Saturday, January 30, 2016

Mungu ni Mmoja Tu

Dini ni kati ya masuala ninayopenda kuyaongelea katika blogu hii. Kwa kitambo sasa, nimekuwa nikielezea imani yangu kwamba kuna Mungu mmoja tu. Nimekuwa nikielezea ulazima wa kuziheshimu dini zote. Nilikuwa nikisema hayo yote nikiwa najitambua kuwa ni m-Katoliki. Sijui wa-Katoliki wenzangu walinionaje, na sijui wa-Kristu wenzangu walinionaje. Sijui watu wa dini zingine walinionaje.

Ninafurahi kwamba mkuu wa kanisa Katoliki, Papa Francis, ana mwelekeo huo huo. Dalili za mwelekeo wake zilianza kujitokeza tangu mwanzo wa utumishi wake kama Papa. Aliongeza kasi ya kujenga mahusiano baina ya dini mbali mbali, akifuata mkondo ulioanzishwa na mapapa waliotangulia.

Leo nimeona taarifa kuwa Papa Francis ameweka msimamo wake kuhusu dini mbali mbali kwa uwazi kuliko siku zilizopita. Amesema kuwa dini zote ni njia mbali mbali za kumwelekeza binadamu kwa Mungu. Nimeona kuwa msimamo huu ni changamoto kubwa ambayo inahitaji kutafakariwa.

Kwa kuzingatia mtazamo huu wa Papa Francis, ninaona kuwa ni ujinga kwa watu wa dini mbali mbali kulumbana kuhusu ipi ni dini ya kweli, au ipi ni dini bora zaidi. Nawazia hali ilivyo Tanzania, kwa mfano, na malumbano baina ya baadhi ya wa-Islam na baadhi ya wa-Kristu, kuhusu usahihi au ubora wa dini zao. Naona ni ujinga mtupu.

Mara kwa mara nimewazia suala hili kwa kutumia mfano wa watu wanaopanda mlima Kilimanjaro. Kuna njia mbali mbali za kufikia kileleni. Itakuwa ni ujinga kwa watumiaji wa njia mbali mbali kugombana juu ya ipi ni njia sahihi. Njia zote zinaishia mahali pamoja, yaani kileleni. Safari ya mbinguni nayo ina njia mbali mbali.

Sunday, January 24, 2016

Nimemkumbuka Shakespeare

Leo, bila kutegemea, nimemkumbuka Shakespeare. Nimeona niandike neno juu yake, kama nilivyowahi kufanya. Nimekumbuka tulivyosoma maandishi yake tukiwa vijana katika shule ya sekondari.

Katika kiwango kile, tulisoma tamthilia tulizozimudu, kama The Merchant of Venice na Julius Caesar. "High school," ambayo kwangu ilikuwa Mkwawa, tulisoma tamthilia ngumu zaidi, kama Othello na Hamlet. Othello ilikuwa katika silabasi ya "Literature."

Nakumbuka sana kuwa hapo hapo Mkwawa High School tuliangalia filamu ya Hamlet, ambamo aliyeigiza kama Hamlet alikuwa Sir Lawrence Olivier. Huyu ni mmoja wa waigizaji maarufu kabisa wa wahusika wakuu wa Shakespeare. Niliguswa na uigizaji wake kiasi cha kujiaminisha kwamba sitaweza kushuhudia tena uigizaji uliotukuka namna ile. Nilipoteza hamu ya kuangalia filamu yoyote baada ya pale, kwa miaka mingi.

Ninavyomkumbuka Shakespeare, ninajikuta nikikumbuka mambo mengi. Kwa mfano, nakumbuka tafsiri murua za Mwalimu Julius Nyerere za tamthilia mbili za Shakespeare: The Merchant of Venice na Julius Caesar. Nakumbuka pia jinsi Shaaban Robert alivyomsifu Shakespeare, kwamba akili yake ilikuwa kama bahari pana ambayo mawimbi yake yalikuwa yanatua kwenye fukwe zote duniani.

