Dini ni kati ya masuala ninayopenda kuyaongelea katika blogu hii. Kwa kitambo sasa, nimekuwa nikielezea imani yangu kwamba kuna Mungu mmoja tu. Nimekuwa nikielezea ulazima wa kuziheshimu dini zote. Nilikuwa nikisema hayo yote nikiwa najitambua kuwa ni m-Katoliki. Sijui wa-Katoliki wenzangu walinionaje, na sijui wa-Kristu wenzangu walinionaje. Sijui watu wa dini zingine walinionaje.
Ninafurahi kwamba mkuu wa kanisa Katoliki, Papa Francis, ana mwelekeo huo huo. Dalili za mwelekeo wake zilianza kujitokeza tangu mwanzo wa utumishi wake kama Papa. Aliongeza kasi ya kujenga mahusiano baina ya dini mbali mbali, akifuata mkondo ulioanzishwa na mapapa waliotangulia.
Leo nimeona taarifa kuwa Papa Francis ameweka msimamo wake kuhusu dini mbali mbali kwa uwazi kuliko siku zilizopita. Amesema kuwa dini zote ni njia mbali mbali za kumwelekeza binadamu kwa Mungu. Nimeona kuwa msimamo huu ni changamoto kubwa ambayo inahitaji kutafakariwa.
Kwa kuzingatia mtazamo huu wa Papa Francis, ninaona kuwa ni ujinga kwa watu wa dini mbali mbali kulumbana kuhusu ipi ni dini ya kweli, au ipi ni dini bora zaidi. Nawazia hali ilivyo Tanzania, kwa mfano, na malumbano baina ya baadhi ya wa-Islam na baadhi ya wa-Kristu, kuhusu usahihi au ubora wa dini zao. Naona ni ujinga mtupu.
Mara kwa mara nimewazia suala hili kwa kutumia mfano wa watu wanaopanda mlima Kilimanjaro. Kuna njia mbali mbali za kufikia kileleni. Itakuwa ni ujinga kwa watumiaji wa njia mbali mbali kugombana juu ya ipi ni njia sahihi. Njia zote zinaishia mahali pamoja, yaani kileleni. Safari ya mbinguni nayo ina njia mbali mbali.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault
Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...
-
Leo ni kumbukumbu ya siku ya kuzaliwa kwangu, ambayo ni tarehe 17 Agosti, 1951. Familia yangu, ndugu, na marafiki wamejumuika nami kushereh...
-
Leo napenda kukitambulisha kwako mdau kitabu muhimu cha ki-Swahili, Tenzi Tatu za Kale . Nilinunua nakala yangu miaka kadhaa iliyopita katik...
-
Kutafsiri kazi ya fasihi ni kazi ngumu ya kuchemsha bongo. Inahitaji ufahamu wa hali ya juu wa lugha husika, na pia hisia makini za kifasih...
13 comments:
Nakubaliana na wewe kuwa Mungu ni mmoja. Lakini ninachojiuliza ni jee Mungu aliumba binaadamu na kuwaachia wajiongoze wenyewe? Jee Mungu hakuleta uongozi ambao alitaka binaadamu waufuate? Jee ina maana dini zimetengenezwa na binaadamu kuwa ni kama njia ya kumtafuta Mungu. Kama dini zimetengenezwa na binaadamu, then nakubaliana na wewe 100% kuwa ni "ujinga" kwa mtu yoyote kuona kuwa dini yake aliyoitengeneza ni bora kuliko ya mwenzake. Lakini kama dini ni uongozi wa Mungu, basi ni lazima kuna uongozi mmoja tu ulio sahihi. Kama unataka kuwa daktari wa watu utakuwa unafanya "ujinga" kama utakuwa unasoma isimu. Hiyo sio njia ya kukupelekea huko. Huwezi kujiamulia nini usome kama unataka kuwa daktari.
Ndugu Anonymous
Shukrani kwa mchango wako. Nimeyapenda masuali yako. Mimi ni mtafiti na mwalimu katika masimulizi ya jadi ya mataifa mbali mbali. Kuna aina ya masimulizi ambayo kwa ki-Ingereza huitwa "myths" ambayo huelezea asili ya ulimwengu, binadamu, na viumbe vingine. Humo unakuta akitajwa Muumba, na aghalabu unakuta ikisimuliwa jinsi binadamu alivyokiuka amri ya Muumba na kusababisha Muumba kujitenga na binadamu au kumwadhibu kwa namna nyingine.
