Wednesday, June 30, 2010

Darasa Chuo Kikuu Dar es Salaam

Leo nilikwenda Chuo Kikuu Dar es Salaam kuongea na wanafunzi wa shahada ya juu katika ki-Swahili. Profesa Mugyabuso Mulokozi, aliyeketi hapo juu mstari wa mbele kushoto, alikuwa amenialika kuongea na wanafunzi wake hao katika somo la tendi.

Walikuwa wakijadili utendi wa Hamziya, nami nilikaribishwa kuongelea tendi kwa ujumla.
Niliongelea dhana kadhaa zihusuzo tendi, hasa dhana ya ushujaa, nikitoa mifano ya tendi kutoka sehemu mbali mbali za dunia, kama vile Illiad, Gilgamesh, Sundiata, Kalevala, Ozidi, na Liongo. Msimamo wangu kama nilivyoulezea katika maandishi kadhaa, ni kwamba dhana ya ushujaa ndio msingi wa tendi.

Niliwaeleza kuwa tendi zinahitaji kuangaliwa kwa uyakinifu, kwa kuzingatia mabadiliko yake, na jinsi zinavyojitokeza katika sura mbali mbali. Kwa mfano, shujaa katika masimulizi ya utendi fulani anaweza asiwe shujaa katika masimulizi hayo hayo katika jamii tofauti.


Wazo moja ambalo lilionekana kuwasisimua wanafunzi ni mchango wa wanawake katika tendi, suala ambalo nililiongelea kwa kirefu kiasi, nikatoa mifano ya utafiti na uandishi wangu kuhusu suala hili. Mfano moja niliotoa ni utafiti wangu juu ya Gindu Nkima, shujaa katika masimulizi ya wa-Sukuma.

Tuliongelea masuala ya utafiti na maadili yake, nikawahimiza wakafanye utafiti, kwani katika utafiti ndipo tunajifunza mengi ambayo si rahisi kujifunza vitabuni. Niliwaelezea juu ya utafiti wangu pwani ya Kenya, kuhusu tungo za kale za ki-Swahili, hasa Liongo Fumo.

Maongezi haya yalikuwa ni changamoto kwangu, kwa sababu daima nimeongelea masuala haya ya tendi kwa ki-Ingereza, iwe ni kwa maandishi au kwa mihadhara. Niliwahi kuandika makala moja tu kwa ki-Swahili kuhusu tendi, “Ushujaa Katika Ras il Ghuli.”
Kutokana na hali hiyo, mara kadhaa katika mhandara wangu niliwajibika kuuliza tafsiri ya ki-Swahili ya dhana kadhaa za ki-Ingereza. Kwa mfano, nilipowauliza tafsiri ya “destiny,” nilifurahi kuambiwa kuwa tafsiri ni hatima.

Niliulizwa masuali mengi ya kufikirisha, baadhi yakiwa yamejengeka katika falsafa. Suali moja ninalolikumbuka lilikuwa maana ya kifo cha shujaa. Suali hili nililiona lenye upana na kina, kwani dhana ya kifo cha shujaa hujitokeza au kutojitokeza kwa namna mbali mbali katika tendi za tamaduni mbali mbali. Dhana ya kifo cha shujaa imefungamana na falsafa, imani, na hisia za jamii husika.

Tuliongea kwa takriban saa mbili. Tulipiga picha darasani, na baada ya kipindi niliomba tupige picha zingine nje, mbele ya ukumbi wa Nkrumah wa hapo Chuoni.

Tuesday, June 22, 2010

Kitabu cha CHANGAMOTO Kimetua Msoga, Bagamoyo

Tarehe 11 Juni, ndani ya basi kutoka Dar es Salaam kwenda Tanga, alikuja mtu moja akakaa kiti cha pembeni yangu. Kama kawaida yangu, nilikuwa na vitabu mkononi. Kimoja kilikuwa kitabu change kipya cha CHANGAMOTO. Sikujua kuwa wakati nasoma kitabu kingine, huyu jamaa alikuwa amekiangalia hicho cha CHANGAMOTO. Hatimaye aliomba kukiangalia, nami nilimpa.


Baada ya muda aliniambia kuwa amekipenda sana kitabu hiki, akataja mambo kadhaa yaliyomvutia, kwamba ni changamoto. Akauliza kama anaweza kununua kitabu kile. Nilivutiwa na jambo hili, kwani, kwa uzoefu wangu, jambo hili la kununua vitabu ni nadra katika Tanzania. Nilimwambia kuwa anaweza kukichukua. Nilimwambia kuwa nimefarijika na kufurahi kumkuta Mtanzania anayependa vitabu.


