Wednesday, May 30, 2012

Warembo Wengine Hawa Hapa

Siku chache zilizopita, niliweka makala kuhusu mrembo hapa katika blogu yangu. Lengo langu lilikuwa kuchochea mjadala kuhusu suala la urembo, ambalo, kama nilivyogusia, nimelijadili katika kitabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences.

Nimeona picha nyingine ya warembo katika mtandao wa Facebook, ambayo naileta hapa. Sisi tuliokulia vijijini Afrika tunaweza kusema kuwa ingekuwa bora kama hao warembo wangejisitiri vizuri zaidi kimavazi. Lakini huenda hao si wa-Afrika. Hapa Marekani, kwa mfano, wakati wa joto, watu wengi huvaa vivazi ambavyo kwetu tunaviona si vya heshima, lakini hapa wanaona ni sawa.

Tuesday, May 29, 2012

Tamko la Askofu Mkuu Kufuatia Vurugu za Zanzibar

TAMKO LA ASKOFU MKUU WA TANZANIA ASSEMBLIES OF GOD, DK.BARNABAS
MTOKAMBALI, KUHUSU MATUKIO YANAYOASHIRIA UVUNJIFU WA AMANI NCHINI.

Kwa kipindi kirefu sasa kumekuwa na mfululizo wa matukio yanayoashiria
uvunjifu wa amani, umoja na utengamano wa taifa letu la Tanzania, haya
ndiyo yanayonisukuma kutoa tamko hili leo ili kuonya na kushauri.

Katika siku za karibu kiumeibuka makundi mbalimbali ya kidini ambayo
yalianza kutoa matamko yenye kuchochea ghasia za kidini Tanzania, na
pengine kauli hizo ndizo zinazotimizwa kwa vitendo hivi sasa.

Miongoni mwa matukio hayo ni:
Januari sita mwaka huu, kikundi kimoja kinachoitwa JUAKATA, kiliitisha
kongamano la kujadili katiba mpya Tanzania, kwa upande wa Waislam.
Katika kongamano hilo lililofanyika kwenye Ukumbi wa Diamond Jubilee,
Dar es Salaam kauli zifuatazo:
1. Lazima Rais ajaye atoke Zanzibar
2. Kukabiliana na ukuaji wa kasi wa dini ya Kikristo
3. Kupinga Muungano ili kuupa nguvu Uislamu
4. Kupigana kufa na kupona kutetea maslahi yao wakati huu wa kuandaa
katiba mpya.

Kauli hizo zilitolewa na Sheikh Nasor Mohameed, kutoka Zanzibar,
ambaye alikuwa mgeni rasmi. Baadaye zikaandaliwa kanda za CD
zilizosambaza ujumbe huo.

Uchunguzi unaonesha kuwa miongoni mwa makanisa yaliyochomwa hivi
karibuni huko Zanzibar ni ya EAGT, Elimu Pentecost na TAG, Anglikana,
Katoliki na FPCT, hivyo kujenga taswira ya ubaguzi wa kidini ambao
kama hautapatiwa dawa unaweza kuligawa taifa la Tanzania kama
ilivyotokea Nigeria na kwingineko barani Afrika.

Hofu yangu ni kuwa, roho hii ya ubaguzi wa kidini ambayo Baba wa Taifa
hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere aliifananisha na dhambi ya kula
nyama ya mtu, imekuwa ikiyatafuna mataifa ya Afrika kama ifuatavyo:

1. Mwaka 2000, vuguvugu la kuanzishwa kwa utawala wa Kiislamu
(Sharia), lilianza kwenye majimbo ya Kaskazini mwa Nigeria, miaka
michache baadaye majimbo kadhaa yakajitangazia sheria hizo na tangu
wakati huo kumekuwa na mapambano yasiyoisha. Takwimu zinaonesha kuwa
katika miaka ya karibuni zaidi ya Wakristo 500 wameuawa kikatili na
makanisa kuchomwa moto.

