Kitabu cha Barua za Shaaban Robert ni mkusanyiko wa barua alizoandika Shaaban Robert kwa mdogo wake Yusuf Ulenge baina ya mwaka 1931 na 1958. Yusuf Ulenge alifanya busara ya kuzihifadhi na sasa zimechapishwa kama kitabu, na Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Mhariri Profesa Mugyabuso Mulokozi amefanya kazi kubwa na watafiti wenzake katika kuzichapisha na kuziwekea maelezo.
Nilikinunua kitabu cha Barua za Shaaban Robert mwaka 2008 katika duka la Taasisi. Nilifurahi na pia kushtuka kugundua kuwa Yusuf Ulenge alikuwa mdogo wa Shaaban Robert. Jina la Yusuf Ulenge nililifahamu tangu kwenye mwaka 1964, nilipokuwa darasa la sita. Nilinunua kitabu kiitwacho Nguzo ya Maji na Hadithi Nyingine, kilichotungwa na Yusuf Ulenge. Miaka yote sikuwa na wazo hata kidogo kuwa huyu alikuwa mdogo wa Shaaban Robert.
Sasa, hizi barua zimenifungua macho kabisa, kwani nimejionea jinsi uhusiano wa hao ndugu wawili ulivyokuwa mkubwa na jinsi Yusuf Ulenge naye alivyokuwa mwandishi mahiri. Katika kitabu hiki kuna taarifa za maandishi mengi ya Yusuf Ulenge, vikiwemo vitabu alivyochapisha na vingine alivyopangia kuchapisha. Mzee Yusuf Ulenge alifariki tarehe 16 Desemba, 2002.
Shaaban Robert ni mfano wa mlezi bora, kwa jinsi alivyokuwa anamshauri na kumwongoza mdogo wake Yusuf katika masuala mbali mbali ya maisha, kama vile elimu. Siwezi kuelezea kwa ufasaha jinsi Shaaban Robert alivyothamini elimu na maadili mema, akawa anamwongoza Yusuf katika njia hiyo. Shaaban Robert alikuwa tayari kutoa gharama zozote zilizohitajika kumlipia Yusuf katika masomo yake, kuanzia daftari hadi usafiri. Ni mfano mzuri sana kwetu wazazi na walezi wa watoto.
Kitabu hiki kinaelimisha sana. Kinautikisa kabisa moyo wangu kwa undani na uzito wa maudhui yake. Kitabu hiki kinafaa kuwemo katika kila nyumba ya wa-Tanzania, ili kisomwe na wazazi na watoto. Hakuna kisingizio cha kutokuwa na kitabu kama hiki, na vitabu vingine vya Shaaban Robert, ambaye ndiye gwiji wa uandishi wa ki-Swahili, mwanafalsafa na mwalimu wa jamii. Hayo nimeyaelezea katika kitabu cha CHANGAMOTO: Insha za Jamii, uk. 30-41
Ingekuwa ni hapa Marekani, tukio la kuchapishwa kitabu kama hiki lingekuwa na kishindo, na watu wangepanga foleni kwenye maduka ya vitabu kukinunua. Kingezungumziwa magazetini na vyombo vingine vya habari. Wa-Tanzania tunapaswa kujiuliza iweje hatuna utamaduni wa aina hiyo. Iweje hatuna hata habari wala hamu ya kujua mwandishi kama Shaaban Robert alizaliwa wapi na aliishi wapi na mchango wake katika jamii na ulimwengu ni upi. Tuko wa-Tanzania yapata milioni arobaini. Ni nyumba ipi katika Tanzania, kuanzia nyumba za walalahoi hadi za hao tunaowaita viongozi, yenye vitabu vya mwandishi muhimu kama huyu?
Kwenye mtandao wa Facebook kuna ukumbi wa wadau na wapenzi wa Shaaban Robert, uitwao Ukumbusho wa Shaaban Robert. Walioanzisha ukumbi huu si wa-Tanzania, bali wa-Kenya. Hii ndio hali halisi, kwamba nabii hakosi heshima, isipokuwa katika nchi yake. Kuthibitisha zaidi jambo hili, jionee jinsi mwanafunzi m-Marekani alivyokichangamkia kitabu hiki cha Barua za Shaaban Robert, akakiandikia uchambuzi huu hapa.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault
Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...
-
Leo ni kumbukumbu ya siku ya kuzaliwa kwangu, ambayo ni tarehe 17 Agosti, 1951. Familia yangu, ndugu, na marafiki wamejumuika nami kushereh...
-
Leo napenda kukitambulisha kwako mdau kitabu muhimu cha ki-Swahili, Tenzi Tatu za Kale . Nilinunua nakala yangu miaka kadhaa iliyopita katik...
-
Kutafsiri kazi ya fasihi ni kazi ngumu ya kuchemsha bongo. Inahitaji ufahamu wa hali ya juu wa lugha husika, na pia hisia makini za kifasih...
5 comments:
Nami nitakwenda duka la vitabu la pale Taasisi ya Taaluma za Kiswahili ili nijipatie nakala ya kitabu hicho.
Lakini huwa najiuliza kila siku, kwa nini isianzishwe tuzo ya umahahiri ya Shaaban Robert? Ingependeza kila mwaka kungekuwa na tuzo kwa waandishi wa Kiswahili. Hii ingependeza sana ili kuzidi kuenzi kazi zake na pia kuchochea wanaandishi kufanya vema zaidi.
Shukrani kwa kutembelea hapa kijiweni pangu. Kwanza, natoa hongera kwa kitabu chako ulichotangaza kuwa kiko jikoni.
Hicho kitabu cha Barua za Shaaban Robert kina mengi sana. Unaona jinsi mtu huyu alivyozingatia mambo mema maishani. Kitabu hiki kingefaa sana iwapo kingekuwa kinatumika katika malezi ya watoto wetu na kuhimiza maadili katika jamii kwa ujumla.
Shukran kwa kazi yako ya kutujulisha kuhusu kitabu chenyewe. Mimi hapa ni Mkenya niliyeanzisha ukumbi wa Ukumbusho wa Shabaan Roberts kwenye Facebook. Nilichochewa sana kufanya hivyo na tovuti moja ya Kitanzania iliyoandika hivi: SHAABAN ROBERTS: THE TANGA'S FORGOTTEN HERO. Jambo hili lilinikera sana na kuamua kuanzisha ukumbi kama ukumbusho wa bingwa huyu.
Si vema kuona bingwa kiasi hicho akisahaulika ila wengine kama waigizaji, waimbaji na wanasiasa wanapigiwa debe bila kuchangia hata kidogo katika kuikuza lugha yetu teule.
Iwapo kuna njia ya kukipata (kitabu hicho ulichozungumzia) hapa Kenya, usikose kutujulisha. Vitabu vingine vyake vyauzwa huku ila hicho sijakiona.
Hakika nnajivunia kuona maandishi yenye mvuto na kuweza kunivutia kutaka kujua zaidi lugha yetu adhimu ya kiswahili naamini ntafanya niwezalo kufika hapo dukani kujipatia nakala yangu....
Wilayani Mpwapwa Mkoa wa Dodoma alifanya kazi kama karani Ofisi ya kutunza wanyama.Ofisi aliyofanyia kazi ipo na nyumba alivyokuwa akiishi marehemu Shaaban Robert ipo.Nashauri kuwe na tuzo ya juu ya kiswahili kuanzia shule ya msingi mpaka Vyuo vikuu.
Post a Comment