Wednesday, January 28, 2015

Katika Blogu, Sijui Ninamwandikia Nani Zaidi Yangu Mwenyewe

Je, mwandishi wa blogu anamwandikia nani? Kwa mtazamo wangu, hili ni suali gumu. Naliona gumu kulitafakari, achilia mbali kulijibu.

Baada ya kuona ugumu wa suali hili, nimeamua kukiri kuwa ninajiandikia mwenyewe. Ndio maana makala ninazoandika aghalabu zinanihusu mimi mwenyewe, shughuli zangu, matatizo na mafanikio yangu, mategemeo yangu na kumbukumbu zangu.

Sipendi sana kuwaongelea watu wengine, wala sipendi sana kuongelea mambo kinadharia, bila kujihusisha mwenyewe. Naweza kusema kuwa ndivyo nilivyoandika kitabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences. Sijajificha nyuma ya pazia la nadharia au taaluma. Nimejiweka wazi kwa namna nilivyoweza.

Mwandishi Ernest Hemingway aliongelea suala hili vizuri alipofafanua dhana ya ukweli katika uandishi. Nilivyomwelewa, anasema kuwa ukweli katika uandishi ni kwa mwandishi kuifungua na kuiweka bayana nafsi yake.

Ningependa sana niweze kuandika namna hii aliyoongelea Hemingway. Ni ndoto inayovutia, sawa na nyota inayong'aa mbali, ambayo mtu unaifuata kwa hamu ingawa haifikiki. Lakini, naona huku ndiko kujiandikia mwenyewe.

Kusema kuwa kuna hadhira ninayoiandikia katika blogu yangu ni kama kuota ndoto. Ni kujidanganya. Nasema hivi sio tu kutokana na tafakari yangu mwenyewe, bali ninakumbuka makala ya kufikirisha ya Walter J. Ong, "The Writer's Audience is Always a Fiction."

(Picha hapo juu nilijipiga mwenyewe jana, kwa ajili ya matangazo ya mihadhara yangu Mankato)

2 comments:

emu-three said...

Ni kweli mkuu, wenye blog hasa za hadithi na mambo muhimu ynye kuelimisha,wanalifahamu hilo....lkn kizuri hakiozi, lkn ipo siku mkuu...kwani ndoto hazikeshi

Mbele said...

Ndugu emu-three,

Shukrani kwa kusoma ujumbe wangu na kuandika maoni. Napenda kukaribisha maoni yoyote, kwa vile suala lenyewe naliona kuwa tata, na wahenga walisema penye wengi haliharibiki neno.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...