2. Roho hii imekuwa ikienea kwa kasi katika maeneo mbali mbali ya
Afrika ambapo imelikumba taifa la Mali, majimbo ya kaskazini tayari
yametangaza kujitenga na kuna vuguvugu lenye kuhusisha mapigano ya
silaha.

3. Itakumbukwa kuwa wiki chache tu zilizopita vuguvugu hili la kudai
utawala wa kidini liliibuka nchini Kenya ambapo watu wanaojiita
wanaharakati walianzisha madai ya kutaka eneo la Pwani kujitenga na
Jamhuri ya Kenya na kujitangazia taifa la Kiislamu.

4. Ni wakati huu ambao kundi la Uamsho linalopinga kuandikwa kwa
katiba mpya kabla ya kuitishwa kwa kura ya maoni ili wanzazibar waamue
kuhusu Muungano liliibuka na kuanzisha ghasia Zanzibar ambazo
zimepelekea makanisa kadhaa kuchomwa moto na mali kuharibiwa, huku
watu wa bara wakitishiwa maisha.

USHAURI WANGU KWA SERIKALI NA VIONGOZI WA DINI

Ni wajibu wa kila Mtanzania kutii sheria na mamlaka kwa kuwa zimewekwa/
kuruhusiwa na Mungu, hivyo kuziasi ni Kumuasi Mungu, yaani ni dhambi.
Hivyo kila Mtanzania anastahili kukumbuka wajibu wake wa kutii
mamlaka.

Viongozi wenzangu wa dini wakumbuke kuwa wana wajibu mkubwa katika
jamii, na jamii inawasikiliza hivyo ni vyema wakawa makini katika
matamshi na maelekezo yao ili wasiwe chanzo cha kuchochea vurugu za
kidini na uvunjaji wa amani.

Ni vyema wakati huu wa kuandikwa kwa katiba mpya, kila kikundi
kikafuata utaratibu uliowekwa badala ya kuchochea ghasia ambazo
madhara yake yatawakumba watanzania wote ikiwa ni pamoja na wao
wenyewe watoto na wajukuu zao.

Pia ningependa kuwashauri viongozi wa serikali kusimama imara katika
kusimamia sheria na haki, na kuepuka kauli au vitendo vitakavyofanya
baadhi ya watanzania kudhani kuwa hawatendewi haki.

Ni vema ieleweke kuwa matukio kama haya ya uvunjaji wa amani
yasipodhibitiwa na kukomeshwa haraka yanaweza kuumba chuki ambayo
inaweza kuibua mlipuko mkubwa na machungu kwa wananchi na matokeo yake
yakawa mabaya kwa Taifa zima. Hekima na busara inatufundisha kuwa
tusipoziba ufa tutajenga ukuta.

Ni vyema wenye dhamana ya kuongoza wakakumbuka kuwa wanawajibu mbele
ya Mungu aliyewaweka au kuwaruhusu kuingia madarakani na siku moja
watatoa hesabu mbele zake.

Mwisho, natoa wito kwa watanzania wenzangu tuulinde umoja, amani na
utengamano wa taifa letu, tuikimbie dhambi ya ubaguzi kwa kuwa
tukiiruhusu itatuangamiza sote. Tuliombee taifa letu na kukiwa na
mbegu ya chuki tuimalize kwa njia ya majadiliano na vikao vya pamoja
vinavyohusisha viongozi wa dini zote na serikali pia.

Imetolewa leo 28/05/2012
Na Dk. Barnabas Mtokambali
Askofu Mkuu wa TAG

Monday, May 28, 2012

Uamsho (Zanzibar): Taarifa kwa Vyombo vya Habari

Jumuia ya Uamsho (Zanzibar) imetoa taarifa kufuatia maandamano na kisha vurugu zilizotokea Zanzibar wiki hii. Nimezipata picha na taarifa kutoka Zanzibar Yetu. Inatia moyo kuona jinsi taarifa hiyo inavyoanza kwa kumtaja Allah na Mtume Muhammad na kisha kusisitiza suala la amani na kuheshimu haki za watu wote. Inatia moyo kuona jinsi taarifa hii inavyotaja wazi kuwa tunawajibika kuheshimiana, kutunza amani, kuheshimu mali na haki za kila mtu, ikiwemo kuheshimu dini na nyumba za ibada. Hayo ni mawaidha mema kabisa.

