Showing posts with label uandishi. Show all posts
Showing posts with label uandishi. Show all posts

Thursday, October 11, 2018

Mchakato wa Kwenda Kuongelea Kitabu

Leo nimepata ujumbe kutoka kwa Dan, ambaye hivi majuzi alikipigia debe kitabu changu, Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, katika duka la Barnes and Noble, kama nilivyoelezea katika blogu hii. Anaendelea na juhudi yake. Ameandika:

Happy to spread the word about your book. Let me know if you are ever interested in doing a talk at our store. I can connect you with our manager.

Tafsiri yangu:

Ninafurahi kukitangaza kitabu chako. Nijulishe iwapo utapenda kuja kukiongelea katika duka letu. Nitaweza kukuunganisha na meneja wetu.

Kuwaalika waandishi kuongelea vitabu vyao ni utamaduni wa kawaida hapa Marekani. Ni fursa ya mwandishi kukutana na watu wanaotaka kujua mambo kama  historia ya mwandishi, changamoto za uandishi, falsafa na mawaidha yake kuhusu uandishi, na kadhalika. Vinakuwepo vitabu vya mwandishi, kwa watu kuvinunua na yeye kuvisaini. Wa-Marekani wanapenda kusainiwa vitabu, kama nilivyowahi kusema katika blogu hii.

Sunday, April 15, 2018

Mialiko kwa Mwandishi wa Kitabu

Kutokana na mawasiliano kutoka kwa waandishi chipukizi Tanzania ninafahamu kuwa hao ni miongoni mwa wasomaji wa blogu yangu hii ambamo ninaandika mara kwa mara kuhusu vitabu. Mbali na kuviongelea vitabu, nimekuwa nikiandika kuhusu uandishi, uchapishaji, na uuzaji wa vitabu kutokana na uzoefu wangu.

Leo ninapenda kuongelea kipengele cha mialiko kwa mwandishi wa kitabu, jadi ninayoiona hapa Marekani, mwandishi kualikwa kuzungumza sehemu mbali mbali baada ya kuchapisha kitabu. Mada hii nimeigusia kwa kiasi fulani katika blogu hii Hata hivyo, nimeona niongezee neno.

Kama wewe ni mfuatiliaji wa blogu yangu hii, utakuwa unafahamu kuwa ninapata mialiko mara kwa mara kuongelea mada zinazohusiana na vitabu vyangu: Matengo Folktales na Africans and Americans: Embracing Cultural Differences. Suali ni je, kwa nini watu wanialike badala ya wao kusoma tu nilichoandika? Wananialika nikawasomee?

Jibu ni hapana. Kinachowafanya wanialike ni kutambua kwao, baada ya kusoma kitabu, kwamba wana mambo yatokanayo na yale yaliyomo kitabuni ambayo wangetaka kuyafahamu zaidi. Kitabu changu si kwamba kinajitosheleza, bali kina madokezo muhimu. Ni chachu ya dukuduku kwa wasomaji. Hata kama hakijitoshelezi, wanavutiwa na mwelekeo wa fikra. Hiyo ni sababu muhimu ya kunialika nikazungumze nao.

Wengine wakishasoma kitabu, wanakuwa na imani kwamba ninaweza kuwasaidia mawazo juu ya mipango wanayotaka kutekeleza au mambo yanayowakabili. Kwa mfano, viongozi wa kampuni au taasisi wanaona kwamba ninaweza kuwasaidia katika kuzielewa na kuzitatua changamoto zitokanazo na kuwa na timu ya watu wa tamaduni mbali mbali. Mfano ni nilivyoalikwa RBC Wealth Management.

Kuhusu kitabu cha Matengo Folktales, watu wanataka kufahamu zaidi juu ya utamaduni wa kusimulia hadithi ulivyo Afrika na pia wanataka kusikiliza hadithi zinavyosimuliwa. Ndivyo ilivyokuwa nilipoalikwa chuo kikuu cha St. Benedict/St. John's na pia maktaba ya Redwing.

Kwa upande wa Tanzania, jadi hii ya kuwaalika waandishi kuzungumzia uandishi na vitabu ingekuwa na manufaa kama ilivyo Marekani. Waandishi wangekuwa wanaielimisha jamii uzoefu wao katika vipengele mbali mbali, kama vile jinsi walivyopata wazo la kuandika au walivyoanza kuandika, mchakato wa uandishi, ugumu au urahisi wake, vipingamizi, uchapishaji, uhusiano na wachapishaji, wasomaji, wahakiki, na wauzaji wa vitabu. Waandishi wangetumia fursa hizi kutoa ushauri kwa waandishi chipukizi.

Katika mkutano na mwandishi, vitabu vya mwandishi vinaweza kuwepo, ili wahudhuriaji wanunue. Huu ni utaratibu unaofanyika sana hapa Marekani. Ni njia nzuri ya vitabu kuifikia jamii. Vile vile, kwa uzoefu wangu hapa Marekani, uwepo wa mwandishi na jinsi anavyojieleza, kunawavutia watu kununua kitabu. Kitu kingine kinachovutia ni kusainiwa kitabu na mwandishi, kama nilivyowahi kuandika katika blogu hii, katika kubadilishana mawazo na mwanablogu Christian Bwaya.

Wednesday, September 6, 2017

Muhula wa Masomo Unaanza

Wiki hii hapa chuoni St. Olaf, tunaanza muhula mpya wa masomo. Nitafundisha madarasa matatu. Mawili ni ya "First Year Writing," na moja ni "Post-colonial Literature." Katika "First Year Writing," tunafundisha uandishi bora wa ki-Ingereza.

Kozi ninayotaka kuongelea hapa  ni "Post-colonial Literature." Niliajiriwa hapa chuoni St. Olaf kuanzisha kozi hiyo, na nilianza kufundisha mwaka 1991. Ni kozi inayohusu fasihi kutoka nchi zilizokuwa katika himaya ya u-Ingereza wakati wa ukoloni ila zilikuja kuwa huru.

Ninapofundisha kozi hii, huwa ninaamua waandishi wepi kutoka nchi zipi nifundishe. Kwa muhula huu, niliamua kufundisha fasihi kutoka Afrika Kusini. Nilichagua waandishi wawili: Alex la Guma na Nadine Gordimer. Wote ni waandishi wa hadithi fupi na riwaya.

Nadhani tangu nilipokuwa mwanafunzi Mkwawa High School, nilisoma hadithi za Alex la Guma katika kitabu cha hadithi fupi kiitwacho Quartet. Baadaye, nilipokuwa mwanafunzi katika idara ya Literature, chuo kikuu cha Dar es Salaam, Alex la Guma alikuja kutoka London akatufundisha kwa siku kadhaa. Alialikwa na mkuu wa idara, mwalimu Grant Kamenju wa Kenya.

Nilifahamu kuwa Alex la Guma alikuja kuwa mwakilishi Uingereza wa chama cha ukombozi cha African National Congress cha Afrika Kusini, (ANC), kisha akawa mwakilishi wa ANC nchini Cuba. Alipofariki, nchini Cuba, nilikuwa ninasoma katika Chuo Kikuu cha Wisconsin Madison.

Nadine Gordimer ni mzungu aliyejihusisha na ANC. Alikuwa mpinzani wa utawala wa makaburu. Baada ya kuja Marekani kufundisha, nimebahatika kumwona Nadine Gordimer kwenye mkutano fulani wa kitaaluma. Sikumbuki ulikuwa ni mwaka gani. Nimefundisha hadithi zake fupi zilizokusanywa katika kitabu Six Feet of the Country, na riwaya zake, The Conservationist, The Pickup, na July's People.

Kufundisha juu ya waandishi hao wawili ni fursa ya kutafakari historia na siasa, hasa ukaburu na harakati za ukombozi katika Afrika Kusini. Yote hayo yamefungamana na fasihi, hasa katika karne ya ishirini, ambayo ndiyo kozi yangu itashughulikia. Tutafakari mitazamo ya waandishi hao wawili kuhusu siasa, mahusiano ya jamii, utamaduni, na itikadi katika Afrika Kusini. Tutaangalia athari za fasihi ya ulimwengu katika maandishi ya waandishi hao wawili na tutatambua mchango wa waandishi hao katika fasihi ya Afrika na ulimwengu.

Wednesday, July 12, 2017

Mazungumzo Global Minnesota Kuhusu Fasihi





Leo nilikwenda Minneapolis, kwa mwaliko wa taasisi iitwayo Global Minnesota, kutoa mhadhara juu ya fasihi simulizi na andishi wa Afrika, kuanzia chimbuko lake barani Afrika hadi Marekani, ambako hii fasihi simulizi ililetwa na watu waliosafirishwa kutoka Afrika kama watumwa. Watoa mada tulikuwa wawili, mwingine ni Profesa Mzenga Wanyama anayefundisha katika chuo cha Augsburg.


