Wednesday, December 31, 2008

Warsha: Utamaduni, Utandawazi na Maendeleo

Kati ya mambo ninayofanya ni kutoa ushauri kwa mashirika, taasisi, vyuo, vikundi na watu binafsi kuhusu masuala ya tofauti baina ya utamaduni wa Mwafrika na ule wa Mmarekani. Ninafanya hivyo kwa njia mbali mbali, kama vile kuandika makala na vitabu, kuendesha warsha, au kukutana watu binafsi ana kwa ana.

Ninaposema utamaduni, namaanisha vitu kama hisia, tabia, maadili, namna tunavyofikiri na tunavyoongea. Vipengele hivi vyote vinatutofautisha watu wa tamaduni mbali mbali, na ni muhimu kuvielewa ili kuepusha migongano. Katika dunia ya leo, ya utandawazi, masuala ya tofauti za tamaduni yanahitaji kupewa kipaumbele, kwani yanaweza kuwa pingamizi kubwa, chanzo cha migogoro, au chachu ya hii migogoro.

Nitaendesha warsha kuhusu masualaa hayo tarehe 4 Julai, 2009, kwenye kituo cha Meeting Point Tanga. Watu kutoka mashirika, makampuni, taasisi, na jumuia mbali mbali watapata fursa ya kuyatafakari masuala kadha wa kadha yanayojitokeza wakati huu ambapo watu wa tamaduni mbali mbali wanalazimika kukutana, kufanya kazi pamoja, kuwasiliana au kuhusiana kwa namna moja au nyingine. Kwa taarifa zaidi soma hapa

Saturday, December 27, 2008

Kijitabu Changu KipyaMiaka miwili iliyopita niliombwa kushiriki katika maonyesho ya utamaduni wa Mwafrika, soma hapa, yaliyofanyika kwa mara ya kwanza mjini Minneapolis katika jimbo la Minnesota, Marekani. Maonyesho hayo yalipangwa kujumlisha mambo mengi: historia ya Mwafrika duniani na harakati alizopitia, mafanikio na mchango wake, na hali yake ya sasa na baadaye.

Wasanii, wabunifu wa mavazi, wanamuziki, na wengine walialikwa kutoa mchango wao. Mimi nilialikwa kuandaa vielelezo vya mambo muhimu katika historia ya Mwafrika, kuanzia chimbuko la binadamu Afrika hadi kusambaa kwa Waafrika sehemu mbali mbali za dunia, kama vile Marekani, Ulaya, na Asia.

Nilifanya utafiti nikaandika habari hizo kwa mtindo wa insha fupi kumi. Kila insha niliiweka kwenye bango kubwa na kila bango liliambatana na picha kadhaa. Siku ya tamasha, niliyabandika mabango hayo kwenye kuta za ukumbi niliopangiwa. Watu walifika humo na kusoma kwa wakati wao, wakiangalia pia zile picha.

Mama mmoja aliyehudhuria na kuangalia maonyesho yangu alipendekeza kuwa nitoe kitabu, ili watu waweze kuendelea kusoma majumbani. Nilifuata ushauri wa huyu mama, na kitabu nilikitoa, chenye habari na picha zile zile zilizomo kwenye mabango.

Kitabu ni kidogo, maana nilikuwa na mabango kumi tu, lakini kinaibua masuala mengi. Kwa mfano, nawakumbusha wasomaji kwamba Afrika ndipo binadamu walipotokea. Pamoja na kuongelea masuala kama utumwa, ukoloni, harakati za kupigania uhuru, na majukumu yanayotukabili leo na siku za usoni, nawakumbusha wasomaji kuhusu mchango wa Waafrika katika nyanja mbali mbali, mchango ambao haujulikani vizuri au umesahaulika kabisa hata miongoni mwa Waafrika wenyewe.

Kuhusu upatikanaji wa kijitabu hiki, tuma barua pepe info@africonexion.com.

Friday, December 26, 2008

CCM: Ni chama cha Mapinduzi?

Sielewi kwa nini watu wanaamini kuwa CCM ni chama cha mapinduzi. Sijawahi kuelewa na bado sielewi kwa nini. Dhana ya mapinduzi ilielezwa vizuri na TANU, katika "Azimio la Arusha," "Mwongozo," na maandishi, hotuba na mahojiano mbali mbali ya Mwalimu Nyerere. Matokeo ya yote hayo ni kuwa Watanzania tulifahamu vizuri na kukubali dhana na maana ya mapinduzi katika nchi yetu. Yeyote ambaye hajasoma maandishi hayo, au kusikiliza hotuba hizo, ningemshauri afanye hivyo, ili aweze kufahamu msingi wa ujumbe wangu.

CCM ilipoanza, ilijinadi kuwa ni chama cha mapinduzi. Lakini baada ya muda si mrefu, mwelekeo wake ulijionyesha kuwa si wa mapinduzi. Badala ya kuendeleza fikra na mwelekeo wa "Azimio la Arusha," "Mwongozo" na mengine yote niliyoyataja hapo juu, CCM ilitoa "Azimio la Zanzibar." Ingawa CCM haikutoa fursa iliyostahili kwa wananchi kuliangalia na kulijadili "Azimio la Zanzibar," habari zilizojitokeza ni kuwa Azimio hili lilikiuka yale yaliyokuwemo katika "Azimio la Arusha." Mwalimu Nyerere alilishutumu "Azimilo la Zanzibar" kwa msingi huo.

Kitu kimoja kilichokuja kufahamika wazi ni kuwa "Azimio la Zanzibar" lilibadilisha masharti ya uongozi yaliyokuwemo katika "Azimio la Arusha" na "Mwongozo." Kwa mfano, "Azimio la Zanzibar" liliondoa miiko ya uongozi iliyokuwepo.

Baada ya CCM kuvunja misingi ya mapinduzi, kilichofuatia ni kuimarika kwa ubepari, matabaka, na ufisadi. Chini ya himaya ya CCM, "Azimio la Arusha" halisikiki, "Mwongozo" hausikiki, wala maandishi na hotuba zingine zilizofafanua maana ya mapinduzi hazisikiki. Inaonekana kuwa CCM ilikusudia tangu mwanzo kuwafanya watu wasahau hayo yote, ili iendelee na sera za kujenga ukoloni mamboleo nchini mwetu.