Hapo alisimama, akaenda mbele na kufungua begi lake ambalo alikuwa ametundika kwenye sehemu ya kuwekea mizigo. Akarudi na vitabu kadhaa, akanionyesha. Kitabu kimojawapo kilikuwa Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania cha Mwalimu Nyerere. Tena ilikuwa kitabu chenyewe asilia si nakala ya kurudufiwa.


Nilivutiwa sana, nikamwambia kuwa nimeshangaa kuona anacho kitabu hiki cha Mwalimu Nyerere, ambacho naamini hakiwapendezi watawala wa Tanzania, kwa jinsi kinavyowaponda. Nikamwelezea hisia zangu kuwa viongozi wetu hawazipendi fikra za Mwalimu Nyerere kuhusu masuala mbali mbali ya siasa, uchumi, na jamii.


Katika maongezi yetu, tulitambulishana majina pia. NIlimpa namba ya simu yangu. Huyu ndugu aliniambia kuwa anaitwa Gilbert Mahenge, na kuwa alikuwa akifanya shughuli kijijini Msoga. Tuliongelea masuala mengi ya maendeleo Tanzania, tukawa tunasikitikia hali ya umaskini katika nchi yetu yenye ardhi na rasilimali nyingi.


Baada ya siku mbili, nikiwa Tanga, huyu ndugu alinipigia simu. Aliongelea kitabu cha CHANGAMOTO, kuwa kimemfungua macho na kimeandikwa kwa mtiririko mzuri. Akasema ameshamwazimisha rafiki yake asome.


Nimeleta taarifa hii kwa sababu huyu ndiye mtu wa kwanza nchini Tanzania kukinunua na kukisoma kitabu changu. Nimeona niandike habari zake hapa, kwani ameweka historia, vile vile amenigusa kwa kuwa anatofautiana mno na waTanzania wengi, kwenye hili suala la vitabu.

Friday, June 18, 2010

Nashiriki Tamasha la Elimu, Dar es Salaam, Juni 24-25

Tarehe 24 na 25 Juni nitakuwa Diamond Jubilee Hall, Dar es Salaam, nikishiriki tamasha la elimu. Nitakuwa na meza yangu na hapo nitaongea na watu kuhusu masuala ya elimu, utamaduni na kadhalika, na hasa shughuli zangu katika nyanja hizo. Vitabu vyangu vitakuwepo.

Nawakaribisha wote; tuonane, tubadilishane mawazo, na tulumbane. Karibuni sana.

Saturday, June 5, 2010

Warsha Zangu Hazina Posho

Tangu mwaka juzi, nimeendesha warsha Tanzania, kuhusu masuala ya utamaduni, utandawazi, na maendeleo. Nina malengo kadhaa katika kufanya hivyo.

Lengo moja ni kuwapa wa-Tanzania ujuzi ambao ninaendelea kuupata huku ughaibuni, kutokana na kusoma vitabu, kuongea na watu, na kuendesha warsha kuhusu masuala niliyotaja hapo juu. Natambua umuhimu wa kutoa fursa kwa wa-Tanzania kuyaelewa masuala hayo, waweze kujizatiti kwa ushindani wa dunia ya leo. Hakuna msingi bora na imara kuliko elimu.

Lengo la pili la kuendesha warsha hizi Tanzania ni kuleta mwamko mpya katika mfumo na uendeshaji wa warsha. Kwanza, kuna mtindo wa kutegemea wafadhili. Watu wamezoea kuona warsha zikifanyika kwa kutegemea fedha kutoka kwa wafadhili au taasisi fulani. Wahudhuriaji wa warsha wanategemea kulipiwa gharama za ushiriki, pamoja na posho. Vibahasha vya posho ni sehemu ya utamaduni wa warsha katika Tanzania.

Ninapinga utamaduni huu. Sitafuti wafadhili wa kulipia warsha zangu, na warsha zangu hazina posho. Badala yake, wanaohudhuria wanalipia.

Kwa mtazamo wangu, warsha ni fursa ya kujielimisha. Elimu ni mtaji mkubwa, pengine muhimu kuliko mitaji yote. Kama mtu analipia trekta limzalishie mazao shambani, kwa nini asilipie mtaji huu mkubwa kuliko yote, yaani elimu?

Huku Marekani, ninaona utaratibu huu wa kulipia warsha. Mimi mwenyewe nimeshalipia hela nyingi kuhudhuria warsha hizi. Ninajua umuhimu wake. Niligusia kidogo jambo hili katika blogu hii, nilipoongelea suala la kununua vitabu.

Ninanunua pia vitabu na kuvisoma. Kati ya vitabu nilivyonunua hivi karibuni ni Global Literacies. Kwa kusoma vitabu na kuhudhuria warsha, ninajiongezea mtaji wa elimu. Ufanisi wangu kama mtoa mada na mwendesha warsha unaendelea kuongezeka.