Ingekuwa mawaidha hayo yanatolewa na kusisitizwa kila wakati, katika mihadhara yote na mahubiri mengine, nje na ndani ya nyumba za ibada, nina imani amani ingedumu katika jamii. Lakini je, mawaidha hayo ndiyo yanayotolewa na kusisitizwa katika mihadhara na mahubiri yote?
Hapa kushoto ni picha mojawapo ya uharibifu uliofanyika wakati wa vurugu za wiki hii, ambapo kanisa lilichomwa moto, sambamba na hilo gari.
Waumini wa dini zote tunaweza kunukuu misahafu na kuthibitisha kuwa dini zetu zinafundisha amani. Lakini jambo la msingi zaidi sio kunukuu na kujadili misahafu, bali matendo yetu katika jamii na mbele ya Muumba. Hiki ndicho kigezo muhimu zaidi cha kupima kama sisi ni waumini kweli.

Taarifa tulizopata katika vyombo vya habari zimesema kuwa maandamano haya ya Uamsho yalikuwa ya kupinga Muungano. Tulisoma pia kuwa wana-Uamsho wanataka kupeleka malalamiko yao Umoja wa Mataifa.

Kilichonishangaza ni jinsi wana-Uamsho walivyojifanya kuwa wao ndio sauti ya wa-Zanzibari. Wanachotaka wao kifanyike. Nashangaa kwa nini wana-Uamsho wawe na msimamo huo, wakati wao ni sehemu tu ya jamii ya Zanzibar na kuna wenzao wenye mitazamo tofauti. Kwa mfano, Sheikh Muhidin Zubeir Muhidin, katibu wa jumuia ya maimam wa Zanzibar (JUMAZA) amenukuliwa kwamba "alisema Jumuiya yake ni tofauti na Jumuiya ya Uamsho hivyo watu wasizichanganye." Soma hapa.

Kwa nini wana-Uamsho wawe na msimamo wao huu hasa wakati huu ambapo wa-Tanzania tuko katika mchakato wa kutafuta maoni kuhusu Katiba na tume imeshaundwa ambayo itasikiliza maoni hayo. Nini kinachowafanya wana-Uamsho wachukue hatua ya kutaka kwenda Umoja wa Mataifa, wakati kuna hiyo fursa ya kuelezea mtazamo wao na kujumuika na wa-Tanzania wengine katika kutafuta suluhu ya matatizo? Kuhusu nani aliyechoma moto kanisa na kufanya uharibifu mwingine, tutajua baada ya uchunguzi kukamilika, na bora zaidi iwapo kesi itafika mahakamani na kuamuliwa.

Baada ya hizo kauli zangu, naleta tamko la Jumuia ya Uamsho:

THE ASSOCIATION FOR ISLAMIC MOBILISATION AND PROPAGATION

P. O. BOX: 1266 
Tel: +255-777-419473 / 434145-
FAX +255-024-2250022
E-Mailjumiki@hotmail.com
MKUNAZINI ZANZIBAR

Tarehe 27MAY2012 

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI 

Kila sifa njema anastahiki ALLAH (S.W) na Rehma na Amani zimuendee 
Mtume Muhammad (S.A.W), ahli zake, Maswahaba zake na walio wema katika
Uislamu.