Inakuwaje basi CCM ijiite chama cha mapinduzi wakati inahujumu mapinduzi? Inakuwaje Watanzania hawahoji jambo hilo? Elimu ni ufunguo wa maisha; bila elimu kuna hatari ya kurubuniwa na kuburuzwa kama vipofu.

Sunday, December 21, 2008

Kuku kwa Mrija

Watanzania wana uwezo mkubwa wa kubuni misemo na kudumisha uhai na utamu wa lugha ya kiSwahili. "Kuku kwa mrija" ni usemi moja ambao umepata hadhi ya pekee katika kiSwahili cha mazungumzo.

Naamini kuwa wengi wanaweza kueleza maana ya usemi huu na matumizi yake, lakini napenda kuelezea machache, kwa kuchambua mantiki yake.

Kuku kwa mrija ni usemi unaobeba dhana ya maisha ya raha, starehe, na vyakula tele. Kwa vile kuku ni nyama inayothaminiwa sana katika utamaduni wetu, kula kuku sana ni dalili ya kuishi maisha ya raha na mafanikio.

Kwa ujumla, Watanzania wanaamini kuwa maisha hayo yanapatikana nchi za nje, hasa Ulaya na Marekani. Mtanzania anayeishi huko anahesabiwa na Watanzania walioko nyumbani kuwa anakula kuku kwa mrija. Maisha yake ni ya starehe na kuku ndio chakula chake kikuu.

Mimi mwenyewe nilikuja Marekani mara ya kwanza mwezi Agosti 1980, kusoma katika chuo kikuu cha Wisconsin-Madison, nikitokea Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ambapo nilikuwa nafundisha. Wakati ule, ninavyokumbuka, dhana ya kuku kwa mrija haikuweko katika kiSwahili. Lakini utamaduni wa kuthamini kuku kuliko nyama zote ulikuwepo, kwani ni utamaduni wa tangu enzi za mababu na mabibi.

Kwa hivyo, nilipofika Marekani, nilikuwa na tabia ya kununua sana kuku. Nina hakika kuwa Watanzania wanaofika huku wanafanya hivyo hivyo, kutokana na utamaduni wetu.

Kitu ambacho sikujua, na Watanzania kwa ujumla hawajui, ni kuwa kuku wa kijijini Tanzania si sawa na kuku wa hapa Marekani. Kuku wa kijijini anakua katika mazingira muafaka kwa afya yake na afya ya wale wanaomla. Anakula punje, mabaki ya ugali au wali, na vidudu mbali mbali ambavyo havina madhara kwa afya yake, na nyama yake haina madhara kwa binadamu.

Kwa ujumla, kuku wa huku Marekani hawako hivyo. Makampuni ya kibepari ndio yameshika hatamu katika kuzalisha kuku na vyakula vingine. Lengo la hao mabepari ni kupata fedha, si kuangalia afya za binadamu. Kuku wao wanakuzwa katika mazingira ya aina yake na kulishwa vyakula na madawa ili wakue upesi, wakauzwe. Baada ya muda mfupi tu wanakuwa wakubwa na tayari kuchinjwa na kuliwa. Madawa wanayolishwa ni hatari kwa afya ya binadamu. Lakini mabepari wakipata mwanya, bila kubanwa, hawaangalii hayo. Naafikiana na Mwalimu Nyerere alivyosema kuwa ubepari ni unyama.

Kwa hivi, Mtanzania anayekuja Marekani au Ulaya na mawazo ya kuku kwa mrija anajitakia matatizo. Hapa Marekani penyewe, na Ulaya pia, baadhi ya watu wameshaanza kampeni ya kuelimishana kuhusu madhara ya ufugaji huu wa kisasa, iwe ni wa kuku au wanyama mbali mbali tunaowala.

Kampeni hii inahusu pia mboga za aina mbali, matunda, mayai, na vyakula vingine. Hofu ya madawa yanayotumika katika kilimo na ufugaji inazidi kuwahamasisha watu waingie kwenye mkondo wa kutafuta vyakula ambayo vimetokana na kilimo kisichotumia madawa, au mifugo isiyotumia madawa.

Watanzania hawaonekani kufahamu suala hilo. Wakati huu, ambapo nchi yetu imefungua milango na kuwaruhusu wawekezaji kuingiza vitu vyao vya kila namna, hata sekta ya vyakula imeathirika. Vyakula vinavyotoka nchi za nje vimejaa madukani, hata vile ambavyo vimetokana na kilimo au ufugaji wa kutumia madawa. Kuku kwa mrija sio tena kitu cha kukiwazia tu, kwamba kinapatikana Ulaya na Marekani. Yeyote mwenye hela Tanzania anakula kuku kwa mrija kutoka nje. Katika hali hii, wale mabepari wanaotafuta hela wanazidi kuneemeka nchini kwetu, na kwa vile sisi inaonekana hatutambui ujinga wetu, wao wataendelea kuchuma, kama methali inavyosema: wajinga ndio waliwao.

Mambo haya yanasikitisha. Jambo linalosikitisha zaidi ni kuwa Tanzania kuna vyakula vya kila aina ambavyo wakulima wanalima bila madawa, kama vile matunda, mboga, viazi, na maharagwe. Kuna mifugo ambayo ni salama kabisa kwa afya ya binadamu, kama vile kuku, mbuzi, na ng'ombe.

Lakini, Watanzania wengi wenye hela wanaona ni fahari kununua vyakula kwenye haya maduka ya kisasa, ambavyo vimetoka nje ya nchi na vimefungwa vizuri kwenye vifurushi, kuliko kwenda sokoni kununua viazi, mchele, na mboga zinazotoka kijijini.

