Thursday, March 29, 2018

Kitabu Kinaendelea Kupigiwa Debe Nebraska

Mfanya biashara au mtoa huduma hufarijika anapoona wateja wakija tena kufuata kile walichokipata kabla. Imekuwa hivyo kwangu kama mwandishi. Mimi si mfanyabiashara, bali ni mwalimu. Uandishi ni sehemu ya ualimu. Ninafarijika na kufurahi ninapoona watu wakifaidika na maandishi yangu.

Ninaandika ujumbe huu kuelezea ujumbe juu ya kitabu changu, Africans and Americans: Embracing Cultural Differences kutoka Nebraska, jimbo mojawapo la Marekani. Waumini wa kanisa la ki-Luteri la Marekani, ELCA, wa sinodi ya Nebraska wana programu ya kuzuru Tanzania iitwayo vision trip, kujifunza masuala ya utamaduni na maisha ya wa-Tanzania na kubadilishana uzoefu, ili kujenga mahusiano na maelewano.

Mwaka hadi mwaka, waratibu wa programu wamekipendekeza kitabu changu hicho. Leo nimeona chapisho la mwongozo kwa ajili safari ya mwaka 2018. Humo, kama ilivyokuwa miaka iliyopita, kitabu changu kimeendelea kupendekezwa kwa wasafiri:

For those persons wanting to more deeply explore cultural differences between Africans and Americans, the book Africans and Americans by Joseph Mbele is recommended. This book is available at: www.africonexion.com

Tafsiri kwa ki-Swahili:

Kwa wale wanaotaka kufuatilia zaidi tofauti za tamaduni baina ya wa-Afrika na wa-Marekani, kitabu "Africans and Americans" cha Joseph Mbele kinapendekezwa. Kitabu hiki kinapatikana www.africonexion.com


Ninafurahi na kushukuru kwamba watu wanaona umuhimu wa kitabu hiki. Kingekuwa hakina manufaa, wangeacha kukipendekeza tangu zamani. Niliwahi kukutana na baadhi ya hao wasafiri wa Nebraska katika safari ya kwenda Tanzania wakiwa na kitabu changu, kama nilivyoandika katika blogu ya ki-Ingereza. Ninafurahi kuwa kitabu changu kinasaidia lengo la kujenga maelewano baina ya wa-Tanzania na wa-Marekani.

Monday, March 19, 2018

Nimenunua CD za "Hamlet"

Leo niliingia katika duka la vitabu la chuoni St. Olaf kununua vitabu ambavyo nilikuwa nimepangia tangu jana. Lakini wakati naangalia vitabu, niliona kifurushi cha CD za Hamlet, tamthilia ya Shakespeare.

Hiyo niliiona kama bahati ya pekee, kwa sababu siku chache zilizopita niliandika katika blogu hii kuwa tunasoma Hamlet. Ilikuwa ni wazi kuwa CD hizi nimeziona wakati muafaka. Nilichukua hicho kifurushi cha CD, nikakijumlisha na vitabu nilivyopangia kununua nikalipia vyote.

Jioni hii nimefungua kifurushi nikaona ziko CD tatu. Zimeandaliwa na Folger Theatre, ambacho ni kitengo cha Folger Shakespeare Library,  ambayo ndio makataba kubwa kuliko zote duniani za kazi za William Shakespeare na machapisho juu yake. Watafiti kutoka duniani kote wanafanya utafiti katika maktaba hii. Hamlet, kama ilivyo tamthilia zingine za Shakespeare, inapatikana katika matoleo mbali mbali. Folger Shakespeare Library ina toleo lake.

Kama nilivyosema, nimeanza kusikiliza jioni hii. Nimevutiwa sana na utambaji wa tamthilia. Wameonyesha uhodari mkubwa wa kuwasilisha sio tu maneno ya tamthilia bali pia vitu kama hisia na mazingira ya matukio. Kwa mfano, nimevutiwa sana na namna wanavyowasilisha tukio la kuonekana mzimu wa baba yake Hamlet. Mtu unasikiliza na unajhisi uko kwenye tukio unashuhudia.

