Saturday, December 17, 2011

Wanafunzi Wangu Wameondoka Tanzania

Mapema leo, wanafunzi niliowaleta Tanzania mwaka huu wameondoka nchini, baada ya kumaliza masomo ya miezi kadhaa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam. Wanafunzi hao nami tunaonekana katika picha hapa kushoto, tuliyopiga kwenye hoteli ya Wilolesi, mjini Iringa, tarehe 10 Agosti.

Kama nilivyoelezea mara kadhaa katika blogu zangu, tulizunguka sehemu mbali mbali, kama vile Kalenga, Matema Beach, Lyulilo na Bagamoyo. Baada ya mizunguko hiyo niliwafikisha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, nami nikarejea Marekani kwani muhula wa masomo ulikuwa unaanza.

Ni faraja kuona wameondoka salama, kwani nilikuwa na wasi wasi kutokana na taarifa za migomo, vurugu na mabomu Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Kwa miaka yote niliyofundisha hapa Marekani nimekuwa mshauri katika programu kadhaa zinazopeleka wanafunzi Tanzania na nchi zingine za Afrika, kama nilivoelezea hapa. Huwa tunawaambia hao wanafunzi kuwa wasishiriki maandamano au migomo katika nchi husika. Kwa upande wa Tanzania, nimekuwa mwepesi kuwaeleza jinsi tulivyo nchi ya amani na utulivu.

Programu hizi zina manufaa mengi sio tu kwa hao wanafunzi, bali kwa wa-Tanzania humo mitaani. Kwa upande wa mahusiano baina ya nchi na nchi, programu hizi zinachangia maelewano baina ya Tanzania na Marekani. Marekani yenyewe kwa miaka mingi imewapokea na kuwaelimisha wa-Tanzania wengi, na wengi wao sasa ni watu wenye madaraka serikalini, katika taasisi mbali mbali, na katika jamii kwa ujumla. Hata kwa upande wa uchumi, mwanafunzi wa kigeni anayesoma Tanzania analiingizia Taifa hela nyingi za kigeni, kumzidi mtalii mara dufu.

Lazima niseme ukweli na kuelezea duku duku yangu. Kutokana na haya mabomu ya polisi ambayo yamekuwa jambo la kawaida vyuoni na mitaani nchini Tanzania, najiuliza kama inawezekana kuendelea kuipigia debe Tanzania kama nilivyozoea. Jambo la kufariji ni kuwa kwa ujumla, wanafunzi wa ki-Marekani wanaoenda Afrika wanaporudi Marekani wanasema kuwa pamoja na matatizo yote, wanakuwa wamejijengea upendo kwa Bara hili. Hii inatokana na ukarimu wanaoupata miongoni mwa watu vijijini, mitaani na mijini.

2 comments:

Masangu Matondo Nzuzullima (MMN) said...

Kweli. Tofauti za kimazingira na kitamaduni zinaogopesha na mtu unapopeleka wanafunzi Tanzania (au sehemu nyingine yo yote ngeni) mtu unakuwa na wasiwasi kama mambo yote yatakuwa salama.

Uzoefu wangu unaonyesha kwamba mara nyingi wanafunzi hawa wanajenga mapenzi ya kudumu na Tanzania na hata baada ya miaka mingi utawaona bado wanahangaika kutafuta njia za kuendeleza mawasiliano na hata kusaidia watu na familia walizokutana nazo huko. Wengine hata huamua kuhamia huko kabisa na kuepuka mikikimikiki ya maisha ya Marekani. Safi sana!
============>
Nilikuwa napita hapa kusema kwamba nimerejea tena rasmi...

http://matondo.blogspot.com/2011/12/wanablogu-wenzangu-na-wapenzi-wote-wa.html

Mbele said...

Mwalimu Matondo, shukrani kwa ujumbe wako. Ni kweli kabisa, kwamba kuwapeleka hao wanafunzi nje ya Marekani ni jambo linalotia wasi wasi sana, kutokana na hisia na utamaduni wa wa-Marekani inapokuja kwenye masuala ya usalama. Wakipata ugonjwa kidogo tu, wanatishika kwa namna ambayo sisi wa-Swahili tutaona kuwa ni kuzidisha mambo.

Hapo kila watu wanayachukulia mambo kwa msingi wa maisha na utamaduni wao, wala hatuwezi kuwalaumu. Ndio maana, katika programu kama hizi, jambo moja na la msingi ni kuwaelimisha wahusika kuhusu tofauti za tamaduni, wazielewe vizuri iwezekanavyo, ili kuepusha kutoelewana na matatizo.

Ni kweli kuwa mwisho wa yote, hao wa-Marekani huishia kuipenda nchi yetu na Afrika kwa ujumla. Sisi wenye uzoefu na masuala hayo tunawajibika kuwaeleza wa-Tanzania wenzetu, maana wengi hawana fununu ya hayo.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...