Watanzania wengi wanaona fahari kununua vikopo vya juisi ya machungwa au maembe ambavyo vimeagizwa kutoka nchi za nje, kuliko kununua maembe au machungwa yanayotoka kijijini hapo hapo Tanzania. Akili ya kuelewa kwamba kadiri vyakula hivi vinavyokaa dukani, ndivyo vinavyopoteza lishe haiko vichwani. Ingawa tunda likikaa dukani wiki nzima baada ya kuchumwa linabaki tunda, thamani yake kama lishe haifanani na thamani ya tunda lililochumwa leo hii kijijini na kuletwa sokoni.

Elimu ni nguzo na kinga ambayo tumeendelea kuipuuzia katika nchi yetu. Matokeo yake ni kuwa tunashabikia kuku kwa mrija na vyakula ambavyo wenzetu Marekani na Ulaya wameanza kuviogopa kwa vile vina madhara kwa afya. Madhara ya vyakula vibovu yanaonekana sana katika nchi zinazosemekana zimeendelea, kama zile za Ulaya na Marekani. Tatizo la watu kunenepa kupita kiasi, kwa mfano, ni tishio, na watu wa huku wanaendelea kutambua hilo. Lakini, Watanzania ndio wanaanza kuvishabikia vyakula vinavyoleta madhara haya, na ambayo huku Marekani vinaitwa "junk food" (vyakula takataka), kwani tunaviona ni vyakula vya kisasa.

Tulipopata Uhuru, mwaka 1961, kiongozi wetu wa kwanza, Julius Nyerere, alitangaza kuwa nchi yetu ina maadui wakuu watatu, ambao itakuwa kazi yetu kuwapiga vita. Maadui hao ni ujinga, maradhi na umaskini. Kwa miaka yote ya maisha yake, Nyerere alijitahidi na kuongoza vita hivi na kutuelimisha kwa kila namna. Leo, inaonekana tunaukaribisha ujinga na hivi kujihumu sisi wenyewe.

Tuesday, December 9, 2008

Ubora wa huduma: msingi wa mafanikio

Ni muhimu kuelewa misingi ya mafanikio katika dunia ya leo, yenye ushindani mkubwa. Ushindani huu uko ndani ya nchi na kimataifa. Wapende wasipende, wafanya biashara na watoa huduma mbali mbali wanajikuta katika mazingira ya mashindano ambayo yanaongezeka kwa kasi na yanazidi kuwa magumu. Katika hali hii, ni muhimu kwa kila mhusika kujua siri za mafanikio.

Siri mmoja ni ubora wa huduma. Kuna usemi kuwa mteja ni mfalme. Nimeona sehemu mbali mbali duniani ambapo dhana hii inazingatiwa sana. Wako watu wanaofahamu vema umuhimu wa mteja. Wawe ni wafanyabiashara au watoa huduma, wanaonyesha kumjali sana mteja. Hata kama mteja ni msumbufu wafanyabiashara na watoa huduma hao wako tayari kumsikiliza, kumvumilia na kumsaidia hadi aridhike. Sio rahisi kuwaona wafanyabiashara au watoa huduma hao wakimkasirikia mteja.

Hapa Marekani, kwa mfano, mteja anaponunua kitu, anapewa risiti, na kama hataridhika na kitu alichonunua, ana uhuru wa kukirudisha na kurudishiwa hela yake, au kubadilisha alichonunua akapata kingine, bora alete ile risiti. Hali hii si ya kawaida Tanzania, ambako risiti mara nyingi huwa imeandikwa kwamba bidhaa ikishauzwa haiwezi kurudishwa dukani. Hata kwenye vyombo vya usafiri Tanzania, hali hii ni ya kawaida. Nimeona mara kwa mara tikiti za kusafiria zimeandikwa ujumbe kwamba tikiti ikishakatwa, haiwezi kurudishwa.

Sehemu ambazo nimepita hapa Marekani, nimeona kuwa wahudumu wanawaheshimu wateja. Wanafanya kila juhudi kumsaidia mteja. Kama mhudumu analegea katika kutoa huduma, labda kwa sababu ya kutoelewa, au kazidiwa na shughuli, mkuu wake wa kazi, hata meneja, yuko tayari kuja kutoa hiyo huduma. Si ajabu hapa Marekani kumwona meneja akitoa huduma ambayo kwa kawaida inatolewa na mfanyakazi wake. Tanzania nimeona mambo tofauti. Meneja wa baa, kwa mfano, hawezi kuchukua kitambaa na kusafisha meza ya wateja. Atamtafuta mhudumu wa baa aje asafishe. Meneja anajiona mtu bora kuliko wahudumu. Ni kawaida kumwona meneja amekaa kwenye meza na watu anaowajua yeye, na kazi yake ni kunywa pombe na kuongea nao.

Nikiwa kwenye baa za Tanzania, nimewahi kuwa na masuala ya kuwaeleza mameneja, iwe ni malalamiko au ushauri kuhusu huduma, lakini imetokea mara kadhaa kuwa meneja alishalewa, na hana uwezo wa kusikiliza na kuzingatia niliyokuwa nasema. Naamini kuwa, ili tuweze kufanikiwa katika dunia ya ushindani, tabia hizi lazima tuzibadili.

Watu wa nje watakuja na taratibu zao za kujali wateja. Kila mteja anafurahia huduma nzuri. Matokeo yake ni kuwa, wafanyabiashara na watoa huduma wasiozingatia suala la kumridhisha na kumfurahisha mteja watapoteza wateja. Na katika ulimwengu huu wa ushindani, mtoa huduma nzuri ndiye atapata wateja wengi. Kutakuwa na wafanya biashara ambao wanauza kitu kile kile, kwa mfano nguo za aina ile ile, lakini baadhi watafanikiwa na baadhi watazorota, kutokana na kiwango cha ubora wa huduma kwa mteja. Mteja akiwa na hela yake, anaweza kuipata nguo hiyo kutoka sehemu yoyote. Lakini anapoamua kuja sehemu moja, wahudumu wa sehemu hiyo wanapaswa kuelewa kuwa hii ni bahati ambayo hawapaswi kuichukulia kijuu juu.