Kusoma ni kutafsiri. Kusoma kwa sauti ni kutafsiri kwa namna ya pekee. Ni tabia ya tafsiri kwamba kila mtu anaibuka na yake. Ndio maana ninasema kuwa hizi CD zinagusa kwa namna ya pekee. Mimi mwenyewe, kwa kuzingatia ukweli huo, nilisoma kwa sauti shairi la W. B. Yeats, "The Second Coming," nikaweka katika blogu hii. Nilitaka niweke wazi kwa kutumia sauti uelewa wangu na hisia zangu juu shairi hili. Ni tafsiri yangu. Ukisikiliza usomaji wa wengine, ambazo zinapatikana mtandaoni, utajionea tafsiri tofauti za shairi hili hili.

Saturday, March 17, 2018

Tunasoma "Hamlet"

Muhula huu nina mwanafunzi mwingine aliyeamua kujitungia kozi yake mwenyewe na kuifanya chini ya usimamizi wangu. Utaratibu huu uko hapa chuoni St. Olaf, kama nilivyowahi kuelezea katika blogu hii.

Kwa kushauriana nami, mwanafunzi alijitungia kozi juu ya "The Living and the Dead: Folklore and Tragedy." Tulikubaliana kusoma Agamemnon (Aeschylus), Beowulf (translated by Seamus Heaney), Inferno (Dante Alighieri), Hamlet (William Shakespeare), Othello (William Shakespeare), Love in the Time of Cholera (Gabriel Marcia Marquez), na As I Lay Dying (William Faulkner). Tumeshasoma Beowulf, na sasa tuna soma Hamlet.Napenda kusema neno kuhusu Hamlet katika mkabala wa kozi yetu hii.
Kwanza napenda kusema kuwa niliwahi kuongelea Hamlet katika blogu hii. Nilifanya hivyo kwa kujikumbusha tamthilia hii maarufu. Lakini sasa tunaisoma tukiwa na lengo la kuihusisha na mada ya kozi "The Living and the Dead: Folklore and Tragedy."

Hamlet ni tamthilia ya tanzia ("tragedy.") Hilo halina utata. Hamlet ana masononeko akikabiliwa na maamuzi magumu kufuatia kifo cha baba take katika mazingira ya kutatanisha. Katika tamthilia hii tunakutana na watu walio hai na pia mzimu wa baba yake Hamlet. Ujumbe wa mzimu ni kuwa aliuawa na mdogo wake, ambaye ni mfalme aliyeko madarakani. Baada ya mauaji hayo, mdogo huyu alimwoa mama yake Hamlet. Kuwepo kwa mzimu kunatupa fursa ya kujionea mfu aliye hai. Katika mazungumzo, wahusika wanaongelea masuala ya kifo na uhusiano wake na uhai. Mama yake anajaribu kumtuliza:

Good Hamlet, cast thy nighted color off,
And let thine eye look like a friend on Denmark.
Do not for ever with thy vailed lids
Seek for thy noble father in the dust.
Thou know't 'tis common, all that lives must die,
Passing through nature to eternity.
                                                       Act 1. Sc II

Hamlet mwenyewe anaonekana akijiuliza iwapo ni bora kuendelea kuishi na kukabiliana na magnum ya maisha au kujiua ili kuyamaliza. Tunamsikia akitafakari suala hilo katika hotuba yake maarufu "To be or not to be" ambayo ni moja kati ya hotuba maarufu kabisa katika tamthilia za Shakespeare:

Ham. To be, or not to be, that is the question:
Whether 'tis nobler in the mind to suffer
The slings and arrows of outrageous fortune
Or to take arms against a sea of troubles,
And by opposing end them. To die--to sleep--
No more; and by a sleep to say we end
The heartache, and the thousand natural shocks
That flesh is heir to. 'Tis a consummation
Devoutly to be wished. To die--to sleep.
To sleep--perchance to dream: ay, there's the rub!
For in that sleep of death what dreams may come
When we have shuffled off this mortal coil,
Must give us pause.... 
                                              Act. III. Sc. I

Ninapenda kusema kuwa mwanafunzi wangu na mimi tumeanza vizuri kuiitafakari mada ya "The Living and the Dead.: Folklore and Tragedy." Kila kitabu kina mchango wake katika kuilezea mada hii. Haya tutayadhihirisha kadiri kozi inavyoendelea.