Pichani hapa kushoto, tunaonekana kama ifuatavyo. Kutoka kushoto ni Tazo kutoka Zambia, ambaye alihitimu chuo cha St. Olaf  mwaka jana, na amajiriwa kwa mwaka huu moja na Global Minnesota. Wa pili ni Carol, rais wa Global Minnesota. Wa tatu ni Profesa Wanyama. Wa nne ni mimi, na wa tano ni Tim, mkurugenzi wa programu wa Global Minnesota, ambaye alikuwa mtu wa kwanza kuniuliza kama ningekuwa tayari kutoa mhadhara Global Minnesota, wakati tulipokutana katika tamasha la Togo miezi michache iliyopita.


















Hapa kushoto ninaonekana nikiongea. Sina kawaida ya kusoma hotuba, hata kama nimeandika vizuri. Ninashindwa kuangalia karatasi badala ya kuangalia watu. Hata darasani, sisomi nilichoandaa kimaandishi. Katika kujiandaa kwa ajili ya kutoa mihadhara, ninaandika sana hoja na maelezo yangu. Lakini wakati wa kutoa mhadhara, ninatumia kumbukumbu tu ya yale niliyoandika.

Kwa hivyo, katika mhadhara wa leo, nimeongelea chimbuko la binadamu ambalo liliendana na uwezo kutembea wima kwa miguu tu, kutumia lugha, na  kutumia na kutengeneza zana za kazi. Hayo yote kwa pamoja yalisababisha kuumbika kwa kiumbe aitwaye binadamu kimwili, kiakili, na kadhalika. Huu ndio msingi wa kukua kwa lugha na fasihi, ambayo ilihitaji ubunifu, kumbukumbu, na uwezo wa kutambua na kuunda sanaa,  ikiwemo fasihi, ambayo ni sanaa inayotumia lugha.

Maendeleo ya tekinolojia, ambayo ilianzia na kutengeneza zana za mawe au miti, yalifikia hatua ya binadamu kuvumbua maandishi. Hapo ndipo ikawezekana kuandika yale yaliyokuwa katika fasihi simulizi, na ushahidi tunauona katika Misri ya miaka yapata elfu nne au tano iliyopita. Hadithi zilizoandikwa wakati ule ni kama "The Tale of Two Brothers," "The Story of Sinuhe," na "The Tale of the Ship-wrecked Sailor."

Lakini pia, uandishi ulimwezesha binadamu kutunga fasihi kimaandishi. Waandishi, hasa wa mwanzo, walikuwa wamelelewa katika fasihi simulizi, kiasi kwamba kazi zao andishi zilibeba athari za wazi za fasihi simulizi. Mifano kutoka Afrika ni The Golden Ass (Apuleus), Chaka (Thomas Mofolo), The Palm Wine Drinkard (Amos Tutuola), Things Fall Apart (Chinua Achebe), The Dilemma of a Ghost (Ama Ata Aidoo). Waandishi weusi wa bara la Marekani kama vile Zora Neal Hurston, Toni Morrison, na Edwidge Dandicat.




Baada ya mimi kuongea, alifuata Profesa Mzenga Wanyama, kama inavyoonekana pichani hapa kushoto. Yeye aliongelea zaidi waandishi weusi wa Marekani, akianzia na Phyllis Wheatley. Aliongelea elimu na itikadi aliyofundishwa msichana na hata alipoandika mashairi yake, akawa anaelezea pia waandishi wa ki-Afrika kama vile Achebe na Ngugi wa Thiong'o, na Chimamanda Ngozi Adichie. Kati ya masuala aliyosisitiza ni utumwa wa fikra na umuhimu wa kujikomboa. Baada ya hotuba zetu, palikuwa na muda mfupi wa masuali na majibu.









Baada ya kikao kwisha, hawakosekani wahudhuriaji wenye kupenda kuongea zaidi na mtoa mada. Hapa kushoto niko na profesa mstaafu wa College of St. Benedict, Minnesota. Ni mzaliwa wa India. Nilimwambia kuwa nilishawahi kualikwa kwenye chuo kile kutoa mihadhara.













Hapa kushoto anaonekana Carol, rais wa Global Minnesota, na binti yangu Assumpta, ambaye aliwahi kufanya kazi na Carol, wakati taasisi ilipokuwa inaitwa International Institute of Minnesota.















Hapa kushoto niko na mama moja kutoka Brazil, ambaye ni mfanyakazi katika Minnesota Department of Human Services. Sikumbuki kama nimewahi kuongea na mama yeyote wa Brazil mwenye asili ya Afrika. Kwa hiyo, hiyo ilikuwa ni kumbukumbu ya pekee.
















Hapa kushoto niko na vijana wawili waliohitimu masomo chuo cha St. Olaf ambapo ninafundisha. Huyu wa kushoto kabisa ni raia wa Swaziland, na huyu wa kulia ni Tazo wa Zambia anayeonekana katika picha ya kwanza hapo juu.













Hapo kushoto niko na binti zangu, Assumpta na Zawadi. Ninafurahi wanapokuja kunisikiliza katika mihadhara. Wataweza kuelezea habari zangu kwa yeyote atakayependa kuelewa zaidi shughuli zangu katika jamii.

Nimalizie kwa kusema kuwa wakati tulipokuwa tunaagana, viongozi wa Global Minnesota walielezea nia yao ya kuniita tena kwenye program nyingine. Tim aliongezea kuwa kama  angekuwa amekumbuka, vitabu vyangu vingekuwepo kwa ajili ya watu waliohudhuria mkutano wa leo. Nami nilikuwa sijawazia jambo hilo. Siku zijazo litaweza kufanyika.

Monday, July 10, 2017

Nitawasilisha Mada Global Minnesota

Nimealikwa na taasisi iitwayo Global Minnesota kutoa mada tarehe 12 Julai juu ya mwendelezo wa fasihi ya ki-Afrika kuanzia chimbuko lake kama fasihi simulizi hadi fasihi andishi ya leo. Mael"ezo zaidi yako mtandaoni

--------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------
Global Conversations: African Folktales to Contemporary Authors

JULY 12 @ 6:00 PM CDT / Free

From ancient oral traditions to contemporary literature, African stories reflect wisdom, cultural identities, and social values developed over countless generations. Join us, St. Olaf College Associate Professor Joseph Mbele, and Augsburg College Associate Professor Mzenga Wanyama for an exploration of how these stories find expression today, both in Africa and in the African diaspora.

Speakers
Joseph Mbele, Associate Professor of English at St. Olaf College, is a folklorist and author. His writings, including Matengo Folktales, illuminate the underlying values that shape cultures. Dr. Mbele has done fieldwork in Kenya, Tanzania, and the U.S., and has given lectures and presented conference papers in Canada, Finland, India, Israel, Kenya, Tanzania, Uganda, and the U.S. After earning a Ph.D. from the University of Wisconsin and before coming to St. Olaf in 1990 to teach post-colonial and third-world literature, he taught in the Literature Department at the University of Dar es Salaam, Tanzania. Over the years, he has taught courses such as Swahili Literature, Theory of Literature, African Literature, Sociology of Literature, Postcolonial and Third World Literature, The Epic, and African-American Literature.

Mzenga Aggrey Wanyama, Associate Professor of English at Augsburg College, was born and raised in Kenya where he received his bachelor’s of education and master’s degrees from the University of Nairobi and then taught English language and literature in Kenyan High schools and at Kenyatta University. In the United States, he had a two-year stint in the graduate program at Howard University in Washington, D.C. before attending the University of Minnesota where he earned a Ph.D. in English. Mzenga also worked as an Assistant Professor of English at St. Cloud State University where he taught courses in literature and writing. His areas of focus are Postcolonial theory and literature and African American literary history.

Presented in partnership with the Friends of the Minneapolis Central Library.

Global Conversations: African Folktales to Contemporary Authors
Wednesday, July 12, 2017
6:00 PM

Saturday, July 1, 2017

Vitabu Nilivyonunua Leo

Ninaamini kuwa kila mtu ana kitu anachokipenda sana. Kuna watu wanaopenda sana soka. Ni mashabiki ambao daima wanafuatilia mechi. Wako tayari kukopa hela ili waende uwanjani kuangalia mechi. Wengine wanapenda bia. Katika baa za Tanzania, nimeona watu wanaokunywa na kuandikiwa deni walipe baadaye. Kama huku kupenda kitu namna hii ni ugonjwa, basi vitabu ndio ugonjwa wangu. Ndio maana katika blogu hii ninaandika mara kwa mara habari za vitabu.

