Wednesday, November 26, 2008

Mahojiano na Profesa Joseph Mbele

Niliwahi kuhojiwa na ndugu Deus Gunza, katika Radio Butiama, kuhusiana na kitabu changu kinachohusu tofauti za utamaduni wa Mmarekani na ule wa Mwafrika. Mahojiano yanasikika hapa:
http://butiama.podomatic.com/entry/et/2006-09-02T06_26_37-07_00

Hadithi Zetu

Kabla ya kuweko maandishi, wanadamu walikuwa wanahifadhi kumbukumbu, taaluma, mafunzo, urithi wa utamaduni wao kwa ujumla, kwa masimulizi ya mdomo. Masimulizi hayo yalikuwa ya aina nyingi, kama vile misemo, methali, vitendawili, nyimbo na hadithi. Mfumo mzima wa masimulizi hayo ilikuwa ni hazina iliyobeba taaluma, falsafa, kumbukumbu, mafundisho na kila aina ya ujuzi ambao wanadamu walihitaji katika maisha na maendeleo yao. Kwa karne na karne, ambapo vitabu wala maktaba hazikuwepo, watu walihifadhi ujuzi wao vichwani mwao. Uwezo wao wa kukumbuka mambo ulikuwa mkubwa kuliko uwezo tulio nao sisi, kwani maandishi yametupunguzia uwezo huo na kutujengea aina ya uvivu. Tunategemea maandishi kuliko vichwa vyetu. Tukienda kusikiliza mhadhara, tunahitaji karatasi ya kuandikia yale tunayoyasikia, tofauti na watu wa zamani, ambao walikuwa wanatumia vichwa vyao tu.

Nilizaliwa na kukulia kijijini. Nilikuwa na bahati ya kusikiliza hadithi, nyimbo, na masimulizi ya aina aina, katika Kimatengo, ambayo ni lugha yangu ya kwanza. Baba yangu alikuwa msimuliaji hodari wa hadithi. Niliwahi kuelezea hayo yote kwa ufupi hapa: http://www.thomsonsafaris.com/newsletter/nl38_matengo.htm

Niliposoma Chuo Kikuu Dar es Salaam, 1973-76, nilifundishwa taaluma ya fasihi simulizi. Mwalimu wetu alikuwa marehamu Mofolo Bulane wa Lesotho. Alitufungua macho, katika taaluma hii, tukaanza kuona utajiri wa fasihi simulizi na umuhimu wake katika maisha ya binadamu, tangu enzi za mwanzo hadi leo.

Mwalimu Bulane alinijengea motisha ya kuwa mwanataaluma katika fasihi simulizi. Tangu nilipokuwa mwanafunzi, nilianza kurekodi hadithi kijijini kwangu. Kisha nikawa nazinukuu kutoka kwenye kinasa sauti, nikawa nazitafsiri kutoka kiMatengo kwenda katika kiSwahili na kiIngereza, nikawa nazitafakari na kuzichambua. Nimeelezea hayo kwa ufupi hapa:
http://www.thomsonsafaris.com/newsletter/nl38_collecting.htm

Mwaka 1999, nilichapisha kitabu kwa kiIngereza, Matengo Folktales, http://www.lulu.com/content/136624. Kitabu hiki kinajumlisha tafsiri za hadithi kumi nilizorekodi miaka ya sabini na kitu. Kila hadithi imefuatiwa na uchambuzi, ambao niliuandika ili kufafanua yaliyomo na kuelezea undani wa hadithi na umuhimu wake. Mwishoni mwa kitabu nimeweka insha moja kamili kuhusu hadithi, inayojumlisha mambo muhimu yanayohusu hadithi, kama mwongozo kwa yeyote anayetaka kujielimisha katika taaluma hii. Kitabu hiki kinasomwa hapa Marekani na watu wa kila aina, hata watoto, na kimeshatumiwa na kinaendelea kutumiwa katika vyuo vikuu vingi.