Jumuia ya UAMSHO inatoa taarifa rasmi kwa umma wa Wazanzibari na 
Watanzania wote kwa ujumla kwamba haihusiki na vitendo vyote vya
uvunjaji wa amani vilivyotokea usiku wa tarehe 26 Mei 2012. Kama
alivyosema Mtume (S.A.W) katika Hijatul Wadaa, kwamba ni haramu
kumwaga damu zenu, kuharibiana mali zenu, kuvunjiana heshma zenu ila
kwa haki ya Uislamu (maana yake pale mtu anapofanya kosa na
likathibitika atahukumiwa kwa hukmu ya Kiislamu). Vile vile Uislamu
unaheshimu nyumba za ibada (Makanisa, Mahekalu na n.k) zisivunjwe wala
zisiharibiwe.

Jumuia inatoa wito kwa Waislamu na Wazanzibari wote kuendelea 
kudumisha amani na utulivu wa nchi na kutoharibu mali za serikali,
mali za wananchi, mali za taasisi za dini zenye imani tofauti, kwani
kufanya hivyo ni kwenda kinyume na mafundisho ya dini ya Kiislamu.
Jumuiya inayachukulia matukio yaliyotokea usiku wa jana, na
yanayoendelea tangu alfajiri leo, kama ni njama za makusudi za wale
wasioipendelea amani nchi hii, pamoja na kutaka kuipaka matope jumuiya
na kutaka kuzuia lengo la Wazanzibari kudai nchi yao.

Tunatoa wito kwa Jeshi la Polisi na Vyombo vyote vya Dola wafanye kazi 
zao kama wanavyotakiwa kwa mujibu wa muongozo wa haki za binadamu kwa
Polisi na vikosi vingine unaosema kwamba polisi na vyombo vingine vya
dola wana jukumu la kutunza amani na utulivu na jukumu la kutoingilia
haki za watu. Kila mtu anayo haki ya kuwekewa mazingira muafaka ya
kitaifa na kimataifa yatakayomuwezesha kupata haki zake za binadamu.

Polisi na vyombo vingine vya dola wana jukumu la kutunza amani na 
utulivu na jukumu la kutoingilia haki za watu isipokuwa tu kwa minajil
ya kulinda haki za wengine.

Polisi na vyombo vingine vya dola wana jukumu la kuheshimu, kulinda na 
kutetea haki za binadamu kwa watu wote.

WABILLLAH TAWFIQ 

Saturday, May 26, 2012

Wa-Tanzania Katika Shughuli za Kila Siku

Ninawawazia watu ninaowaona mitaani, kila mtu akiwa na harakati zake, mategemeo yake, na bila shaka wasi wasi na shida pia. Laiti ingewezekana kuongea na kila mtu na kuzipata habari zake.


Hapa ni Ubungo. Nilipiga picha hii nikiwa ndani ya basi kutokea mikoani. Nilivutiwa na huyu kijana mwenye mkokoteni, akiwa katika kujitafutia riziki. Barabara inavyopinda kushoto inaelekea Chuo Kikuu na Mwenge.
Hapa ni mjini Moshi.
Hapa ni kituo cha mabasi cha Msamvu, Morogoro.
Hapa ni Lyulilo, karibu na Matema Beach, Ziwa Nyasa. Ni siku ya soko, kama nilivyoelezea hapa.

Tuesday, May 22, 2012

Makaa Yetu ya Mawe Yanakwenda Wapi?

Hapa ni Bandari ya Ndumbi iliyopo mwambao mwa ziwa Nyasa.Bandari hii inatumika kusafirishia makaa ya mawe ambayo yanachimbwa katika kijiji cha Ngaka wilayani Mbinga mkoani Ruvuma.Takwimu zinaonesha kuwa kila wiki zaidi ya tani 600 za makaa ya makaa ya mawe zinasafirishwa kupitia bandari hii kupelekwa sehemu mbalimbali ndani na nje ya nchi.Hata hivyo hakuna anayefahamu ukweli kuhusu kile ambacho kinasafirishwa kupitia bandari hiyo ambayo haina ofisi muhimu za serikali.
 (Picha na maelezo na Albano Midelo, Maendeleo ni Vita)