Waumini wa dini kama u-Islam na u-Kristu wamejiaminisha kuwa masimulizi ya kuumbwa dunia, binadamu, na viumbe vyote yamo katika, Qur'an tu au Biblia tu. Wamejiaminisha kuwa misahafu yao ndio pekee neno la Mungu (Allah) na hawana wazo kuwa masimulizi yaliyomo katika misahafu yao yalikuwemo kabla ya kuandikwa misahafu hiyo.
Kwa mfano, masimulizi ya tufani iliyoletwa na Mungu kama adhabu kwa binadamu ni ya kabla ya kuwepo hii misahafu. Yalikuwepo, kwa mfano, katika himaya ya Sumer, iliyokuwepo katika nchi aambayo leo inaitwa Iraq. Masimulizi ya tufani ile yalikuweko sehemu zingine za dunia pia. Katika haya masimulizi, inaonekana wazi kuwa Mungu alijidhihirisha kwa mataifa yote. Kila jamii ilifahamu mabaya na mema.
Dhana yetu wa-Islam na wa-Kristu kwamba neno la Mungu liliwafikia au linawafikia watu pale tu wanapoletewa Qur'an au Biblia si ya kweli. Ninapofundisha somo la "Folklore," ambamo "mythology" ni sehemu muhimu, tunajithibitishia mambo hayo kwa kusoma masimulizi ya sehemu mbali mbali za dunia, yaliyokuwepo kabla ya kuwepo u-Islam au u-Kristu, na yapo mahali ambapo hakuna u-Islam wala u-Kristu.
Mungu ni mwema kuliko tunavyodhani. Aliwapenda watu tangu alipoumba mtu wa kwanza. Popote walipoenda kuishi watu, iwe ni Afrika, Asia, Ulaya, Marekani, au Visiwani vya Pacific, walifahamu kuwa kuna Mungu na anakataza yepi na anaruhusu yepi. Wahenga wetu wa kabla ya kuja u-Islam au u-Kristu walikuwa na dini. Tena wao ni mfano wa kuigwa kwani hawakuwa wanagombana na kuuana kwa kisingizio cha dini kama tunavyofanya sisi tuliojivisha dini za kigeni.
Asante kwa maelezo yako japokuwa hukutaka kujibu moja kwa moja kuwa watu hujitengenezea maelekezo yao wenyewe kujiongoza na miongozo hiyo haitokani na Mungu. Waislamu wanaamini kuwa Quran ni kitabu cha mwisho kilicho kwenye maandishi kutoka kwa Allah. Biblia (Injili) ni kitabu kilichoandikwa kutokana na mafundisho aliyoletewa Nabii Issa(Yesu). Kabla ya vitabu hivi Waislamu wanaamini kuwa Allah amekuwa akituma miongozo na maonyo tokea alipoumbwa binaadamu wa kwanza(Adam). Miongozo hii ilitumwa kwa jamii ndogo ndogo na baadae kwa jamii kubwa.Quran na Biblia na "vitabu" vya mwisho. Ni wazi kuwa maneno ya mitume mingi hayakuandikwa.Na kama mwalimu wa fasihi najua unajua kuwa kuna fasihi simulizi ambayo iliishi miaka mimgi bila kuandikwa.
Maneno ya suala la dini kama ni "myths" kama ilivosimuliwa katika History Channel kutokana na mwanahistoria E.A.Wallis Budge ni maneno ya juhudi za mwanadamu kujitambua. Lakini pia ni maneno ya watu wasiojua Quran kwa undani. Kuna watu husoma tafsiri ya Quran na kufikiri kuwa wameelewa kilichomo bila ya kusoma "lugha ya Quran".Ni sawa na mtu anaejua Kiswahili au Kiingereza baadae akafikiri kuwa anawezakuwa mwana fasihi kwa kuwa anajua lugha. Tunasahau kuwa fasihi is more than a language. Pia Quran ni zaidi ya ile tafsiri. Ili ujue kilichomo kwenye Quran ni lazima mtu asome Quran yenyewe na sio tafsiri.
