Showing posts with label Hemingway. Show all posts
Showing posts with label Hemingway. Show all posts

Thursday, March 8, 2018

Nimenunua Vitabu Vipya vya Mashairi

Katika siku chache zilizopita, nimenunua vitabu vipya viwili vya mashairi. Kimoja ni Collected Poems: 1974-2004  cha Rita Dove, ambacho nilikinunua mjini Moscow, Idaho. Kingine ni Diwani ya Tuzo ya Ushairi ya Ibrahim Hussein ambacho nilikinunua mtandaoni Amazon.

Nilipokuwa Moscow katika tamasha la Hemingway, niliingia katika duka la Book People of Moscow. Niliangalia, nikaona kitabu hiki Collected Poems, ambacho sikukifahamu kabla. Nilivutiwa kwa sababu nilifahamu habari za Rita Dove, kwamba ni mshairi maarufu sana, aliyepata tuzo kadhaa ikiwemo tuzo ya Pulitzer.

Zaidi ni kuwa niliwahi kusoma insha yake "Either I'm Nobody, or I'm a Nation," ambayo ni uchambuzi wa mashairi ya Derek Walcott. Nilikuwa ninafundisha tungo za Walcott, nikaitafuta makala hii na niliona ilivyojaa tafakari na ilivyoandikwa kwa ustadi. Makala hii ilinithibitishia kuwa Rita Dove ana akili sana. Hii ikawa sababu kubwa ya mimi kununua Collected Poems.

Diwani ya Tuzo ya Ushairi ya Ibrahim Hussein niliinunua baada ya kuiona imetajwa mtandaoni Amazon. Nilikuwa sifahamu kuwepo kwake, lakini kwa jinsi ninavyomwenzi Ebrahim Hussen ambaye nilimfahamu tulipokuwa wote katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, yeye akiwa mhadhiri wakati ninasoma, na hatimaye tukawa tunafundisha wote, niliona ninunue kitabu hiki. Mimi mwenyewe nimechapisha makala juu ya tungo za Ebrahim Hussein katika Encyclopedia of African Literature iliyohaririwa na profesa Simon Gikandi.

Nimeanza kuyasoma mashairi yaliyomo katika vitabu vyote viwili. Tayari nimeona kuwa Rita Dove anaandika kwa nidhamu ya hali ya juu, ya kutumia maneno yanayohitajika tu, na anatupeleka sehemu mbali mbali za dunia, tangu enzi za kale hadi leo, kama anavyofanya Derek Walcott katika tungo zake, iwe ni mashairi au tamthilia. Diwani ina washairi wengi chipukizi. Ni fursa yao kuonekana kwa wasomaji.

Sunday, March 20, 2016

Tukio Katika Nyumba ya Hemingway, Oak Park

Tarehe 27 Februari, nilizuru nyumba alimozaliwa mwandishi Ernest Hemingway, na pia jumba la kumbukumbu ya Hemingway, kama nilivyoandika katika blogu hii na blogu ya ki-Ingereza. Ilikuwa ni siku ya pekee, siku ambayo ndoto yangu ya miaka ilitimia.

Kati ya watu niliokutana nao katika nyumba ya Hemingway, ambao nao walikuwa wamekuja kuitembelea, ni binti aliyejitambulisha kuwa ni wa ukoo wa Hemingway. Alinipa kadi yake, iliyoonyesha kuwa jina lake ni Laura Hemingway.

Nilishangaa na kufurahi, nikaanza kuongelea namna ninavyomwenzi Hemingway. Niliongelea kozi yangu ya Hemingway, na jinsi ninavyowasiliana na mzee Patrick Hemingway. Binti huyu na wengine tuliokuwa tunasubiri kuanza ziara walivutiwa na taarifa hizo. Ninajitambua kuwa siwezi kuiachia fursa yoyote ya kuongelea habari za Hemingway.

Kwa bahati mbaya, niliporejea kutoka Chicago, niligundua kuwa nilikuwa nimepoteza anwani ya binti huyu. Leo amejitokeza katika facebook kuanzisha mawasiliano nami. Baada ya kuweka uhusiano huo, nimeweza kuipata picha tuliyopiga siku tulipokutana, ambayo inaonekana hapa juu.

Sunday, March 15, 2015

Darasa la "Hemingway in East Africa 2013" Kando ya Ziwa Babati

Mwezi Januari, 2013, nilikuwa Tanzania na wanafunzi kutoka Chuo cha St. Olaf katika kozi ya "Hemingway in East Africa."

Niliitunga kozi hii mwaka 2006, kwa ajili ya Chuo cha Colorado. Kwa miaka kadhaa, kabla ya kutunga kozi hiyo, nilisoma maandishi ya Ernest Hemingway aliyoandika kufuatia safari zake mbili Afrika Mashariki, miaka ya 1933-34 na 1953-54.

Lengo la kozi lilikuwa kuwafundisha wanafanuzi kwa kusafiri nao katika baadhi ya maeneo alimopita Hemingway, huku tukisoma maandishi yake kuhusu safari zake katika maeneo haya. Maandishi hayo ni pamoja na kitabu cha Green Hills of Africa na Under Kilimanjaro, hadithi ya "The Short Happy Life of Francis Macomber," barua, na insha kadhaa katika magazeti.

