Wednesday, July 25, 2012

Nimesifiwa kwa Kutumia Lugha Vizuri

Jana jioni nilikuwa kwenye baa moja karibu na Lion Hotel, Sinza, ambapo nilikutana na daktari mmoja rafiki yangu wa miaka mingi. Alikuwa na kaka yake, ambaye naye ni msomi. Kisha akaja rafiki yao mmoja, ambaye ni mfanyabiashara.

Baada ya takriban saa moja ya maongezi yetu, huyu mfanyabiashara alisema ameguswa na namna ninavyoongea ki-Swahili vizuri, ingawa nimekaa Marekani miaka mingi. Alisema ameguswa na jinsi ninavyoongea bila kutumia maneno ya ki-Ingereza. Daktari akachangia mada hii kwa kusema kuwa hata ninapoongea ki-Ingereza, huwa siigi namna wanavyoongea wa-Marekani.

Hapo waheshimiwa hao wakalalamika kuhusu watu ambao hata wakienda Marekani kwa miezi sita tu, wanakuja hapa na kujifanya hawawezi kuongea kama wa-Tanzania. Daktari aliigiza mikogo ya watu hao, tukawa tunacheka.

Nilifurahi kusifiwa hivyo. Nilichukua fursa hii kuwaeleza kuwa hata ninapokuwa kijijini kwangu watu wanashangaa jinsi ninavyoongea ki-Matengo vizuri kabisa, ingawa nimekaa Marekani miaka mingi. Tena nina uwezo wa kutumia maneno na misemo ya zamani, ambayo vijana wa leo hawaijui.

Mazungumzo hayo yalinikumbusha jinsi ninavyokerwa ninapowasikia watu wakichanganya lugha. Kwa mfano, wabunge wetu wengi wanafedhehesha kwa tabia yao ya kuchanganya ki-Swahili na ki-Ingereza wanapoongea Bungeni. Ninakerwa pia ninaposikiliza vipindi mbali mbali vya redio, ambamo watangazaji au waongeaji huchanganya ki-Swahili na ki-Ingereza.

Kila lugha ina heshima yake, na kuitumia ipasavyo ni namna ya kuienzi. Katika mazingira rasmi kama vile bungeni au redioni, ni sherti kutumia lugha rasmi kwa ufasaha. Kuiheshimu lugha yako ni kielelezo kizuri kujiheshimu, kwani lugha ni chombo kinachohifadhi utamaduni, na utambulisho wa kila binadamu au jamii. Ki-Swahili kinajitosheleza, sawa na lugha nyingine yoyote. Kutokitumia ipasavyo, kwa kukichanganya na ki-Ingereza, ni dalili mbaya.

Kwa kuzingatia yote hayo, ninajivunia kitabu changu cha CHANGAMOTO: Insha za Jamii, nilichoandika kwa kiSwahili. Nilikiandika ili kujipima uwezo wangu wa kutumia lugha hii, kujithibitishia kuwa ninaiheshimu. Hii ilitokana na ukweli kwamba maandishi yangu mengi yamekuwa katika ki-Ingereza, somo ninalofundisha katika Chuo cha St. Olaf. Kwa maoni zaidi kuhusu suala hili, soma makala yangu hii hapa, ambayo ilizua mjadala mzuri katika ukumbi wa Readable Blog.

Monday, July 23, 2012

Ziara Chuo Kikuu cha Dar es Salaam

Baada ya mizunguko yangu Songea, nimerejea Dar es Salaam jana jioni. Leo nilienda Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Nilionana na walimu na watafiki kadhaa, katika masomo ya uhandisi, :"Literature," na Kiswahili.

Nilitumia muda katika maktaba. Katika hifadhi ya "East Africana", niliangalia miswada kadhaa ya tungo za zamani za ki-Swahili. Halafu nilipita kwenye sehemu ya majarida ("Periodicals") na sehemu ya "Reference".

Kuna changamoto zinazoikabili maktaba hii, kama ilivyo kwa maktaba zote hapa nchini. Vinahitajika vitabu vipya na majarida. Hapo "Reference," niliona kwa mfano, nakala ya "MLA Handbook" iliyopo ni ya zamani, toleo la tatu. Itabidi safari ijayo niwaletee nakala ya toleo jipya. Nimewahi kuleta vitabu katika maktaba ile na wala sio jambo gumu. Wa-Tanzania tunaoishi nje au tunaosafiri nje, tungeweza kabisa kutoa mchango mkubwa kwa maktaba zetu kwa kuleta vitabu viwili vitatu. Sio jambo gumu, tukizingatia kuwa tuna utamaduni wa kuleta vipodozi au mizinga ya vinywaji vikali kama Jack Daniels.