Shaaban Robert alitoboa ukweli; Shakespeare ni mwalimu asiye na mfano. Aliingia katika nafsi za wanadamu akaelezea silika na tabia zao kwa ustadi mkubwa, na alitafakari uhalisi wa maisha yetu akatuonyesha maana na mapungufu yake. Alitukumbusha kwamba dunia ni kama jukwaa la maigizo, ambapo kila mmoja wetu anakuja na kutimiza yanayomhusu na kisha anatoweka.

Ningeweza kusema mengi juu ya Shakespeare. Ninapenda tu kuleta moja ya tungo zake ziitwazo "sonnets." Hii ni "sonnet" namba 2. Labda kuna siku nitapata hamu ya kuutafsiri utumgo huu, kujipima uwezo wangu wa kutafsiri na ufahamu wangu wa ki-Swahili.

Sonnet 2

When forty winters shall besiege thy brow
And dig deep trenches in thy beauty’s field,
Thy youth’s proud livery, so gazed on now,
Will be a tattered weed, of small worth held.
Then being asked where all thy beauty lies,
Where all the treasure of thy lusty days,
To say within thine own deep-sunken eyes
Were an all-eating shame and thriftless praise.
How much more praise deserved thy beauty’s use
If thou couldst answer, “This fair child of mine
Shall sum my count and make my old excuse,”
Proving his beauty by succession thine.
  This were to be new made when thou art old,
  And see thy blood warm when thou feel’st it cold.

Monday, January 18, 2016

Kupigwa Marufuku kwa Gazeti la "Mawio"

Nimesoma taarifa kuwa serikali ya Tanzania imelifuta gazeti la "Mawio." Taarifa hizi nimezisoma mitandaoni, kama vile blogu ya Michuzi. Napenda kusema kwamba siafiki hatua hii ya serikali. Msimamo wangu tangu zamani ni kutetea haki na uhuru wa kutoa mawazo. Ninatetea uhuru wa waandishi na uhuru wa vyombo vya habari.

Nimewahi kugusia suala hili katika blogu hii.  Msimamo wangu unaendana na tangazo la kimataifa la haki za binadamu, ambalo limetamka:

Everyone has the right to freedom of opinion and expression; this right includes freedom to hold opinions without interference and to seek, receive and impart information and ideas through any media and regardless of frontiers.

Kupiga marufuku gazeti ni kuhujumu haki ya waandishi na wamiliki wa gazeti kueneza habari na mawazo, na ni kuhujumu haki ya wasomaji kupata habari na mawazo. Kwa msingi huu, ninapinga hatua ya serikali ya kulipiga marufuku gazeti la "Mawio."

Serikali ya CCM inapiga marufuku magazeti kwa kutumia sheria kandamizi ambazo zimekuwa zikilalamikiwa kwa miaka na miaka. Serikali inadai kuwa hatua zake ni sahihi kisheria. Lakini msimamo huu una matatizo.

Kwanza hii sheria haitendi haki, bali inahujumu haki. Ni kama zilivyokuwa sheria za utawala wa kikaburu Afrika Kusini, ambazo zilikuwa halali kwa misingi ya sheria lakini si za haki. Mfumo mzima wa ukaburu ulikuwa halali kisheria, lakini haukuwa wa haki.

Pili, kazi ya kutafsiri sheria si ya serikali wala mamlaka nyingine yoyote, bali ni ya mahakama. Kama serikali inaona gazeti limekiuka sheria, wajibu wake ni kulipeleka gazeti mahakamani. Tufanye hima kuondoa sheria za kikaburu ili mahakama ziwe zinatoa haki.

Kwa mtazamo wangu, kufungia au kupiga marufuku gazeti ni dharau kwa jamii. Ni kusema kuwa jamii haina akili ya kuweza kusoma na kuchambua kilichoandikwa. Kama wa-Tanzania wameridhika kutukanwa namna hiyo, mimi simo. Ninajitambua kuwa nina akili timamu, na ninatetea, ninaheshimu na kutumia haki na uhuru wangu wa kusoma nitakacho.