Mtu anaweza kuuliza, inakuwaje katika ulimwengu huu wa vitabu pepe, tuko watu ambao tunaendelea kung'ang'ania vitabu vya jadi? Je, hatuoni udhia wa kubeba vitabu hivyo, na pia udhia wa kuvitafutia sehemu ya kuviweka, badala ya kutumia kifaa cha kuhifadhia vitabu pepe, ambacho kinaweza kubeba mamia ya vitabu au zaidi? Ukweli ni kwamba, mazoea yana taabu. Sio rahisi kuachana na mazoea.

Leo nilikwenda Minneapolis, na wakati wa kurudi, nilipita katika duka la vitabu la Half Price Books, mjini Apple Valley. Kama kawaida, niliangalia kwanza sehemu vinapowekwa vitabu vya Ernest Hemingway au vitabu juu ya Hemingway. Sikuona kipya, nikaelekea sehemu vinapouzwa vitabu vya bei rahisi kabisa. Hapo nilichagua vitabu vinne.

Kitabu kimoja ni Gilgamesh: A Verse Narrative, cha Herbert Mason. Wafuatiliaji wa fasihi simulizi za kale wanafahamu juu ya Gilgamesh, mtu maarufu katika masimulizi ya watu wa himaya ya Sumer, katika nchi ambayo leo inaitwa Iraq, na pia nchi zingine za Mashariki ya Kati. Masimulizi haya hatimaye yaliandikwa, katika lugha kadhaa za wakati ule, kwa hati iitwayo "cuneiform," ambayo ni tofauti kabisa na hizi hati tunazotumia leo, kama vile ya ki-Rumi, au ki-Arabu. Ugunduzi wa maandishi yale ulitokana na juhudi za wana akiolojia.

Lakini baada ya ugunduzi, hakuna aliyeweza kusoma hati ya "cuneiform." Baadaye sana siri ya hati hii iligunduliwa na usomaji wake ukawezekana. Tafsiri za masimulizi ya Gilgamesh zikaanza. Kwa upande wangu, kwa miaka mingi nimefundisha masimulizi ya Gilgamesh kwa kutumia tafsiri ya N. K. Sandars. Nilifahamu, hata hivyo, kwamba ziko tafsiri zingine pia. Kwa hivyo, leo niliona ninunue hii tafsiri ya kishairi ya Herbert Mason.

Kitabu kingine nilichonunua leo ni A Play of Giants, ambayo ni tamthilia ya Wole Soyinka. Nimesoma na kufundisha maandishi ya Soyinka kwa miaka mingi, kuanzia tamthilia, riwaya, mashairi na insha. Ninavyo vitabu vyake kadhaa, lakini si A Play of Giants. Hata hivyo, nilifahamu tangu zamani kuwa tamthilia hii inawaumbua madikteta wa Afrika. Sasa nitaisoma.

Kitabu cha tatu nilichonunua ni Theban Plays of Sophocles. Ni tafsiri ya David R. Slavitt ya tamthilia tatu za Sophocles. Huyu ni mwanatamthilia maarufu wa u-Griki ya kale. Ninazo tatsiri tofauti za tamthilia hizo, lakini niliamua kununua hii pia. Ni jambo bora kusoma tafsiri mbali mbali za kazi ya fasihi, kwani kila tafsiri inaleta ladha tofauti na hata tofauti za ujumbe.

Kitabu cha nne nilichonunua ni Speaking of Books: The Best Things Ever Said About Books and Book Collecting, kilichohaririwa na Rob Kaplan na Harold Rabinowitz. Hicho sikuwahi hata kukisikia, lakini nilivyoangalia ndani, nilivutiwa. Ni mkusanyiko wa kauli za watu mbali mbali kuhusu vitabu, usomaji, uandishi, waandishi, wasomaji, na kadhalika. Nilikuwa ninafahamu baadhi ya mambo ambayo yamewahi kusemwa kuhusu vitabu, kama vile kauli ya Ernest Hemingway, "There is no friend as loyal as a book," yaani hakuna rafiki wa kweli kama kitabu. Kutokana na kupendezwa kwangu na mambo hayo, niliona ninunue kitabu hiki.

Friday, April 14, 2017

Neno Kuhusu Matokeo ya Kuchapisha Kitabu

Mimi kama mwandishi wa vitabu ninafurahi ninapopata wasaa wa kuelezea uzoefu wangu na kutoa ushauri kwa waandishi wengine au wale wanaowazia kuwa waandishi. Mara kwa mara ninaandika kuhusu mambo hayo kwa kujiamulia mwenyewe, lakini mara kwa mara ninaandika kuwajibu wanaoniulizia. Baadhi ya mawasiliano hayo huwa ni ya binafsi, na mengine hufanyika katika blogu hii.

Leo nimeona niseme neno kuhusu matokeo ya kuchapisha kitabu. Ninaandika kufuatia uzoefu wangu wa hapa Marekani. Kuchapisha kitabu ni aina ya ukombozi kwa mwandishi kutakana na jambo lilolokuwa linakusonga mawazoni. Ni kama kutua mzigo. Baada ya kumaliza kuandika, unajisikia mwenye faraja, tayari kuanza au kuendelea na majukumu mengine. Ni aina ya ukombozi.

Kuna waandishi chipukizi wanaoamini kuwa kuandika kitabu kutawaletea umaarufu au fedha. Wazo hili ni bora kuliweka kando. Fedha si jambo la kulipa kipaumbele; kwa kiasi kikubwa ni kubahatisha. Kwanza, kuna vitabu vingi mno vinavyochapishwa kila mwaka. Kwa hapa Marekani tu, vitabu zaidi ya milioni huchapishwa kila mwaka, kwa mujibu wa taarifa zilizopo. Sio rahisi mwandishi anayeanza safari ya uandishi ajipambanue na kuwa maarufu. Kwa wastani, nakala za kitabu zinazouzwa kwa mwaka ni 250, na ukomo wa mauzo kwa miaka yote ya kuwepo kitabu ni pungufu ya nakala 3,000.

Kwa hapa Marekani, kuna jadi kwamba waandishi, wakishachapisha kitabu, hufanya safari za kutangaza kitabu hicho. Safari hizi hupangwa na kuratibiwa na wadau wa vitabu kama vile wachapishaji wa vitabu, wauzaji wa vitabu, waendeshaji wa majarida yanayojihusisha na vitabu, na vikundi vya wasomaji katika miji na maeneo mbali mbali. Wote hao wanashiriki katika kufanikisha ziara ya mwandishi. Wanatangaza kwa namna yoyote ile ziara hiyo, magazetini, katika redio, katika televisheni, au mitandao ya kijamii.

Popote anapofika mwandishi, watu hujitokeza kumsikiliza akiongelea kitabu chake. Wanapata fursa ya kumwuliza masuali. Nakala za kitabu zinakuwepo, na watu wanapata fursa ya kununua na kusainiwa. Wenye maduka ya vitabu hupenda kuandaa mikusanyiko hiyo. Mbali na kwamba wanampa mwandishi fursa ya kukutana na wasomaji, na kutangaza kitabu chake, ni fursa kwa hayo maduka ya vitabu kujitangaza. Ni jadi iliyozoeleka kwamba nyakati hizo, kunakuwa na punguzo la bei ya kitabu kinachotangazwa, na hiki kinakuwa ni kivutio cha ziada kwa wateja.

Lakini jambo la msingi ni kuwa watu wa Marekani wanathamini sana fursa ya kukutana na mwandishi. Mimi mwenyewe, ingawa bado si mwandishi aliyetunukiwa tuzo maarufu kama Pulitzer, ninashuhudia jinsi watu wanavyovutiwa na fursa ya kukutana nami, iwe ni kwenye matamasha au kwenye mihadhara ninayotoa.

Hizi fursa za waandishi za kwenda kuongelea vitabu vyao ndio njia moja kuu ya waandishi kujijenga katika jamii. Mwandishi kuonekana na kusikilizwa moja kwa moja na wasomaji na wadau wengine wa vitabu ni njia ya kujijenga mioyoni mwao. Kukutana na mwandishi namna hiyo kunaleta picha na hisia ya pekee pale msomaji anaposoma kitabu cha mwandishi huyo. Bila shaka wote ambao tumewahi kukutana na waandishi tunajisikia hivyo tunaposoma maandishi yao.