Nilipokuwa katika taasisi ya Taaluma za Kiswahili, nilielezwa kuhusu mipango ya kuanzisha digirii ya juu katika fasihi.Niliambiwa kuwa wanahitaji nakala ya tasnifu yangu ya shahada ya udaktari, iitwayo "The Hero in the African Epic," ambayo niliiandika na kuitetea katika Chuo Kikuu cha Wisconsin-Madison. Nimeahidi kuwaletea, Insh/Allah.

Tena wamesema wana mipango ya kuanzisha mitihani ya ki-Swahili kama ile ya ki-Ingereza iitwayo TOEFL. Hii ni habari njema kabisa.

Katika idara ya Literature, ambapo nilifundisha kuanzia mwaka 1976, tuliongelea mambo kadhaa, likiwemo suala la wanafunzi tunaowaleta kutoka Marekani. Nilielezwa chagamoto za utaratibu uliiopo sasa, wa mihula mifupi, tofauti na zamani tulipokuwa tunafundisha somo kwa mwaka mzima.

Saturday, July 21, 2012

Ziara ya Peramiho

Jana nilienda Peramiho, mji ulio karibu na Songea. kwa kweli, Peramiho haifahamiki kama mji. Ni misheni kubwa ya Kanisa Katoliki. Kuna kanisa kubwa, seminari kuu, hospitali, duka la vitabu, na kiwanda cha uchapishaji.

Nimefurahi kuona sehemu kadhaa za Peramiho.Picha nilizopiga nitaziweka katika blogu hii hivi punde, Insh'Allah.

Vile vile, nimepata fursa ya kutembelea chuo kikuu cha Songea, kinachoendeshwa na Kanisa Katoliki. Taarifa nitazileta hivi punde, Insh'Allah.

Friday, July 20, 2012

Bado Niko Songea

Bado niko Songea. Jana asubuhi sikumsikia muadhin. Nadhani nilizidiwa na usingizi. Lakini baadaye kidogo nilisikia mlio wa kengele za Kanisa Katoliki. Nadhani zilikuwa za kanisa kuu la Jimbo, ambalo liko hapa mjini Songea.

Kama nilivyosema katika ujumbe wangu wa juzi, naona ni jambo jema kukumbushana kwamba kuna Muumba. Haijalishi kwangu kama nakumbushwa na muadhin msikitini au kengele kanisani.Mimi sio mtu wa dini sana, ni muumini wa kawaida sana, isipokuwa naona umuhimu wa kuikumbuka dini na kujitahidi kufuata maadili yake.

Jana mchana nilienda Ruhuwiko, kumtembelea dada yangu. Tulipata fursa ya kuongea masuala ya familia na mengine mengi. Nilitegemea pia kwenda kutembelea chuo kikuu kipya kilichofunguliwa hivi karibuni na Kanisa Katoliki hapa mjini. Ratiba ya jana haikuniwezesha kufanya hivyo. Nategemea nitapata fursa hiyo leo.

Mimi nilisomeshwa na Kanisa Katoliki. Sitasahau msisitizo katika taaluma, nidhamu na maadili ya kazi nilivyofundishwa katika shule zao, ambayo yamenifikisha hapa nilipo. Nitashukuru daima.

Leo, Insh'Allah, nitaendelea na ziara zangu hapa Songea, na pia kukutana na wadau mbali mbali.


Thursday, July 19, 2012

Nimefika Songea Tena, Alhamdullilah

Jana jioni nimefika Songea tena. Alhamdullilah. Nimeshinda hapa leo. Nimekutana na ndugu na jamaa, na pia Mheshimiwa Sikapundwa, mmiliki wa blogu ya Tujifunze Kusini. Soma taarifa yake hapa.

Asubuhi sana, kabla hatujaamka, nilisikia jogoo akiwika, na wakati huo huo nilimsikia muadhin akitukumbusha wajibu wetu kwa Muumba. Nilimsikia akisema Allah u akbar. Ni jambo jema sana kwetu waumini, iwe ni wa-Kristo au wa-Islam, kukumbuka au kukumbushwa dhana hiyo ya Allah u akbar, kwamba Mungu ndiye mwenye mamlaka juu ya kila kitu, ndiye mwenye uwezo kuliko mwingine yeyote.

Sunday, July 15, 2012

Nimetoka Arusha Salama

Jana nimetoka Arusha, nikasafiri salama hadi Dar es Salaam. Nilikuwa na wasi wasi kiasi kikubwa nilipokuwa kwenye baadhi ya mitaa ya Arusha, kutokana na namna watu wanavyoendesha magari, piki piki, baiskeli, na kadhalika. Kwenye mitaa hiyo, uendeshaji ni wa kutisha, nami nilikuwa nikitembea mitaani kwa woga, roho mkononi.