Hoja ya serikali kwamba gazeti la "Mawio" linaandika taarifa za uchochezi haina mashiko. Serikali inadai kwamba tangu mwezi Juni mwaka 2013 gazeti la "Mawio" limekuwa likiambiwa libadili mwelekeo likakaidi. Sasa basi, kama gazeti limeandika linavyoandika kwa miaka yote hii na jamii imeendelea kuwa na amani, hili wazo la uchochezi linatoka wapi na lina ushahidi gani?

Serikali au mamlaka yoyote inayotumia ubabe ndio inahatarisha amani. Uvunjifu wa haki ndio uchochezi. Gazeti likiripoti hayo halifanyi uchochezi, kwani jamii inayoumia haihitaji kuambiwa na gazeti kuwa inaumia. Jamii hiyo ikizuiwa hata kusema, na machungu yakabaki yanafukuta moyoni, ni hatari ya kutokea mlipuko. Hilo ni jambo linaloeleweka katika taaluma ya saikolojia. Ni bora watu wawe huru kuelezea mawazo na hisia zao. Wanaozuia uhuru huo wakumbuke kauli ya wahenga kuwa kimya kingi kina mshindo mkuu.

Friday, January 15, 2016

Vitabu vya Kozi: Waandishi Wanawake wa ki-Islam

Jana, kama ninavyofanya kila siku, niliingia katika duka la vitabu la hapa chuoni St. Olaf, kuona kama vitabu vya kozi zangu za muhula ujao vimefika. Ni utaratibu wetu kwamba miezi au wiki kadhaa kabla ya kuanza masomo, tunapeleka dukani orodha ya vitabu tunavyotaka kutumia, na idadi yake, ili wanafunzi wavinunue.

Lengo langu hasa lilikuwa kuona kama vitabu vya kozi yangu mpya, "Muslim Women Writers," vimefika. Nimeona kuwa vyote vimefika, na hapa naleta orodha ya waandishi na vitabu, na majina ya wachapishaji:

1. Aboulela, Leila. Minaret. Grove. 
2. Ali, Monica. Brick Lane. Scribner.
3. Ba, Mariama. So Long a Letter. Waveland Press, Inc.
4. el Saadawi, Nawal. The Fall of the Imam. Telegram Books.
5. Hossein, Rokeya S. Sultana's Dream. Feminist Press.
6. Mattu, Ayesha. & Nura Maznavi. Love, InshAllah. Soft Skull Press.
7. Nafisi, Azar. Reading Lolita in Tehran. Random.

Nimekuwa nikiandika kuhusu kozi hii mpya katika blogu hii, kuelezea ninavyojiandaa kuifundisha. Nina hamasa juu ya kozi hii kwa sababu ya umuhimu wake, sio tu kwa maana ya kuelimisha jamii juu ya u-Islam, bali juu ya uwepo wa fasihi inayoandikwa na wanawake wa ki-Islam. Upekee wa kozi hii ni kwamba inahoji dhana iliyoenea miongoni mwa wengi kwamba wanawake wa ki-Islam hawana sauti au hawapaswi kuwa na sauti katika jamii.

Kama ilivyo kawaida yangu ninapofundisha fasihi yoyote, huwa napenda kufundisha vitabu nilivyowahi kusoma na vingine ambavyo sijavisoma. Wakati mwingine naweka zaidi vile ambavyo sijavisoma. Ninafanya hivyo kwa sababu fasihi ni bahari kubwa inayoendelea kujaa. Kuna waandishi wa zamani ambao wamefariki na kuna walio hai, na wengine watajitokeza baadaye. Haiwezekani kusoma kila kilichoandikwa. Fasihi ni bahari inayoendelea kujaa.

Katika orodha niliyoweka hapa juu, nimefundisha kazi za waandishi watatu. Wa kwanza ni Mariama Ba wa Senegal. Nilishafundisha riwaya zake mbili: So Long a Letter na Scarlet Song. Halafu nilifundisha riwaya mbili za Nawal el Saadawi: wa Misri: Woman at Point Zero na The Fall of the Imam. Mwaka juzi nilifundisha Minaret, riwaya ya Leila Aboulela wa Sudan Nitakuwa na urahisi fulani katika kufundisha maandishi yao katika kozi ya "Muslim Women Writers."

