Sunday, December 20, 2009

Bia za Kuzindulia Kitabu

Miaka michache iliyopita, nilichapisha kijitabu kuhusu Things Fall Apart. Nilimtumia ujumbe rafiki yangu aliyekuwa anaishi Dar es Salaam, kuhusu kuwepo kwa kijitabu hicho, naye akaniandikia hima. Nanukuu sehemu ya ujumbe wake:

Kuhusu habari ya kitabu nitajitahidi ili niweze kujulisha watu ila, naomba kitu kimoja ukija Tanzania tutafanya kitu kinachoitwa uzinduzi maana yake tutaalika waandishi wa habari jambo ambalo ni rahisi sana hapa kwetu ili mradi kinywaji kipatikane na tunaweza kualika kundi moja la mziki basi.

Aliendelea kufafanua mkakati huo, ikiwa ni pamoja na kuwaalika wageni muhimu, kama vile waziri wa elimu au naibu wake.

Wazo ambalo lilinata kichwani mwangu zaidi ni hili la kuandaa kinywaji. Kwa maneno mengine, nilitegemewa kununua bia nyingi. Bado sijafanya huu uzinduzi wa kufa mtu, nikinukuu usemi wa mitaani. Badala yake, najiuliza nchi yetu inakwenda wapi.

Wazo la bia za kuzindulia vitabu linaelezea vizuri hali halisi ya jamii ya Tanzania. Tumefikia mahali ambapo bia ndio njia ya kuwavutia watu kwenye shughuli mbali mbali. Nimewahi kuhudhuria maonesho ya kimataifa ya biashara Dar es Salaam. Nimejionea jinsi bia zinavyofurika kwenye viwanja vya maonesho, mwaka hadi mwaka. Inakuwa kama vile baa za Dar es Salaam zinahamia kwenye viwanja hivyo.

Nimehudhuria pia tamashala la Taifa la vitabu Dar es Salaam. Kama nilivyosema tena na tena katika blogu hii, mahudhurio kwenye tamasha hilo huwa ni duni sana, isipokuwa watoto wa shule na walimu. Sitashangaa iwapo tutaanza utaratibu wa kusogeza bia kwenye tamasha la vitabu ili kuwavutia watu. Bila shaka tutafikia mahali ambapo zitahitajika bia kuwavutia watu waende vyuoni.

5 comments:

Simon Kitururu said...

Na mpaka kwenye Semina za kuelimisha usipotangaza kuna Posho na Mlo ingawa ni kwa manufaa ya wahudhuriaji , pia kuna wengi hugoma kwenda kwenye hizo semina.:-(

Nikiongea kama mpenda BIA na ELIMU:...

-Kama katika jamii BIA inamvuto kuliko ELIMU, basi kazi ipo sana tu katika anga nzima ya elimu kuelimisha JAMII angalau ni nini muhimu maishani!:-(

Godwin Habib Meghji said...

Profesa Mbele ninakushangaa sana kuona kitu hichi kama ni kipya. Huu ni utamaduni wetu Wa-afrika toka enzi na enzi

Kuna vijiji vingi Tanzania nimetembelea nikakuta wanakijiji wa huko WANATISHA POMBE ili kukusanya watu wa kwenda kulima kwenye mamshamba yao.

Wenyeji wa Kilimanjaro toka enzi na enzi lazima kuwe na mbege kwa wazee kukutana kwa maamuzi mazito.
Nimejaribu kuuliza uliza waafrika wengine ninaoishi nao jirani, na kwao mambo ni kama haya haya

Kwa hiyo swala la KILAURI kwenye shughuli za Waafrika ni kitu cha kawaida kabisa.

SITETEI HUO UTAMADUNI ila ninakumbusha tu si swala jipya.

Mbele said...

Mheshimiwa Godwin, hoja yako naiona ina mantiki nzuri. Ningekumbuka hilo suala la utamaduni unaloongelea, nadhani ningepunguza malalamiko yangu.

Naafiki hoja yako kufuatana na mabadiliko ya mazingira, hizi bia zinachukua wadhifa ambao ulishikiliwa na mbege, rubisi au wanzuki enzi za wahenga wetu.

Hata hivyo, wahenga walikuwa wanazingatia kazi. Kama unavyosema, waliitisha pombe ya kulimia. Na ukweli ni kuwa lengo lilikuwa ni kulima.

Leo hii, tumepoteza lengo. Watu wataitisha bia za kuzindulia kitabu na watazitwanga kweli hizo bia. Lakini vitabu hawatanunua wala hawatasoma, labda viwe vya udaku. Wakishamaliza bia za uzinduzi wa kitabu, pesa zao wataenda nazo baa asubuhi kununua bia za kuzimulia.

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...

bia bia, pombe za kuzindua kitabu????????

sikubali

Mbele said...

Ndugu Kamala, suala unaloibua ni zuri. Ingawa tafsiri ya neno "beer" ni pombe, tunakumbana na suala la jinsi lugha inavyotumika katika jamii. Nadhani taaluma hii inaitwa isimu-jamii. Kwa ki-Ingereza wanasema "socio-linguistics."

Kwa kuzingatia hilo, ni kwamba ingawa neno bia lina maana ya "beer," jamii inalitumia kwa maana ya pombe zinazotengenezwa viwandani ambazo tunazinunua kwenye vyupa au vikopo.

Katika jamii, neno bia limepewa hii maana na linaeleweka hivyo, ili kutofautisha na rubisi, kayoga, kimpumu, nipa, au pingu.

Ukisema "pombe," kwa kawaida watu wanaelewa hizi zinazoitwa pombe za kienyeji.

Halafu, hata neno lenyewe "beer" nalo limechukua tabia hii hii. Tukiwa na maana ya kuitaja pingu, rubisi, au kimpumu, hatusemi "beer" bali tunasema "local beer" au "local brew."

Kwa hivi, tunapozungumza, tunajikuta tukifanya mahesabu yote hayo ili tueleweke.

Ukiwaita watu kwenye uzinduzi wa kitabu chako, ukawatangazia kuwa unatayarisha pombe nyingi za kuzindulia hiki kitabu, wengine wanaweza kuingia mitini, kwa kudhani kuwa unawatayarishia komoni na wanzuki, badala ya bia :-)

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...