Kuna kula uwezekano kuwa baadhi Waislamu wanaamini kuwa kwa kuwa binaadamu tumeumbwa na Allah basi amekuwa akituletea miongozo. Kwa Waislamu haiingii akilini kuwa Mungu aliumba kisha akatuachia tuishi tu kama wanyama. Alituletea muongozo lakini pia ametupa hiari. Enzi za zamani kama inavyooneshwa katika maandiko, ilikuwa Allah anaweza kuwaadhibu wanaadamu kwa kukataa mafunzo. Hili limekoma hivi sasa na kwa kuwa Allah ndie mmiliki wa kila kitu, basi ameweka siku ya hukumu kwa wale wote ambao hawakutenda wema hapa duniani na waliishia kufanya ufisadi dhidi ya nafsi zao na dhidi ya watu wengine.
Narudia kusema kwamba kama tunaamini kuwa tumeumbwa na Mungu basi
Ndugu Anonymous, Nami katika jibu langu hapa juu nimeelezea kuwa Mungu alijidhihirisha kwa jamii zote za wanadamu, na ushahidi uko wazi, kwamba hata kabla ya u-Kristu na u-Islam kuwepo, ushahidi ni wazi kuwa watu wote walimtambua Mungu. Hata leo, kuna jamii nyingi ambazo haziijui Biblia wala Qur'an, lakini nazo zinamtambua Mungu. Tuzingatie kuwa, kama ni misahafu, kuna pia misahafu ya dini zingine, kama vile u-Hindu. Hii ni dini sawa na u-Kristu au u-Islam. Wa-Hindu wanamtambua Mungu, sawa na ninavyomtambua mimi n-Kristu, na sawa anavyomtambua mu-Muislam. Huu ndio msimamo wangu.
Kwamba kuna msahafu bora kuliko mingine siafiki. Hakuna ushahidi. Ni waumnini tu wanalumbana, kama wawamba ngoma, ambao kila mmoja anavutia ngozi kwake. Mwisho wa haya malumbano ni uhasama, magomvi na mauaji, ambayo siamini ni kazi ya Mungu, bali kazi ya shetani. Hakuna vita za kidini. Vita ni ushahidi wa kukosekana dini. Wala siamini kama Mungu anahitaji kutetewa kwa umwagaji wa damu ya wanadamu wenzetu. Mungu ana uwezo wote, hahitaji kutetewa na binadamu.
Tumeumbwa na Mungu, na Mungu huyu amewafundisha wanadamu wote njia itakiwayo. Haijawa lazima wawe na msahafu, na hata leo wengi wanamtambua Mungu na wanaishi kwa kufuata imani yao juu ya nini akitakacho Mungu, ingawa hawana hiyo Qur'an, Biblia, Bhagavad Gita, na kadhalika.
Prof.
Siamini kuwa dini zote ni sawa. Imani yangu hiyo inatokana na elimu yangu ya Quran. Kwa bahati nzuri mimi nimeisoma Quran na sio kusoma tafsiri ya Quran. Mimi siwezi wala sithubutu kupingana na wewe katika elimu yako ya fasihi. Kwasababu najua ulivyobobea na ni wazi tokea hapo kale umekuwa ukizitizama dini kwa mtizamo wako wa kifasihi. Hilo sina ubavu wa kukupinga kwa kuwa mimi si mwana fasihi.
"Wala siamini kama Mungu anahitaji kutetewa kwa umwagaji wa damu ya wanadamu wenzetu. Mungu ana uwezo wote, hahitaji kutetewa na binadamu". Hapa uko sawa 100%. Hakuna ushahidi popote katika Quran unaosema kuwa Mungu anahitaji kutetewa. Tatizo ni kuwa kuna watu wanajifanya wanaijua Quran kumbe wamekaa wakasikiliza uchambuzi wa watu na baadae kuitumia dini kwa matamanio yao. Ni sawa na wale wanaotetea gun law kwa kutumia katiba ya US.
Lakini mimi sijaona ushahidi wako unaoweza kuthibitisha kuwa Quran sio neno la Allah. Najua itakuwa ngumu kwa wewe kwa sasa bila ya elimu ya lugha ya Quran kuja na ushahidi huo. Utakachokitegemea itakuwa ni tafsiri za watu za Quran. Hata waarabu hawawezi kuielewa Quran bila ya kujua lugha ya Wuran.