Pichani wanaonekana wanafunzi na madereva wetu pembeni mwa Ziwa Babati. Katika Green Hills of Africa, Hemingway aliandika kuhusu Babati na Ziwa Babati:

     We left, soon after midnight, ahead of the outfit, who were to strike camp and follow in the two lorries. We stopped in Babati at the little hotel overlooking the lake and bought some more Pan-Yam pickles and had some cold beer (uk. 143).

Friday, September 5, 2014

Leo Nimeanza Tena Kufundisha

Baada ya kuumwa kwa miezi mingi, na kuwa katika likizo ya matibabu, leo nimeanza tena kufundisha. Hali yangu inaendelea kuimarika, na ingawa naendelea na matibabu kidogo kidogo, madaktari wameridhia ombi langu kuwa nirudi darasani. Wameniwekea sharti kuwa nisibebe mzigo mkubwa wa kozi za kufundisha, na nisihusishwe na shughuli nyingine ambazo walimu huzifanya, kama vile ushiriki katika kamati mbali mbali na mikutano. Hiyo picha hapa kushoto nimejipiga mwenyewe leo, baada ya kutoka darasani.

Hali itakuwa hiyo kwa muhula mzima, ambao umeanza leo, na utamalizika katikati ya mwezi Desemba. Ninafundisha kozi mbili, ya kwanza ni "South Asian Literature," na ya pili ni "Writing." Katika hiyo kozi ya kwanza, ambayo niliitunga miaka michache iliyopita, nafundisha riwaya kutoka India, Pakistan, na Sri Lanka. Riwaya hizo ni, Untouchable, iliyoandikwa na Mulk Raj Anand (India); Twilight in Delhi, iliyoandikwa na Ahmed Ali (India); The Crow Eaters, iliyoandikwa na Bapsi Sidhwa (Pakistan); Shalimar the Clown, iliyoandikwa na Salman Rushdie (India); na Reef, iliyoandikwa na Romesh Gunesekera (Sri Lanka).

Ninapangia kufundisha pia mashairi kutoka katika nchi hizo. Kwa wakati huu, katika kujiandaa, ninasoma kitabu cha mashairi ya Michael Ondaatje kiitwacho The Cinnamon Peeler. Michael Ondaatje alizaliwa Sri Lanka, ila anaishi Canada. Ninafanya pia uchunguzi wa vitabu vya mashairi ambayo nitaweza kuyatumia. Kila ninapofundisha kozi hii, nabadilisha, kwa kiasi fulani, vitabu au waandishi.

Fasihi ya hiyo sehemu ya dunia imejengeka katika historia, siasa, dini, tamaduni, na harakati za watu wa kule tangu miaka elfu tano au zaidi iliyopita hadi kwenye kipindi cha ukoloni, na baada ya kupata uhuru. Waandishi wengi wa India na Pakistan, kwa mfano, wanaelezea janga kubwa lililotokea kabla tu ya kupata uhuru na wakati nchi ilipogawanyika na kuwa nchi hizi mbili, mwaka 1947.

Katika kozi ya "Writing," ninafundisha uandishi bora wa ki-Ingereza. Kadiri miaka ilivyokwenda, nami kujijengea uzoefu zaidi na zaidi wa kufundisha kozi hii, nimekuwa nikitafuta mbinu mpya za kufundisha. Leo nimewaambia wanafunzi kuwa, tofauti na miaka yote iliyopita, na tofauti na wanavyofanya waalimu wengine, muhula huu tutatumia vitabu viwili tu. Kitabu kimoja ni The Trickster, kilichoandikwa na Paul Radin, na kingine ni The Elements of Style, kilichoandikwa na William Strunk Jr. na E.B. White.

Lengo langu katika hii kozi ya uandishi ni kuwafundisha kwanza kabisa namna ya kuandika sentensi bora kabisa ya ki-Ingereza, kama alivyoelekeza mwandishi maarufu Ernest Hemingway, na baada ya hapo tutaendelea hadi kuweza kuandika insha bora kabisa. Nimewaeleza wanafunzi kwamba uandishi bora ni jambo la lazima kwa mafanikio maishani mwao, nikatoa mifano mbali mbali ya namna watakavyohitaji uwezo wa kuandika ipasavyo. Wameona uzito wa hoja na mifano niliyotoa.

Nimefurahi kuwa nimefikia hali ya kuweza kuingia tena darasani, nikizingatia hali yangu kiafya ilivyokuwa mbaya kabla sijalazwa hospitalini. Kwa mara nyingine tena, namshukuru Mungu, na nawashukuru madaktari na wauguzi, familia yangu, marafiki, na wote wanaonitakia mema. Mungu awabariki wote.

Thursday, August 14, 2014

Nimezawadiwa Kitabu: "Picturing Hemingway's Michigan"

Leo nimepata zawadi ya kitabu, Picturing Hemingway's Michigan kilichotungwa na Michael R. Federspiel. Kinahusu sehemu ya kaskazini ya jimbo la Michigan, ambapo familia ya Ernest Hemingway ilikuwa inakwenda kwa mapumziko.