Mnadani Karatu


Tanzania ni nchi kubwa, yenye mengi ya kuvutia. Mwaka 2008, kwa mfano, nilishuhudia mnada katika mji wa Karatu. Watu walijaa hapo kwenye viwanja vya mnada. Walikuwepo wauzaji na wateja wa bidhaa na huduma mbali mbali. Wengine, kama mimi, tulienda kuangalia. Kulikuwa na mengi ya kuyaona na hata kustaajabia.
Mnada hufanyika Karatu kila mwezi, tarehe 7. Katika pitapita zangu katika sehemu kama Mbulu, Karatu na Arusha, nimeona kuwa utamaduni huu wa minada umejengeka sana.


Siku ya mnada ni siku muhimu katika maisha ya watu wa sehemu hizo. Nami nikiwa maeneo hayo, sitakosa kuhudhuria.

Saturday, May 19, 2012

Mteja Anaporudi Tena

Niliwahi kuandika habari ya hao akina mama wanaoonekana nami katika hii picha, jinsi walivyonitembelea ofisini. Huyu aliyesimama kulia kanipigia simu wiki hii akiulizia upatikanaji wa nakala za kitabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences". Nakala aliyokuwa nayo imeazimwa na rafiki yake. Anataka nakala nyingine kwa ajili yake na kwa marafiki zake wengine. Mmoja wao anaenda Ghana, aende akifahamu atakayokumbana nayo kule, niliyoelezea kitabuni.

Basi, kwa kuzingatia yale ninayojifunza na kuwahubiria wengine kuhusu huduma kwa mteja, nimelitekeleza ombi hilo haraka na kumpelekea vitabu. Mteja anapokuja tena, kwa hiari yake mwenyewe, ni dalili nzuri. Inamaanisha karidhika au kafurahia huduma. Nawashangaa wanaoamini kuwa wateja huvutwa kwa mitishamba.

Thursday, May 17, 2012

Safari ya Afrika Kusini

Nimepata mwaliko kutoka mamlaka inayojumuisha vyama vya taaluma hapa Marekani, ACLS. Ni mwaliko wa kwenda kushiriki mkutano wa wanataaluma utakaofanyika katika Chuo Kikuu cha Witwatersrand, Afrika Kusini, Juni 15-17. Tutakutana katika kitengo cha utafiti kiitwacho WISER. Ni fursa ya wanataaluma mbali mbali kubadilishana mawazo na kutathmini hali na mwelekeo wa taaluma katika Afrika na ulimwenguni.

Sijawahi kukanyaga Afrika Kusini. Kwa hivi ninaingojea safari hii kwa hamu. Chuo Kikuu cha Witwatersrand ni maarufu. Kwa upande wangu, ninaposikia jina la Witwatersrand, au Johannesburg kwa ujumla, huwa nakumbuka mengi. Mbali ya harakati za ukombozi kama zile zilizoibuka Soweto, na mbali ya maandishi mbali mbali ambayo nimesoma na kufundisha katika masomo ya fasihi, jambo jingine muhimu kwangu ni kwamba baadhi ya vitabu vya Shaaban Robert vilichapishwa na Witwatersrand University Press. Hii ni kumbukumbu muhimu sana kwangu, na ningependa kuitembelea taasisi hiyo, ikiwezekana.

Kama kawaida, ninapokuwa katika mizunguko, nitachukua kamera yangu. Insh'Allah, wadau mtaona picha katika blogu hii.