Nimegusia hapo juu kuwa kuna watu wanaowazia kuwa kuchapisha kitabu kutawaletea umaarufu au fedha. Ni kweli, kutegemeana na kukubalika kwa kitabu katika jamii, mwandishi anaweza kupata umaarufu na fedha kiasi fulani. Lakini, kwa uzoefu wangu, ninapoalikwa kwenda kuongelea kitabu ndipo pana malipo makubwa, ukiachilia mbali kuwa vile vile nakala za vitabu zinauzwa hapo hapo. Vitabu ninavyoongelea hapa ni viwili: Africans and Americans: Embracing Cultural Differences na Matengo Folktales. Kipo kingine ambacho nimekuwa nikiandika kwa miaka kadhaa, kuhusu athari za tofauti za tamaduni, ambacho nina hakika kuwa kitawagusa watu kwa namna ya pekee.

Ningependa mambo hayo niliyoelezea yafanyike Tanzania. Ninatamani uje wakati ambapo, mwandishi akishachapisha kitabu muhimu, kiwe ni cha fasihi au maarifa, awe na fursa ya kuzunguka nchini kuongelea kitabu chake. Ninatamani uje wakati ambapo wananchi watakuwa na utamaduni wa kuvipenda vitabu na kupenda kukutana ana kwa ana na waandishi na kuongea nao.

Sunday, February 12, 2017

Nimemaliza Kusoma The Highly Paid Expert

Leo nimemaliza kusoma The Highly Paid Expert, kitabu kilichotungwa na Debbie Allen, ambacho nilikitaja katika blogu hii. Nimekifurahia kitabu hiki, kwa jinsi kilivyoelezea misingi na mbinu za kumwezesha mtu kuwa mtoa ushauri mwenye mafanikio kwake na kwa wateja.

Mambo anayoelezea mwandishi Debbie Allen yananihusu moja kwa moja katika ya kampuni yangu ya Africonexion: Cultural Consultants. Kwa hivi, kitabu hiki kimekuwa na mvuto wa pekee kwangu. Nimevutiwa na namna mwandishi anavyoelezea mbinu za mtu kujijenga katika uwanja wake hadi kufikia kileleni. Anaelezea mategemeo ya wateja na namna ya kushughulika nao. Anaelezea umuhimu wa kujifunza kutoka kwa wataalam wengine, matumizi ya tekinolojia katika kuwasiliana na wateja, kuendesha mikutano, na kujitangaza. Vile vile anasisitiza uaminifu na uwajibikaji.

Ameelezea vizuri namna wengi wetu tunavyoshindwa kujitangaza na tunavyoshindwa au kusita kutambua umaarufu na umuhimu wetu na thamani ya ujuzi wetu, jambo ambalo linatufanya tusitegemee malipo yanayoendana na ubingwa wetu. Tunaridhika na malipo hafifu, wakati tulistahili malipo makubwa.

Sura ya 24 ya The Highly Paid Expert inaelezea uandishi wa kitabu. Mwandishi anasema kuwa kitabu ni nyenzo muhimu ya mtaalam katika fani yake. Kitabu kinamjengea sifa na kuonekana. Kinamfanya mtaalam aaminike. Mwandishi anaeleza wazi kuwa kitabu hakileti utajiri, bali kinafungua milango ya fursa.

Hayo nimejionea mwenyewe. Kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences kimenifungulia fursa nyingi. Nimepata mialiko ya kwenda kutoa mihadhara au ushauri katika taasisi na jumuia mbali mbali, kama vile makanisa, vyuo, na makampuni.

Nimevutiwa na mambo anayoelezea mwandishi wa The Highly Paid Expert kuhusu uandishi na uuzaji wa kitabu. Yanafanana na yale ambayo nami nimekuwa nikieleza katika blogu hii. Kwa mfano, anasema kuwa jukumu kubwa la kutangaza na kuuza kitabu ni la mwandishi.

The Highly Paid Expert ni kati ya vitabu ambavyo nimevifurahia kwa dhati. Mawaidha yake mengi ni ya kukumbukwa daima. Mfano ni msisitizo wake juu ya kushirikiana na wengine. Mtu hufanikiwi kwa uwezo wako mwenyewe tu na kutojihusisha na wengine wenye utaalam, hata kama ni washindani wako.

Wednesday, October 26, 2016

Miaka 80 ya "The Snows of Kilimanjaro"

Kwa mara nyingine tena, ninaandika ujumbe kuhusu kutimia kwa miaka 80 tangu hadithi ya Ernest Hemingway, 'The Snows of Kilimanjaro" ilipochapishwa kwa mara ya kwanza. Niliandika ujumbe wa aina hiyo katika blogu hii. Leo nimesoma tena ujumbe wangu, nikajiridhisha kwamba niliyosema ndiyo ninayoamini hadi sasa.

Jambo moja kubwa kabisa ni kuwa wa-Tanzania tunajipotezea fursa za wazi za kutumia hazina kama hii hadithi ya Hemingway kuitangaza nchi yetu. Niliandika katika ujumbe wangu baadhi ya mambo ambayo tungeyafanya mwaka huu wa kumbukumbu. Lakini mwaka unaelekea ukingoni, na hakuna tulichofanya. Hii ni hasara ya kukosa utamaduni wa kusoma vitabu. Tunashindwa hata kutumia fursa zilizo wazi.

Nimeona niandike ujumbe huu leo kwa sababu wiki hii, hapa katika Chuo cha St. Olaf ninapofundisha, litatokea jambo la pekee linalohusiana na Ernest Hemingway. Keshokutwa, tarehe 28, pataonyeshwa kwa mara ya kwanza filamu ya "Papa's Shadow," ambayo niliwahi kuielezea katika blogu hii.

Hiyo ni filamu iliyotokana na kozi niliyofundisha Tanzania mwaka 2013 iitwayo Hemingway in East Africa. Nilisafiri na wanafunzi 29 wa Chuo cha St. Olaf, tukazunguka maeneo kadhaa ya Tanzania kaskazini, ambamo alipita Ernest Hemingway mwaka 1933-34. Katika safari hiyo, tulikuwa tunasoma maandishi ya Hemingway kuhusu maeneo hayo na maeneo mengine ambayo alipitia mwaka 1953-54.

Maandishi hayo ni pamoja na Green Hills of Africa na Under Kilimanjaro, ambavyo ni vitabu, kadhalika hadithi fupi mbili: "The Short Happy Life of Francis Macomber" na "The Snows of Kilimanjaro." Pia aliandika makala katika magazeti na barua nyingi akielezea aliyoyaona na kufanya katika safari zake. Kwa ujumla wake, maandishi haya ya Ernest Hemingway yanaitangaza nchi yetu na Afrika Mashariki kwa ujumla kwa namna ambayo sisi wenyewe hatujaweza kujitangaza.

Hiyo filamu ya "Papa's Shadow" inawasilisha vizuri mambo muhimu ya uhusiano wa Ernest Hemingway na Afrika Mashariki. Sehemu kubwa ya filamu hii ni mazungumzo baina yangu na Mzee Patrick Hemingway, mtoto pekee aliyebaki wa Ernest Hemingway. Tunajadili kwa kina na mapana fikra za Ernest Hemingway kuhusu Afrika, uandishi, na maisha kwa ujumla.

Kwa kuwa hiyo filamu inaonyesha sehemu mbali mbali za Tanzania na maelezo kuhusu mambo yanayoifanya Tanzania kivutio kwa watalii, kama vile Mlima Kilimanjaro, na kwa kuwa filamu hii imejengeka katika maandishi ya Ernest Hemingway, mwandishi maarufu sana ulimwenguni, ni wazi kuwa filamu hii itakuwa chachu ya kuitangaza Tanzania kwa namna ya pekee. Taarifa zaidi Kuhusu "Papa's Shadow," zinapatikana kwenye tovuti ya Ramble Pictures.

Monday, October 24, 2016

Ninarekebisha Kitabu Nilichochapisha Mtandaoni

Mara kwa mara, ninaongelea suala la kuchapisha vitabu mtandaoni, kutokana na uzoefu wangu. Ninatarajia kuwapa wengine uzoefu wangu wa kutumia tekinolojia za uchapishaji mtandaoni, ambazo zinatoa fursa tele kwa yeyote kujikomboa na taabu na vikwazo vya uchapishaji wa jadi.

Faida mojawapo ya uchapishaji wa aina ninayotumia kuchapishia vitabu vyangu ni fursa isiyo na mipaka ya kurekebisha kitabu chako wakati wowote uonapo dosari ndani yake au fursa ya kukiboresha. Hilo linawezekana kwa kuwa mswada wako unakuwa umehifadhiwa kama faili la kielektroniki mtandaoni, hata kama hukuuhifadhi katika kompyuta, disketi, au kifaa kingine.

