Wednesday, December 30, 2009

CHANGAMOTO: Insha za Jamii

Leo nimechapisha kitabu kipya. Kinaitwa CHANGAMOTO: Insha za Jamii. Ni mkusanyiko wa makala mbali mbali nilizoandika mwaka 2009, juu ya masuala ya uchumi, siasa, jamii, na utamaduni yanayoihusu Tanzania na dunia kwa ujumla.

Hiki ni kitabu changu cha kwanza katika lugha ya ki-Swahili. Naamini kuwa uzoefu niliopata utanisaidia siku zijazo.

Kwa kuanzia, kitabu hiki kinapatikana mtandaoni, pamoja na vitabu vyangu vingine. Bofya hapa.

Wednesday, December 23, 2009

KWA KINA NA PROF. JOSEPH MBELE

Ili kuwapa mwanga zaidi wasomaji wa blogu hii kuhusu fikra zangu, naleta tena mahojiano ambayo niliwahi kufanyiwa na blogu maarufu ya Bongo Celebrity. Bofya hapa.

Sunday, December 20, 2009

Bia za Kuzindulia Kitabu

Miaka michache iliyopita, nilichapisha kijitabu kuhusu Things Fall Apart. Nilimtumia ujumbe rafiki yangu aliyekuwa anaishi Dar es Salaam, kuhusu kuwepo kwa kijitabu hicho, naye akaniandikia hima. Nanukuu sehemu ya ujumbe wake:

Kuhusu habari ya kitabu nitajitahidi ili niweze kujulisha watu ila, naomba kitu kimoja ukija Tanzania tutafanya kitu kinachoitwa uzinduzi maana yake tutaalika waandishi wa habari jambo ambalo ni rahisi sana hapa kwetu ili mradi kinywaji kipatikane na tunaweza kualika kundi moja la mziki basi.

Aliendelea kufafanua mkakati huo, ikiwa ni pamoja na kuwaalika wageni muhimu, kama vile waziri wa elimu au naibu wake.

Wazo ambalo lilinata kichwani mwangu zaidi ni hili la kuandaa kinywaji. Kwa maneno mengine, nilitegemewa kununua bia nyingi. Bado sijafanya huu uzinduzi wa kufa mtu, nikinukuu usemi wa mitaani. Badala yake, najiuliza nchi yetu inakwenda wapi.

Wazo la bia za kuzindulia vitabu linaelezea vizuri hali halisi ya jamii ya Tanzania. Tumefikia mahali ambapo bia ndio njia ya kuwavutia watu kwenye shughuli mbali mbali. Nimewahi kuhudhuria maonesho ya kimataifa ya biashara Dar es Salaam. Nimejionea jinsi bia zinavyofurika kwenye viwanja vya maonesho, mwaka hadi mwaka. Inakuwa kama vile baa za Dar es Salaam zinahamia kwenye viwanja hivyo.

Nimehudhuria pia tamashala la Taifa la vitabu Dar es Salaam. Kama nilivyosema tena na tena katika blogu hii, mahudhurio kwenye tamasha hilo huwa ni duni sana, isipokuwa watoto wa shule na walimu. Sitashangaa iwapo tutaanza utaratibu wa kusogeza bia kwenye tamasha la vitabu ili kuwavutia watu. Bila shaka tutafikia mahali ambapo zitahitajika bia kuwavutia watu waende vyuoni.

Wednesday, December 2, 2009

Darasa Chini ya Mti

Makala hii, inayotokana na picha inayoonekana hapa chini, ilichapishwa katika gazeti la KWANZA JAMII. Ni makala ya pili. Kusoma makala ya kwanza, bofya hapa.


Darasa Chini ya Mti

Na Profesa Joseph L. Mbele

Nimeona picha kwenye blogu kadhaa ambayo inamwonyesha mwalimu na watoto wa darasa la kwanza, chini ya mbuyu. Ubao wa kuandikia umepigiliwa kwenye mbuyu. Kama inavyotegemewa, Watanzania wanalalamikia hali hiyo. Wanauliza kwa nini watoto wasome katika mazingira ya aina hii. Wengine, kama kawaida, wanaishutumu serikali.

Napenda kuliangalia zaidi suala la darasa kufanyika chini ya mti. Je, ni balaa kama tunavyodai au kunaweza kukawa na mtazamo mwingine?

Kuna vijiji na jumuia nyingi nchini mwetu ambazo hazina shule. Sababu moja ni kuwa idadi ya watu katika nchi yetu inaongezeka muda wote. Vijiji vinaenea sehemu za mbali ambazo zamani zilikuwa mapori au mashamba. Watoto wanatembea mwendo mrefu kwenda shuleni. Na kadiri watu wanavyoendelea kujenga mbali na shule, mwendo wa kutembea hadi shuleni unaongezeka.

Sasa je, ni bora watoto hao waendelee kwenda mwendo mrefu kila siku hadi kwenye shule au ni bora wapate fursa ya kusoma chini ya mti, hapo kijijini pao? Je, wangoje hadi wajengewe shule ya matofali iliyoezekwa bati, au ni bora wapewe fursa ya kuanza masomo chini ya mbuyu hapa hapa kijijini?