Kitabu kina picha na maelezo kuhusu sehemu hiyo, ambapo Hemingway alitembelea tena na tena wakati wa utoto na ujana wake. Hapa ni chimbuko la matukio ya riwaya ya mwanzo ya Hemingway, The Torrents of Spring na hadithi zake ziitwazo Nick Adams Stories.







Nimeletewa kitabu hiki na Bwana David Cooper wa Ohio na mwanae Clay ambaye ni mwanafunzi wangu aliyekuja Tanzania mwezi Januari, 2013 katika kozi yangu ya "Hemingway in East Africa."

Baba huyu ndiye aliyetupeleka Montana kwa ndege yake mwaka jana, kuonana na Mzee Patrick Hemingway. Hapa kushoto ni picha tuliyopiga mjini Lakeville, Minnesota, kabla ya kuruka kwenda Montana. Bwana Cooper anaonekana kulia kabisa, halafu anafuata mwanae, halafu mwanafunzi wangu mwingine aliyekuwemo katika kozi ya "Hemingway in East Africa," na mimi naonekana kushoto kabisa.


Mwanafunzi aliyeniletea kitabu anaonekana nami pichani hapa kushoto, tukiwa kwenye mpaka baina ya hifadhi za Ngorongoro na Serengeti.

Nilipokipata kitabu hiki, yapata saa saba mchana, nilijawa na furaha, nikaanza kukisoma mara, lakini nikaona nipige kwanza simu kwa walioniletea. Nilimpata Bwana Cooper, nikamshukuru sana. Ameniambia kuwa yeye na mwanae walikiona kitabu hiki katika duka kule sehemu ya Michigan Kaskazini, wakaniwazia. Baada ya maongezi nimeendelea kukisoma, nikamaliza baada ya masaa mawili hivi..

Wameninunulia nakala yenye sahihi ya mwandishi, kama inavyoonekana hapa kushoto. (Ninaposema hivi, mawazo yangu yameshakwenda kwenye mazungumzo baina yangu na Ndugu Christian Bwaya kuhusu suala hili la kusainiwa vitabu).

Nilifahamu kuwa sehemu hii ya Michigan Kaskazini ni muhimu katika utoto na ujana wa Hemingway, lakini kitabu hiki kimenifungua macho zaidi kwa kuonyesha sehemu mbali kwa picha na maelezo. Picha nyingi ni za mtoto Hemingway na watoto wengine katika familia yao, picha za wanaukoo, na sehemu mbali mbali. Nyingi katika ya picha hizo sikuwa nimeziona kabla. Kwa yote hayo, nimefurahi sana.

Friday, May 30, 2014

Tembo wa Hifadhi ya Tarangire, Tanzania

Tarangire ni moja ya hifadhi maarufu Tanzania, yenye wanyama mbali mbali.

Nimefika katika hifadhi hii mara nne, kwa miaka tofauti. Mwezi Januari, mwaka juzi, 2013, nilipiga picha mbali mbali. Baadhi ni picha za tembo zinazoonekana hapa. Nilikuwa naongoza darasa la wanafunzi 29 wa chuo cha St. Olaf, katika kozi ambayo nilikuwa nimeitunga, kumhusu Ernest Hemingway.





Mwandishi Ernest Hemingway aliitembelea hifadhi hii mwaka 1933. Aliandika hayo katika kitabu chake cha Green Hills of Africa ambamo amezitaja na kuzielezea sehemu nyingi za Tanganyika alimopita.

Green Hills of Africa, kwa mtazamo wangu, ni kitabu bora sana, ambacho kiliitangaza nchi yetu vizuri kabisa, kuliko ambavyo sisi wenyewe tumefanya, kuliko tunavyoweza. tunaendekeza uzembe katika lugha na katika nidhamu ya uandishi kama ille ya Hemingway.. 



Kila ninapofika sehemu kama Tarangire, ninamkumbuka Hemingway na maandishi yake, hasa hiki kitabu chake cha Green Hills of Africa. Haiwezekani kujizuia.

Saturday, June 8, 2013

Nimetoka Mbali na Kozi ya Hemingway

Kila siku, nawazia habari za mwandishi Ernest Hemingway. Kila siku nawawazia pia waandishi wengine, kutoka sehemu mbali mbali za dunia.

Hakuna siku inayopita nisisome angalau kurasa kadhaa za maandishi yao, au uchambuzi wa maandishi hayo. Kwa hilo, naweza kusema Hemingway ndiye anayetawala mawazo yangu kila siku.

Nilifanya utafiti na tafakari ya miaka kama sita hivi, kabla sijaunda kozi ya "Hemingway in East Africa." Kozi hii imeniwezesha kuzifahamu sehemu nyingi za Tanzania kaskazini, na  kufahamiana na watu wengi katika sehemu hizo.

Cha zaidi ni kuwa nimefahamiana na wanafunzi wengi wa ki-Marekani, waliokuja Tanzania kwenye kozi hiyo. Katika picha hapa kushoto, ambayo ilipigwa na Profesa Bill Davis wa chuo cha Colorado, ninaonekana nikitoa mhadhara juu ya Hemingway. Wanafunzi walikuwa kutoka chuo hicho. Huo ulikuwa ni mwaka 2008. Mara ya kwanza kufundisha kozi hiyo ilikuwa ni mwaka 2007, na wanafunzi walitoka chuo hicho hicho. Hapo ni katika viwanja vya chuo cha MSTCDC kilichopo eneo la Usa River, Arusha.