Mimi ninatumia mtandao wa lulu.com. Hapo, ukishachapisha kitabu, nakala ya mswada inahifadhiwa hapo hapo mtandaoni. Unapotaka kurekebisha kitabu chako, unachofanya ni kuuingiza "(down-loading") mswada katika "flash drive" na kuufanyia marekebisho. Kisha unaurudisha ("up-loading") sehemu ya kuchapishia. Yeyote atakayekinunua baada ya hapo atakuwa ananunua kitabu kilichoboreshwa.

Hatua zote hizi zinafanyika bila mtu yeyote kutambua kinachotokea, bali wewe mhusika tu. Na wakati wote, unaporekebisha mswada, kitabu hakitoweki hapo mtandaoni. Kinakuwa kama kilivyokuwa mwanzo, na yeyote anaweza kukinunua, wakati wewe unaendelea na marekebisho. Unapomaliza marekebisho na kukiingiza tena mtandaoni ("up-loading"), ndipo kitabu kilichoboreshwa kinachukua nafasi ya kile cha awali.

Sasa hivi, niko katika kurekebisha kitabu changu, Notes on Okot p'Bitek's Song of Lawino. Hakuna anayetambua kuwa kinafanyiwa marekebisho, kwani kinaonekana hapo mtandaoni kama kawaida. Nitakapomaliza marekebisho na kukichapisha tena, itakuwa kama vile hakuna lililotokea.

Urahisi huu wa kurekebisha kitabu hauko katika uchapishaji wa jadi, ambapo inabidi kungoja hadi wakati wa kutoa toleo jipya la kitabu. Aghalabu, wachapishaji huwa hawana uwezo wa kifedha wa kutoa toleo jipya. Nakala zikiisha, huwa ndio mwisho wa kuchapishwa kitabu.

Lakini tatizo hili haliko katika uchapishaji wa mtandaoni kama huu ninaotumia. Kitabu hakiwezi kutoweka, yaani kuwa "out of print," labda mtu uamue kukiondoa wewe mwenyewe hapo mtandaoni. Ukibadili mawazo ukataka kukirudisha tena ulimwenguni, ni hiari yako kufanya hivyo, wakati wowote. 

Saturday, May 14, 2016

Nimepita Tena Katika Duka la Half Price Books

Leo alasiri nilikwenda eneo la Minneapolis, mwendo wa maili 40, kwa shughuli binafsi. Ilikuwa siku nzuri, ya jua la wastani na hali ya hewa ya kupendeza. Wakati wa kurudi, nilipita mjini Apple Valley, nikaamua kupitia katika duka la Half Price Books. Nilitaka hasa kuangalia kama kuna chochote juu ya mwandishi Ernest Hemingway. Kufuatilia vitabu juu ya Hemingway imeshakuwa mazoea kwangu, wala siwezi kujizuia.

Ninajua kuwa sitakikuta kitabu kipya kilichoandikwa na Hemingway. Inafahamika kwamba miswada yote ya vitabu vya Ernest Hemingway imeshachapishwa. Kinachotokea ni kuwa yanachapishwa matoleo mapya ya vitabu vyake, kama vile matoleo yanayohaririwa na mjukuu wake, Sean Hemingway, ambavyo Mzee Patrick Hemingway, mtoto wa Ernest Hemingway, anaviandikia utangulizi.

Maandishi mapya kabisa ya Ernest Hemingway yanayochapishwa ni barua zake. Kuna mradi wa kukusanya barua zote za Ernest Hemingway tangu utotoni mwake. Wahariri wa mradi huu ni maprofesa Sandra Spanier na Robert W. Trogdon, ambao wamebobea katika utafiti juu ya Ernest Hemingway. Hadi sasa majuzuu matatu yamechapishwa, na kila juzuu ni mkusanyo wa barua za miaka michache. Inatarajiwa kuwa mradi huu ambao utachukua miaka mingi, utatoa majuzuu yatachapishwa 17.

Vitabu vingine vipya ambavyo vinaendelea kuchapishwa ni matokeo ya utafiti juu ya maisha na maandishi ya Ernest Hemingway. Tangu zamani, kumekuwa na watafiti wengi wanaojishughulisha na utafiti huu, na vitabu ambavyo wamechapisha na wanaendelea kuchapisha ni vingi. Si rahisi kwa mtu yeyote kufuatilia suala hili kikamilifu, lakini ninakuwa na duku duku ya kuona kuna vitabu gani vipya juu ya Hemingway katika duka la vitabu.

Nimefurahi leo kukikuta kitabu juu ya Hemingway ambacho sikuwa hata nimekisikia, The True Gen: An Intimate Portrait of Hemingway by Those Who Knew Him kilichoandikwa na Denis Brian. Katika kukipitia, niliona kuwa kitabu hiki ni taswira ya Hemingway inayotokana na kumbukumbu za watu waliomfahamu. Niliamua hapo hapo kukinunua. Baada ya kufika nyumbani, nimeanza kukisoma.  Kuna maelezo ya watu wengi, kuanzia wale waliokuwa watoto wakienda shule na mtoto Ernest Hemingway hadi waandishi, wake zake, na watu wengine.

Kama ilivyo kawaida, nilipokuwa hapo dukani Half Price Books niliwaona watu wengi humo wakizunguka zunguka kuangalia vitabu na kuvinunua. Wazazi wengi walikuwa na watoto wao. Kama kawaida, inavutia kuwaona watoto wa ki-Marekani wanavyolelewa katika utamaduni wa kupenda vitabu.

Sikukaa sana humo. Baada ya kununua kitabu changu, niliona niwahi nyumbani nikaanze kukisoma.


Tuesday, February 23, 2016

"So Long a Letter" Katika Kozi ya "Muslim Women Writers"

Kozi yangu ya Muslim Women Writers inaendelea vizuri. Tulianzia India, na hadithi ya Sultana's Dream ya Rokeya Sakhawat Hossain. Baada ya hapo tunasoma So Long a Letter, utungo wa Mariama Ba wa Senegal, nchi mojawapo maarufu katika uwanja wa fasihi ya Afrika.

Senegal imetoa watunzi kama Leopold Sedar Senghor, Cheikh Hamidou Kane, Birago Diop, na Sembene Ousmane, kwa upande wa wanaume, na kwa upande wa wanawake kuna watunzi kama Aminata Sow Fall na Mariama Ba.

So Long a Letter ni utungo ulioandikwa kwa mtindo wa barua, ambayo mhusika mkuu anamwandikia mwanamke mwenzake, rafiki yake. Kwa hali hiyo, utungo huu unafuata jadi ambayo wanafasihi huiita "epistolary." Neno "epistolary" linatokana na neno la ki-Latini ambalo maana yake ni barua.

Suala moja muhimu linaloongelewa ni la wake wenza. Ni suala lenye chimbuko lake katika Qur'an, Sura iv aya 3:

     If ye fear that ye shall not
Bes able to deal justly
With the orphans,
Marry women of your choice,
Two, or three, or four;
But if ye fear that ye shall not
Be able to deal justly (with them),
Then only one, or (a captive)
That your right hand possess.
That will be more suitable,
To prevent you
From doing injustice.

Yusuf Ali, ambaye tafsiri yake ya Qur'an nimeinukuu hapa juu, anafafanua aya hii vizuri. Anakumbushia kwamba aya hii ilitokea katika mazingira maalum, ambamo kutokana na vita ya Uhud, jamii ya wa-Islam ilikuwa na wajane na yatima wengi, pamoja na mateka wa vita. Ilikuwa lazima watu hao watendewe kwa ubinadamu na haki kwa kiwango cha juu kabisa. Ruhusa ya kuwaoa wajane hao imewekewa masherti.

Kabla ya u-Islam, watu walikuwa wanaoa walivyopenda, lakini aya hii inaweka mipaka. Mtu anaweza kuoa hadi wake wanne, si zaidi, lakini kama Yusuf Ali anavyosema, "provided you could treat them with equality, in material things as well as in affection and immaterial things." Yaani masherti ni kwamba uweze kuwatendea wake hao kwa usawa katika mahitaji ya vitu, katika upendo, na mengine ya aina hiyo.

Kutokana na masherti hayo, Yusuf Ali anasema: "As this condition is most difficult to fulfill, I understand the recommendation to be towards monogamy." Yaani, kwa jinsi masherti yalivyo magumu kutekelezeka, nachukulia kwamba agizo hili linaegemea kwenye kuwa na mke moja.

Huu ndio msingi katika Qur'an wa suala la mitara. Wanawake wa-Islam wamekuwa wakilalamika kwamba fundisho la Qur'an limepotoshwa. Wanaume wamejitwalia mamlaka ya kupindisha mafundisho ya Qur'an na kuhalalisha mambo wanayoyapenda wao.  Hii ndio hali inayojitokeza katika So Long a Letter.