Katika kuendesha warsha zangu Tanzania, nataka kujenga utamaduni wa kuthamini elimu. Msimamo huu unanipa wajibu mkubwa. Nawajibika kujielimisha kwa uwezo wangu wote, ili niweze kuwa mwelimishaji bora. Ndio maana ninafanya bidii kuhudhuria warsha, kununua vitabu na kuvisoma, na pia kuendesha warsha. Ninaelimika hata ninapoendesha warsha.

Nawakaribisheni kwenye warsha zangu za mwaka huu:

Juni 12, "Culture, Globalization and Development," Meeting Point Tanga.

Julai 3, "Culture and Globalization," Arusha Community Church.

Julai 10, "Cultural Tourism," Arusha Community Church.

Natarajia kupanga warsha nyingine moja au mbili. Wasiliana nami: info@africonexion.com

Thursday, June 3, 2010

Umuhimu wa Warsha Zangu

Sijui kama kuna jambo ninaloongelea mara nyingi zaidi katika blogu hii kuliko suala la tofauti za tamaduni duniani, athari zake, na umuhimu wa kuzielewa. Ni suala muhimu sana, hasa katika dunia hii ya utandawazi.

Nimekuwa nikiendesha warsha kuhusu masuala haya huku Marekani, na miaka ya karibuni nimeanza kufanya hivyo Tanzania. Masuala haya yanaendelea kufahamika vizuri katika makampuni, mashirika,taasisi, vyuo na jumuia mbali mbali huku Marekani na sehemu zingine za ughaibuni.

Lakini haya si mambo ya ughaibuni tu, na wala pasiwe na mtu akadhani ni mambo ya ughaibuni tu. Ndio maana naendesha warsha Tanzania. Kama kuna asiyeamini hayo, napenda kuleta tangazo la ajira lilitolewa na World Food Program la Umoja wa Mataifa hapa Tanzania, kama lilivyoripotiwa katika blogu ya Michuzi. Bofya hapa.

Kigezo cha ufahamu wa tamaduni tofauti, ufahamu wa namna ya kushughulika na watu wa tamaduni mbali mbali, kimesisitizwa kama sifa mojawapo ambayo mwomba ajira anatakiwa awe nayo. Watu waliohudhuria warsha zangu wanafahamu kuwa hapo ndipo kwenye msisitizo wa warsha zangu. Warsha zangu hazina mbwembwe wala madoido. Ni darasa, kama inavyoonekana hapa, hapa, na hapa.

Nimefurahi kuona tangazo hili la World Food Program, hasa kwa kuwa zimebaki siku chache tu kabla sijasafiri kuelekea Tanzania, ambako nitaendesha tena warsha. Kitu kimoja kinachotajirisha warsha hizi na kuzipa umuhimu wa pekee ni kuwa washiriki wanachangia uzoefu wao katika kuhusiana na watu wa tamaduni mbali mbali, sehemu zao za kazi au katika shughuli zingine. Hapo najifunza mengi, na natambua umuhimu wake. Warsha yangu ya kwanza ni tarehe 12 Juni, mjini Tanga, kama nilivyoeleza hapa.

Kwa taarifa zaidi, wasiliana nami: info@africonexion.com

Tuesday, June 1, 2010

Nataka Kuandika Vitabu Bora Zaidi

Mimi ni mwandishi. Naweza kusema ninaendelea vizuri katika uwanja huo, kwani watu wanavitumia vitabu nilivyoandika, kama vile Africans and Americans, na Matengo Folktales, wakiwemo walimu vyuoni, katika masomo mbali mbali, hasa huku Marekani. Hata kijitabu kidogo cha Notes on Achebe's Things Fall Apart kimewahi kupendekezwa katika Chuo Kikuu cha Cornell, ambacho kinajulikana kwa masomo mengi, likiwemo somo la ki-Ingereza.

Kutokana na mafanikio hayo, ningeweza kusema niendelee kuandika kama ninavyoandika. Lakini mimi nataka kuandika vitabu bora zaidi, na ningependa kila kitabu ninachoandika kiwe bora kuliko vile vilivyotangulia.

Bado kuna fursa ya kufanya vizuri zaidi, na ni wajibu kuitumia fursa hiyo. Ninajua kuwa nikifanya juhudi, nitaandika vitabu bora zaidi. Ingawa naandika ki-Ingereza kiasi cha kuwaridhisha wale tunaowaita wenye lugha yao, na ingawa nakifahamu ki-Ingereza kiasi cha kuweza kuwafundisha hao watu, sijafikia kiwango cha Shakespeare. Kwa nini niridhike? Kuridhika kwa namna hii ni jambo baya. Kilichobaki ni kufanya bidii ili niandike vizuri zaidi.

Ningependa hili liwe somo kwa waandishi chipukizi. Wasiridhike na uandishi wao, bali wajitahidi muda wote kufanya vizuri zaidi.