Saturday, January 31, 2009

Raha ya Kununua Vitabu

Tangu nilipokuwa kijana mdogo, nilipenda kununua na kusoma vitabu. Niliwahi hata kununua vitabu ambavyo vilikuwa vigumu mno kwangu kuvielewa. Nakumbuka, kwa mfano, kitabu kimoja cha falsafa, kilichoandikwa kiIngereza, ambacho nilinunua ila nilipata taabu sana kukisoma. Pamoja na kuwa somo la kiIngereza nilikuwa nalipenda na kuliweza kuliko masomo yote, kitabu hiki kilinishinda kwa wakati ule wa ujana wangu. Lakini nilifurahi kuwa nacho katika maktaba yangu ndogo.

Nilinunua pia vitabu vya kiSwahili. Kwa mfano, nakumbuka vizuri kitabu cha Shaaban Robert, Maisha Yangu. Vile vile, nakumbuka kitabu cha Yusuf Ulenge, Nguzo ya Maji na Hadithi Nyingine. Wakati ule, sikujua kabisa kuwa Yusuf Ulenge alikuwa mdogo wa Shaaban Robert. Hayo nimekuja kujua mwaka 2008, baada ya kununua na kusoma kitabu kiitwacho Barua za Shaaban Robert 1931-1958, kilichochapishwa na Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa mara ya kwanza mwaka 2002. Nimefurahi sana kufahamu kuwa Yusuf Ulenge alikuwa mdogo wa Shaaban Robert, na barua zilizomo katika kitabu hiki ni hazina kubwa kwa yeyote anayemwenzi Shaaban Robert.

Nilipoingia Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kusoma, mwaka 1973, niliendelea na tabia ya kununua vitabu. Nilinunua vitabu vingi sana, kiasi kwamba, wanafunzi wenzangu wakinitembelea bwenini walikuwa wanashangaa uwingi wa vitabu vyangu. Niliendelea hivyo nilivyokuwa masomoni katika chuo kikuu cha Wisconsin-Madison, 1980-86. Kwa miaka sita niliyokaa pale, nilinunua vitabu vingi sana, na nakisia nilitumia yapata dola 2000 kununulia vitabu. Nilikuwa nimepata ufadhili wa shirika la Fulbright, na haikuwa vigumu kwangu kutumia sehemu ya hela hizo kwa kununulia vitabu. Siku moja, nakumbuka, nilitumia dola 100 kununulia seti nzima ya hadithi za Alfu Lela u Lela zilizotafsiriwa kwa kiIngereza na Sir Richard Burton. Niliporudi Tanzania na shehena hiyo ya vitabu, kuendelea kufundisha katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, watu walinishangaa kwa kununua vitabu badala ya gari.

Utamaduni wa kununua na kusoma vitabu ninauona sana hapa Marekani. Ni kawaida watu kwenda kwenye maduka ya vitabu, kuangalia vitabu na kuvinunua. Wanahudhuria sana tamasha za vitabu. Mara nyingi, watu wanapotaka kumpelekea mtu zawadi, wanamnunulia kitabu, awe ni rafiki, ndugu, mzazi, au mchumba. Zawadi ya kitabu inapendwa. Watu wakienda kupumzika kwenye sehemu za mapumziko, kama vile bustani za mijini, aghalabu wanakuwa na kitabu cha kujisomea.

Ninafahamu tabia za Wamarekani kuhusu suala la kununua vitabu na kujisomea. Hapa siongelei wanafunzi, bali raia wa kawaida, wafanyakazi na kadhalika. Ninakutana nao mara kwa mara ninaposhiriki katika maonyesho ya vitabu, au ninapokwenda kutoa mihadhara. Hapa naleta picha chache za matukio haya.


Hapo naonekana nikiwa na mama mmoja kwenye warsha mjini St. Paul, Minnesota. Anaangalia kwa makini vitabu vyangu. Tabia hii inanivutia na pia ndio tabia inayohitajika, kwani kujielimisha ni wajibu wa kila binadamu. Kusoma vitabu ni njia moja ya kujielimisha.















Hapa juu nimesongwa na wataalam mbali mbali katika sekta ya elimu, ambao walikuwa wanahudhuria mkutano kwenye Chuo Kikuu cha Iowa. Nilikuwa hapo na vitabu vyangu. Kama inavyoonekana, tuko katika shughuli nzito ya masuali na majibu.



Hapa niko na akina mama kwenye warsha niliyosaidia kuendesha, kwenye mji wa Grantsburg, Wisconsin. Wanaonekana wakiwa na furaha kwa kuvipata vitabu. Hii hali ya kufurahi kwa sababu ya kupata kitabu ni nadra nchini Tanzania. Hapo kwenye picha, mama moja anaonekana ameshika hela. Bei ya kitabu kimoja ni dola 14. Lakini anaonekana mwenye furaha. Ninapokuwa Tanzania, nikiwaambia watu kuwa bei ya kitabu changu ni dola 14, wanastuka na wengi wanaishia hapo. Wako wanaoomba wapunguziwe bei, na wako wanaoomba wapewe bure. Sio kila anayeomba kupunguziwa bei au kupewa kitabu cha bure ana tatizo la hela. Watanzania wengi wana hela sana. Hela wanazonunulia bia, kwa mfano, ni nyingi sana, kila wiki. Msimamo wangu ni kuwa hao wenye kuthamini bia kuliko vitabu wanao uhuru wa kuendelea na msimamo wao huo. Tunapishana mawazo, kwani mimi naamini kuwa mawazo yaliyomo katika vitabu vyangu yana thamani kuliko bia. Halafu, najiuliza, inakuwaje watu hao wasiombe kupunguziwa bei ya bia, ambayo inapanda muda wote?

Hapo ni pale kwenye mkutano Chuo Kikuu cha Iowa. Niko katika mjadala na mtaalam wa masuala ya elimu baada ya yeye kununua kitabu.


Picha hii inanivutia labda kuliko zote na ni hazina ya pekee kwangu. Huyu mama ni wa kutoka Nigeria. Hapa tulikuwa kwenye mkutano katika mji wa Minneapolis. Alifika na mwanae kwenye meza yangu na tuliongea kuhusu shughuli zangu za ufundishaji, utafiti, na uandishi. Kilichonivutia zaidi ni kitendo chake cha kuja na binti yake. Kumlea mtoto katika hali hii ya kupenda vitabu ni jambo la kupigiwa mfano. Je, ni wazazi wangapi katika nchi yetu wanafanya hivyo? Lazima tujitafiti, na tujizatiti ipasavyo katika kukuza taifa la kesho.

3 comments:

Simon Kitururu said...

Profesa umemaliza!Sina chakuongezea na asante sana kwa ujumbe na changamoto!

Christian Bwaya said...

Mimi hununua walau vitabu viwili kwa semester. Napenda kusoma ilivyo kula.

Kila ninapokuwa huwa sikosi cha kusoma. Uliposema watu walikushangaa, naelewa kwa sababu ndicho kinachonitokea mara nyingi.

Katika umri mdogo nilionao, nimejiridhisha kwamba vitabu vinalipa. Elimu ya kweli imo vitabuni. Maarifa ya kweli yameandikwa, hayasimuliwi.

Namshukuru mzee wangu aliyenilea nipende vitabu.

Nakushukuru Prof. kwa changamoto hii.

Mbele said...

Tuko pamoja wadau.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...