So Longer a Letter ni andiko linalohuzunisha kwa jinsi Ramatulaye anavyoelezea roho mbaya ya baadhi ya wanaume. Mume wake mwenyewe alijiolea binti kinyemela, na wanawake wengine wanakutana na adha za aina hiyo. Lakini, hasemi kuwa wanawake muda wote hawana dosari. Anakiri kuwa katika ndoa zingine, wanawake wanawatesa wanaume.

Hatimaye, So Long a Letter inaelezea matumaini ya kubadili mambo na kuwawezesha wanawake kushika nafasi wanazostahili katika jamii, wakitumia vipaji ambavyo wanavyo.

Monday, January 4, 2016

Nawazia Dini na Uandishi wa Wanawake wa ki-Islam

Muhula ujao, kuanzia mwezi Februari hadi Mei, nitafundisha kozi mpya hapa chuoni St. Olaf ambayo nimeiita "Muslim Women Writers." Ni kozi ya fasihi kwa ki-Ingereza, ambamo tutasoma maandishi ya wanawake wa-Islam kutoka Bangladesh, India, Iran, Misri, Sudan, Senegal, na Marekani. Taarifa fupi ya kozi hiyo nimeandika hapa.

Wakati huu ninapongojea kufundisha kozi hii katika mazingira ya leo ambamo maelewano miongoni mwa waumini wa dini na madhehebu mbali mbali yanatatanisha, ninajikuta nikiwazia mara kwa mara masuala ya dini. Katika siku zijazo, labda kwa miezi kadhaa, ninategemea kuandika tena na tena katika blogu hii kuhusu dini na kozi yangu.

Nimeshaandika mara kadhaa kuhusu dini. Nimeandika kuhusu umuhimu wa mijadala ya dini, umuhimu wa kuziheshimu dini zote, na nilivyozuru nyumba za ibada za dini nyingine. Sioni mantiki kwa dini yoyote kuwafundisha waumini wake kwamba Muumba anawapenda wao zaidi kuliko watu wa dini nyingine. Msimamo wangu ni kwamba Mungu (Allah) hana ubaguzi.

Ninafurahi na kujivunia kwamba kanisa langu Katoliki linasimama katika msingi huo, kama ilivyodhihirishwa katika ziara na ujumbe wa Papa John Paul wa Pili nchini Nigeria, ziara ya Papa Francis katika msikiti Uturuki, na katika sala ya Papa Francis ya kuuombea ulimwengu. Na zaidi ni kuwa Kanisa Katoliki lina baraza la kujenga maelewano miongoni mwa dini mbali mbali liitwalo Pontifical Council for Inter-religious Dialogue.

Katika kujiandaa kwa kozi yangu, nimekuwa nikiwazia kuwa ingekuwa vizuri kama ningesoma Quran yote. Ninayo Quran takriban tangu mwaka 1982. Nimekuwa nikisoma visehemu hapa na pale, lakini si yote kikamilifu. Ingawa ninafahamu misingi ya u-Islam kiasi cha kuridhisha, wazo la kuisoma Quran linanivutia.

Kuna mambo mengine ambayo nimekuwa nikifanya, kama vile utafiti ili kufahamu misimamo na mitazamo ya wanawake wa-Islam kuhusu u-Islam na nafasi yao katika dini hiyo. Nimeanza pia kuwatafuta wanawake wasomi wa ki-Islam na kujitambulisha kwao, ili waweze kuniongezea elimu kwa manufaa yangu na ya wanafunzi wangu. Ninafurahi kwa mafanikio ya kutia moyo ambayo nimeanza kuyaona.

Nimeandika ujumbe huu kwa kuzingatia kuwa wengi wanaosoma blogu yangu ni waumini wa dini. Wana wajibu wa kuchangia mawazo, hasa wakiona nimepotosha jambo lolote. Kwa muumini yeyote, hili si  suala la hiari, bali ni wajibu.

Saturday, December 19, 2015

Kuchapisha Vitabu Mtandaoni

Kutokana na taarifa ninazoandika katika blogu hii, na sehemu zingine, watu wengi wanafahamu kuwa nimechapisha vitabu vyangu mtandaoni. Nimeshawasaidia waandishi kadhaa wa mataifa mbali mbali kuchapisha vitabu vyao kwa mtindo huo. Kwa upande wa Tanzania, niliwahi kuongea na wanataaluma wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kuhusu suala hilo, na nilinukuliwa katika gazeti la Mwananchi.

Mara kwa mara, watu huniulizia kuhusu kuchapisha vitabu vyao. Napenda kuongelea tena suala hili, hasa matokeo ya kuchapisha vitabu mtandaoni. Kwanza, ni muhimu kufahamu kwamba kuna njia nyingi za kuchapisha vitabu mtandaoni. Ni juu ya mwandishi kuchagua. Binafsi, ninatumia njia ambayo ni rahisi kabisa, isiyo na gharama, au yenye gharama ndogo kiasi kwamba haiwi kizuizi kwangu.

Kuchapisha kwa namna hii ni rahisi sana. Mbali ya kutokuwa na gharama, haichukui muda, ili mradi mswada umeshaandaliwa kama faili la kielektroniki. Kinachobaki ni kuuingiza mswada kwenye tovuti ya kuchapishia, na haichukui dakika kumi kumaliza shughuli hii na kitabu kikawa tayari kununuliwa na watu popote ulimwenguni.

Jambo moja linalovutia sana katika kuchapisha vitabu mtandaoni kwa namna nifanyavyo ni kwamba vitabu hupatikana bila kikomo. Vinahifadhiwa kama mafaili ya kielektroniki, na huchapishwa kama kitabu halisi pale tu mdau anapoagiza nakala. Akiagiza nakala moja, inachapishwa hiyo hiyo. Akiagiza mia au elfu ni hivyo hivyo. Hakuna udhia wa kutunza shehena ya vitabu ghalani na kungojea wateja, huku vikiwa katika hatari ya kuharibiwa na unyevu, mende, au panya.

Hata hivi, nimeona kuna matatizo. Kwanza kwa upande wa mnunuzi. Ni lazima awe na namna ya kununua mtandaoni. Kwa kawaida hii inamaanisha awe na "credit card" kama vile VISA na Mastercard. Jambo la pili ni bei. Nikiangalia vitabu vyangu, naona wazi kuwa kama vingechapishwa mahali kama Tanzania kwa mtindo wa jadi, vingekuwa na bei nafuu kuliko ilivyo sasa.

Lakini, kwa upande mwingine, kama kitabu kinachapishwa kama kitabu pepe, yaani "e-book," kinaweza kuuzwa kwa bei ndogo sana, kuliko bei ya kuchapisha kwa mtindo wa jadi. Mdau anatakiwa awe na kifaa cha kuhifadhia na kusomea kitabu pepe, yaani "e-reader" au "e-book reader," kama vile Kindle au Nook.

Pamoja na kuwepo kwa vitabu pepe na vifaa vya kuhifadhia na kusomea vitabu hivyo, imethibitika tena na tena kwamba wadau wengi bado wanavitaka vitabu vya jadi, yaani vya karatasi na majalada. Mazoea haya na mapenzi ya vitabu vya jadi yamejengeka na hayaonekani kutoweka mioyoni mwa wengi.

Tekinolojia ya kuchapisha vitabu mtandaoni inawaathiri wachapishaji wa jadi kwa namna mbali mbali. Kadiri siku zinavyopita, wengi wao wanaona faida ya kuchapisha vitabu mtandaoni. Tekinolojia hii mpya inawasukuma kwenda na wakati ili wasipoteze biashara katika mazingira ya ushindani na mabadiliko yasiyoisha.

Thursday, December 3, 2015

Kuhusu Kublogu

Nimekuwa mwanablogu tangu mwaka 2008. Ninaendesha blogu hii ya Hapa Kwetu na nyingine ya ki-Ingereza. Kublogu kuna mambo mengi. Kublogu kunanipa fursa ya kujieleza kwa uhuru. Hili ni jambo la msingi, kama alivyoelezea mwanablogu Christian Bwaya.

Lakini kublogu kuna matokeo yenye manufaa. Kumeniwezesha kuwafikia watu mbali mbali ambao wanatembelea blogu zangu. Siwezi kujua wanapata ujumbe gani katika maandishi yangu. Kama taaluma inayotufundisha, hili ni suala tata.