Quran inajitetea wenyewe kuwa ni neno la Allah. Quran imetoa changamoto kwa watu kuwa kama ingekuwa inatoka kwa yoyote asiekuwa Allah basi "ingekuwa na makosa ndani yake". Hakuna alieweza kuitoa makosa Quran. Wanaojaribu huwa ama wanaangalia "Waislamu mbumbumbu" wanavyofanya au wanatoa makosa tafsiri ya Quran lakini sijaona makosa katika Quran yenyewe.
Mimi pia sijaona vita vya dini katika dunia ya leo. Vita vya dini vilikuwepo enzi za Mtume Muhammad(SAW) pekee. Baada ya hapo watu wanapigania matumbo yao tu.
Najua kwa kuwa hivi sasa una priorities nyingi zaidi, hutakuwa tena na nafasi ya kusoma Quran katika lugha yake ya asili(hii sio kujua kiarabu tu). Najua kwa upeo wako hivi sasa utategemea zaidi tafsiri za watu(I can understand this, wala sitakulaumu). Lakini bila ya kuwa na elimu ya Quran nahisi si sahihi kuihukumu Quran.Utapokuwa na elimu ya Quran nitakukaribisha tuijadilini ili tuone ni wapi Quran haioneshi "uungu" ndani yake bali ni kama maneno ya Biblia au "dini" nyengine.
Ndugu Anonymous,
Shukrani kwa kuendelea kutoa mchango wako. Samahani, labda sikujieleza vizuri. Msimamo wangu ni kwamba neno la Mungu lilijulikana kwa mataifa yote, mataifa yenye misahafu na yasiyo na misahafu. Kwa maana hiyo, naamini kabisa kuwa Qur'an ni neno la Mungu kama vile ninavyoamini kuwa Biblia ni neno la Mungu, na Bhagavad Gita ni neno la Mungu. Waliyoamini wahenga wetu, kabla ya kuja u-Islam na u-Kristu, nayo ni neno la Mungu. Na huyu Mungu ni mmoja. Ni huyu huyu ambaye kwa ki-Arabu huitwa Allah, na kwa ki-Chagga huitwa Ruwa. Hii ndio imani yangu, ambayo nimeifikia baada ya tafakari ya muda mrefu. Nitawajibika mbele ya Muumba kwa kuamini hivyo, sawa na mtu mwingine yeyote atakavyowajibika kwa imani yake.
Ningetamani kuweza kusoma Qur'an katika lugha yake ya asili, kwani tafsiri hazikosi utata. Ni hivyo hivyo kwa Biblia. Tunategemea tafsiri, ambazo nazo zina utata.
Nimekuelewa sawasawa Profesa. Na nimeelimika kwa majibu yako. Nukta yangu ya mwisho ni kuwa kama vile ambavyo Allah hahitaji watu wa kumpigania kwa kuwa yeye ni mkamilifu.Basi na Quran inajilinda yenyewe kwa kuwa inajitosheleza na imetoa changamoto kwa yoyote ambae anahisi ina makosa.
Pia sifa za Allah zote zimo katika Quran. Hakuna binaadamu ambae amemtengezea sifa zake. Kwa mfano kuwa Mungu hakuzaa (sifa hii imo katika Quran kaisema Allah mwenyewe), kama yeye hakuzaliwa(pia imo kwenye Quran), kama yeye anazuliwa kuwa ana mtoto kaisema mwenyewe na sifa nyenginezo. Waislamu hawawezi kumvisha Allah sifa yoyote ambayo hana(hajaitaja kwenye Quran) na hawewawezi kuikataa sifa yake yoyote. Kuzidisha au kuikataa sifa ya Allah inakuwa ni kukufuru katika Uislamu.
Kwa mujibu wa Allah sisi kwake ni "slaves" na yeye ni "lord"(our owner). Yeye ndio anaetumiliki. Akiamua kutuondoa hakuna mwenye ujanja.
Nashukuru tena kwa taaluma uliyonipa.Mimi ni msomaji mkubwa wa blog yako na makala zako.Mungu akuzidishie uzima na umri uzidi kuelimika na kutuelimisha.
Salaam zao huko St.Olaf.
Ndugu Anonymous, Shukrani kwa ujumbe wako. Haya ni masuala magumu sana, nami ninajikongoja hivi hivi katika kuyatafutia majawabu. Nakushukuru kwa mchango wako. Nafurahi kusikia wewe ni msomaji wa blogu yangu. Ukiona jambo la kuchangia au kukosoa, nitashukuru ukileta mchango wako. Ubarikiwe sana.