Saturday, June 1, 2013

Mama wa Mwanafunzi wa Kozi ya Hemingway Kanitembelea

Leo nimepata bahati ya kuonana na mama wa mwanafunzi mojawapo wa kozi ya Hemingway, ambayo niliifundisha Tanzania mwezi Januari. Mama huyu, mtoto wake, na mimi tunaonekana pichani hapa kushoto.

Mama kaja kutoka kwao Connecticut kujumuika na wahitimu wenzake wa chuo cha St. Olaf. Ni utaratibu wanaouita "reunion." Wanakuwepo chuoni kwa siku mbili tatu, wakiongelea masuala mbali mbali, pamoja na kujikumbusha miaka waliyosoma hapa. Laiti tungekuwa na utamaduni huu Tanzania.

Mama huyu alikuwa ameleta taarifa kabla, kupitia kwa mtoto wake, kwamba atapenda tuonane. Alisema ana nakala za kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, ambazo alitaka nizisaini. Ndivyo ilivyokuwa leo. Tulikutana, akanielezea jinsi mwanae alivyofaidi na kufurahia kozi ya Hemingway na fursa ya kuwepo Tanzania. Kisha ilisaini nakala zake tatu za hicho kitabu.

Kitabu hiki ni kati ya vile ambavyo wanafunzi walitakiwa kusoma kwa maandalizi ya safari ya Tanzania. Nimeshakutana na wazazi wengine ambao wamekisoma pia, na wanaponiona wanakizungumzia.

Mama huyu alishaniandikia barua kunishukuru kwa kufundisha kozi ya Hemingway, nami niliandika taarifa hii hapa. Maoni ya aina hii nimekuwa nikiyapata kutoka kwa wazazi wengine. Yananigusa sana na kunihamasisha nijibidishe zaidi katika kutekeleza wajibu wangu wa mwalimu na mlezi wa hao vijana. Mungu kanibariki kwa kunipa uwezo, nami nawajibika kutumia vipaji hivyo kwa faida ya walimwengu.

Saturday, May 18, 2013

Ziara Namanga, Januari 26

Katika mizunguko yangu na wanafunzi nchini Tanzania mwezi Januari tukisoma na kujadili maandishi ya Ernest Hemingway, tulifanya ziara ya mji wa Namanga tarehe 26. Mji huo uko mpakani baina ya Kenya na Tanzania.

Hemingway na msafara wake walipita hapa, tarehe 20 Desemba, 1933, wakitokea Kenya, wakaingia Tanganyika. Katika vitabu vya watu kama Carlos Baker na Michael Reynolds kuna masimulizi ya jinsi wasafiri hao walivyopita hapa. Hemingway na wenzake hawakukaa Namanga. Walikamilisha tu taratibu za uhamiaji na forodha, wakaelekea Arusha.

Katika kuandaa kozi yangu, niliona ni muhimu nikawafikishe wanafunzi Namanga. Ingekuwa tuna muda, tungeenda hadi Kenya na kuzunguka sehemu ambamo Hemingway alipita, kabla ya kuja Tanganyika.

Kwangu kama mtafiti, nina masuala ya kuyafanyia kazi. Kwa mfano, je, kuna picha za Namanga za wakati ule Hemingway alipopita hapa? Je, ofisi ya forodha na uhamiaji ilikuwaje siku zile? Kuna hifadhi yoyote ambayo ina taarifa za kupita kwa msafara wa Hemingway hapa mpakani?

Pamoja na maandishi ya hao akina Baker, Reynolds, na wengine, labda Hemingway mwenyewe aliandika kuhusu tukio la kuingia Tanganyika. Hatujui. Labda uchapishaji wa barua zote za Hemingway unaoendelea utasaidia, endapo itapatikana barua ya aina hiyo. Kwa sasa hatuwezi kujua, isipokuwa ni faraja kujua kuwa Hemingway alikuwa mwandishi wa barua wa aina yake, aliyeandika maelfu ya barua.


Saturday, March 30, 2013

Wa-Marekani Watua kwa Mama Lishe, Usa River

Mwezi Januari mwaka huu, nilipokuwa Tanzania nikifundisha kozi ya Hemingway, niliandaa fursa mbali mbali za kuwawezesha wanafunzi, ambao ni wa-Marekani, kushiriki katika utamaduni wa wa-Tanzania, ili kujifunza. Tulikuwa tumefikia Colobus Mountain Lodge, iliyomo pembeni mwa Arusha National Park. Siku moja, mara tu baada ya wanafunzi hao kuwasili nchini niliwapeleka kwenye mji mdogo wa Usa River, ili wakazunguke na kujionea. Niliamua kuwasafirisha katika dala dala, tukiwa tumebanana. Usafiri ule ulikuwa kitu kipya kabisa kwao, lakini niliona ni muhimu kwao, wajifunze. Tulifika Usa River, tukazunguka mitaa kadhaa, na kisha tukasogea tena pembeni mwa barabara kuu. Hapo wanafunzi walimwona mama lishe akiwa kazini, wakapanga foleni kujipatia chipsi mayai.



