Tuesday, November 25, 2008

Migogoro ya kidini na hadithi zingine

Kuna hadithi nyingi duniani. Hadithi moja ninayoifuatilia ni ya migogoro ya kidini. Katika historia ya binadamu, kumekuwepo migogoro na vita baina ya watu wa dini mbali mbali, na migogoro hiyo bado inaendelea. India kumekuwepo migogoro baina ya Wahindu na Waislamu, na pia baina ya Wahindu na Wakristu. Ulaya kulikuwako vita maarufu za "Crusades." Ireland kumekuwapo migogoro baina ya Wakatoliki na Waprotestanti. Nigeria kumekuwapo migogoro baina ya Waislam na Wakristu. Hii ni mifano tu.

Ni kawaida kwa migogoro hii kuitwa migogoro ya kidini. Suali ninalojiuliza ni je, hii migogoro ni ya kidini kweli? Mimi nadhani hapa pana tatizo kubwa kinadharia. Ninavyofahamu, dhana ya dini ni kumwamini Muumba na kufuata amri zake: katika ibada, katika maisha yetu binafsi, na katika kuishi kwetu na wanadamu wenzetu. Dhana ya dini inajumlisha yote hayo.

Kwa msingi huo, mtu mwenye dini atakuwa mcha Mungu, mwema, mpole, mwenye haki, mwadilifu, mwumilivu, na mwenye huruma. Binadamu ni binadamu; anaweza kupotoka: anaweza akafanya ugomvi, hujuma, au jambo jingine baya. Lakini, mtu huyu atajirudi mara na kumwangukia Muumba kuomba msamaha, ili aendelee kuwa katika njia iliyo sahihi kwa msingi wa dini.

Kwa mantiki hiyo, penye dini ni mahali penye amani, maelewano, na kuheshimiana. Migogoro na vita ni dalili ya kukosekana kwa dini. Vita ni ishara ya kukosekana kwa dini. Dini ni kama mwanga, na vita na migogoro ni kama giza. Penye mwanga hapana giza. Ndio maana nasema, penye dini hapana magomvi wala vita. Vita na migogoro ni ufedhuli, na ufedhuli hauko kwenye dini. Kupigana au kuwa na migogoro ni kuisaliti dini.

Kwa msingi huo, mimi siafiki kuwa kunaweza kukawa na vita vya kidini, au migogoro ya kidini. Dhana ya vita vya kidini au migogoro ya kidini ni hadithi isiyo na mantiki, kama hadithi zingine zozote zisizo na mantiki.

2 comments:

Christian Bwaya said...

Mimi naona penye imani/uhusiano na Mungu(spirituality) ndiko penye yote hayo uliyoyataja.

Penye dini (vyama vya waumini wanaopapasa kujua anachotaka Mungu) hapawezi kuwa na amani wala upendo wala uvumilivu.

Penye dini hapakosi migogoro. penye dini hapana umoja.

Sababu dini yenyewe ndilo tatizo la msingi. Na nionavyo mimi dini si kumwamini Muumba na kufuata amri zake. Hiyo ni imani ambayo si lazima itokane na dini. Dini ni chama cha kumtafuta Muumba kinadharia hata kama haiwasaidii wanachama husika kufikia lengo hilo.

Waumini wa dini hawapendani. hawaheshimiani. Hawavumiliani. Kwa sababu kila chama kinataka kuonekana chenyewe ndicho kina uhusiano wa moja kwa moja na Mungu kuliko vyama vingine.

Mbele said...

Shukrani kwa ufafanuzi huu baina ya imani na dini. Naiona hoja yako vizuri.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...