Mteja anapoingia dukani, hotelini, au sehemu yoyote inayotoa huduma, ajisikie kuwa yuko mahali anapothaminiwa na kufurahiwa. Wako wahudumu ambao wanampokea mteja kama vile angekuwa mtu asiyetakiwa, adui, au mhujumu. Wanampa maneno ya mkato, kuudhi, au kukatisha tamaa. Watoa huduma wa aina hii, au wenye biashara wa aina hii, wanahujumu wenyewe hizo biashara au huduma zao.

Fundisho hili, ingawa rahisi, halijaingia vichwani mwa wengi katika Tanzania. Wengi wanapoona biashara zao zinazorota au huduma zao hazivutii wateja, wanatafuta visingizio kama vile kulogwa na washindani. Wengi wanaamini kuwa ili wafanikiwe katika biashara, lazima watumie mizizi na mambo ya kishirikina. Huku Marekani, kuna vitabu vingi ambavyo vinafundisha masuala ya aina aina, likiwemo suala la kuendesha biashara na huduma mbali mbali. Vitabu hivi vinafundisha mbinu, misingi na mikakati. Vinaelezea saikilojia ya wateja, umuhimu wa kuwajibika, kujenga mahusiano na wengine, na kadhalika. Sijawahi kuona kitabu hata kimoja kinachoelezea umuhimu wa kutumia mizizi. Hiyo mbinu ya mizizi inaonekana inafanya kazi huko kwetu tu. Suali linalonijia kichwani ni je, katika ushindani wa kimataifa, ambamo wenzetu wanatumia ujuzi, maarifa na elimu, sisi tutafanikiwa kwa kutumia mizizi?

Dunia ya leo inaendeshwa na ujuzi na maarifa. Hilo linafahamika sana duniani. Tanzania bado tuko nyuma. Suala la kutafuta ujuzi, elimu, na maarifa tumelipuuzia. Hatutaweza kufanikiwa katika dunia ya leo iwapo tutaendekeza hali hii. Ushindani wa kimataifa utakuwa ni tishio kwetu. Wakati huu, tayari, uwoga wa ushindani wa kimataifa umeshaanza kujitokeza nchini mwetu. Hayo ni matokeo ya kupuuzia suala la elimu, suala ambalo Mwalimu Nyerere alilizingatia tangu tulipopata uhuru, pale aliposema kuwa tuna maadui watatu: ujinga, umaskini, na maradhi.

Wednesday, November 26, 2008

Mahojiano na Profesa Joseph Mbele

Niliwahi kuhojiwa na ndugu Deus Gunza, katika Radio Butiama, kuhusiana na kitabu changu kinachohusu tofauti za utamaduni wa Mmarekani na ule wa Mwafrika. Mahojiano yanasikika hapa:
http://butiama.podomatic.com/entry/et/2006-09-02T06_26_37-07_00

Hadithi Zetu

Kabla ya kuweko maandishi, wanadamu walikuwa wanahifadhi kumbukumbu, taaluma, mafunzo, urithi wa utamaduni wao kwa ujumla, kwa masimulizi ya mdomo. Masimulizi hayo yalikuwa ya aina nyingi, kama vile misemo, methali, vitendawili, nyimbo na hadithi. Mfumo mzima wa masimulizi hayo ilikuwa ni hazina iliyobeba taaluma, falsafa, kumbukumbu, mafundisho na kila aina ya ujuzi ambao wanadamu walihitaji katika maisha na maendeleo yao. Kwa karne na karne, ambapo vitabu wala maktaba hazikuwepo, watu walihifadhi ujuzi wao vichwani mwao. Uwezo wao wa kukumbuka mambo ulikuwa mkubwa kuliko uwezo tulio nao sisi, kwani maandishi yametupunguzia uwezo huo na kutujengea aina ya uvivu. Tunategemea maandishi kuliko vichwa vyetu. Tukienda kusikiliza mhadhara, tunahitaji karatasi ya kuandikia yale tunayoyasikia, tofauti na watu wa zamani, ambao walikuwa wanatumia vichwa vyao tu.

Nilizaliwa na kukulia kijijini. Nilikuwa na bahati ya kusikiliza hadithi, nyimbo, na masimulizi ya aina aina, katika Kimatengo, ambayo ni lugha yangu ya kwanza. Baba yangu alikuwa msimuliaji hodari wa hadithi. Niliwahi kuelezea hayo yote kwa ufupi hapa: http://www.thomsonsafaris.com/newsletter/nl38_matengo.htm

Niliposoma Chuo Kikuu Dar es Salaam, 1973-76, nilifundishwa taaluma ya fasihi simulizi. Mwalimu wetu alikuwa marehamu Mofolo Bulane wa Lesotho. Alitufungua macho, katika taaluma hii, tukaanza kuona utajiri wa fasihi simulizi na umuhimu wake katika maisha ya binadamu, tangu enzi za mwanzo hadi leo.

Mwalimu Bulane alinijengea motisha ya kuwa mwanataaluma katika fasihi simulizi. Tangu nilipokuwa mwanafunzi, nilianza kurekodi hadithi kijijini kwangu. Kisha nikawa nazinukuu kutoka kwenye kinasa sauti, nikawa nazitafsiri kutoka kiMatengo kwenda katika kiSwahili na kiIngereza, nikawa nazitafakari na kuzichambua. Nimeelezea hayo kwa ufupi hapa:
http://www.thomsonsafaris.com/newsletter/nl38_collecting.htm

Mwaka 1999, nilichapisha kitabu kwa kiIngereza, Matengo Folktales, http://www.lulu.com/content/136624. Kitabu hiki kinajumlisha tafsiri za hadithi kumi nilizorekodi miaka ya sabini na kitu. Kila hadithi imefuatiwa na uchambuzi, ambao niliuandika ili kufafanua yaliyomo na kuelezea undani wa hadithi na umuhimu wake. Mwishoni mwa kitabu nimeweka insha moja kamili kuhusu hadithi, inayojumlisha mambo muhimu yanayohusu hadithi, kama mwongozo kwa yeyote anayetaka kujielimisha katika taaluma hii. Kitabu hiki kinasomwa hapa Marekani na watu wa kila aina, hata watoto, na kimeshatumiwa na kinaendelea kutumiwa katika vyuo vikuu vingi.

