Thursday, March 8, 2018

Nimenunua Vitabu Vipya vya Mashairi

Katika siku chache zilizopita, nimenunua vitabu vipya viwili vya mashairi. Kimoja ni Collected Poems: 1974-2004  cha Rita Dove, ambacho nilikinunua mjini Moscow, Idaho. Kingine ni Diwani ya Tuzo ya Ushairi ya Ibrahim Hussein ambacho nilikinunua mtandaoni Amazon.

Nilipokuwa Moscow katika tamasha la Hemingway, niliingia katika duka la Book People of Moscow. Niliangalia, nikaona kitabu hiki Collected Poems, ambacho sikukifahamu kabla. Nilivutiwa kwa sababu nilifahamu habari za Rita Dove, kwamba ni mshairi maarufu sana, aliyepata tuzo kadhaa ikiwemo tuzo ya Pulitzer.

Zaidi ni kuwa niliwahi kusoma insha yake "Either I'm Nobody, or I'm a Nation," ambayo ni uchambuzi wa mashairi ya Derek Walcott. Nilikuwa ninafundisha tungo za Walcott, nikaitafuta makala hii na niliona ilivyojaa tafakari na ilivyoandikwa kwa ustadi. Makala hii ilinithibitishia kuwa Rita Dove ana akili sana. Hii ikawa sababu kubwa ya mimi kununua Collected Poems.

Diwani ya Tuzo ya Ushairi ya Ibrahim Hussein niliinunua baada ya kuiona imetajwa mtandaoni Amazon. Nilikuwa sifahamu kuwepo kwake, lakini kwa jinsi ninavyomwenzi Ebrahim Hussen ambaye nilimfahamu tulipokuwa wote katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, yeye akiwa mhadhiri wakati ninasoma, na hatimaye tukawa tunafundisha wote, niliona ninunue kitabu hiki. Mimi mwenyewe nimechapisha makala juu ya tungo za Ebrahim Hussein katika Encyclopedia of African Literature iliyohaririwa na profesa Simon Gikandi.

Nimeanza kuyasoma mashairi yaliyomo katika vitabu vyote viwili. Tayari nimeona kuwa Rita Dove anaandika kwa nidhamu ya hali ya juu, ya kutumia maneno yanayohitajika tu, na anatupeleka sehemu mbali mbali za dunia, tangu enzi za kale hadi leo, kama anavyofanya Derek Walcott katika tungo zake, iwe ni mashairi au tamthilia. Diwani ina washairi wengi chipukizi. Ni fursa yao kuonekana kwa wasomaji.

No comments: