga debe wa kitabu hiki. Siku hiyo alimleta rafiki yake m-Kenya, Dorothy Rombo, naye akapata kunifahamu na kukifahamu kitabu changu.

Julia hakuishia hapo. Siku moja ulifanyika mkutano mkubwa wa wa-Kenya hapa Minnesota, ambao uliwakutanisha wana-diaspora wa Kenya na viongozi mbali mbali waliofika kutoka Kenya ili kuongelea fursa zilizopo nchini kwao katika uwekezaji na maendeleo kwa ujumla, na namna wana-diaspora wanavyoweza kushirikiana na wenzao walioko nyumbani.

Nilihudhuria mkutano ule sambamba na wengine waliokuwa wanaonesha bidhaa na huduma zao. Nilikuwa na meza ya vitabu vyangu. Julia alimleta ofisa wa ubalozi wa Kenya, Washington DC kwenye meza yangu, akatutambulisha. Alimwelezea kuhusu kitabu changu cha Africans Americans: Embracing Cultural Differences, naye akanunua nakala. Baada ya siku kadhaa aliniandikia ujumbe kama nilivyoandika katika blogu hii. Maneno ya afisa huyu yalinigusa, na baadhi ni haya:

Kuhusu kitabu chako, hivi sasa nafikiri kimesomwa na watu kadri ya watano hapa ubalozi wetu na kimependwa sana. Ni matumaini yangu kuwa ukipata wasaa mzuri utaandika vitabu zaidi katika fani hii ili upate kunufaisha watu juu ya swali hili muhimu la tafauti ya mila na utamaduni

Siku nyingine nilikuwa natoa mhadhara katika Chuo cha Principia. Aliyeanzisha mchakato wa kunialika ni m-Kenya ambaye alikuwa amesoma taarifa zangu mtandaoni. Mama mmoja m-Kenya aliyehudhuria aliamua kuniunganisha na jamii ya wa-Kenya wa Kansas City, ambako alikuwa anaishi, ili niweze kwenda kutoa mhadhara. Mipango ilikamilika nikaenda, kama nilivyoelezea hapa.

Mara kwa mara, nimeona jinsi wa-Kenya wanavyojitokeza katika matamasha ya vitabu ninayoshiriki. Katika Afrifest, kwa mfano, hawakosekani. Nimewahi kuelezea jambo hilo, miaka michache iliyopita na mwaka jana.

Nimeona niandike taarifa hii kwa kuwa naguswa na tabia za majirani zetu hao wa-Kenya. Walinifanyia ukarimu mkubwa nilipokuwa nafanya utafiti nchini mwao baina ya mwaka 1989 na 1991, hata kunialika kutoa mihadhara kuhusu utafiti wangu. Naendelea kuguswa na moyo wao huku ughaibuni. Nimejithibitishia kuwa wanaheshimu taaluma, nami nawaheshimu kwa hilo. Nategemea kuandika zaidi kuhusu suala hilo hapa katika blogu yangu.

Friday, October 9, 2015

Nimepata Toleo Jipya la "Green Hills of Africa"

Leo ni siku ya furaha kwangu. Nimepata nakala ya toleo jipya la Green Hills of Africa, kitabu cha Ernest Hemingway, kilichochapishwa kwa mara ya kwanza mwaka 1935. Taarifa kwamba toleo hili lilikuwa linaandaliwa nilielezwa na Mzee Patrick Hemingway, kama nilivyoandika katika blogu hii. Kwa hivi, nilipogundua kwamba limechapishwa, niliagiza nakala hima.

Katika Green Hills of Africa, Hemingway anaelezea mizunguko yake katika nchi ya Tanganyika, mwaka 1933-34, akiwa na mke wake wa pili Pauline Pfeiffer. Anaelezea uzuri wa nchi, watu wa makabila, tamaduni, na dini mbali mbali, na wanyama katika mbuga alimowinda, kama vile Serengeti na eneo la Ziwa Manyara. Anaelezea miji alimopita, kama vile Mto wa Mbu, Babati, Kondoa, Handeni, na Tanga.

Toleo hili la Green Hills of Africa lina mambo ambayo hayakuwemo katika toleo la mwanzo, kama vile maandishi ya awali ambayo hayakutokea kitabuni, picha, na hata "diary" aliyoandika Pauline alipokuwa safarini na mumewe. Nilijua kuwa "diary" hii imehifadhiwa katika maktaba ya Chuo Kikuu cha Stanford, na nilikuwa nawazia kwenda kuisoma. Kuchapishwa kwake katika toleo hili ni jambo la kufurahisha sana.

Kutokana na jinsi Hemingway alivyoielezea nchi yetu, tukio la kuchapishwa kwa toleo hili la Green Hills of Africa mwaka huu ilipaswa tulipokee kwa shamra shamra. Pangekuwa na shughuli za uzinduzi wa toleo hili, makongamano, na tahakiki magazetini. Nakala zingejaa katika maduka ya vitabu, na wateja wangekuwa wanapigana vikumbo kuzinunua.