Hadithi zetu ni hazina kubwa inayoweza kutumiwa kwa namna nyingi. Kwa mfano, hadithi na fasihi simulizi kwa ujumla, zinaweza kuwa sehemu muhimu katika utalii. Nimewahi kuzisaidia kampuni za utalii za hapa Marekani katika suala hilo. Mbali na kuendesha semina kadhaa, mwaka 2002 niliongoza kundi kubwa la watalii wa Thomson Safaris kutoka maeneo ya Boston, kuja Tanzania, na mchango niliotoa ni kuwaelimisha watalii hao namna wenyeji katika maeneo ya utalii ya mkoa wa Arusha, Tanzania, walivyobuni masimulizi mbali mbali kuhusu yale yote ambayo watalii walikuwa wanakuja kuyaangalia: iwe ni wanyama, ndege, mimea, au milima. Yote hayo yamo katika fasihi simulizi, na hiyo fasihi simulizi ni njia muhimu ya kuelewa mahusiano ya binadamu na mazingira yake. Kwa kutumia fasihi simulizi katika utalii, utalii unakuwa ni njia ya kujielimisha. Mtalii anaondoka akiwa ameelimika, badala ya kuishia kuzunguka tu mbugani na kupiga picha za wanyama au kupanda Mlima Kilimanjaro.

Hayo yanahitaji juhudi. Watanzania wanatakiwa kuwa makini katika utafiti na katika kujielimisha kuhusu utamaduni wao na historia yake. Bila hivyo, fursa hii ya kutumia fasihi simulizi na vipengele vingine vya utamaduni itatupitia mbali, wakati wenzetu katika sehemu zingine za dunia wanaitumia vizuri. Mwalimu Nyerere alituhimiza kuukumbuka utamaduni wetu, kujifunza, na kuuenzi, lakini je, ni Watanzania wangapi wanaokumbuka hayo mafundisho ya Mwalimu Nyerere? Wangapi wanafahamu ni lini na wapi Mwalimu Nyerere aliongelea masuala muhimu ya utamaduni wetu?

Tuesday, November 25, 2008

Migogoro ya kidini na hadithi zingine

Kuna hadithi nyingi duniani. Hadithi moja ninayoifuatilia ni ya migogoro ya kidini. Katika historia ya binadamu, kumekuwepo migogoro na vita baina ya watu wa dini mbali mbali, na migogoro hiyo bado inaendelea. India kumekuwepo migogoro baina ya Wahindu na Waislamu, na pia baina ya Wahindu na Wakristu. Ulaya kulikuwako vita maarufu za "Crusades." Ireland kumekuwapo migogoro baina ya Wakatoliki na Waprotestanti. Nigeria kumekuwapo migogoro baina ya Waislam na Wakristu. Hii ni mifano tu.

Ni kawaida kwa migogoro hii kuitwa migogoro ya kidini. Suali ninalojiuliza ni je, hii migogoro ni ya kidini kweli? Mimi nadhani hapa pana tatizo kubwa kinadharia. Ninavyofahamu, dhana ya dini ni kumwamini Muumba na kufuata amri zake: katika ibada, katika maisha yetu binafsi, na katika kuishi kwetu na wanadamu wenzetu. Dhana ya dini inajumlisha yote hayo.

Kwa msingi huo, mtu mwenye dini atakuwa mcha Mungu, mwema, mpole, mwenye haki, mwadilifu, mwumilivu, na mwenye huruma. Binadamu ni binadamu; anaweza kupotoka: anaweza akafanya ugomvi, hujuma, au jambo jingine baya. Lakini, mtu huyu atajirudi mara na kumwangukia Muumba kuomba msamaha, ili aendelee kuwa katika njia iliyo sahihi kwa msingi wa dini.

Kwa mantiki hiyo, penye dini ni mahali penye amani, maelewano, na kuheshimiana. Migogoro na vita ni dalili ya kukosekana kwa dini. Vita ni ishara ya kukosekana kwa dini. Dini ni kama mwanga, na vita na migogoro ni kama giza. Penye mwanga hapana giza. Ndio maana nasema, penye dini hapana magomvi wala vita. Vita na migogoro ni ufedhuli, na ufedhuli hauko kwenye dini. Kupigana au kuwa na migogoro ni kuisaliti dini.

Kwa msingi huo, mimi siafiki kuwa kunaweza kukawa na vita vya kidini, au migogoro ya kidini. Dhana ya vita vya kidini au migogoro ya kidini ni hadithi isiyo na mantiki, kama hadithi zingine zozote zisizo na mantiki.

Wednesday, October 15, 2008

Mwalimu Nyerere na Elimu


Mwalimu Julius Nyerere alikuwa mwalimu. Naamini ni sahihi kusema kuwa silika ya ualimu iliathiri siasa na matendo ya Mwalimu Nyerere kama kiongozi wa Tanganyika na hatimaye Tanzania. Aliiona nchi yake kama darasa, na daima alikuwa anafundisha.

Ninachotaka kuongelea hapa ni mchango wa Mwalimu Nyerere katika uwanja wa elimu. Elimu ni suala mojawapo ambalo Mwalimu Nyerere alilishughulikia sana. Katika kuelezea suala la elimu, Mwalimu aliweka na kufuata misingi kadhaa muhimu.

Tanganyika ilipopata Uhuru, Mwalimu Nyerere alikuwa ameshajizatiti kubadilisha mfumo wa elimu uliokuwepo wakati wa ukoloni, ambao ulikuwa mfumo wa kibaguzi. Kulikuwa na shule za wazungu, za Wahindi, na za watu weusi. Mara tulipopata Uhuru, Nyerere alifuta ubaguzi na kuwachanganya wanafunzi mashuleni. Tangu mwanzo, Mwalimu Nyerere aliamini dhana ya usawa wa binadamu.