Thursday, March 8, 2018

Nimenunua Vitabu Vipya vya Mashairi

Katika siku chache zilizopita, nimenunua vitabu vipya viwili vya mashairi. Kimoja ni Collected Poems: 1974-2004  cha Rita Dove, ambacho nilikinunua mjini Moscow, Idaho. Kingine ni Diwani ya Tuzo ya Ushairi ya Ibrahim Hussein ambacho nilikinunua mtandaoni Amazon.

Nilipokuwa Moscow katika tamasha la Hemingway, niliingia katika duka la Book People of Moscow. Niliangalia, nikaona kitabu hiki Collected Poems, ambacho sikukifahamu kabla. Nilivutiwa kwa sababu nilifahamu habari za Rita Dove, kwamba ni mshairi maarufu sana, aliyepata tuzo kadhaa ikiwemo tuzo ya Pulitzer.

Zaidi ni kuwa niliwahi kusoma insha yake "Either I'm Nobody, or I'm a Nation," ambayo ni uchambuzi wa mashairi ya Derek Walcott. Nilikuwa ninafundisha tungo za Walcott, nikaitafuta makala hii na niliona ilivyojaa tafakari na ilivyoandikwa kwa ustadi. Makala hii ilinithibitishia kuwa Rita Dove ana akili sana. Hii ikawa sababu kubwa ya mimi kununua Collected Poems.

Diwani ya Tuzo ya Ushairi ya Ibrahim Hussein niliinunua baada ya kuiona imetajwa mtandaoni Amazon. Nilikuwa sifahamu kuwepo kwake, lakini kwa jinsi ninavyomwenzi Ebrahim Hussen ambaye nilimfahamu tulipokuwa wote katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, yeye akiwa mhadhiri wakati ninasoma, na hatimaye tukawa tunafundisha wote, niliona ninunue kitabu hiki. Mimi mwenyewe nimechapisha makala juu ya tungo za Ebrahim Hussein katika Encyclopedia of African Literature iliyohaririwa na profesa Simon Gikandi.

Nimeanza kuyasoma mashairi yaliyomo katika vitabu vyote viwili. Tayari nimeona kuwa Rita Dove anaandika kwa nidhamu ya hali ya juu, ya kutumia maneno yanayohitajika tu, na anatupeleka sehemu mbali mbali za dunia, tangu enzi za kale hadi leo, kama anavyofanya Derek Walcott katika tungo zake, iwe ni mashairi au tamthilia. Diwani ina washairi wengi chipukizi. Ni fursa yao kuonekana kwa wasomaji.

Tuesday, March 6, 2018

Mdau wa Kitabu Amekuja Tena

Hapa pichani ninaonekana na De'Vonna, mmoja wa waandaaji wa maonesho ya waandishi yaliyoitwa Minnesota Black Authors Expo, ambayo niliyaelezea katika blogu hii. Anaonekana ameshika kitabu changu, Africans and American:Embracing Cultural Differences. Picha tulipiga wakati wa maonesho. Amenilitea ujumbe kuwa anahitaji nakala nyingine ya hiki kitabu.

Kwa kuzingatia jinsi mama huyu alivyo na ushawishi katika jimbo hili la Minnesota, hasa miongoni mwa wenzake wa-Marekani Weusi, nimeguswa na ujumbe wake kwa namna ya pekee. Tangu nilipoandika kitabu hiki, nilikuwa na dukuduku ya kujua wa-Marekani Weusi watakuwa na maoni gani kuhusu yale ninayosema juu ya mahusiano yao na sisi wa-Afrika. Nilielezea dukuduku hiyo katika blogu ya ki-Ingereza.

Kama inavyoeleweka, mahusiano hayo yanawatatiza baadhi ya watu. Kwa hivyo ninapopata mrejesho kutoka kwa hao wenzetu, ninauchukulia kwa uzito wa pekee. Nimefarijika na kufurahi kwamba De'Vonna anataka nakala nyingine ya kitabu changu. Sijui anakipeleka wapi, au atakitumia vipi, lakini hii si hoja.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...