Prof Joseph, Wewe huamini juu ya utatu mtakatifu? au unauelezeaje utatu huo kama unavyohusishwa na maandiko ya John katika biblia na kuaminiwa na wakristo wengi lakini sio wote.
Ndugu Khalfan Abdallah Salim, Shukrani kwa ulizo lako. Mimi kama m-Kristu (m-Katoliki) ninaamini juu ya Utatu Mtakatifu kwa asili mia 100%. Ninafahamu kabisa maana ya hii dhana ya Utatu Mtakatifu. Inamaanisha Mungu Mmoja katika nafsi tatu. Kwa nini ninasema kwa kujiamini hivyo?
Mbali ya kuwa nilizaliwa na kulelewa na wazazi waliozama katika u-Katoliki, na mbali ya kufundishwa dini hiyo nilipokuwa shule ya msingi katika kile kiitwacho Katekisimu, nilisoma kuanzia darasa la tano hadi la 12 katika seminari za Katoliki za Hanga na Likonde katika mkoa wa Ruvuma. Huko, pamoja na masomo ya kawaida, nilifundishwa pia somo la dini kwa undani zaidi. Katika mtihani wa "Bible Knowledge" wa kidato cha nne, niliibuka na "distinction" namba moja.
Naandika yote hayo kuthibitisha kuwa ninayafahamu mafundisho ya dini yangu kiasi fulani, ingawa si bingwa. Ni muumini ninayejua mambo ya msingi. Ninajua fika kuwa kuna watu nje ya u-Kristu ambao wanadhani kuwa Utatu Mtakatifu maana yake ni kuwa sisi wa-Kristu tuna amini kuna Mungu watatu. Hakuna kitu kama hicho. Kila m-Kristu anaamini kuna Mungu mmoja tu.
Kadhalika dhana ya kwamba Yesu ni mwana wa Mungu. Nje ya u-Kristu, kuna watu wanadhani kuwa wa-Kristu tunaamini kuwa Mungu alikuwa na mke au mwanamke, akampa mimba kama tunavyofanya sisi akina Abdallah au Joseph hapa duniani. Ukweli ni kwamba u-Kristu hau fundisho hivyo inavyodhaniwa.
Jambo la maana ni kwa kila waumini wa dini fulani kutojiingiza katika kuhoji au kuzibeza imani za dini za wengine. Si busara kwa mimi m-Kristu kuhoji imani ya m-Hindu kwamba ng'ombe ni kiumbe mtakatifu. Si busara kwangu kuhoji kwa nini mmoja wa miungu wao, Hanuman, ana umbo la tumbili, au kwa nini mungu wao mwingine, Ganesha, ana kichwa cha tembo. Na kadhalika. Si busara kwangu kuhoji kwa nini katika hajj, wa-Islam humpiga mawe shetani. Wala si busara kwangu kuhoji kwa nini wa-Islam wanaamini watapata raha fulani huko Peponi ambazo hazimo katika mafundisho ya u-Ukristu.
Busara ni kuwaacha kila watu na imani zao. Busara ni kwa waumini wa kila dini kuheshimiana. Dini zote zimejengeka katika imani. Tukizihoji kwa vigezo vya sayansi, tutaona mengi ambayo hayana mantiki kisayansi. Pamoja na kuwa sayansi imeshamiri na inaendelea kushamiri, binadamu ni kiumbe wa ajabu, ambaye anaonekana kuhitaji mambo ya aina aina, hata yale ambayo hayaendani na sayansi.
Professor nashukuru kwa ufafanuzi huo jambo juu ya Mungu mmoja katika nafsi tatu. Nini maana yake?Mungu baba, Roho Mtakatifu na Mwana wa Mungu. Je umeichunguza imani hii kuwa ndio msingi wa mafundisho ya Yesu au ni Yesu amesingiziwa tu?
Natumai unacho kitabu Jesus-the prophet of Islam, unaweza kueleza vipi juu ya hoja za mwandishi huyo ambaye ameweka ushahidi kuwa huo utatu matakatifu sio mafunzo ya Yesu kwa kurejea katika historia, kauli za Yesu zisizo na mashaka (nyingine kwa mujibu wa wanazuoni wa kikristu amesingiziwa Yesu) na wafuasi wa mwanzo wa Yesu kabla ya mkutano wa kanisa katika miaka ya 1600's. Mimi bado sijapata mjuzi yoyote aliyeweza kujibu hoja za mwandishi huyo, kwa nini hakuna majibu?