Nashukuru nimesalimika hadi kuja tena Dar es Salaam, ambapo napo katika sehemu mbali mbali, uendeshaji ni roho mkononi. Lakini naamini Arusha ni zaidi.

Thursday, July 12, 2012

Arusha ni ya CHADEMA

Juzi usiku hapa Arusha, nilipanda teksi kuelekea hotelini nilikofikia. Humo njiani nilimwuliza dreva wa teksi kuhusu hali ya kisiasa Arusha baada ya mbunge Godbless Lema wa CHADEMA kuachishwa ubunge.

Alinijibu bila kusita kuwa mbunge wa Arusha ni Godbless Lema, pamoja na kuwa halipwi mshahara. Akaongezea kuwa hata ukifanyika uchaguzi, halafu liwekwe jiwe kugombea, likiwa limeandikwa CHADEMA, jiwe hilo litapigiwa kura na kushinda.

Kwangu hizo ni kauli zenye uzito mkubwa. Kwenye masuala ya jamii, nauheshimu sana uchambuzi wa madereva wa teksi. Niliwahi kusema hivyo katika makala hii hapa.

Wednesday, July 4, 2012

Tanga, Mji wa Baiskeli Nyingi

Kitu kimoja kilichovuta hisia yangu, tangu nilipofika Tanga mara ya kwanza, miaka yapata kumi iliyopita, ni jinsi watu wengi wanavyotembelea baiskeli. Mji huu una baiskeli nyingi sana. Hali ni hiyo hadi sasa.

Jambo moja linalonishangaza ni jinsi baiskeli nyingi zinavyopita mitaani usiku bila taa. Sijui watu wa hapa wanawezaje kuimudu hali hiyo, bila wasi wasi. Wanaume kwa wanawake wanatembelea baiskeli mjini hapa.  Jana, tukiwa kwenye Barabara ya Nne, nilimwona mama mmoja amevaa ile aina ya hijab ambayo inafunika hadi uso, kasoro macho. Alikuwa akipita mtaani akiwa amepanda baiskeli.

Hali hiyo ya mji wa Tanga kuwa ni mji wa baiskeli inanipa mawazo kadhaa. Kwanza, kupanda baiskeli namna hiyo, badala ya magari, ni mazoezi bora kwa mwili na afya. Pili, kutumia baiskeli ni jambo jema kwa mazingira, tofauti na utitiri wa magari ambao huchafua hewa ya miji kama Dar es Salaam.

Huu utumiaji wa baiskeli kiasi hicho unanikumbusha mji wa Lamu, kule Kenya. Kule watu wengi hutumia usafiri wa punda. Sijawahi kuona mji wenye punda wengi kama Lamu, na ni usafiri ambao nadiriki kusema una mantiki nzuri kuliko utitiri wa magari kama ilivyo Dar es Salaam.

Ninatalii Tanga

Kwa siku kadhaa sasa nimekuwa mtalii katika mji wa Tanga. Kama wanavyojua ambao wamefika mjini hapa, Tanga ni mji uliotulia sana, ukifananisha na Dar es Salaam, ambao ni mji wa kero nyingi na wajuaji wengi pia.

Jana mchana nilikuwa nimekaa nje ya hoteli ambapo nimefikia. Hapo nje kuna viti vingi na meza, kwani ni sehemu ya wateja kujipatia vyakula na vinywaji. Alipita muuza gazeti nami nikatoa pochi yangu nikanunua magazeti mawili. Muuza gazeti akaenda zake.

Dakika chache baadaye, alipita mtu mmoja akanisogelea na kuniambia kuwa pochi yangu iko chini ya kiti nilichokalia. Nikaangalia, nikaiona. Huyu jamaa hakusimama, bali aliendelea na safari yake, ila najua alinisikia nilipomshukuru. Ingekuwa hajaniambia, sijui mambo yangekuwaje, maana nina hakika ningesimama na kuondoka, bila kujua pochi iko wapi. Pochi ilikuwa na kadi za hela (credit cards), vitambulisho, na kadhalika.

Nimeshapita mitaa kadhaa ya hapa mjini, ambayo nilikuwa siifahamu. Vile vile, nimeona ilipo shule ya Galanos, ambayo ina historia na umaarufu wa pekee sio Tanga tu bali nchini. Nilipokuwa nasoma Mkwawa High School, 1971-72, tulikuwa tunaisikia sana shule ya Galanos.

