Thursday, January 7, 2016

Qur'an na Mwanamke

Siku chache zilizopita, niliandika kuhusu maandalizi ninayofanya kwa ajili ya kufundisha kozi mpya "Muslim Women Writers," hapa chuoni St. Olaf. Niliandika maelezo mafupi ya lengo la kozi hii katika blogu yangu ya ki-Ingereza.

Katika maandalizi ya kozi hiyo, na wakati wa kuifundisha, na siku za baadaye, ninawazia kuisoma Qur'an. Lakini, mbali na fasihi nitakayofundisha, fasihi iliyoandikwa na wanawake wa-Islam, nimeona itakuwa vizuri pia nikitafuta maandishi ya wanawake yanayoichambua Qur'an. Kwa bahati nzuri, nimeona kuwa maandishi haya yako, vikiwemo vitabu.

Baada ya kuzipitia taarifa za vitabu hivi, nimeagiza kitabu cha Amina Wadud, Qur'an and Woman: Rereading the Sacred Text From a Woman's Perspective. Kwa mujibu wa maelezo niliyosoma, kitabu hiki kinafuatilia historia ya maandishi kuhusu Qur'an na mwanamke, historia inayothibitisha jinsi wanaume walivyopotosha mafundisho ya Qur'an na kuhalalisha mfumo unaowapendelea wanaume na kuwakandamiza wanawake. Maelezo yanabainisha pia kuwa mwandishi amefafanua maana za maneno ya ki-Arabu yalivyotumika katika Qur'an. Taarifa kuwa mwandishi amezingatia taaluma ya maana za maneno, ambayo kwa ki-Ingereza inaitwa "semantics," imenivutia.

Kuna misimamo mbali mbali miongoni mwa wanawake wasomi wa ki-Islam kuhusu suala la u-Islam na mwanamke. Wako ambao wanasema kuwa u-Islam ni dini kandamizi kwa wanawake. Mfano ni Wafa Sultan kutoka Syria, aliyeandika kitabu kiitwacho A God Who Hates na Ayaan Hirsi Ali kutoka Somalia, aliyeandika vitabu kama Infidel na Heretic.

Wako pia ambao wanasema Qur'an inawapa haki na uhuru wanawake, bali jadi ya kuichambua imekuwa ya upotoshaji ambao umesababisha kuhalalisha unyanyasaji na ukandamizaji wa wanawake. Kati ya wanawake wenye mtazamo huo ni huyu Amina Wadud ambaye nimemtaja na Fatima Mernissi wa Morocco, ambaye ameandika vitabu kama Beyond the Veil na The Male Elite: A Feminist Interpretation of Women's Rights in Islam.

Haya ni malumbano katika nyanja za elimu jamii kama historia, soshiolojia, na falsafa. Yana nafasi yake katika mijadala kuhusu fasihi, lakini fasihi inajieleza yenyewe. Nitasubiri hadi kozi yangu ianze ndipo nitaweza kuelezea yatakayokuwa yanajitokeza katika kusoma hizi kazi za fasihi.

2 comments:

Khalfan Abdallah Salim said...

Ni kweli misimamo juu ya Qur'an na Wanawake, imegawika katika makundi hayo mawili na Zaidi. Wapo ambao wanatambua kuwa Qur'an hii iliyofasiriwa na wanaume haina tatizo lolote. Tatizo la akina Wadud na akina Ayan Hirsi ni zaidi ya uhalisia. Mathalan huwezi kuihukumu Qur'an moja kwa moja kuwa inamkandamiza mwanamke bila kurejea historia ya wanawake wakati ikiteremshwa na bila ya kutazama mapungufu ya hao wanaoisoma hiyo Qur'an kama wanadamu waliolelewa katika tamaduni ambayo siyo tamaduni ya Kiislamu bali ya Kisomali, Kizungu, Kiasia, Kiarabu. Ni mambo mengi leo yamewashinda watu kama Hirsi, kutofautisha tamaduni za jamii yao na mafunzo halisi ya Qur'an.

Jambo la pili na ni muhimu, ni kuwa wakati unaisoma Qur'an inahitajika ufahamu kuwa mfasiri wa mwanzo wa hiyo yaliyoo katika Qur'an ni Mtume Muhammad s.a.w mwenyewe ambaye mapokezi yake mengi yamepokewa na mkewe, Bi 'Aisha bint Abu Bakar r.a'. Hivyo hutokuwa mtimilifu katika somo hili iwapo hutotafiti walau kidogo kujuwa Mfasiri huyu wa mwanzo aliielewa vipi Qur'an. Napenda usome kitabu 'Interractions of Greatest Leader' by Sheikh Munajjid kwa maelezo ya namna Mtume huyu chini ya muongozo wa Qur'an alivyoishi na wanawake na watu mbalimbali.

Kila la kheri.

Mbele said...

Ndugu Khalfan Abdallah Salim

Shukrani kwa kurejea kwako tena katika ukumbi wangu huu na kuchangia mawazo. Ni kweli kuwa mada hii ina mambo mengi. Nimegundua hayo katika kusoma soma kwa miaka kadhaa, kidogo kidogo Qur'an, kiasi hadith, na kiasi maandishi ya wataalam.

Suala hili uliloleta la tamaduni mbali mbali, ni muhimu, na ndio maana nililitaja katika tamko langu la lengo la kozi hii, kwa kutahadharisha kuwa ulimwengu wa u-Islam si "homogeneous." Nitasisitiza sana suala hili wakati wa kufundisha kozi.

Suala jingine ni hilo la hali ilivyokuwa wakati u-Islam ulipoanza, suala ambalo umeligusia pia. Watu wengi hawafahamu kwamba utamaduni wa wa-Arabu kabla ya kuja u-Islam ulikuwa kandamizi sana kwa wanawake. Mtume Muhammad aliboresha hali yao. Na kwa kweli, nafasi ya wanawake kwa kile kipindi cha kwanza cha u-Islam ilikuwa bora kuliko ilivyokuja kuwa baadaye, baada ya wanaume kujitwalia jukumu la kufundisha mafundisho yaliyohujumu uhuru na haki za wanawake. Tabia hii ya wanaume imeendelea hado leo, na ndio kitu kinacholalamikiwa na hao wanaharakati wa "Islamic feminism."

Ninakubaliana na hao wanaharakati kwa msingi kwamba Muhammad alikuwa na mwelekeo wa kuleta mapinduzi. Ninaamini kuwa angekuwepo nasi leo angekuwa sambamba na wanaharakati wanaopigania ukombozi wa wanawake. Nikikumbuka jinsi mke wake Aisha alivyokuwa na uhuru na mamlaka katika jamii, ninaamini kabisa kuwa Muhammad hangekuwa mtu wa kuwawekea vizuizi wanawake ambavyo vinadaiwa kuwa ndio u-Islam katika tamaduni nyingi leo.