Monday, January 4, 2016

Nawazia Dini na Uandishi wa Wanawake wa ki-Islam

Muhula ujao, kuanzia mwezi Februari hadi Mei, nitafundisha kozi mpya hapa chuoni St. Olaf ambayo nimeiita "Muslim Women Writers." Ni kozi ya fasihi kwa ki-Ingereza, ambamo tutasoma maandishi ya wanawake wa-Islam kutoka Bangladesh, India, Iran, Misri, Sudan, Senegal, na Marekani. Taarifa fupi ya kozi hiyo nimeandika hapa.

Wakati huu ninapongojea kufundisha kozi hii katika mazingira ya leo ambamo maelewano miongoni mwa waumini wa dini na madhehebu mbali mbali yanatatanisha, ninajikuta nikiwazia mara kwa mara masuala ya dini. Katika siku zijazo, labda kwa miezi kadhaa, ninategemea kuandika tena na tena katika blogu hii kuhusu dini na kozi yangu.

Nimeshaandika mara kadhaa kuhusu dini. Nimeandika kuhusu umuhimu wa mijadala ya dini, umuhimu wa kuziheshimu dini zote, na nilivyozuru nyumba za ibada za dini nyingine. Sioni mantiki kwa dini yoyote kuwafundisha waumini wake kwamba Muumba anawapenda wao zaidi kuliko watu wa dini nyingine. Msimamo wangu ni kwamba Mungu (Allah) hana ubaguzi.

Ninafurahi na kujivunia kwamba kanisa langu Katoliki linasimama katika msingi huo, kama ilivyodhihirishwa katika ziara na ujumbe wa Papa John Paul wa Pili nchini Nigeria, ziara ya Papa Francis katika msikiti Uturuki, na katika sala ya Papa Francis ya kuuombea ulimwengu. Na zaidi ni kuwa Kanisa Katoliki lina baraza la kujenga maelewano miongoni mwa dini mbali mbali liitwalo Pontifical Council for Inter-religious Dialogue.

Katika kujiandaa kwa kozi yangu, nimekuwa nikiwazia kuwa ingekuwa vizuri kama ningesoma Quran yote. Ninayo Quran takriban tangu mwaka 1982. Nimekuwa nikisoma visehemu hapa na pale, lakini si yote kikamilifu. Ingawa ninafahamu misingi ya u-Islam kiasi cha kuridhisha, wazo la kuisoma Quran linanivutia.

Kuna mambo mengine ambayo nimekuwa nikifanya, kama vile utafiti ili kufahamu misimamo na mitazamo ya wanawake wa-Islam kuhusu u-Islam na nafasi yao katika dini hiyo. Nimeanza pia kuwatafuta wanawake wasomi wa ki-Islam na kujitambulisha kwao, ili waweze kuniongezea elimu kwa manufaa yangu na ya wanafunzi wangu. Ninafurahi kwa mafanikio ya kutia moyo ambayo nimeanza kuyaona.

Nimeandika ujumbe huu kwa kuzingatia kuwa wengi wanaosoma blogu yangu ni waumini wa dini. Wana wajibu wa kuchangia mawazo, hasa wakiona nimepotosha jambo lolote. Kwa muumini yeyote, hili si  suala la hiari, bali ni wajibu.

2 comments:

Khalfan Abdallah Salim said...


Prof.Mbele nikupongeza kwa fikra pevu na ya kibunifu kwa kuja na somo juu ya maudhui hii. Uandishi wa wanawake wa Ki-islam ni mkongwe sana na kwenye maudhui nyingi. Ningetamani iwapo ungeenda mbali na kuangaza kazi zao zaidi ya yale uliyoyataja. Mathalani, wapo walioandika 'autobiography' zao kama Zainab Al Ghazal au Yvonne Ridley na wengine wengi.

Kila la kheri.

Mbele said...

Ndugu Khalfan Abdallah Salim

Shukrani kwa ujumbe wako. Tunakubaliana, na ni ukweli usiopingika, kwamba uwanja huu wa uandishi wa wanawake wa ki-Islam ni mkongwe, wenye maudhui na vipengele vingi. Hata ukiangalia uandishi katika lugha moja tu, kama vile ki-Arabu, utakutana na uwingi huo. Uje kwenye ki-Faransa, ni hivyo hivyo. Kwenye ki-Swahili, nako unaweza ukaunda kozi kamili ya tungo (kuanzia simulizi hadi andishi) za wanawake wa ki-Islam wa ki-Swahili.

Ndio maana, mtu aliyeelimika anapaswa daima kukiri kuwa kile anachokijua ni kama tone tu katika bahari. Na jamii inatakiwa iamke pia, iwe na utamaduni wa kutafuta elimu kama alivyohimiza Mwalimu Nyerere. Binafsi sina tatizo, kwani ni msomaji wa vitabu na maandishi mengine daima. Daima ninajaribu kujiongezea hilo tone akili mwangu. Hayo mahangaiko yangu ya kutafuta elimu nimeyaelezea katika ujumbe wangu, wa hapo juu, na nyakati zingine.

Katika kufundisha kozi, mtu unawajibika kuchagua maandishi kadhaa tu, kwa sababu unakuwa na muda kiasi fulani tu wa kufundisha somo. Muda ni kipingamizi. Kitu kingine ni kuwa hili ni somo la fasihi, kwa hivi unazingatia zaidi kazi za sanaa. Katika somo hilo, maandishi ambayo ni "biographical," au "autobiographical" yanaweza kuwa na mchango, lakini msisitizo unatakiwa kuwa katika fasihi.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...