Mwalimu Nyerere aliamini kuwa elimu ni haki ya kila mtu. Alifanya kila juhudi kutoa elimu kwa watu wote, kuanzia watoto hadi watu wazima. Mwalimu alijitahidi kujenga mfumo wa elimu ambao ulitoa nafasi kwa yeyote kutokana na uwezo wa akili yake, bila kujali kama alikuwa maskini au tajiri. Kwa msingi huu, watu wengi ambao hawangeweza kulipia masomo walisoma hadi vyuo vikuu.

Mwalimu Nyerere alitaka elimu iwe inamjenga mwanafunzi kuwa mdadisi wa mambo na mwenye kiu ya kutafuta elimu. Yeye mwenyewe alikuwa mwanafalsafa, mtu wa kutafakari mambo. Na hivyo ndivyo alivyotaka elimu iwe. Mwalimu alitaka elimu iwe nyenzo ya kumkomboa mwanadamu, tofauti na elimu ya kikoloni, ambayo ilikuwa inaendeleza fikra tegemezi, fikra za kujidhalilisha, fikra za kitumwa. Alitaka elimu ijenge tabia ya kuheshimiana, sio kiburi cha usomi.

Mwalimu Nyerere alitaka elimu ijumlishe nadharia na vitendo, na ijenge tabia ya kushirikiana, si kushindana na ubinafsi. Vijana mashuleni alitaka wawe pia wanajishughulisha na kazi za mikono, kama vile kulima au kufuga na useremala. Hii nayo ni elimu, na ni fursa ya kufahamu mengi ambayo hayapatikani darasani. Kazi za mikono aliziona ni njia moja ya shule kujenga msingi wa kujitegemea kwa mahitaji yake.

Mwalimu Nyerere alifundisha kuwa elimu haina mwisho. Aliwahimiza watu kujibidisha katika kutafuta elimu. Mbali ya kushughulikia elimu ya watoto na vijana mashuleni, alianzisha mpango wa elimu ya watu wazima. Vijijini na mijini watu walihimizwa na walipata fursa ya kujiongezea elimu, kuanzia kujifunza kusoma na kuandika hadi kujipatia ujuzi na maarifa katika fani na taaluma mbali mbali.

Kwa utaratibu ulioitwa kisomo chenye manufaa, wavuvi, wakulima, seremala, wafugaji, na wengine katika shughuli mbali mbali, walihimizwa kujiongezea ujuzi kwenye fani na shughuli zao. Vitabu vilichapishwa katika fani za aina aina, ambavyo viliwapa watu fursa ya kujifunza kusoma na pia kujiongezea maarifa na ujuzi.

Kama Watanzania tungefuata mawazo ya Mwalimu, leo tungekuwa mbali kimaendeleo, na tungekuwa na mategemeo ya kufanikiwa zaidi. Katika dunia ya leo ya utandawazi, elimu, ujuzi na maarifa ndio msingi wa mafanikio. Lakini, Tanzania tuna matatizo makubwa, kwani ari ya kujielimisha imepungua sana, na watu wanatafuta vyeti badala ya elimu. Wengi wanaamini kuwa njia ya mafanikio ni kutumia mambo ya ushirikina, badala ya kujiongezea maarifa katika fani na shughuli mbali mbali, iwe ni kilimo, uvuvi, au biashara.

Nimeona jinsi Wamarekani wanavyojali elimu. Wanatumia fedha kununua vitabu, kulipia semina, na fursa nyingine kadha wa kadha za kujiongezea elimu, ujuzi na maarifa, ili wapate mafanikio katika shughuli zao, kama vile biashara. Watanzania tungekuwa tumefuata nyayo za Mwalimu Nyerere tungefanya hivyo hivyo: tungeona umuhimu wa kutumia fedha kununulia vitabu na kulipia warsha za kujiongezea ujuzi na maarifa katika shughuli mbali mbali. Imani ya kuwa maendeleo na mafanikio yanatokana na mambo ya kishirikina ni dalili za kuanguka kwa ule msingi aliokuwa anaujenga Mwalimu Nyerere. Je, Watanzania tutaweza kushindana katika dunia ya leo na kufanikiwa bila elimu, ujuzi na maarifa? Hilo wimbi la ushindani wa kimataifa tutaliweza au litatuzamisha? Hilo ni suala la kulitafakari.

Kuufahamu mchango wa Mwalimu Nyerere katika elimu ni sherti kuyapitia maandishi yake na hotuba zake. Baadhi ya maandisho hayo na hotuba hizo zilihusu elimu moja kwa moja, na baadhi ya kazi zake hizo ni hazina ambayo inatuwezesha kukusanya dondoo mbali mbali za kutuwezesha kuielewa falsafa na sera ya Mwalimu Nyerere kuhusu elimu. Kwa bahati nzuri, kuna kitabu kimechapishwa, kinachokusanya maandishi muhimu ya Mwalimu Nyerere kuhusu elimu. Kinaitwa Nyerere on Education/ Nyerere Kuhusu Elimu. Ni kitabu muhimu sana ambacho kinapatikana hapa: http://msupress.msu.edu/bookTemplate.php?bookID=3032

Wednesday, October 8, 2008

Watoto wa Marekani


Ingawa kazi yangu kuu hapa Marekani ni kufundisha katika kiwango cha chuo kikuu, kufanya utafiti katika taaluma zangu, na kutoa mchango wa mawazo na uzoefu kwa walimwengu kwa ujumla, napenda sana kukutana na kuongea na watoto, kuwasilimulia hadithi za Afrika, na kuwaeleza kuhusu maisha ya Afrika na masuala mengine ya maisha kwa ujumla, katika nchi yao na duniani.