Katika vijiji vingi Tanzania, vikiwemo hivi vinavyoendelea kujitokeza, watu wana dhiki kifedha. Wanaishi kwenye nyumba za makuti na hawana kipato cha uhakika. Hawana uwezo kifedha lakini wanataka watoto wao waanze angalau kujifunza kusoma na kuandika. Wanafurahi kumpata mwalimu na wako tayari kuanzisha darasa chini ya mti. Kwa mtazamo wangu, watu hao wakifanikiwa kumpata mwalimu akaanzisha shule chini ya mti, ni hatua moja mbele.

Tuliangalie suala hili kwa mtazamo wa wanakijiji. Bila shaka walikaa, wakatathmini hali ya kijiji chao na mahitaji ya watoto wao, wakaamua kuanzisha shule. Walimtafuta mwalimu, wakatafuta huo ubao, na pia wakasogeza mbao za kukalia watoto. Walipitisha uamuzi kila mzazi atafute sare ya shule. Kwa kipato cha watu wa hapo, huenda huu mradi wa sare ulikuwa mgumu sana. Lakini wamejitahidi, na kila mtoto ana sare.

Hapo ubaoni zinaonekana hesabu za kujumlisha. Haya ni maendeleo kwa hao watoto na kwa hicho kijiji. Si sahihi kupuuzia ukweli huu. Tuwape wanakijiji wa hapo heshima wanayostahili, kwa juhudi waliyofanya hadi sasa. Sisemi turidhike na hali. Nasema kuwa wanakijiji hao wamepiga hatua inayostahili kutambuliwa.

Katika elimu, jambo la msingi si jengo. Wakristu tunafahamu kuwa Yesu alifundisha watu popote, na mafanikio yake hayakuathirika kwa sababu ya kukosa jengo. Watu wengi maarufu katika nchi yetu walianza shule chini ya mti. Marehemu Oscar Kambona, kwa mfano, alisoma shule ya msingi chini ya mwembe kijijini kwake Kwambe, karibu na Mbamba Bay. Mwembe huo bado uko.

Mwalimu Nyerere alipohamasisha kisomo cha watu wazima na kisomo chenye manufaa hakusema kuwa lazima pawe na majengo. Wengi walisoma chini ya mwembe au mkorosho.

Mambo mengi muhimu, kama vile mazungumzo na mijadala, yanaweza kufanyika chini ya mti. Mwalimu Nyerere alipoongelea demokrasia ya enzi za wahenga wetu, alisema kuwa wazee walikuwa wanakaa chini ya mti na kujadiliana hadi wakubaliane. Hakusema kuwa walikaa katika jumba la mikutano, nasi hatujawahi kulaumu kwa nini walikaa chini ya mti. Iweje suala la darasa kuwa chini ya mti litukera namna hii?

Katika kufundisha kwangu Marekani, nimeona kuwa nyakati ambapo jua linawaka vizuri, wanafunzi wanaomba tukafanyie darasa nje, chini ya mti. Ingawa mwanzoni, kutokana na mazoea, sikuwa napenda kuondoka darasani, hatimaye nilizoea. Siku inapokuwa nzuri, ni kawaida kuona madarasa yakifanyika chini ya miti. Ingawa Wamarekani hawafanyi darasa chini ya mti sababu ya kukosa majengo, hoja yangu ni kuwa kufanyia darasa chini ya mti haimaanishi kuwa elimu inadunishwa. Kuna mambo kadha wa kadha ya kuangalia kabla ya kutoa hukumu kama tunayotoa tunapoona watoto wakisoma chini ya mti.

Watanzania tunapoongelea elimu tuwe tunatofautisha kati ya mambo ya msingi na yasiyo ya msingi. Tukiona watoto wanasoma chini ya mti, tusitoe hukumu za upesi bila tafakari. Jambo la msingi ni somo au elimu, sio kuwepo au kutokuwepo kwa jengo. Jengo linaweza kuchangia ubora wa elimu katika mazingira fulani, lakini sio kila penye jengo bora pana elimu bora.

Tabia hii ya kutoangalia mambo ya msingi inajitokeza kwa namna nyingine pia katika nchi yetu. Watanzania wengi wanaamini kuwa watoto wakifundishwa kwa kiIngereza, elimu inakuwa bora. Wengi wanaamini kuwa watoto wakiweza kuongea kiIngereza wanakuwa wameelimika vizuri. Ndio maana kuna utitiri wa shule zinazotumia kiIngereza.

Siku hizi umezuka mtindo wa watoto kuvaa majoho na vikofia maalum wakati wanapohitimu shule. Majoho na vikofia vinachukuliwa kama dalili ya shule bora au elimu bora. Ukweli ni kuwa elimu si majoho wala vikofia. Watoto wanaweza kuwa wameelimika vizuri hata kama wanavaa kaptula na shati siku ya kuhitimu. Vivyo hivyo, kusoma chini ya mti si hoja. Cha msingi ni masomo yenyewe.

Ninaposema hayo yote simaanishi kuwa majengo hayana umuhimu. Lakini si vizuri kusema kuwa kila jamii ingoje hadi ijenge majengo mazuri ndipo watoto waanze kufundishwa na mwalimu. Ni bora mwalimu aanze darasa chini ya mti. Kama watoto wana daftari na kalamu, na mwalimu wao ana ubao na chaki, inatosha, kwa kuanzia.
Kadiri kijiji kinavyopata nguvu, kinaweza kujikongoja na shughuli ya majengo na mahitaji mengine.