Kwao hili lilikuwa jambo jipya, ila walifurahia hicho chakula. Niliridhika sana kwamba wanafunzi walipata fursa hiyo ya kujionea na kufaidi huduma ya mama lishe, kwani ni sehemu muhimu katika utamaduni wa Tanzania ya leo.











Wanafunzi walikuwa wengi zaidi ya hao wanaoonekana pichani. Mama lishe alifanya kazi kubwa ya kuwahudumia. Wala hiyo haikuwa mara yao ya mwisho kuja hapa. Walifika tena, na kama tungekaa siku nyingi eneo hili la Usa River, wangefika tena na tena.

Kwa vile wengi wanaosoma blogu hii ni wa-Tanzania, naomba tukumbushane tu kuwa mbali ya elimu inayotokana na safari za aina hii, kwa wageni na wenyeji, na mbali na fedha nyingi inayoingia katika hazina ya nchi, shughuli hizi za kuwapeleka wanafunzi Tanzania ni zinachangia kipato cha watu wa kawaida, kama vile mama lishe, dobi, mwenye nyumba ya kulala wageni, na muuza ndizi sokoni. Safari hii, hata vinyozi nao walijipatia biashara.

Friday, December 21, 2012

Habari Njema: Kitabu cha "Hemingway and Africa" Kimefika

Leo nina furaha sana. Kisa? Kitabu nilichoagiza, Hemingway and Africa, kimefika leo.

Kila ninapojipatia kitabu kipya ninafurahi. Ukizingatia kuwa hadi sasa nina vitabu zaidi ya elfu tatu, utaona kuwa nimekuwa mwenye furaha, tena na tena. Huenda nitaishi miaka kadhaa ya ziada kutokana na hiyo furaha.

Pamoja na hayo yote, hiki kitabu cha Hemingway and Africa ni cha pekee. Mwanzo kukiona ni pale nilipokiazima kutoka maktaba ya Chuo Kikuu cha Minnesota, nikakisoma. Kilinigusa kwa namna ya pekee, kwa jinsi kilivyosheheni taarifa na uchambuzi mpya, nikaamua lazima niwe na nakala.

Kama unavyoniona pichani, nimekishika kitabu hiki nikiwa nimefurahi sawa na mtu aliyejishindia kreti ya bia. Ninataja bia kwa makusudi. Kitabu hiki, chenye kurasa 398, bei yake ni dola 80 ambayo kwa madafu ni zaidi ya 120,000. Ukienda baa na hela hizo, unapata kreti mbili za bia, kuku mzima, na nauli ya teksi ya kukurudisha kwenu Mbagala. Kama wewe si mtu wa baa, hizo hela ni mchango tosha wa sherehe kama vile "send-off."

Sasa inakuwaje Krismasi yote hii mtu ufurahie kitabu cha bei mbaya, badala ya kujichana na bia? Ukweli ni kwamba kila mtu ana udhaifu wake. Udhaifu wangu mojawapo ni kuvipenda sana vitabu.

Kuhusu mwandishi Hemingway, ni kwamba kwa miaka na miaka nimekuwa msomaji na shabiki mkubwa wa maandishi yake: kuanzia riwaya na hadithi fupi, hadi insha na barua. Nayapenda kwa namna ya pekee maandishi yake yanayohusu uhusiano wake na Afrika, kwani alitembelea na kuishi miezi mingi Afrika Mashariki, hasa Kenya na Tanganyika. Aliandika kuhusu mazingira ya nchi hizo, kuhusu watu na tamaduni zao, na kuhusu wanyama katika mbuga za hifadhi, kwa kiwango cha ustadi ambacho sisi wenyewe hatujakifikia. Alituachia hazina kubwa katika maandishi yake, hazina ambayo hatujafunguka macho na kuitumia.

Saturday, December 8, 2012

Simba wa Tsavo

Leo napenda kuongelea habari ya simba wa Tsavo. Ni habari iliyokuwa inatusisimua sana tulipokuwa shuleni, baina ya darasa la tano na la nane. Kulikuwa na kitabu, Simba wa Tsavo, ambacho kilichapishwa mwaka 1966. Ni tafsiri ya kitabu cha J.H. Patterson kilichoitwa The Man Eaters of Tsavo.

Kitabu hiki kilielezea matukio ya kutisha wakati ujenzi wa daraja la reli kwenye mto Tsavo, nchini Kenya, miaka mia na kitu iliyopita. Kilielezea namna simba walivyokuwa wakiwavizia, kuwadaka na kuwaua wafanya kazi kwenye eneo la hili daraja wakawaua watu zaidi ya mia, hadi, hatimaye, Patterson alipofanikiwa kuwaua, mwezi Desemba 1898. Hiyo ndio habari tuliyosoma tukiwa shuleni, miaka hiyo ya sitini na kitu.

Lakini, kwa miaka hii ya karibuni, yapata miaka kumi, nimekutana na taarifa nyingine nyingi kuhusu simba wa Tsavo. Je, unajua wale simba waliishia wapi? Katika kusoma habari za mwandishi Ernest Hemingway, ambaye alizaliwa mwaka 1899 eneo la jirani na Chicago, nimegundua kuwa alipokuwa mtoto alipelekwa na baba yake katika hifadhi ya Field Museum of Natural History mjini Chicago. Hapo alipata kuziona maiti za wanyama mbali mbali kutoka Afrika ambazo zilikuwa zimehifadhiwa kitaalam ili zionekane kama vile ni wanyama hai.