Hadithi zetu ni hazina kubwa inayoweza kutumiwa kwa namna nyingi. Kwa mfano, hadithi na fasihi simulizi kwa ujumla, zinaweza kuwa sehemu muhimu katika utalii. Nimewahi kuzisaidia kampuni za utalii za hapa Marekani katika suala hilo. Mbali na kuendesha semina kadhaa, mwaka 2002 niliongoza kundi kubwa la watalii wa Thomson Safaris kutoka maeneo ya Boston, kuja Tanzania, na mchango niliotoa ni kuwaelimisha watalii hao namna wenyeji katika maeneo ya utalii ya mkoa wa Arusha, Tanzania, walivyobuni masimulizi mbali mbali kuhusu yale yote ambayo watalii walikuwa wanakuja kuyaangalia: iwe ni wanyama, ndege, mimea, au milima. Yote hayo yamo katika fasihi simulizi, na hiyo fasihi simulizi ni njia muhimu ya kuelewa mahusiano ya binadamu na mazingira yake. Kwa kutumia fasihi simulizi katika utalii, utalii unakuwa ni njia ya kujielimisha. Mtalii anaondoka akiwa ameelimika, badala ya kuishia kuzunguka tu mbugani na kupiga picha za wanyama au kupanda Mlima Kilimanjaro.

Hayo yanahitaji juhudi. Watanzania wanatakiwa kuwa makini katika utafiti na katika kujielimisha kuhusu utamaduni wao na historia yake. Bila hivyo, fursa hii ya kutumia fasihi simulizi na vipengele vingine vya utamaduni itatupitia mbali, wakati wenzetu katika sehemu zingine za dunia wanaitumia vizuri. Mwalimu Nyerere alituhimiza kuukumbuka utamaduni wetu, kujifunza, na kuuenzi, lakini je, ni Watanzania wangapi wanaokumbuka hayo mafundisho ya Mwalimu Nyerere? Wangapi wanafahamu ni lini na wapi Mwalimu Nyerere aliongelea masuala muhimu ya utamaduni wetu?

Tuesday, November 25, 2008

Migogoro ya kidini na hadithi zingine

Kuna hadithi nyingi duniani. Hadithi moja ninayoifuatilia ni ya migogoro ya kidini. Katika historia ya binadamu, kumekuwepo migogoro na vita baina ya watu wa dini mbali mbali, na migogoro hiyo bado inaendelea. India kumekuwepo migogoro baina ya Wahindu na Waislamu, na pia baina ya Wahindu na Wakristu. Ulaya kulikuwako vita maarufu za "Crusades." Ireland kumekuwapo migogoro baina ya Wakatoliki na Waprotestanti. Nigeria kumekuwapo migogoro baina ya Waislam na Wakristu. Hii ni mifano tu.

Ni kawaida kwa migogoro hii kuitwa migogoro ya kidini. Suali ninalojiuliza ni je, hii migogoro ni ya kidini kweli? Mimi nadhani hapa pana tatizo kubwa kinadharia. Ninavyofahamu, dhana ya dini ni kumwamini Muumba na kufuata amri zake: katika ibada, katika maisha yetu binafsi, na katika kuishi kwetu na wanadamu wenzetu. Dhana ya dini inajumlisha yote hayo.

Kwa msingi huo, mtu mwenye dini atakuwa mcha Mungu, mwema, mpole, mwenye haki, mwadilifu, mwumilivu, na mwenye huruma. Binadamu ni binadamu; anaweza kupotoka: anaweza akafanya ugomvi, hujuma, au jambo jingine baya. Lakini, mtu huyu atajirudi mara na kumwangukia Muumba kuomba msamaha, ili aendelee kuwa katika njia iliyo sahihi kwa msingi wa dini.

Kwa mantiki hiyo, penye dini ni mahali penye amani, maelewano, na kuheshimiana. Migogoro na vita ni dalili ya kukosekana kwa dini. Vita ni ishara ya kukosekana kwa dini. Dini ni kama mwanga, na vita na migogoro ni kama giza. Penye mwanga hapana giza. Ndio maana nasema, penye dini hapana magomvi wala vita. Vita na migogoro ni ufedhuli, na ufedhuli hauko kwenye dini. Kupigana au kuwa na migogoro ni kuisaliti dini.

Kwa msingi huo, mimi siafiki kuwa kunaweza kukawa na vita vya kidini, au migogoro ya kidini. Dhana ya vita vya kidini au migogoro ya kidini ni hadithi isiyo na mantiki, kama hadithi zingine zozote zisizo na mantiki.