Monday, March 19, 2018

Nimenunua CD za "Hamlet"

Leo niliingia katika duka la vitabu la chuoni St. Olaf kununua vitabu ambavyo nilikuwa nimepangia tangu jana. Lakini wakati naangalia vitabu, niliona kifurushi cha CD za Hamlet, tamthilia ya Shakespeare.

Hiyo niliiona kama bahati ya pekee, kwa sababu siku chache zilizopita niliandika katika blogu hii kuwa tunasoma Hamlet. Ilikuwa ni wazi kuwa CD hizi nimeziona wakati muafaka. Nilichukua hicho kifurushi cha CD, nikakijumlisha na vitabu nilivyopangia kununua nikalipia vyote.

Jioni hii nimefungua kifurushi nikaona ziko CD tatu. Zimeandaliwa na Folger Theatre, ambacho ni kitengo cha Folger Shakespeare Library,  ambayo ndio makataba kubwa kuliko zote duniani za kazi za William Shakespeare na machapisho juu yake. Watafiti kutoka duniani kote wanafanya utafiti katika maktaba hii. Hamlet, kama ilivyo tamthilia zingine za Shakespeare, inapatikana katika matoleo mbali mbali. Folger Shakespeare Library ina toleo lake.

Kama nilivyosema, nimeanza kusikiliza jioni hii. Nimevutiwa sana na utambaji wa tamthilia. Wameonyesha uhodari mkubwa wa kuwasilisha sio tu maneno ya tamthilia bali pia vitu kama hisia na mazingira ya matukio. Kwa mfano, nimevutiwa sana na namna wanavyowasilisha tukio la kuonekana mzimu wa baba yake Hamlet. Mtu unasikiliza na unajhisi uko kwenye tukio unashuhudia.

Kusoma ni kutafsiri. Kusoma kwa sauti ni kutafsiri kwa namna ya pekee. Ni tabia ya tafsiri kwamba kila mtu anaibuka na yake. Ndio maana ninasema kuwa hizi CD zinagusa kwa namna ya pekee. Mimi mwenyewe, kwa kuzingatia ukweli huo, nilisoma kwa sauti shairi la W. B. Yeats, "The Second Coming," nikaweka katika blogu hii. Nilitaka niweke wazi kwa kutumia sauti uelewa wangu na hisia zangu juu shairi hili. Ni tafsiri yangu. Ukisikiliza usomaji wa wengine, ambazo zinapatikana mtandaoni, utajionea tafsiri tofauti za shairi hili hili.

No comments:

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...