Hao wengine ni wapya kwangu. Nimewahi kusikia majina yao tu, na sijawahi hata kuwa na vitabu vyao, isipokuwa kimoja cha Monica Ali, ambacho pamoja kuwa nilikinunua miaka michache iliyopita, sijawahi kukisoma, hata ukurasa moja. Kwa hali hiyo, kuwasoma waandishi hao itakuwa ni kupanua na kutajirisha akili yangu.


Nina dukuduku zaidi kusoma Love, InshAllah, kitabu ambacho ni mkusanyo wa maandishi ya waandishi wengi, wanawake wa ki-Islam, waishio hapa Marekani. Baada ya kufundisha kozi hii kwa mara ya kwanza, nitaifundisha tena muhula utakaofuata, na wakati ule nitaweza kuingiza riwaya za waandishi wengine, kama vile Assia Djebar wa Algeria, na Alifa Rifaat wa Misri, ambaye kitabu cha hadithi zake, Distant View of a Minaret nimewahi kufundisha.

Tuesday, January 12, 2016

Kitabu "Qur'an and Woman" Kimewasili

Ninafurahi kwamba kitabu nilichoagiza hivi karibuni, Qur'an and Woman, kilichotungwa na Amina Wadud, nilikipata jana. Siku chache zilizopia, katika blogu hii, niliandika kuwa nimeagiza kitabu hiki.

Niliagiza kitabu hiki ili nikisome, kama sehemu ya maandalizi ya kufundisha kozi mpya, "Muslim Women Writers" hapa chuoni St. Olaf, juu ya fasihi iliyoandikwa na wanawake wa ki-Islam kutoka sehemu mbali mbali za dunia.

Mara nilipokipata, nilisoma utangulizi, ambao umenivutia, kwa jinsi ulivyoelezea mambo yaliyomo kitabuni. Mwandishi alifanya utafiti wa miaka kadhaa katika kuandaa kitabu hiki, ambacho kinaweka wazi vigezo vya kutathmini nafasi ya mwanamke katika u-Islam.

Mwandishi anasema kuwa aliamua kusimama na kuzama katika Qur'an, kwa kuwa hiki ni kitabu kinachokubalika na kuheshimiwa na wa-Islam wote, pasipo wasi wasi wala ubishi. Kwa hivi, ili kuelezea nafasi ya mwanamke katika u-Islam, aliona ni muhimu kujikita katika Qur'an.

Mwandishi anasema kwamba katika jamii za ki-Islam, wanawake wana hadhi duni kwa kulinganisha na wanaume. Lakini, ili kubaini hadhi ya wanawake katika u-Islam, hatuwezi kuzingatia hali yao katika jamii, bali turudi katika Qur'an. Katika utafiti wake wa kina wa Qur'an, amethibitisha kuwa Qur'an haimweki mwanamke chini ya mwanamme. Inamweka kama mshirika wa mwanaume, na wote wawili wanategemeana, bila mmoja kuwa bora au juu ya mwenzake. Anaandika:

Mercifully, the more research I did into the Qur'an, unfettered by centuries of historical androcentric reading and Arabo-Islamic cultural predilections, the more affirmed I was that in Islam the female person was intended to be primordially, cosmologically, eschatologically, spiritually, and morally a full human being, equal to all who accepted Allah as Lord, Muhammad as prophet, and Islam as din.

Huu ndio mtindo wa uandishi anaotumia Amina Wadud, lugha pevu inayopiga shabaha kwenye hoja. Kwa leo, sitataja kila kilichomo katika utangulizi wake. Nitabakiza  kiporo, nimpe msomaji fursa ya kucheua hicho kiasi. Nitaendelea siku nyingine, Insh'Allah. Ninaandika mambo hayo kama namna ya kujidhihirishia maendeleo yangu katika kutafuta elimu.

Thursday, January 7, 2016

Qur'an na Mwanamke

Siku chache zilizopita, niliandika kuhusu maandalizi ninayofanya kwa ajili ya kufundisha kozi mpya "Muslim Women Writers," hapa chuoni St. Olaf. Niliandika maelezo mafupi ya lengo la kozi hii katika blogu yangu ya ki-Ingereza.