Nimeshaongea na watoto kwenye miji mbali mbali, katika mikoa ya Colorado, Minnesota, Pennyslvania, na Wisconsin. Watoto ni watoto. Kitu kimoja wanachopenda ni hadithi. Nami nimekuwa na fursa nyingi za kuwasimulia hadithi za Kiafrika. Kitu kimoja kinachofurahisha ni jinsi watoto walivyo na akili ya kufuatilia hadithi na kuzichambua. Hata watoto wanaodhaniwa kuwa hawana akili sana au hawana moyo wa kupenda masomo, wanaonyesha msisimko wanaposimuliwa hadithi. Hapa kuna taarifa kuhusu nilivyokutana na watoto wa shule ya LeTort, Pennsylvania. Soma hapa


Jambo hili limenifanya nikumbuke habari moja niliyosoma kuhusu mwanasayansi maarufu Einstein. Inasemekana aliulizwa na wazazi kuhusu mkakati bora wa kuwaandaa watoto kuwa wanasayansi makini. Wazazi walidhani kuwa angeshauri watoto wafundishwe sana masomo ya sayansi tangu utotoni. Lakini Einstein aliwajibu kuwa watoto wasimuliwe hadithi. Alipoulizwa nini kifanyike baada ya hizo hadithi, yeye alilisitiza kuwa watoto wasimuliwe hadithi zaidi.


Habari hii niliisoma nilipokuwa masomoni katika Chuo Kikuu cha Wisconsin-Madison, katika kujisomea mwenyewe vitabu. Mwanzoni sikuelewa kwa nini Einstein alikuwa na mawazo hayo. Lakini baada ya miaka mingi, nilipojaribu kusoma zaidi mawazo ya Einstein, nilianza kufahamu alikuwa na maana gani. Yeye aliamini kabisa kuwa kitu cha maana kwa mtoto ni kumhamasisha awe mbunifu. Ubunifu--dhana ambayo Waingereza wanaita "imagination"--ndio msingi, kwa mujibu wa Einstein. Nilivyozidi kufuatilia habari za Einstein, nilikuja kuelewa kuwa yeye mwenyewe kama mwanasayansi alikuwa anatagemea sana ubunifu, sio tu majaribio katika maabara. Alikuwa na ubunifu wa hali ya juu; hata baadhi ya nadharia zake wataalam wenzake waliziona kuwa ni ndoto. Lakini miaka mingi baadaye, kutokana na kuwepo vifaa vya uchunguzi, nadharia zake zimethibitishwa kuwa kweli.

Watoto wa Marekani ni sawa na watoto wengine. Wana dukuduku, na wanapenda kujua mambo. Wana masuali mengi. Sehemu kadhaa nilipoenda kuongea na hao watoto, walimu wao walikuwa na wasi wasi kuwa labda watoto wataniuliza masuali ya kijinga. Lakini mimi niliwaambia walimu kuwa watoto wana haki ya kuuliza masuali, hata yawe ya aina gani.

Watoto wanaoonekana katika picha hizi hapa walikuwa wanafunzi kwenye shule za mji wa Faribault, Minnesota. Mwalimu wao alikuwa ameniomba awalete hao watoto ili niwape mawaidha na motisha. Hakufafanua zaidi, bali mimi nilichukulia hii kama fursa ya kuwaeleza hao watoto jinsi dunia ilivyo pana na yenye fursa nyingi kwao, jinsi dunia ilivyo na nchi nyingi, kila moja ikiwa na mazuri yake. Ilikuwa ni siku nzuri kwa watoto hao na kwangu.