Tuesday, May 15, 2012

Burudani Longido

Hapa kushoto ni mpiga gitaa tuliyemkuta Longido mwaka 2008. Longido ni mji mdogo kwenye barabara itokayo Arusha kwenda Namanga. Ni karibu na Namanga. Nilikuwa hapo na wanafunzi katika kozi kuhusu mwandishi Hemingway.
Tulikaa hapo siku mbili, tukifuatilia habari za Hemingway, ambaye alikuwa Kenya na Tanganyika miaka ya 1933-34 na 1953-54, akaandika mambo kadhaa kutokana na kuwepo kwake pande hizi. Hapo Longido tulikuwa wageni wa programu ya utalii inayoendeshwa na wenyeji wa hapo.
Akina mama walitupikia vizuri na baada ya chakula cha jioni ilifuata burudani ya muziki.
Huyu ndugu alikuwa anapiga gitaa na kuimba nyimbo mbali mbali, zikiwemo "zilipendwa" za Afrika Mashariki na za Marekani. Tulifurahi sana kwa burudani hiyo.

Friday, May 11, 2012

Mrembo

Katika kitabu changu kiitwacho Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, pamoja na masuala mengine, nimeongelea suala la urembo. Nimesema kuwa dhana ya urembo ni tofauti katika tamaduni mbali mbali na katika mazingira mbali mbali. Kwa mfano, nimenukuu hadithi ya mapokezi ya kabila la Efik-Ibibio, Nigeria, inayoelezea unene kama kigezo cha urembo: There was once a very fat woman who was made of oil. She was very beautiful and many young men applied to her parents for permission to marry her and offered a dowry; but the mother always refused.

Kifungu hiki nimekinukuu katika ukurasa 54 wa kitabu changu, na naweza kutoa tafsiri hii: Alikuwepo mwanamke mnene sana aliyeumbwa kwa mafuta. Alikuwa mzuri sana na vijana wengi waliwaomba wazazi wake ruhusa ya kumwoa wakatoa mahari, lakini mama mtu daima alikataa.

Katika kitabu changu cha CHANGAMOTO: Insha za Jamii, kuna sehemu ambayo inaongelea mashindano ya urembo, kukumbushia kuwa kila jamii inayojitambua na kujiheshimu ina dhana yake na vigezo vyake vya urembo. Mambo hubadilika, ila jambo la kulitafakari ni mchakato wa mabadiliko hayo ni wa aina gani na misingi yake ni ipi. (Picha niliyoweka hapa nimeiona Facebook}

Monday, May 7, 2012

Kituoni Mbamba Bay

Hapa ni eneo la kituo cha mabasi Mbamba Bay. Kama hakuna basi, unachoona ni huu uwanja na maduka pembeni, Nilikuwepo Mbamba Bay mwaka jana, kama nilivyoelezea hapa. Picha zinazoonekana hapa nilipiga wakati huo. Upande wa kulia wa mlima unaoonekana ndipo ziwani.
Maduka yameuzunguka uwanja huu, kama nilivyogusia hapa. Nyumba inayoonekana kulia katika picha hii hapa ndio ofisi ya kukatia tiketi. Kwa vile mji ni mdogo sana, na mabasi ni labda mawili tu kwa siku, ofisi haina kazi nyingi kama ilivyo katika miji mikubwa.
Basi likishafika, uwanja huu unapata uhai, kwa maana ya kuwepo na watu wengi, wakiwemo wasafiri wanaoshuka na wengine wanaopanda basi. Basi hili lilikuwa linatoka Liuli, likiwa njiani kwenda Songea.

Sunday, May 6, 2012

Mama Mjasiriamali, Baina ya Matema Beach na Tukuyu

Mwaka jana, nilifika hadi mkoani Mbeya, nikiwa na wanafunzi kutoka Marekani, kama nilivyoelezea hapa. Tukiwa njiani kutoka Matema Beach kuelekea Tukuyu, tulimkuta mama anauza soda na bidhaa zingine katika kibanda kando ya barabara. Mama huyu anaonekana hapa kushoto kabisa.Tulisimama hapo na kununua vitu viwili vitatu.
Kila ninapomkumbuka mama yule najiwa na mawazo ambayo yalinijia siku ile. Ni kuhusu wajasiriamali wanawake. Nimesoma taarifa kuwa akina mama hao wenye kipato hafifu wakiwezeshwa, huwa wajasiriamali makini. Mama kama huyu akipata mtaji mkubwa anaweza kufanya mambo makubwa.