Katika maandalizi ya kozi hiyo, na wakati wa kuifundisha, na siku za baadaye, ninawazia kuisoma Qur'an. Lakini, mbali na fasihi nitakayofundisha, fasihi iliyoandikwa na wanawake wa-Islam, nimeona itakuwa vizuri pia nikitafuta maandishi ya wanawake yanayoichambua Qur'an. Kwa bahati nzuri, nimeona kuwa maandishi haya yako, vikiwemo vitabu.

Baada ya kuzipitia taarifa za vitabu hivi, nimeagiza kitabu cha Amina Wadud, Qur'an and Woman: Rereading the Sacred Text From a Woman's Perspective. Kwa mujibu wa maelezo niliyosoma, kitabu hiki kinafuatilia historia ya maandishi kuhusu Qur'an na mwanamke, historia inayothibitisha jinsi wanaume walivyopotosha mafundisho ya Qur'an na kuhalalisha mfumo unaowapendelea wanaume na kuwakandamiza wanawake. Maelezo yanabainisha pia kuwa mwandishi amefafanua maana za maneno ya ki-Arabu yalivyotumika katika Qur'an. Taarifa kuwa mwandishi amezingatia taaluma ya maana za maneno, ambayo kwa ki-Ingereza inaitwa "semantics," imenivutia.

Kuna misimamo mbali mbali miongoni mwa wanawake wasomi wa ki-Islam kuhusu suala la u-Islam na mwanamke. Wako ambao wanasema kuwa u-Islam ni dini kandamizi kwa wanawake. Mfano ni Wafa Sultan kutoka Syria, aliyeandika kitabu kiitwacho A God Who Hates na Ayaan Hirsi Ali kutoka Somalia, aliyeandika vitabu kama Infidel na Heretic.

Wako pia ambao wanasema Qur'an inawapa haki na uhuru wanawake, bali jadi ya kuichambua imekuwa ya upotoshaji ambao umesababisha kuhalalisha unyanyasaji na ukandamizaji wa wanawake. Kati ya wanawake wenye mtazamo huo ni huyu Amina Wadud ambaye nimemtaja na Fatima Mernissi wa Morocco, ambaye ameandika vitabu kama Beyond the Veil na The Male Elite: A Feminist Interpretation of Women's Rights in Islam.

Haya ni malumbano katika nyanja za elimu jamii kama historia, soshiolojia, na falsafa. Yana nafasi yake katika mijadala kuhusu fasihi, lakini fasihi inajieleza yenyewe. Nitasubiri hadi kozi yangu ianze ndipo nitaweza kuelezea yatakayokuwa yanajitokeza katika kusoma hizi kazi za fasihi.

Tuesday, January 5, 2016

Yule Binti Bukola Ametua Ikulu ya Marekani Leo

Siku kadhaa zilizopita, niliandika kuhusu binti Bukola Oriola katika blogu hii. Huyu ni binti kutoka Nigeria ambaye alipatikana na mkasa wa kutumikishwa na kunyanyaswa huku Marekani kwa miaka miwili na mtu ambaye alikuwa ni mume wake, ambaye naye alikuwa m-Nigeria.

Hatimaye, kwa bahati nzuri, aliokolewa, na katika ujumbe wangu nilitoa taarifa ya kuteuliwa kwake kama mjumbe katika tume ya serikali ya Marekani ya kutoa ushauri kuhusu majanga haya ya watu kusafirishwa kwa ghilba, kutumikishwa na kunyanyaswa.

Leo, Bukola na wanatume wenzake wamekutana kwa mara ya kwanza katika Ikulu ya Marekani, kama inavyoonekana pichani, wakiwa na Mheshimiwa John Kerry, "Secretary of State," wa tano kutoka kulia. Bukola anaonekana amevaa kilemba chekundu. Nimeona nilete taarifa hii hapa kuonyesha hatua hii ya safari ya Bukola. Vile vile, nataka kusema kwamba tatizo tunaloongelea hapa ni la dunia nzima. Tusijiziuke, hata wa-Tanzania wanakumbana nalo. Ni tatizo lisilojali jinsia, umri, dini, au rangi ya mtu.