Ujumbe wa andiko ni zao la kazi anayofanya msomaji juu ya andiko. Na kwa kuwa wasomaji wana akili zinazotofautiana, na wana nidhamu na uzoefu tofauti wa kusoma, kila mmoja anaibuka na ujumbe tofauti, kwa kiwango kidogo au kikubwa.

Niliwahi kuelezea kwa nini ninablogu, lakini sidhani kama nilikuwa na majibu ya uhakika. Baadaye, katika kutafakari suala hili, nilifikia hatua ya kutamka kwamba ninablogu kwa ajili yangu mwenyewe. Labda huu ndio ukweli wa mambo.

Imani iliyojengeka katika jamii ni kuwa mwandishi anawaandikia wasomaji. Tumezoea kuona waandishi wakiulizwa wanamwandikia nani, nao wanaelezea walengwa wao. Jadi hii na imani hii imekosolewa kwa uhodari na Roland Barthes katika makala yake, "The Death of the Author."

Makala hii ya Barthes naona inaipa uzito hoja yangu kuwa ninapoblogu ninajiandikia mwenyewe. Sijui ni nani atasoma au anasoma ninachoandika. Kusema kwamba ninawaandikia wasomaji ni kama kuota ndoto. Ni kujiridhisha kwa jambo ambalo halina uhakika bali ni bahati nasibu. Nikisema ninajiandikia mwenyewe ninasema jambo la uhakika.

Wednesday, October 28, 2015

Maprofesa na Wajibu wa Kuandika

Profesa ni mtu aliyefikia kiwango cha juu cha ufanisi katika ufundishaji, utafiti, uandishi, na kutoa ushauri kwa jamii katika masuala mbali mbali yanayohusiana na utaalam wake. Siwezi kuongelea hapa vipengele vyote vya suala hili, kama vile vigezo vinavyotumika katika kupima ufanisi wa mhusika hadi kumfikisha kwenye hadhi ya uprofesa. Ninakumbushia tu suala la wajibu wa profesa wa kuandika.

Baadhi yetu wa-Tanzania tumeliwazia na kuliongelea suala hili kwa miaka mingi, kwa manufaa ya jamii, tukiliunganisha na masuala kama sera ya elimu, matatizo ya uchapishaji, na kukosekana kwa utamaduni wa kununua na kusoma vitabu.

Kilichonifanya nirejeshe mada hii leo ni kwamba nimejikumbusha tamko la Rais Kikwete, "Maprofesa Wananisikitisha," ambalo lilijadiliwa katika blogu yangu hii na blogu ya Profesa Matondo. Mambo yaliyosemwa katika majadiliano yale ni muhimu na yataendelea kuwa muhimu. Wajibu wa profesa wa kuandika, kama njia mojawapo ya kufundisha na kuchangia maendeleo ya taaluma ni jambo lililo wazi.

Hata hivi, kwa kuzingatia kuwa dunia inabadilika muda wote, kuna umuhimu wa kulitafakari suala hili kwa mtazamo unaozingatia mabadiliko haya. Fikra zilizokuwa sahihi miaka michache iliyopita, huenda zimepitwa na wakati. Wataalam katika nyanja mbali mbali, kama vile ujasiriamali, elimu, na biashara wanatufundisha kuwa mabadiliko yanatulazimisha kuwa wabunifu na wepesi wa kubadilisha fikra, mahusiano, mbinu na utendaji wetu. Ndio maana ni muhimu kusoma daima na kujielimisha kwa njia zingine.

Katika dunia ya utandawazi wa leo, ambamo tekinolojia mbali mbali zinastawi, zikiwemo tekinolojia za mawasiliano, tunawajibika kuwa na fikra mpya kuhusu usomaji, uchapishaji na uuzaji wa vitabu, na kadhalika. Shughuli nyingi sasa zinafanyika mtandaoni, ikiwemo ufundishaji, kama nilivyowahi kugusia katika blogu hii. Tunawajibika kufunguka akili na kuacha kujifungia katika hiki tunachokiita sera ya elimu ya Tanzania. Je, inawezekana kuandika kitabu chenye umuhimu kwa Tanzania lakini si kwa ulimwengu? Taaluma inaweza kufungiwa katika mipaka ya nchi? Kuna dhana katika ki-Ingereza tunayopaswa kuitafakari: "The local is global."

Naona ni jambo jema kuirejesha mada hii, tuendelee kuitafakari katika mazingira ya leo. Lakini, naona tusome kwanza mjadala uliofanyika katika blogu hii na blogu ya Profesa Matondo.

Tuesday, September 22, 2015

Nimenunua Kitabu cha Golding, "Lord of the Flies"

Zimepita siku nyingi kidogo tangu niandike ujumbe kuhusu vitabu nilivyonunua, au nilivyojipatia kwa namna nyingine. Viko vitabu kadhaa, hasa riwaya, ambavyo sikuvielezea.

Leo, baada ya kufundisha vipindi vyangu viwili, nilipita kwenye duka la vitabu la hapa chuoni. Niliangalia sehemu vinapouzwa vitabu kwa bei nafuu, nje ya duka, nikaona, kati ya vitabu vingi, kitabu cha William Golding, Lord of the Flies. Hapo hapo nilikumbuka miaka ya ujana wangu. Tulisoma kitabu hiki tulipokuwa kidatu tano Mkwawa High School, mjini Iringa. Huku nikikumbuka hayo yote, nilikinunua hima, ingawa nina hakika ninayo nakala nyingine niliyonunua zamani, ila itakuwa vigumu kuigundua ilipo katika utitiri wa vitabu vyangu.

Lord of the Flies ni riwaya niliyoipenda sana na ambayo ninaikumbuka sana. Ilinigusa kwa namna ya pekee kwa jinsi ilivyowachora wahusika, ambao ni watoto wa shule waliojikuta kwenye kisiwa peke yao baada ya ndege waliyokuwa wanasafiria kuanguka kisiwani humo na wao wakawa abiria pekee waliosalimika. Riwaya inaonyesha jinsi watoto hao, waliokulia katika jamii ya maadili na ustaarabu, walivyoanza kubadilika, wakawa wabaya na katili kupindukia.

Miaka ile, nilikuwa najikongoja katika uandishi wa hadithi fupi. Lord of the Flies ilinigusa kwa namna ya pekee, kwa ustadi wake wa kuelezea mazingira, ikachangia katika uandishi wa hadithi yangu, "A Girl in the Bus," ambayo ilichapishwa katika jarida la Busara. Hili lilikuwa ni jarida maarufu Afrika Mashariki, lililokuwa linachapishwa Nairobi.

Kuchapishwa kwa hadithi hii kulinipa furaha isiyoelezeka. Nilikuwa na mazoea ya kwenda katika maktaba ya mkoa Iringa, na daima nilikuwa napendezwa kuona jarida hili lenye hadithi yangu. Hata nilipoingia Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kusoma, mwaka 1973, nilikuwa najisikia raha kuliona jarida hili  katika maktaba.

Lord-Flies of the Flies ni riwaya iliyowagusa watu ulimwenguni. Wanadamu kwa ujumla tunaamini kuwa watoto wana silika ya wema na usafi wa moyo. Wanafalsafa kama Jean-Jacques Rousseau walichangia kujenga imani hiyo. Lakini William Golding, katika riwaya yake hii ameelezea jinsi watoto wanavyobadilika na kuwa wabaya. Ni hadithi iliyowashtua walimwengu kwa namna ilivyoihoji dhana ya kwamba watoto ni kama malaika.

Nikizingatia kuwa Lord of the Flies ni moja kati ya riwaya maarufu kabisa katika lugha ya ki-Ingereza, nitaisoma kwa furaha, nikikumbuka ilivyonigusa enzi za ujana wangu. Miaka ilivyopita, nimesoma hadithi na tamthilia mbali mbali ambazo zimeelezea dhamira hii ya watu waliopotelea kwenye kisiwa mbali na walimwengu. Mifano ni The Odyssey ya Homer, Robinson Crusoe ya Daniel Defoe, na mashairi kadhaa ya Derek Walcott, kama vile "The Castaway." Hata baadhi ya wanafalsafa wa mkondo wa "existentialism" wameongelea uwepo wetu hapa duniani kwa kuufananisha na upweke wa watu waliotupwa na kusahauliwa. Ni dhamira ambayo imekuwa na mashiko ya pekee katika fikra na hisia za wanadamu.