Sehemu zingine duniani wanatumia vilivyo bahati ya kutembelewa na Hemingway na kuandikwa katika maandishi yake. Ni kivutio kikubwa kwa watalii, kama ninavyosema katika blogu hii. Sisi tumeifanya nchi yetu kuwa kwenye miti ambako hakuna wajenzi.

Thursday, October 8, 2015

Wanafunzi Wangu wa Ki-Ingereza

Ni yapata mwezi sasa tangu tuanze muhula mpya wa masomo hapa chuoni St. Olaf. Ninafundisha kozi mbili, South Asian Literature na "First Year Writing." Hii ya kwanza ni kozi ya fasihi ya ki-Ingereza kutoka India, Pakistan, na Sri Lanka. Ya pili ni kozi ya uandishi wa ki-Ingereza. Picha hii kushoto, ya darasa la ki-Ingereza (FYW), tulipiga leo. Mwanafunzi mmoja hayumo. Niliweka picha ya darasa kama hili katika blogu hii.

Nilipenda ualimu tangu utotoni. Ninawapenda wanafunzi. Ninawaambia hivyo tangu siku ya kwanza ya masomo, nao wanashuhudia hivyo siku zote. Wanajionea ninavyojituma kuwaelimisha kwa uwezo wangu wote na kwa moyo moja. Sina ubaguzi, dhulma, wala upendeleo. Hiyo imekuwa tabia yangu tangu nilipoanza kufundisha, mwaka 1976, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Ninajivunia jambo hilo.

Kwa miezi mingi, hasa mwaka jana, afya yangu haikuwa njema, na nilichukua likizo ya matibabu. Ingawa nimeanza tena kufundisha, inatokea mara moja moja kwamba sijisikii vizuri. Juzi ilitokea hivyo, ikabidi niwaambie wanafunzi hao waendelee kuandika insha niliyowaagiza kabla, nikawaaga.

Jana, nilipofika ofisini, nilikuta kadi mlangoni pangu, ambayo picha yake inaonekana hapa kushoto. Wanafunzi hao walikuwa wameniandikia hiyo kadi na ndani walikuwa wamesaini majina yao. Maneno yanayoonekana pichani yanatokana na michapo yangu darasani. Nilivyoipata kadi hii, niliguswa. Nimewaambia hivyo leo, tulipoanza kipindi.

Ualimu si kazi rahisi. Inahusu taaluma. Inahusu malezi. Inahusu kuwashauri na kuwasaidia wanafunzi katika hali mbali mbali za maisha. Lakini, hayo ndiyo mambo yanayonivutia katika ualimu. Mafanikio ya wanafunzi masomoni na maishani ndio mafanikio na furaha yangu.

Sunday, October 4, 2015

Uzushi wa Abdulrahman Kinana

Siku kadhaa zilizopita, niliiona mtandaoni makala iliyoandikwa na Abdulrahman Kinana, katibu mkuu wa CCM. Ilikuwa ni makala kali. Kinana anazitahadharisha nchi za magharibi kwamba mgombea urais Edward Lowassa na umoja wa vyama vya siasa ninavyomwunga mkono, yaani UKAWA, wakishinda uchaguzi, Tanzania itageuka kuwa ngome ya magaidi.

Makala yake imejibiwa na watu wengi, lakini nimeona nilete hapa uchambuzi wa Ahmed Rajab huu hapa. Ahmed Rajab amethibitisha vizuri uwongo na uzushi uliomo katika makala ya Kinana, nami sina sababu ya kurudia uchambuzi wake.

Ninapenda kuongezea mawili matatu. Kwanza, ni jambo la kushangaza kwamba Kinana anazielekea nchi za magharibi kama vile ni marafiki zetu wa kuaminiwa, au kama vile ni nchi zenye maslahi sawa na yetu. Ukweli ni kwamba nchi hizo zinafuata maslahi yao. Nchi kama Marekani imethibitisha katika historia yake kwamba haisiti kuwageuka wale waliojiaminisha kuwa ni marafiki wake. Mfano ni Saddam Hussein. Kinana angezingatia hilo.

Ni mradi gani huu anaofanya Kinana kwa kuziambia nchi za Magharibi kuhusu ugaidi Tanzania? Anadhani kwamba kwa kuongelea ugaidi Tanzania anajenga urafiki na hizo nchi za Magharibi?

Kinana anafanya mchezo wa hatari kwa usalama wetu. Hizi nchi za Magharibi, zikiongozwa na kinara wao Marekani, hazina mchezo wala subira na sehemu yoyote duniani ambayo inasemekana ina magaidi. Kwa mtu mwenye wadhifa mkubwa na nyeti kama Kinana kuwasema hao wa-Tanzania anaowasema kwamba ni magaidi ni kuyaweka maisha yao rehani.

Marekani imewakamata watu sehemu mbali mbali duniani ambao walisemw
a kuwa magaidi, hata kwa kusingiziwa, ikawapeleka Guantanamo na sehemu zingine. Wengine wamepoteza maisha kwa kushambuliwa na "drones" za Marekani. Hata hapa jirani Somalia imetokea hivyo. Na "drone" haina macho, inalipua hata wasiohusika, ambao huitwa "collateral damage." Tusipomdhibiti Kinana na uzushi wake, na CCM yake, tunaweza kuishia kuwa "collateral damage."