Saturday, May 5, 2012

The Snows of Kilimanjaro

Wiki hii, nimesoma tena "The Snows of Kilimanjaro," hadithi maarufu ya Ernest Hemingway mwandishi m-Marekani aliyezaliwa mwaka 1899 akajiua kwa risasi mwaka 1960. Baada ya kusoma hadithi kwa makini, nimeangalia tena DVD iliyotokana na hadithi hii, ambamo waigizaji wakuu ni Gregory Peck na Ava Gardner.

Nimefuatilia maandishi na maisha ya Hemingway kwa muda mrefu. Hakuna siku inayopita bila mimi kusoma, kuwazia, au kuongelea habari za Hemingway. Ni mwandishi ambaye amenigusa kwa namna mbali mbali, kuanzia kipaji cha uandishi hadi falsafa yake kuhusu mambo mengi. Nimeunda hata kozi kuhusu mwandishi huyu, kama nilivyoelezea hapa na hapa.

"The Snows of Kilimanjaro" ni hadithi mojawapo maarufu kuliko zote katika lugha ya ki-Ingereza. Inamhusu mwandishi aitwaye Harry, ambaye tunamwona mbugani karibu na Kilimanjaro, akiwa anauguza kidonda mguuni, kilichotokana na kuchomwa mwiba wakati akiwinda. Ni kidonda kibaya, ambacho kinaonekana kutishia maisha ya Harry. Tunamwona mke wake Harry akifanya kila awezalo kumuuguza Harry, papo hapo akitegemea kuwa itakuja ndege ya kumchukua na kumpeleka hospitalini.

Katika hali hiyo ya kunyemelewa na kifo, Harry anakumbuka maisha yake na safari zake Ulaya na sehemu mbali mbali zingine. Anajutia jinsi alivyochelewa au kushindwa kuandika kuhusu mambo mengi aliyoyashuhudia na kuyafanya maishani, na sasa anafahamu kuwa hataweza kuandika tena. Jambo hilo linamwongezea msongo wa mawazo. Yeyote anayefahamu habari za Hemingway ataona kuwa Hemingway mwenyewe, katika miaka ya mwisho ya maisha yake, alisongwa na mawazo ya aina hiyo hiyo, kwa kutambua kuwa kipaji chake cha kuandika vizuri kilikuwa kinadidimia.

Katika hadithi ya "The Snows of Kilimanjaro" hatusikii sana habari za Kilimanjaro, ingawa tunajua fika kuwa wahusika wako mbugani karibu na mlima huo. Hemingway alianza hadithi yake kwa utangulizi ambao umekuwa maarufu sana:

Kilimanjaro is a snow-covered mountain 19,710 feet high, and is said to be the highest mountain in Africa. Its western summit is called the Masai "Ngaje Ngai," the House of God. Close to the western summit there is the dried and frozen carcass of a leopard. No one has explained what the leopard was seeking at that altitude.

Ajabu ya chui huyu na masuali anayozua, ni kama kielelezo cha masuali tata yanayojitokeza katika hadithi nzima, kuhusu maana ya maisha, mahusiano baina ya wanadamu, kama vile baina ya wanawake na wanaume, athari za utajiri wa fedha katika maisha, na kadhalika. Pamoja na yote mengine, Hemingway alikuwa mwanafalsafa aliyetafakari sana suala la uandishi na changamoto zake. Hadithi zake nyingi, kama vile Green Hills of Africa na A Moveable Feast, zinafafanua suala hili.

