

Binafsi, naona kuwa malumbano haya ni upuuzi mtupu. Dini haiko katika misahafu tu. Ni mfungamano wa nadharia na vitendo. Dini ni mfungamano wa mafundisho ya misahafu na maisha ya kila muumini. Bila mfungamano huo, dhana ya dini inapwaya.
Kuna maana gani kwa muumini wa dini kuringia msahafu wa dini yake iwapo maisha yake hayaendani na mafundisho yaliyomo katika msahafu? Badala ya kulumbana kuhusu misahafu, tuangalie maisha ya waumini. Je, tabia za mu-Islam ni bora kuliko za m-Kristu? M-Kristu ni bora kuliko mu-Islam? Jamii ya wa-Islam ni bora kuliko jamii ya wa-Kristu? Wa-Kristu ni bora kuliko wa-Islam? Tofauti za imani zina uzito gani? Je, wa-Kristu, ambao wanaamini kuwa Yesu ni mwana wa Mungu, ni watu waovu kuliko wa-Islam, ambao hawaamini kuwa Yesu ni mwana wa Mungu bali ni nabii?
Kama waumini wa dini fulani ni wema, waungwana, wakarimu, wastahimilivu, wenye huruma, wa amani kuliko wengine, ninaamini kuwa waumini hao watawavutia hata watu wasio na dini. Dini si misahafu tu; ni mfungamano wa nadharia na vitendo.
No comments:
Post a Comment