Saturday, October 4, 2008

Wasomaji wa Maandishi Yangu

Uandishi ni shughuli inayohitaji juhudi na ustahimilivu. Inaweza kuleta mema au mabaya katika jamii. Kwa hivi, mwandishi anapaswa kuwa makini. Uandishi unaweza kuwa na manufaa mengi, kwa mwandishi mwenyewe na kwa jamii. Kuandika kunatupa fursa ya kutumia akili katika kupanga mawazo na lugha. Ni zoezi la kuchangamsha na kuboresha akili. Kitu kimoja kinachonipa faraja sana na motisha pia, ni kufahamiana na watu mbali mbali, kwa njia ya maandishi yangu. Najifunza mengi kutokana na maoni ya wasomaji. Napenda kwenda sehemu mbali mbali kuwaonyesha watu maandishi yangu na kuongelea shughuli zangu za ufundishaji, utafiti, na uandishi. Napenda pia kuelezea ninavyojishughulisha katika kutoa ushauri kwa wageni mbali mbali, hasa Wamarekani, wanaokwenda Afrika, kama wanafunzi, watafiti, watalii, na washiriki katika shughuli za kujitolea. Baadhi ya picha zinazoonekana hapa zilipigwa Minneapolis, tarehe 4 Oktoba, 2008, wakati wa sherehe za kumbukumbu ya Uhuru wa Nigeria. Nilipata fursa ya kushiriki, nikiwa na meza yangu ya vitabu na maandishi mengine. Mama anayeonekana pichani na binti yake walikuwa miongoni mwa wengi waliokuja kuongea nami na kuangalia vitabu, au kuvinunua. Nilifurahi kuona wazazi wakiwa na watoto wao. Kwa vile mimi ni mwalimu, naamini hii ni namna bora ya kuwalea watoto. Utamaduni huu uko sana hapa Marekani. Kwenye maduka ya vitabu, ninawaona wazee, vijana, watoto, wake kwa waume wakiangalia vitabu, wakivisoma, na kuvinunua. Hata watoto wadogo kabisa wanaletwa humo na wazazi wao, na hivi kujengewa tabia ya kusoma. Majumbani, utamaduni wa wazazi kuwasomea vitabu watoto wao wadogo umejengeka. Inakuwa kama vile hao wenzetu ndio wanafuata ule ushauri wa wahenga kwamba samaki mkunje angali mbichi. Utamaduni huu kwa kiasi kikubwa hauonekani Tanzania. Kwenye maduka ya vitabu, ambayo ni machache sana, na kwenye matamasha ya vitabu, watu wazima ni nadra kuonekana. Hii ni dalili ya tatizo kubwa katika jamii yetu. Tutawezaje kustahimili ushindani wa dunia ya leo, au kustawi na kufanikiwa katika dunia ya leo, ambayo inategemea elimu na maarifa? Hapo juu niko na mama moja na mume wake. Huyu mama ni mratibu wa mpango wa uhusiano baina ya jimbo moja la kanisa na kiLuteri hapa Marekani na Waluteri wa Malawi. Baada ya kusoma kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, http://www.lulu.com/content/105001, amekuwa akiwasiliana nami mara kwa mara, akitafakari vipengele mbali mbali vya vinavyojitokeza katika mahusiano baina ya Wamarekani na Waafrika. Masuali yake mengi kuhusu vipengele vya maisha ya watu wa Malawi yamenipa changamoto ya pekee. Hapo juu naonekana na akina mama wawili kutoka Ethiopia, ambao wanaishi Marekani. Wote wamesoma kitabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences. Huyu mama wa kushoto alinieleza kuwa laiti angekuwa amesoma kitabu hiki kabla hajaja Marekani, angekuwa amejiandaa kwa mengi aliyoyapitia hapa Marekani. Niliguswa sana na hii kauli yake. Nayasikia maoni ya aina hiyo muda wote, kutoka kwa Waafrika wanaoishi Marekani. Nami nawashukuru, kwani ni changamoto kwangu, niongeze juhudi ya kutafakari masuala na kuandika zaidi. Hapo juu niko na vijana wa Mto wa Mbu, Tanzania, wanaoshughulika na utalii unaolenga kwenye utamaduni. Waliniambia kuwa wamesoma Matengo Folktales, http://www.lulu.com/content/136624, na Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, na wanavitumia katika shughuli zao. Vimewapa uwezo wa kuelezea fasihi simulizi ya Mtanzania. Hicho cha pili kimewapa mawazo mengi ya kuelezea utamaduni wa Mtanzania na Mwafrika kwa ujumla. Pia kimewapa mwanga wa kuuelewa utamaduni wa watalii wanaowakaribisha Mto wa Mbu, hasa Wamarekani. Nilifurahi na kufarijika kuwasikia vijana hao wakinieleza kuwa vitabu hivi vimewapa moyo wa kujiamini katika kutekeleza majukumu yao. Ninafurahi kuwa nao bega kwa bega. Kama nilivyosema, Wamarekani wengi wanakwenda Afrika, kama watalii, wanafunzi, watu wa kujitolea, watafiti, na kadhalika. Nimekuwa na bahati ya kuwa bega kwa bega na watu wa aina hiyo. Hapo kulia kuna hao wazungu wawili ambao wanashughulika na miradi ya elimu, afya na kadhalika huko Kenya na Tanzania. Huyu aliye kushoto ni Mkenya ambaye wanashughulika wote kule Kenya. Huyu mama, baada ya kusoma Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, amekuwa na mawasiliano ya mara kwa mara nami, akitaka kujua zaidi vipengele vya maisha ya Waafrika, ili aweze kuishi na kufanya nao kazi vizuri bila mikwaruzano wala vipingamizi. La msingi ni kuwa nashukuru kuwa nimepata fursa ya kuwa karibu na watu wengi namna hiyo, na fursa ya kutoa mchango katika maisha na shughuli zao. Sitasahau ujumbe niliopata kutoka kwa mama mmoja Mwamerika, ambaye sijawahi kumwona. Aliniambia alikuwa anakamilisha mipango ya kufunga ndoa na mwanamme Mwafrika, lakini kwa muda mrefu walikuwa na mikwaruzano, ambayo hakuelewa kwa nini ilikuwa inatokea. Aliongeza kuwa katika kusoma Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, aligundua mizizi ya mikwaruzano yao. Taarifa kama hizi ni changamoto kwangu. Nawajibika kuendelea kuandika. Vitabu vilivyotajwa hapa juu vinapatikana Dar es Salaam, simu namba 0754 888 647.

Friday, October 3, 2008

Mwalimu Julius Nyerere

Nimeona kuwa andiko la kwanza liwe juu ya Mwalimu Julius Nyerere. Mwalimu Nyerere ni mtu maarufu katika historia ya Tanzania. Katika ukumbi huu athari za mawazo na siasa za Mwalimu Nyerere zitajitokeza mara kwa mara, kwani alichangia kuiwezesha Tanzania kupitia hatua ilizopitia, akishirikiana na wazalendo wenzake, ambao nao watakuwa wanatajwa hapa ukumbini, kila itakapobidi.

Mwalimu Nyerere anastahili kukumbukwa, kwa mchango wake mkubwa, sio tu kwa nchi yetu bali kwa dunia. Tunapaswa kusoma maandishi yake na kuyajadili, kuyatathmini, na kuyakarabati inapobidi, ili yaendelee kuwa mwongozo wetu.

Mwalimu Nyerere alikuwa mtu wa fikra, ambaye daima alikuwa anaangalia maslahi ya nchi yetu, na jitihada alizofanya katika kubadilisha siasa, uchumi, utamaduni, na vipengele vingine vya nchi yetu ilikuwa ni kwa nia ya kuikomboa na kuijenga katika misingi ya uhuru, usawa, haki, na kujitegemea. Yako makosa ambayo alifanya, lakini alikuwa mzalendo, aliyeamini kuwa aliyokuwa anafanya ni kwa maslahi ya nchi. Makosa yake yanahitaji kuwekwa katika mkabala huo. Huu ndio mtazamo nitakaokuwa nao katika kuelezea na kujadili mchango wa Mwalimu Nyerere kwa Tanzania na dunia.

Karibu, hapa kwetu

Karibu. Hapa ni kwetu--Watanzania, Waafrika, na wengine wanaotumia kiSwahili. Ninategemea kuwa huu utakuwa ukumbi wa masuala yanayotuhusu: katika siasa, uchumi, utamaduni, na jamii kwa ujumla. Namshukuru sana ndugu Freddy Macha, ambaye alinipa wazo la kuanzisha blogu. Freddy ni Mtanzania mwenye uwezo wa pekee katika fani mbali mbali, hasa muziki na uandishi. Anafanya kazi kubwa ya kuwaelisha na kuwaunganisha walimwengu. Namshukuru sana pia ndugu Jeff Msangi kwa kunihamasisha kwa namna mbali mbali. Jeff ni hodari katika kuelimisha umma kwa namna mbali mbali.

Karibuni.