Saturday, February 13, 2016

U-Islam ni Dini ya Amani?

Wiki hii, tumeanza muhula mpya wa masomo hapa chuoni St. Olaf. Kozi mojawapo ninayofundisha ni Muslim Women Writers, ambayo nimeshaiongelea katika blogu hii.

Nimeshaanza kuwaelezea wanafunzi kuhusu u-Islam. Nimeongelea kuhusu Muhammad, Qur'an, hadith, na nguzo tano za u-Islam: shahadah, salah, zakah, sawm, na hajj. Nimefafanua maana ya kila nguzo. Nimeuelezea u-Islam kwa mtazamo wangu kama mtu ninayeziheshimu dini zote.

Kozi yangu hii ni muhimu kwa wanafunzi hao, ambao wengi wao hata msikiti hawajawahi kuuona na hata adhan hawajawahi kuisikia. Ni muhimu katika mazingira ya sasa ya Marekani, ambapo kuna propaganda nyingi dhidi ya u-Islam na wa-Islam. Kwa mfano, siku chache zilizopita, hapa mjini petu, kuna mtu ameandika katika Northfiled News, akiushambulia u-Islam kwamba si dini ya amani.

Kwangu ambaye ninatoka Tanzania, nchi ya watu wa dini mbali mbali, makala hii ambayo imezuka hapa ninapofundisha si ya  kuifumbia macho. Nitaipeleka darasani nikaijadili na kisha wanafunzi watoe dukuduku na mitazamo yao. Darasa la chuo kikuu ni mahala pa kuchambua masuala kwa uhuru na uwazi. Yeyote kati ya wasomaji wa blogu hii ambaye ana jambo la kuchangia namkaribisha afanye hivyo.  Mawazo muafaka yatasaidia juhudi zangu za kuwaelimisha wanafunzi wangu.

Kutokana na hali ilivyo hapa Marekani, na kutokana na kuwa nimeamua kufundisha kozi juu ya waandishi wa kike wa ki-Islam, kuna uwezekano wa mimi kuitwa kwenye mahojiano katika vyombo vya habari hapa Northfield au kwenye mikutano, kuongelea u-Islam. Iliwahi kutokea hivyo baada ya shambulio la kigaidi la tarehe 11 Septemba, 2001, lililoangusha majengo New York. Uliandaliwa mkutano mkubwa wa watu wa mji huu, pia jopo la maprofesa, nami nikiwemo, kujadili tukio lile na mengineyo. Mimi nilielezea u-Islam na kuupambanua na ugaidi.

7 comments:

Mbele said...

Baada ya mimi kuchapisha ujumbe wangu, nimeona kuwa Profesa Cherif Keita amemjibu yule mtu aliyandika katika "Northfield News" dhidi ya u-Islam. Profesa Keita, ambaye anaishi hapa Northfield, ameandika jawabu lake katika "Northfield News."

Khalfan Abdallah Salim said...

Profesa mada hii ni fikirishi na kwa hakika haikupaswa hata kujadiliwa. Ni bahati mbaya kuwa vyombo vya habari na matendo ovu ya baadhi ya watu wachache sana wasioujua uislamu japo wanadai ni wafia Uislam.

Uislam ndio dini pekee ambayo jina lake chimbuko lake ni Amani. Na kilugha tunasema kuwa mwenye kuufuata Uislam kwa kuyasalimisha matashi yake mbele ya matashi ya Mola wake atapata Amani ya kweli duniani na ahera.

Watu wamesahau kuwa sio tu zamani bali hata sasa Waislam wanaishi katika nchi zao kwa Amani na kama sio kuingiliwa na mataifa ya nje tusingekuwa na Libra na Iraq na Syria iliyopo leo sehemu ambazo ndio kielelezo cha hao wanaishambulia dini hii bila kuichambua historia yake, changamoto iliyokutana nazo, kukua kwake na kufika sehemu mbalimbali ulimwenguni.

Nchi nyingi zilizobaki ni Amani na uvumilivu wa kidini na kitamaduni. Kwa hakika, wamefanikiwa kwa kiasi Fulani baadhi ya watu katika kufanya propaganda chafu dhidi ya Uislam. Kwa Maslahi ya Nani? Kwa nini leo watu wanauogopa Uislam hadi kuushambulia kwa njia za Uongo na ulaghai wenye maslahi kwa hao wenye kulaghai.

NN Mhango said...