Monday, June 8, 2015

Nimerekebisha Kitabu Changu

Kwa zaidi ya wiki moja, nimekuwa nikikipitia kitabu changu cha Matengo Folktales kwa ajili ya kukiboresha. Rekebisho moja nililofanya ni kuongeza ukubwa wa herufi ili kitabu kisomeke kwa urahisi zaidi. Nilikuwa pia naangalia kama kuna kosa lolote katika uandishi wa maneno. Nimerekebisha dosari zilizoziona katika maneno yapata matano

Ingawa nimetumia masaa mengi katika shughuli hiyo, kwangu si kitu, nikifananisha na kazi niliyofanya kwa miaka yapata ishirini na tatu katika kukiandaa kitabu hiki, tangu kuzitafuta na kuzirekodi hadithi, kuziandika kwa kuzitafsiri kwa ki-Swahili, kuzitafsiri kwa ki-Ingereza, kuzichambua, kusoma nadharia mbali mbali ili kutajirisha uchambuzi, na kurekebisha tafsiri na uchambuzi tena na tena.

Bahati ni kwamba miaka ya sabini na kitu, nilianza pia kufundisha somo la fasihi simulizi ("Oral Literature") na nadharia ya fasihi (Theory of Literature") katika idara ya "Literature" ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Katika kufundisha nilijionea mwenyewe kuwa hapakuwa na kitabu nilichoona kinafaa kwa somo la fasihi simulizi kwa wanafunzi wa kiwango cha chuo kikuu. Kuna usemi kuwa kama kitabu unachosoma huridhiki nacho, andika hicho kitabu unachokitaka.

Hali hiyo ya kukosekana kitabu kilichofaa katika ufundishaji wangu ilinihamasisha kutafakari masuala niliyokuwa nakumbaba nayo katika kuandika kitabu changu. Nilipania kuwa kiwe kinafaa kwa kufundishia. Miaka ilipita, nami nikawa natafiti, natafakari, na kuandika kiasi nilivyoweza. Wakati huo huo, nilikuwa nahangaika kuziboresha tafsiri za hadithi katika muswada. Shughuli hii ilinifundisha mengi kuhusu tafsiri, kama nilivyogusia katika makala iliyochapishwa katika jarida la Metamorphoses.

Historia ya kitabu hiki ni ndefu, na labda nitaweza kuiandika kiasi fulani siku za usoni. Ninakumbuka, kwa mfano, kwamba nilipokuwa nasomea masomo ya juu katika Chuo Kikuu cha Wisconsin, 1980-86, nilichukua somo la nadharia ya fasihi katika idara ya "Comparative Literature" lililofundishwa na Professor Keith Cohen. Kati ya nadharia tulizojifunza ni "Structuralism." Professor Cohen alitupa "homework" ya kuchambua hadithi yoyote kwa kutumia nadharia ya "Structuralism."

Nilitumia fursa hii kuichambua hadithi ya "The Tale of Two Women," ambayo imo katika Matengo Folktales. Mtu anayefahamu angalau kidogo nadharia ya "Structuralism" ataona athari zake, japo kidogo,  katika uchambuzi wangu.

Baada ya harakati za aina aina kwa miaka mingi, nilichapisha kitabu hiki mwaka 1999. Ndoto yangu ya kuandika kitabu cha kutumiwa katika ufundishaji wangu Chuo Kikuu cha Dar es Salaam haikutimia nilivyotarajia. Niliondoka Tanzania mwaka 1991, nikaja kufundisha katika idara ya ki-Ingereza Chuoni St. Olaf, huku  nikiwa bado naufanyia kazi mswada wangu. Kwa hivi kitabu kilichapishwa huku Marekani, na wanaokisoma ni wa-Marekani, kuanzia katika jamii hadi vyuoni, kama nilivyoelezea hapa na  hapa.

Masimulizi ni mengi, na kama nilivyogusia, labda nitafute wasaa miaka ijayo niandike kumbukumbu zangu za historia ya kitabu hiki.

Wednesday, June 3, 2015

Nadharia ya Uandishi

Uandishi ni nini? Je, kila uandishi ni uandishi wa kweli? Uandishi wa kweli ni nini? Naona haya ni masuali ya msingi. Ningependa tuyatafakari. Waandishi wengi maarufu wameandika kuhusu masuala hayo. Katika kitabu chake, Letters to a Young Novelist, Mario Vargas Llosa, mwandishi maarufu kutoka Peru, aliandika:

The defining characteristic of the literary vocation may be that those who possess it experience the exercise of their craft as its own best reward, much superior to anything they might gain from the fruits of their labors. That is one thing I am sure of amid my many uncertainties regarding the literary vocation: deep inside, a writer feels that writing is the best thing that ever happened to him, or could ever happen to him, because as far as he is concerned, writing is the best possible way of life, never mind the social, political, or financial rewards of what he might achieve through it.

Nitafsiri kwa ki-Swahili:

Utambulisho mahsusi wa wito wa uandishi labda ni kwamba wale wenye wito huo huutambua uandishi kama tunu kubwa kuliko zote, bora kuliko chochote wanachoweza kukipata kutokana na juhudi yao. Hiki ni kitu kimoja ambacho nina uhakika nacho ingawa nimezingirwa na masuali yaletayo wasiwasi kuhusu wito wa uandishi: ndani ya nafsi yake, mwandishi hujisikia kuwa uandishi ni kitu bora kabisa kumtokea au kinachoweza kumtokea, kwa sababu kwa mtazamo wake, uandishi ni mkondo bora kabisa wa maisha, bila kujali manufaa ya kijamii, kisiasa, au kifedha anayoweza kuyapata kwa uandishi.

Kama ilivyo tafsiri yoyote, tafsiri yangu hainasi kila kipengele cha ujumbe wa mwandishi, hasa tukizingatia kuwa tafsiri yangu ni tafsiri ya tafsiri, kwani Mario Vargas Llosa aliandika kwa ki-Hispania. Hata hivi naamini kuna mambo muhimu yanayojitokeza. Mfano ni msisitizo kuwa uandishi kwa wenyewe ni tunu ya thamani kuliko zote. Ni kama kusema kuwa uandishi wa kweli ni ule unaomletea mwandishi faraja kamili na kumfanya asijali matokeo mengine ya uandishi wake, kama vile sifa na fedha.

Nilipokinunua kitabu hiki cha Mario Vargas Llosa, miaka michache iliyopita, nilianza kukisoma nikakutana na dhana fulani ambazo nilishakutana nazo katika maandishi ya Shaaban Robert. Waandishi maarufu wa lugha yoyote ni watu wenye utajiri wa fikra. Hili ni fundisho kwa waandishi chipukizi.

Wakati huu ninaposoma Letters to a Young Novelist, ninasoma pia The Naïve and the Sentimental Novelist, kitabu cha Orhan Pamuk, ambacho nilikinunua hivi karibuni. Orhan Pamuk ni mwandishi maarufu wa U-Turuki, ambaye alipata tuzo ya Nobel. Kitabu chake hiki nacho kinaelezea mtazamo wake kuhusu uandishi. Niliwahi kumtaja mwandishi huyu katika blogu hii, katika kulalamika kuwa maisha hayaturuhusu kusoma vitabu vyote muhimu.

Sunday, February 1, 2015

Uandishi ni Kazi ya Upweke

Waandishi kadhaa maarufu wametamka kuwa uandishi ni kazi ya upweke. Mmoja wa waandishi hao ni Ernest Hemingway, ambaye picha yake inaonekana hapa kushoto.

Katika hotuba yake ya kupokea tuzo ya Nobel, alisema:

Writing, at its best, is a lonely life. Organizations for writers palliate the writer's loneliness but I doubt if they improve his writing. He grows in public stature as he sheds his loneliness and often his work deteriorates.

Najaribu kuitafsiri kauli hii:

Uandishi, katika hali yake bora kabisa, ni maisha ya upweke. Vyama vya waandishi hupunguza upweke wa mwandishi lakini sidhani kama vinaboresha uandishi wake. Hadhi yake katika jamii hukua kwa kadiri anavyoupunguza upweke wake na aghalabu ubora wa kazi yake hudorora.

Hemingway alilitafakari na kuliongelea sana suala la uandishi. Alifanya hivyo katika riwaya, insha na barua zake na pia katika mahojiano na maongezi mengine. Nami ninajifunza mengi kutoka kwake.

Katika makala yangu ya juzi nilitamka kwamba ninapoandika katika blogu yangu hii, ninajiandikia mwenyewe. Sijui na sijali kama kuna atakayesoma ninachoandika. Lengo langu la msingi ni kutimiza haja yangu ya kuutua mzigo uliokuwepo mawazoni mwangu.

Ni wazi kuwa fikra yangu hii inahusiana na yale ninayojifunza kutoka kwa Hemingway. Siko tayari kusukumwa na imani kwamba ninaiandikia jamii. Ningependa kuzingatia kauli ya Hemingway kwamba, "Writing, at its best, is a lonely life."

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...