Wako ambao wanarubuniwa kwenda nchi za nje kwa ahadi au mategemeo ya mafanikio lakini wanaishia kuwa mateka na kunyanyasika kama watumwa. Sio lazima kwenda nje ya nchi. Wengine hurubuniwa kutoka vijijini au sehemu nyingine nchini na kupelekwa sehemu tofauti humo humo nchini, hasa mijini, ambako wanatumikishwa na kunyanyaswa. Yote hayo ni matatizo yanayotambuliwa kama "human trafficking" kwa ki-Ingereza.

Napenda kumalizia kwa kusema kwamba, kwa kufuatana na ukaribu wangu na huyu binti Bukola, na kwa kufahamu alivyo na uchungu na tatizo hili, na ari ya kuwasaidia wanaoteseka nalo, na ufahamu wake wa fursa zilizopo za kuwasaidia waathirika, napenda kusema, hasa kwa wa-Tanzania walioko hapa Marekani, lakini kwa wengine pia, kuwa yeyote mwenye kuhitaji msaada, nitaweza kumwunganisha na Bukola hima, ili tatizo lake lianze kushughulikiwa. Mambo hayo ni nyeti, na usiri unazingatiwa vilivyo.

Hapa kushoto anaonekana Bukola katika "selfie" na Bwana John Kerry.

Monday, January 4, 2016

Nawazia Dini na Uandishi wa Wanawake wa ki-Islam

Muhula ujao, kuanzia mwezi Februari hadi Mei, nitafundisha kozi mpya hapa chuoni St. Olaf ambayo nimeiita "Muslim Women Writers." Ni kozi ya fasihi kwa ki-Ingereza, ambamo tutasoma maandishi ya wanawake wa-Islam kutoka Bangladesh, India, Iran, Misri, Sudan, Senegal, na Marekani. Taarifa fupi ya kozi hiyo nimeandika hapa.

Wakati huu ninapongojea kufundisha kozi hii katika mazingira ya leo ambamo maelewano miongoni mwa waumini wa dini na madhehebu mbali mbali yanatatanisha, ninajikuta nikiwazia mara kwa mara masuala ya dini. Katika siku zijazo, labda kwa miezi kadhaa, ninategemea kuandika tena na tena katika blogu hii kuhusu dini na kozi yangu.

Nimeshaandika mara kadhaa kuhusu dini. Nimeandika kuhusu umuhimu wa mijadala ya dini, umuhimu wa kuziheshimu dini zote, na nilivyozuru nyumba za ibada za dini nyingine. Sioni mantiki kwa dini yoyote kuwafundisha waumini wake kwamba Muumba anawapenda wao zaidi kuliko watu wa dini nyingine. Msimamo wangu ni kwamba Mungu (Allah) hana ubaguzi.

Ninafurahi na kujivunia kwamba kanisa langu Katoliki linasimama katika msingi huo, kama ilivyodhihirishwa katika ziara na ujumbe wa Papa John Paul wa Pili nchini Nigeria, ziara ya Papa Francis katika msikiti Uturuki, na katika sala ya Papa Francis ya kuuombea ulimwengu. Na zaidi ni kuwa Kanisa Katoliki lina baraza la kujenga maelewano miongoni mwa dini mbali mbali liitwalo Pontifical Council for Inter-religious Dialogue.

Katika kujiandaa kwa kozi yangu, nimekuwa nikiwazia kuwa ingekuwa vizuri kama ningesoma Quran yote. Ninayo Quran takriban tangu mwaka 1982. Nimekuwa nikisoma visehemu hapa na pale, lakini si yote kikamilifu. Ingawa ninafahamu misingi ya u-Islam kiasi cha kuridhisha, wazo la kuisoma Quran linanivutia.