Kati ya wanyama hao ni wale simba wa Tsavo, ambao picha yao inaonekana hapa juu. Habari hii ilinishtua sana, kwani sikujua kabisa kuwa simba wa Tsavo wamehifadhiwa na kwamba wako Chicago. Hiyo ni faida ya wazi ya kusoma vitabu, kwamba mtu unagundua mambo ambayo hukuyajua. Pamoja na kuangalia wanyama hao waliohifadhiwa, mtoto Hemingway alisoma kitabu cha The Man Eaters of Tsavo. Hayo yote yalichangia katika kumjengea Hemingway mapenzi makubwa aliyokuwa nayo juu ya Afrika kwa maisha yake yote.

Mwaka 1933, Hemingway na mke wake Pauline walifunga safari wakitokea Ulaya, wakaja Afrika Mashariki. Walishuka meli Mombasa, wakapanda treni kuelekea Nairobi. Walipita Tsavo, wakaenda hadi Machakos, kisha Tanganyika. Kuhusu safari yake ya Tanganyika, Hemingway aliandika kitabu maarufu kiitwacho Green Hills of Africa, ambacho ni kimoja ya vitabu vyake ambavyo nimevisoma na kuwafundisha wanafunzi.

Wednesday, December 5, 2012

Barua za Ernest Hemingway, 1907-1922

Leo nimekipata kitabu cha barua za Hemingway ambacho nilikitaja katika blogu hii siku chache zilizopita. Kama nilivyoandika, nilikiona kwa mara ya kwanza katika duka la vitabu hapa Chuoni St. Olaf. Lakini nakala ile ilinunuliwa hima, ikabidi niagize.

Hemingway alikuwa mwandishi makini wa barua. Hata mwanae, Mzee Patrick Hemingway, amethibitisha hivyo. Kwa ujumla, Hemingway hakutaka wala kutarajia kuwa barua zake zichapishwe. Alikuwa na mazoea ya kuandika barua zake kwa uwazi na hata kutumia lugha ambayo inaonekana kali au yenye kukiuka maadili.

Baada ya Hemingway kufariki, mwaka 1961, suala la kuchapisha au kutochapisha maandishi ya Hemingway ambayo alikuwa hajayachapisha lilijitokeza na kuwa kubwa. Maandishi yake mengine alikuwa hajamaliza kuyarekebisha. Barua zake alikuwa hajaazimia zichapishwe. Suala likawa nini kifanyike.

Wasomaji wa maandishi ya Hemingway walisukumwa na kiu ya kutaka kusoma maandishi yake yote. Wahariri na watafiti walitaka hivyo pia. Familia yake ilikuwa katika mtihani mgumu. Lakini hatimaye, iliamuliwa kuwa bora kuchapisha maandishi hayo, hata barua zake. Ndivyo tulivyovipata vitabu vya Hemingway kama vile The Garden of Eden, Islands in the Stream, A Moveable Feast, na Under Kilimanjaro. Ni matokeo ya maamuzi magumu, na juhudi za wahariri kuhariri miswada aliyoicha Hemingway ikiwa haijakamilika, wakiongozwa na wazo kwamba bila shaka Hemingway mwenyewe angeafiki uhariri huo.

Tunaposoma vitabu hivi bado tunajiuliza iwapo kama Hemingway angeishi zaidi, angerekebisha vipi maandishi haya, hasa ikizingatiwa kuwa alikuwa mwandishi mwenye nidhamu ya hali isiyo ya kawaida katika kusahihisha na kuboresha maandishi yake. Alitaka kila neno liwe mahali pake na liwe kweli ni neno hilo, si jingine, na kila sentensi iwe imekamilika kwa kiwango cha juu kabisa.

Leo nilitaka nikumbushie pia kitabu cha barua za Shaaban Robert, ambacho niliandika habari zake katika blogu hii. Nilitaka nivijadili vitabu hivi vya barua kwa pamoja, kuelezea umuhimu wa vitabu vya aina hii, ambamo tunapata kuwafahamu waandishi hao maarufu kupitia njia ya barua walizoandika. Barua hizi ni kioo muhimu cha kutuwezesha kuyafahamu mambo ambayo pengine hatungeyafahamu kwa kuangalia tu vitabu vyao vingine. Nangojea nipate wasaa wa kuandika na kuzihusianisha barua za Hemingway na zile za Shaaban Robert.

Saturday, December 1, 2012

Mwandishi Hemingway: Vitabu Vipya

Ernest Hemingway ni kati ya waandishi maarufu kabisa duniani. Alizaliwa mwaka 1899 karibu na mji wa Chicago, akafa kwa kujipiga risasi nyumbani kwake kwenye jimbo la Idaho mwaka 1961. Katika maisha yake, aliandika sana, akianzia kama ripota wa gazeti la Kansas City Star. Maandishi yake ni pamoja na riwaya, hadithi fupi, insha, masimulizi ya safari zake, barua magazetini, mashairi, na maelfu ya barua. Tangu wakati wa uhai wake hadi leo, watu wengi sana wamechambua maandishi yake na kuelezea maisha yake.