Kinana si wa kwanza katika CCM kuzua hii habari ya ugaidi. CCM ilishawazulia CUF kwamba wana ajenda ya ugaidi. Mwigulu Nchemba alishawazulia viongozi wa CHADEMA kwamba ni magaidi. Alishindwa kuthibitisha madai yake mahakamani
.

Kutokana na huu mchezo wa hatari anaofanya Kinana, endapo Marekani italeta "drone" kuwashambulia hao anaowaita magaidi, naombea ipotee njia, imlipue Kinana. Anayataka mwenyewe. Sisi wengine hatumo. Wakiturushia "drone" nyingine, naomba ipotee njia iilipue kamati au halmashauri kuu ya CCM. Wanajitakia wenyewe, kupitia kauli za katibu mkuu wao. Sisi wengine hatumo. Ikija "drone" nyingine, naomba ipotee njia iwalipue wana CCM. Wanajitakia wenyewe kwa kukishabikia chama hiki ambacho kinatishia usalama wetu raia tusio na hatia na ambao tunaitakia mema nchi yetu.

Jisomee makala ya Kinana hii hapa:

http://thehill.com/blogs/congress-blog/foreign-policy/253142-tanzania-cannot-be-allowed-to-be-the-new-front-for

Thursday, October 1, 2015

Kwa Wanadiaspora: Fursa ya Kuitangaza Tanzania

Naandika ujumbe huu kwako mwanadiaspora mwenzangu, kuelezea mradi ambao nimehusika nao, wa kitaaluma na wenye fursa ya kuitangaza Tanzania. Mradi huo ni filamu juu ya mwandishi maarufu Ernest Hemingway, ambaye aliwahi kutembelea nchi yetu na Afrika Mashariki kwa ujumla mwaka 1933-34 na 1953-54.

Kutokana na safari hizo, Hemingway aliandika vitabu, hadithi, insha, na barua. Maandishi hayo ni hazina, kwa jinsi yanavyoitangaza nchi yetu, iwapo tutaamua kuwa makini katika kuyatumia. Mfano ni hadithi ambayo wengi wamesikia angalau jina lake, "The Snows of Kilimanjaro."

Nilifanya utafiti wa miaka kadhaa juu ya mwandishi huyu, hatimaye nikatunga kozi, Hemingway in East Africa. Nilisafiri na wanafunzi wa ki-Marekani kwenda Tanzania, tukatembea katika baadhi ya maeneo alimopita Hemingway, huku tukisoma maandishi yake.

Kozi hii imemhamasisha Jimmy Gildea, mmoja wa wanafunzi hao, kutengeneza filamu, Papa's Shadow. Sehemu kubwa ya filamu hiyo ni mazungumzo baina yangu na Mzee Patrick Hemingway, mtoto pekee wa Ernest Hemingway aliye hai. Tunaongelea umuhimu wa Afrika katika maisha, safari, uandishi, na fikra za Ernest Hemingway. Filamu inaonyesha sehemu mbali mbali alimopita Hemingway, kama vile Longido, Arusha, Mto wa Mbu, Karatu, na Babati, na hifadhi kama Serengeti na Ngorongoro. Inaonyesha pia wanafamilia wa mtengeneza filamu wakipanda Mlima Kilimanjaro.

Filamu imekamilika, na mimi nimeiangalia, nikaipenda sana. Lakini, kwa mujibu wa taratibu na sheria, inatakiwa kulipia gharama kadhaa kabla haijaonyeshwa au kusambazwa. Kuna kampeni ya kuchangisha fedha, na mimi ni mchangiaji mojawapo. Zinahitajika dola 10,000, kama inavyoelezwa hapa.

Tofauti na miaka iliyopita, wanadiaspora tunatajwa na serikali ya Tanzania siku hizi kwa sababu tunapeleka fedha ("remittances"). Ni mchango muhimu kwa uchumi wa nchi yetu. Lakini huu mradi ninaoelezea hapa ni njia nyingine ya kuifaidia Tanzania. Filamu hii, mbali ya kuelimisha juu ya Hemingway, ni kivutio kwa watalii. Nasema hivi kwa kuwa najua namna jina la Hemingway na maandishi yake yanavyotumiwa na wenzetu sehemu zingine za dunia ambako Hemingway alipita au kuishi. Mifano ni miji kama vile Paris (Ufaransa) na Pamplona (Hispania), na nchi ya Cuba. Wanapata watalii wengi sana.

Hiyo ninayoelezea hapa ni fursa kwetu wanadiaspora wa Tanzania. Tukishikamana na kuchangia filamu hii hata hela kidogo tu kila mmoja wetu, tutasaidia kumalizia kiasi kinachobaki. Imebaki wiki moja tu na kidogo. Ukitaka, tafadhali tembelea na toa mchango wako hapa katika tovuti ya Kickstarter.