Kuna mambo mengine ambayo nimekuwa nikifanya, kama vile utafiti ili kufahamu misimamo na mitazamo ya wanawake wa-Islam kuhusu u-Islam na nafasi yao katika dini hiyo. Nimeanza pia kuwatafuta wanawake wasomi wa ki-Islam na kujitambulisha kwao, ili waweze kuniongezea elimu kwa manufaa yangu na ya wanafunzi wangu. Ninafurahi kwa mafanikio ya kutia moyo ambayo nimeanza kuyaona.

Nimeandika ujumbe huu kwa kuzingatia kuwa wengi wanaosoma blogu yangu ni waumini wa dini. Wana wajibu wa kuchangia mawazo, hasa wakiona nimepotosha jambo lolote. Kwa muumini yeyote, hili si  suala la hiari, bali ni wajibu.

Saturday, January 2, 2016

Kitabu Kinaposainiwa

Leo napenda kuirejesha mada ya kusainiwa vitabu, ambayo nimewahi kuileta katika blogu hii. Wanablogu wengine nao wameiongelea. Kwa mfano, Christian Bwaya amelielezea suala la kusaini vitabu kama jambo la ajabu, akatumia dhana ya muujiza. Nakubaliana na dhana hiyo, kutokana na uzoefu wangu kama mwandishi ambaye nimesaini vitabu vyangu mara nyingi, na pia mnunuaji wa vitabu ambaye nimesainiwa vitabu mara kwa mara. Hapa kushoto ninaonekana nikisaini kitabu changu mjini Faribault, Minnesota. Huyu ninayemsainia ni binti kutoka Sudan.


Ninafahamu muujiza huu unavyokuwa kwa pande zote mbili, mwenye kusaini kitabu chake na mwenye kusainiwa. Ninadiriki kusema kuwa kitendo cha kusainiwa kitabu kinafanana na ibada. Natumia neno ibada kwa maana ile ile ya dhana ya ki-Ingereza ya "ritual." Hapo kushoto anaonekana mwandishi Seena Oromia akinisainia kitabu chake mjini Minneapolis.

Ibada ni sehemu ya kila utamaduni, na kila ibada ina utaratibu wake, iwe ni misa kanisani, mazishi, au kitendo cha watu kula pamoja. Wahusika katika ibada wanapaswa kuzifahamu na kuzifuata taratibu hizo. Ibada ya kusainiwa kitabu ni tukio linalogusa nafsi na hisia ya anayesaini kitabu na yule anayesainiwa kitabu.

Ni tukio linaloambatana na heshima ya aina yake. Angalia tu picha nilizoweka hapa; utaona zinavyojieleza. Kuna usemi katika ki-Ingereza kwamba "A picture is worth a thousand words," yaani picha ina thamani sawa na maneno elfu. Hapa kushoto anaonekana mwandishi Jim Heynen akisaini kitabu chuoni St. Olaf.

Kwa ujumla wewe mwandishi huwajui watu wanaotaka kusainiwa vitabu. Inabidi uwaulize uandike jina gani. Wengine huwa wamenunua vitabu viwili au zaidi. Unawauliza usaini jina gani, kwa kila kitabu, nao wanakutajia jina lao au la mtu mwingine au watu wengine.  Hapa kushoto ninaonekana nikisaini vitabu vyangu katika mkutano Grantsburg, Wisconsin.

Kifalsafa, suala la kumsainia kitabu mtu ambaye humwoni ni jambo linalofikirisha. Mwandishi unajifanya unamjua unayemsainia, ingawa humjui. Naye, atakapokipata kitabu, atajiona kama vile kuna uhusiano baina yake na wewe mwandishi. Anafurahi kama vile mmeonana. Hii dhana ya kuonana imejengeka katika usomaji. Tunaposoma, tunakuwa na hisia ya kukutana na mwandishi, hata kama hayuko mbele yetu kimwili. Lakini tunaposhika kitabu ambacho tumesainiwa, ukaribu huo unakuwa mkubwa zaidi. Ni aina ya undugu.

Hapa kushoto naonekana nikisaini kitabu mjini Brooklyn Park, Minnesota. Ninayemsainia ni Adrian Mack, Mmarekani Mweusi.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...