Ndugu Mbele kama utaangalia historia na chimbuko vya dini zote duniani isipokuwa za kiasili ambazo ziliuawa na dini nyemelezi za kigeni, hakuna hata dini moja ni ya amani. Dini zote-hasa za kigeni- ni nyemelezi, shari na vamizi. Katika kitabu change cha kurasa 470 cha AFRICA REUNITE OR PERISH nimejadili suala hili kwa utuo hasa jinsi wakoloni wa kidini na kisiasa walivyovamia Afrika wakatendewa ukarimu wakaamua kutuita washenzi ambao hawakuwa na ustaarabu wakati tulivyowapokea tulionyesha utu wa hali ya juu. Kimsingi, dini zote zilizoletwa Afrika ni za kikoloni zilizolenga kutunyonya na kutugawana ili tuchukiane na kutawaliwa kama ilivyo sasa. Hakuna historia inayoonyesha mapigano mkubwa au utendaji wa dhambi kubwa kama kufirana wenye kuhusishwa na waafrika pamoja na historia ya waafrika kupotoshwa na washenzi wa kizungu kama dini zilivyokuja kusema. Hivyo, bila kupoteza muda, hakuna dini ya amani hata moja hasa kwenye dini za kimamboleo. Rejea kwa mfano Wakatoliki wakati wa Inquisition walivyowanyonga na kuwachoma moto wenzao wa Ulaya bila kusahau Uislam ambao wakati fulani ulienezwa kwa upanga. Huwezi kwenda sehemu ukatukana mila zao na kuzipindua huku ukipandikiza zako ukawa mtu wa amani. Huwezi kuiba majina ya watu ukapandikiza yako ukawa mtu wa amani.Huwezi kuwa mbaguzi bado ukawa mtu wa amani. Kwa muafrika ambaye siku zote amenyonywa na mila zake kuitwa za kishenzi isipokuwa vyakula vyake na madini yake, hakuna dini ya amani. Dini zote za kigeni ni nyemelezi na zenye shari. Leo nenda ukapinge kwa mfano ushirikina wa Waislam kwenda Makka, utatishiwa kifo. Ukitaka kujua kuwa dini hizi ni za amani au shari, soma historia zake na angalia waumini wake walivyowatenza wenzao. Sijui kama dini zilizofikia hata kuhalalisha utumwa zinaweza kuwa za amani vinginevyo amani iwe na maana tofauti na ninayojua.

Pascal Bacuez said...

Swala hilo unalozungumzia leo katika makala yako, mzee Mbele, lina utata mwingi kwa sababu uislamu haulinganui siasa na dini. Pamoja na hayo ni dini inayochanganya maada na itikadi. Mara ukishasema kwamba uislamu umebeba jukumu kubwa sana katika matokeo ya ujeuri na ubedui yaliyotukia katika dunia yetu hivi karibuni, tayari umeshakashifu uislamu, unatukana na unakufuru Mungu (wao). Uislamu hautaki kujikosoa, hilo ni wazi. Mara ukishasema kwamba ukatili umekithiri katika dini hiyo, na uthabiti upo katika matukio ya hivi karibuni (angalia https://en.wikipedia.org/wiki/List_of_Islamist_terrorist_attacks), tunaambiwa kwamba matokeo hayo hayakutokea kwa sababu ya uislamu bali kwa sababu ya watu wajeuri ambao hawajaelewa maana halisi ya uislamu, na hali kadhalika. Nani anaweza kusadiki, siku hizi, kwamba uislamu ni dini ya amani (ingawa amani ipo pia katika dini hiyo, kwa sababu waislamu wengi wameghadhibika kwa ugaidi unaofanyika siku hizi) hadi waislamu wengi hapa na pale duniani wamekubali (kisirisiri lakini…) kutanasari (mfano Iran na Algeria). Si propaganda kusema kwamba, tangu miaka kadhaa, Uislamu umekwenda tenge, bali ni kujitahidi kuisaidia dini hiyo ijijengee nadhari tambuzi ili kuepuka mfarakano unaozidi kujitokezea kila kukicha.

Mbele said...

Wakuu ndugu Khalfan Abdallah Salim, NN Mhango, na Pascal Bacuez, Asanteni kwa michango yenu ya kusisimua akili. Mmenisaidia kupiga hatua katika lengo langu.

Mbele said...

Ndugu Mhango

Umesema, "Sijui kama dini zilizofikia hata kuhalalisha utumwa zinaweza kuwa za amani vinginevyo amani iwe na maana tofauti na ninayojua."

Naafiki kauli yako. "Biblia" na "Qur'an" zinaongelea utumwa kama vile ni jambo la kawaida, linalokubalika. Misahafu yote miwili inahalalisha utumwa. Amani inaweza kuwepo katika mazingira ya aina hii? Kwa fikra tulizo nazo leo, fikra za kutambua haki za binadamu, ni wazi kuwa hayo yanayosemwa katika hii misahafu hayakubaliki. Waumini wasome misahafu, lakini sio kikasuku, bali watumie akili.

NN Mhango said...

Ndugu Mbele,
Samahani kuchelewa kujibu. Usemayo ni kweli ila ujue imani hupofusha na kufanya watu waache kufikiri kwa uhuru. Huu ndiyo ugomvi wangu na hizi imani nyemelezi ambazo kimsingi zimechangia kikubwa kukwamisha bara la Afrika. Mada hizi nimezijadili kirefu kwenye kitabu changu kipya cha AFRICA REUNITE OR PERISH. Kwa sasa niko namalizia kingine cha THE NEED TO DECONSTRUCT COLONIAL EDUCATION: COLONIAL RELICS AND THEIR IMPACTS ON THE REALPOLITIK.