Sijui unakusudia nini juu ya kuwaacha kila watu na imani zao, maana Yesu alifanya kazi ya kufundisha imani sahihi kwa utashi wa mungu na hata kusema kwa wale aliutumwa kwao kuwa njia ya kufika kwa baba ni yeye. Mimi naunga mkono juu ya kuheshimiana kwa watu wa imani tofauti na naunga mkono juu ya majadiliano juu ya dini zetu kwa heshima na uvumilivu.
Prof. unafahamu natija inayoweza kupatikana kwa majadiliano ya namna hii hata katika masuala ya fasihi, ni jambo la maana sana iwapo wasomi watajadili kazi mbalimbali za fasihi au mwandishi fulani na uandishi wake na kila mtu akawa na mtazamo wake-sidhani kuwa ni jambo jema kusema tuwaache waandishi hawa na kazi zao. Tusihoji au kujadili hata tunapoona kuwa mwandishi kwa mtazamo fulani ameshindwa kuitendea haki maudhui fulani au imani husika si tu kuwa wafuasi wake pengine hawajaielewa ipasavyo au kwa kufichwa ukweli hawajapata fursa na wakati wa kutafuta kweli hiyo.
Juu ya kuhoji kwa mujibu wa vigezo vya sayansi, sifikiri kuwa sayansi imejitosheleza kujibu masuala mazito ya imani, sayansi inayomengi ambayo kwa kanuni zake zimesaidia kwenye mambo fulani lakini zimepwaya katika maeneo mengine. Sayansi na njia zake za kutafuta maarifa mapya ni njia muwafaka kwa watu wa imani kuzitumia njia hizo 'scientific methods of inquiry', mathalani tunapotaka kujuwa iwapo utatu mtakatifu ni mafunzo ya Yesu au la, njia za kisayansi za kupata jibu hilo zinaweza kutusaidia sana. Lakini sayansi inaweza isiwe na mchango mkubwa sana kuelezea usahihi au vinginevyo wa 'utatu mtakatifu' japo wapo wanaoweza kuthibitisha jambo hilo kisayansi, hata kama baadhi yetu tutaona zipo dosari katika kufanya hivyo.
Ndugu Khalfan Abdallah Salim
Shukrani kwa ujumbe wako. Sijui undani wa mafundisho ya madhehebu mengine ya u-Kristu, lakini sisi wa-Katoliki tunatakiwa kufuata sio tu yale ambayo tunaamini ni amri za Mungu na mafundisho ya Yesu, bali pia amri na mafundisho ya Kanisa Katoliki. Kwa mfano, tunaamini dhana ya "Papal infallibility." Hii maana yake ni kwamba Papa, anapotoa kauli ya kichungaji kwa wadhifa wake kama mkuu wa Kanisa Katoliki, hakosei. Huu ni msingi madhubuti mojawapo wa imani yetu sisi wa-Katoliki.
Kwa hivi, ingawa kuna watu walioko nje ya u-Katoliki ambao wanapekua maneno ya Yesu tu, na wanatafuta ushahidi katika maneno ya Yesu tu, sisi wenye dini Yetu tunafuata pia mafundisho ya viongozi wa Kanisa. Kwa mfano, mafundisho kama ya Mtakatifu Augustine ni nguzo muhimu, au hizo nyaraka za kichungaji za mapapa, kama huu waraka wa hivi karibuni wa Papa Francis uitwao "Laudato Si." Mafundisho ya Kanisa Katoliki kwa maana hiyo ni "dynamic," yaani yanakwenda na wakati.
Ni kweli, ninacho hiki kitabu, "Jesus: Prophet of Islam," kama nilivyoripoti katika blogu hii, na nilianza kukisoma mara baada ya kukinunua. Ni kitabu kinachohoji mafundisho ya u-Kristu. Waandishi wamefanya utafiti wa muda mrefu, na kwa mtazamo wangu kama msomi, ninawaheshimu kwa hilo. Tatizo nililoliona ni kuwa kitabu hiki hakizingatii ahadi ya kuthibitisha kuwa Yesu ni "Prophet of Islam." Waandishi wamekazana kuyashambulia mafundisho ya wa-Kristu, wakasahau kutuelimisha kuhusu dhana ya Yesu kama nabii au mtume wa u-Islam.