Vitabu kumhusu Hemingway vinaendelea kuchapishwa. Miezi ya karibuni, vimechapishwa vitabu kama Hemingway and Africa, Hemingway's Boat, na The Letters of Ernest Hemingway: Volume 1,1907-1922.

Kitabu cha The Letters of Ernest Hemingway: Volume 1, 1907-1922 nilikiona kwa mara ya kwanza miezi michache iliyopita katika duka la vitabu la Chuo cha St. Olaf. Ni kitabu muhimu sana kwa jinsi kinavyojumlisha kila barua ya Hemingway inayojulikana kwa kipindi cha miaka iliyotajwa. Ninapangia kujipatia nakala.

Ninayo nakala ya kitabu cha mwanzo cha barua za Hemingway, kiitwacho Ernest Hemingway: Selected Letters: 1917-1961. Lakini hiki cha sasa kinafunika kila kitu. Ni juzuu la kwanza, na inategemewa kwamba kutachapishwa majuzuu mengine, hadi kukamilisha maisha yote ya Hemingway.

Wakati wa maonesho ya vitabu yaliyofanyika wiki chache zilizopita mjini Minneapolis, mzee mmoja alifika kwenye meza yangu, na katika mazungumzo yetu nilimtaja Hemingway. Hapo hapo mzee akaniuliza kama nimeshasoma Hemingway's Boat.

Niligutuka kuona mzee huyu keshasoma kitabu hiki ambacho kimetoka karibuni tu. Lakini papo hapo nikakumbuka kuwa hapa ni Marekani, sio Tanzania. Usomaji wa vitabu hapa ni jambo la kawaida kabisa. Nilimwambia kuwa kitabu hicho nimekiona katika duka la vitabu Chuoni St. Olaf, na kwamba nimekiangalia angalia, ila sijakisoma. Hata hivi, tuliendelea na mazungumzo kuhusu mambo ya aina hiyo.

Kitabu cha Hemingway and Africa nilikiazima kutoka maktaba ya Chuo Kikuu cha Minnesota nikakisoma. Niko njiani kujipatia nakala. Hiki ni kimoja kati ya vitabu muhimu sana vinavyochambua uhusiano wa Hemingway na Afrika. 

Najihesabu kama mmoja wa wapenzi na wafuatiliaji wakubwa wa Hemingway. Nimefanya na naendelea kufanya utafiti juu yake na maandishi yake, hasa uhusiano wake na Afrika. Imekuwa ni furaha kwangu kuwapeleka wanafunzi Tanzania, kwa somo hilo.

Saturday, April 2, 2011

Kitabu Kumhusu Hemingway

Leo nilipita tena katika duka la vitabu la Half Price Books la mjini Apple Valley. Kama kawaida, kutokana na ushabiki wangu wa maandishi ya Ernest Hemingway, nilianza kwa kwenda moja kwa moja kwenye sehemu vinapouzwa vitabu vyake: vile alivyoandika yeye mwenyewe au vilivyoandikwa juu yake.

Hadi sasa nina vitabu vingi vya Hemingway, lakini kila ninapoona kitabu kipya, au ambacho sina, napenda niwe nacho. Leo nimevikuta vitabu kadhaa vya aina hiyo, ila nilivutiwa zaidi ni Hemingway in Cuba, kilichoandikwa na Norberto Fuentes.

Sikuwa nimekiona kitabu hiki kabla. Nilikiangalia, nikaona kina utangulizi ulioandikwa na Gabriel Garcia Marquez. Hapo niliishiwa nguvu, kwani Marquez ni mmoja wa waandishi maarufu kabisa duniani.

Mawazo mengine yakafurika akilini mwangu. Ninajua kuwa Marquez ni rafiki mkubwa wa Fidel Castro, Castro ambaye watu wa kizazi changu tumemwenzi tangu tulipopata Uhuru. Najua pia kuwa Castro ni mshabiki wa maandishi ya Marquez. Cha zaidi ni kuwa najua kuwa Hemingway katika uhai wake alifahamiana na Castro, na pia kuwa Castro amekuwa shabiki wa Hemingway tangu miaka ile.

Pamoja na yote hayo, katika kusoma utangulizi wa Marquez, nimevutiwa kwa namna ya pekee na maelezo yake kuwa Hemingway ni mwandishi ambaye Castro anamsoma kuliko mwandishi mwingine yeyote. Hata anapozunguka nchini kwenye safari rasmi, Castro anakuwa na maandishi ya Hemingway. Marquez anatueleza kuwa Castro anaweza kuelezea maandishi ya Hemingway na kujibu masuali kwa uhodari wa kiwango cha juu.

Mimi kama shabiki mkubwa wa Hemingway najiandaa kukisoma kitabu hiki. Nimekipitia juu juu, nikaona kina mengi mapya kwangu, ingawa kilichapishwa mwaka 1984. Nina vitabu vingine vinavyoelezea maisha ya Hemingway Cuba, lakini hiki cha Fuentes kinazama zaidi katika maelezo yake.