Insh'Allah leo au kesho nitaenda maktaba ya Tanga, ambayo nimeshaitembelea mara kadhaa. Nitapenda kuona hali yake ya sasa. Mara ya mwisho nilipopita hapo niliona kuwa inahitaji ukarabati mkubwa. Ilijengwa na wakoloni wa ki-Ingereza. Mwalimu Nyerere, ambaye wapika majungu wa Tanzania wanakazana kumbeza, alizienzi maktaba, sambamba na suala zima la elimu. Lakini leo, wa-Tanzania tumepania zaidi kuwekeza katika baa kuliko maktaba au shule. Huko maktabani wa-Tanzania hawaonekani, labda wawe wanafunzi wanaojiandaa kwa mitihani.

Watu wa Tanga walikuwa na bahati ya pekee ya kujengewa maktaba kubwa namna hii. Wangeitumia vizuri, pia kuiwekea vitabu na majarida, leo wangekuwa mbali sana kielimu, ukifananisha na sehemu nyingine za nchi.Lakini sijui ni wangapi katika mji huu wenye mazoea ya kusoma katika maktaba hii.

Ninajiona ni mtalii hapa Tanga. Mbali ya kuangalia sehemu mbali mbali za mji, ninalipia malazi, chakula, vinywaji, usafiri, na huduma zingine kadha wa kadhaa. Ni faraja kubwa kutambua kuwa pesa ninazotumia hapa zinachangia uchumi wa mji huu. Ni pesa ambazo ninaolipwa kule Marekani, ambako nafanya kazi wakati huu. Wazo hili la kuchangia uchumi wa hapa nchini linanifanya nijisikie vizuri.

Monday, July 2, 2012

Nimetua Tanga

Niko Tanga, ambapo niliwasili juzi tarehe 30, nikitokea Dar es Salaam. Tulisafiri na basi la Tashriff, ambalo nililifurahia sana. Kwanza, kwa kipindi kirefu katika safari, tulikuwa tunaangalia video za hotuba za Mwalimu Nyerere. Jambo hilo lilinifurahisha sana, nikizingatia umuhimu wa mchango wa Mwalimu Nyerere, umuhimu wa kuukumbuka na kuuenzi mchango huo, na pia nikizingatia jinsi umbumbumbu uliochanganyika na majungu unavyozidi kushamiri nchini Tanzania kuhusu Mwalimu Nyerere.

Baada ya hizo hotuba, tuliwekewa miziki. Lakini jambo la kuvutia pia ni jinsi dreva alivyokuwa anaendesha gari kwa ustaarabu na hekima, akiwa anaangalia mwendo vizuri. Kwa kweli, nawajibika kuipa hongera kampuni ya Tashriff kwa yale niliyoyashuhudia.

Nimeshafika Tanga mara kadhaa. Ni mji maarufu katika historia na utamaduni Tanzania. Katika safari zangu hizo, nimepiga picha kadhaa, na niliandika habari za maktaba ya Tanga. Safari hii, kama ningekuwa nimejiandaa vizuri, ningekwenda hadi Machui, kijiji alikozaliwa Shaaban Robert. Ningekwenda kuona kaburi lake.

Ninamwenzi mwandishi huyu. Nimeandika makala juu yake ambayo imechapishwa katika Encylopedia of African Literature, na makala nyingine ambayo nimeichapisha katika kitabu cha CHANGAMOTO: Insha za Jamii. Pia nimeandika kuhusu kitabu chake kilichochapishwa miaka michache tu iliyopita, kiitwacho Barua za Shaaban Robert. Soma hapa. Mchango aliotoa Shaaban Robert, mwenyeji wa mji huu wa Tanga, katika uandishi Tanzania na duniani kwa ujumla ni mkubwa sana. Ingetakiwa tuwe na maadhimisho yake ya mara kwa mara, tuwe na maandishi na makongamano kuhusu mchango wake, tuwe na kozi mbali mbali mashuleni kutathmini maandishi yake; tuwe na makala magazetini kuhusu kazi zake, na mambo mengine ya aina hiyo. Kampuni za utalii zingekuwa mstari wa mbele katika kuzihifadhi na kuzitumia kumbukumbu hizi. Lakini hilo halitafanikiwa kwa hali tuliyo nayo nchini, ya kutokuwa na utamaduni wa kusoma vitabu.

Haya ndio baadhi ya mawazo niliyo nayo, wakati huu, nikiwa katika mji huu wa Tanga. Kama sitafika kijijini Machui safari hii, nitahakikisha ninafanya hivyo safari nyingine, Insh'Allah.


Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...