Pamoja na hayo, ninakihesabu kitabu hiki kuwa ni kitabu muhimu. Ninavyo vitabu vingine pia vinavyohoji mafundisho ya u-Kristu. Ninaviheshimu. Ninavyo pia vitabu vinavyohoji u-Islam. Ninafuatilia taarifa za waandishi wanaopinga u-Islam, sawa na ninavyofuatilia habari za waandishi wanaopinga u-Kristu. Huu ni wajibu wa kisomi, wajibu wa kutafuta elimu.
Lakini hapo kuna jambo ambalo linahitaji ufafanuzi. Hutasikia sisi wa-Kristu tukiwatishia uhai watu wanaoandika kuhoji mafundisho ya dini yetu. Hatuwatishi hao walioandika kitabu cha "Jesus: Prophet of Islam." Lakini ninaona jinsi waandishi wanaohoji u-Islam wanavyotishwa na wengine kulazimika kuishi ufichoni. Kanisa lilikuwa likifanya hivyo hivyo miaka mingi iliyopita, lakini si miaka ya leo.
Kanisa linakwenda na wakati. Linafahamu kwamba imani ya dini hailazimishwi. Linafahamu kwamba mwenye hukumu ya haki kabisa juu ya imani ya mtu ni Mungu pekee. Vile vile, leo si kama karne za zamani. Leo tuna tangazo la kimataifa la haki za binadamu, na haki ya kuamini dini yoyote au kubadili dini au kuishi bila dini inatambuliwa.
Ukizingatia hayo, turejee kwenye suali lako, unavyoniuliza ninakusudia nini kwaacha watu waamini watakavyo. Ni kwamba nazingatia haki ya binadamu na kwamba dini ni suala la mtu binafsi, kwa uhuru na hiari yake kamili.
Professor,
Kutishwa kwa waandishi sio suala linalowakabili waandishi wanaoandika dhidi ya Uislamu pekee bali hata waandishi wa mambo mengine. Natumai unatambua kilichowakumbwa kina Snowden na Assange na waandishi wengi wanaokosoa juu ya dola ya Israel, kama Prof. Norman japo kuwa yeye mwenyewe ni yahudi. Hapo Marekani utaingia katika matatizo makubwa ukikosoa hadharani vitendo vya dola ya Israel.
Wapo wengine wameuwawa si kwa kukosoa dini bali kukosoa serikali zetu hizi na wengine wamelazimika kuishi uhamishoni. Hili sio tatizo la dini fulani pekee bali ni tatizo linalotukabili sote mbele ya wale ambao hawapendi rai zetu. Watu hao hutafuta sababu ya kufanya uovu wao, wengine husema kwa sababu za dini wengine kwa sababu za kisiasa na kadhalika.
Unakumbuka wakati Salman Rushdie alipotangaziwa zawadi kwa atakaye muuwa, waislamu hawajashughulika na fatwa hiyo na baadhi ya wanavyuoni wamekosoa fatwa hiyo. Iyaan Hirsi mathalan simuoni kuwa ni mtu mkweli zaidi ya opportunist aliyetaka kuishi ulaya na kukimbia familia yake na njia aliyotumia ni hayo aliyoandika ili apate hifadhi. Unajua wapo vijana wetu leo wapo tayari kujinasibisha na ushoga ili wakaishi ulaya na wanatumia ushoga kuwa ndio sababu ya kuweza kuishi Ulaya eti katika nchi zao watauwawa.
Mimi naona kuwa vitisho wapewavyo waandishi vina sababishwa na mambo mengi sio tu wao kushambulia tu mafunzo ya dini fulani. Vile vile wengine wamevuka mipaka itakiwayo katika 'freedom of speech' na kuibua hasira za watu na kuishia kupata vitisho vibaya. Mwenye hasira haijui sheria wala dini!
Kuhusu Jesus: A prophet of Islam,uchambuzi wa waandishi umeweza sana kuthibitisha kuwa Akida-imani yake ipo sambama na Imani ya Uislam. Hata hivyo, jina hilo la kitabu kwa haraka haraka msomaji anaweza kuwa na matarajio fulani tofauti na lakini ujumbe wake mkuu ni kuwa Jesus alifunza Imani ambayo waislam wanaamini juu yake leo. Hii ndio hoja yao na kwa mantiki hiyo, Jesus ni nabii wa Uislam.
Post a Comment