Kwa wale ambao hawajui, Hemingway, ambaye ni m-Marekani aliyezaliwa mwaka 1899 karibu na Chicago, aliishi Cuba miaka 22. Hata alivyosafiri kuja Afrika Mashariki, mwaka 1933 na mwaka 1953, alitokea Cuba, na baada ya safari zake alirejea Cuba. Kuna vitu kadhaa alivyovipata Kenya na Tanganyika, kama vile vichwa vya wanyama aliowawinda, mikuki, na kinyago cha ki-Makonde. Vyote viko katika nyumba yake ya Finca Vigia, ambayo iko nje ya mji wa Havana, ambayo serikali ya Cuba inaihifadhi kwa heshima kubwa na vitu vyote vya Hemingway vilivyokuwamo humo, ingawa yeye alishaondoka na kurejea Marekani, ambako alijiua kwa bunduki mwaka 1961.

Cuba inamwenzi Hemingway kwa namna ambayo ingepaswa sisi wa-Tanzania tuwe tunawaenzi waandishi wetu kama vile Mgeni bin Faqihi wa Bagamoyo, aliyetunga Utendi wa Rasi l'Ghuli, au Shaaban Robert.

Thursday, February 3, 2011

Mji wa Moshi, Tanzania

Moshi ni mji maarufu kaskazini mwa Tanzania, chini ya Mlima Kilimanjaro. Siufahamu sana mji huu, ingawa nimepita hapo mara kadhaa, na hata kulala, mara mbili tatu.






Kama ilivyo katika miji mikubwa ya Tanzania, Moshi kuna hoteli nzuri za kufikia wageni. Wakati moja nililala katika hoteli hii hapa kushoto.









Moshi ni maarufu kwa usafi. Wa-Tanzania wanajua kuwa uongozi wa Moshi una sheria kali kuhusu usafi. Hapo kushoto nipo kituo cha mabasi, pasafi kama vile pamepigwa deki. Nilikuwa safarini baina ya Arusha na Dar es Salaam. Nimechoka, shaghalabaghala; msafiri kafiri na kitabu changu cha Under Kilimanjaro.

Tangu mara yangu ya kwanza kuingia mjini Moshi, nilivutiwa na msikiti unaoonekana kushoto, ambao uko pembeni mwa kituo cha mabasi.







Wakati mmoja nilikuwa Moshi na wanafunzi kutoka Chuo cha Colorado, niliowaleta nchini kuwafundisha kuhusu mwandishi Ernest Hemingway alivyosafiri nchini mwetu akaandika juu yake. Niliwapeleka hadi Chuo cha Mweka, kinachoonekana kushoto. Kiko nje kidogo ya mji.

Ninapokuwa katika mji wowote napenda kujua maktaba ilipo. Hapo kushoto ni maktaba ya mkoa. Niliingia ndani, nikaona ilivyo nadhifu. Ina majarida na vitabu kiasi cha kuridhisha, nikifananisha na maktaba nilizoziona mikoani Tanzania. Nilivutiwa kuwaona watu wakisoma, sio watoto wa shule tu, kama ilivyo kwenye maktaba zingine.

Nilitembea kutoka Lutheran Uhuru Hostel kuelekea barabara kuu itokayo Arusha, nikaiona hoteli hii inayoonekana kushoto. Nilivutiwa na tangazo la mchemsho, ingawa sikupata kuingia ndani. Hamu ya kuingia nilikuwa nayo, kwa mategemeo ya kupata chakula cha ki-Chagga. Ni suala muhimu la kuzingatiwa siku za usoni, panapo majaliwa.

Friday, December 10, 2010

Laiti Ningekuwa Kama Hemingway

Laiti ningekuwa kama Hemingway, mwandishi maarufu sana duniani. Ningeandika kuhusu nchi yangu na watu wake kwa umakini, ubunifu, na ukweli wa kumgusa kila msomaji. Ningeandika kuhusu maziwa, mito, milima na mabonde. Ningeandika kuhusu fukwe, nyanda na visiwa. Ningeandika kuhusu miji na vijiji, mitaa na vitongoji.

Nimetamka hayo, na nimeanza kufanya mazoezi. Lakini bado njia ni ndefu mbele yangu.

Laiti ningekuwa kama Hemingway, aliyeangalia mazingira, matukio, na tabia za wanadamu kwa macho na akili yote, aliyejawa nidhamu ya kutumia lugha, akiangalia kila neno, tena na tena, akibadili na kusahihisha tena na tena, akitafuta namna ya kuandika sentensi sahihi yenye ukweli mtupu.

Laiti ningekuwa kama Hemingway, aliyetufundisha kuwa kazi ya mwandishi ni kujitoa mhanga ili nafsi yake yote ibakie katika kitabu tu, asibakishe hata chembe nje ya kitabu. Kila kitabu kiwe ni mauti ya mwandishi, vinginevyo kitabu hiki ni mzaha na udanganyifu. Je, nitayaweza hayo?

Hemingway aliandika kuhusu nchi mbali mbali alizozitembelea, ikiwemo nchi yangu. Nimekutana na watu wa nchi mbali mbali wanaomshukuru Hemingway kwa hilo. Tutalipaje fadhila, isipokuwa kwa kujijengea nidhamu ya kuyaangalia mazingira na maisha, nidhamu ya kuiheshimu lugha na sentensi, tuweze nasi kuandika mambo ya thamani? Tutalipaje fadhila kama hatuna ushujaa wa kuwa wakweli kama Hemingway?

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...