Waliotengeneza filamu hawakufuata kila kipengele au mtiririko kamili wa alichoandika Hemingway. Wameichukulia hadithi ya Hemingway kama kianzio au kichocheo cha ubunifu wao. Pamoja na kwamba wamefanya mabadiliko ya hapa na pale, filamu hiyo inatuwezesha kuona kwa vitendo yale tunayosoma katika hadithi, na pia inatuwezesha kuona taswira za sehemu mbali mbali zinazotajwa katika hadithi.

Kwa upande wetu wa-Tanzania, tungekuwa taifa makini katika kuvithamini vitabu, tungetumia vilivyo maandishi ya watu kama Hemingway kuitangaza nchi yetu. Lakini, jamii yetu ina umaskini wa fikra. Haivithamini vitabu, na matokeo yake ni kama wahenga walivyosema, kwamba kuku wa maskini hatagi. Watakuja wengine, wageni, kuzitumia fursa hizi, na kwa kweli wako ambao wanazitumia.

Friday, May 4, 2012

Nkrumah Hall, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam

Ukumbi wa Nkrumah ni moja ya sehemu muhimu sana katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Tangu nilipojiunga na Chuo hiki kama mwanafunzi, mwaka 1973, nilishuhudia umuhimu wa ukumbi huu wa mikutano.

Kwanza, napenda kusema kuwa ni jambo la heshima kuwa ukumbi huu ulipewa jina la Nkrumah, kiongozi maarufu wa harakati za ukombozi Afrika na duniani. Watu maarufu walihutubia katika ukumbi huu. Miaka niliyosoma na kufundisha pale, tuliwasikiliza watu kama Mwalimu Nyerere, William Tolbert, Gatsha Buthelezi, Robert Mugabe, Agostino Neto, Gora Ibrahim, Ali Mazrui, na Samir Amin.

Ukumbi huu ulikuwa ni sehemu ya mijadala baina ya watafiti na walimu maarufu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kama vile Walter Rodney, Wadada Nabudere, Yash Tandon, Mahmoud Mamdani, na Issa Shivji.

Kila aliyesoma au kufundisha hapa chuoni atakuwa na kumbukumbu za mambo au matukio ya ukumbi wa Nkrumah. Nami nina kumbukumbu zinazonihusu moja kwa moja. Kwa mfano, nilipokuwa mhadhiri msaidizi, bado kijana, jumuia ya walimu wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam, UDASA, ilinichagua kuwemo kwenye jopo la wahadhiri ambalo lilipewa jukumu la kulumbana na Profesa Ali Mazrui. Tulipambana na Profesa Mazrui, ambaye alipenda kuja chuoni hapo kulumbana na wasomi, akihoji msimamo wa ki-Marxisti ambao ulikuwa unatawala hapa chuoni. Fursa hii niliyopewa na UDASA ilinifanya nijisikie vizuri sana.

Nakumbuka kuwa baada ya mjadala, Profesa Mazrui aliniita na tukaongea kwa zaidi ya saa nzima kuhusu masuali mbali mbali ya mwelekeo wa chuo, taaluma, siasa na kadhalika.

Tukio jingine ninalolikumbuka lilitokea kwenye mwaka 1986 mwishoni. Uliandaliwa mjadala kuhusu mwelekeo na athari za siasa za Marekani kwa Tanzania na Afrika kwa ujumla. Niliteuliwa tena kuwa kwenye jopo ambamo alikuwepo Balozi wa Marekani, Bwana Don Petterson, na wahadhiri wengine kama wawili hivi. Nilikuwa nimerejea tu Tanzania kutoka Marekani, ambako nilisomea shahada ya uzamifu, 1980-86. Nilirejea na mawazo mengi na msisimko kuhusu suala hili la uhusiano baina ya Marekani na Tanzania. Ndio maana niliikaribisha kwa furaha fursa ya kuongelea mada hiyo mbele ya jumuia ya Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam.  Kwa taarifa, Balozi Don Petterson ameandika kitabu kuhusu Sudan na kingine kiitwacho Revolution in Zanzibar: An American Cold War Tale, ambacho ninacho, na nakipendekeza kwa wadau wote.