Kwa siku kadhaa sasa, nimekuwa nikisoma Leading Beyond the Walls: How High-Performing Organizations Collaborate for Shared Success, kitabu kilichohaririwa na Frances Hesselbein, Marshall Goldsmith, na Iain Somerville. Ni mkusanyo wa makala 23 zilizoandikwa na wataalam mbali mbali katika tasnia ya uongozi, wakizingatia hali halisi ya utandawazi wa leo, na umuhimu wa kwenda na wakati.
Kwenda na wakati kunahitaji wepesi wa kubadilika kifikra, kimwenendo, kimfumo na hali zingine, ili kumudu mahitaji na hali halisi ya mabadiliko yanayotokea ulimwenguni, ambayo hayakwepeki. Mafanikio ya shirika, taasisi, au kampuni
yanategemea utayari wa kujibadili. Mazoea ni kipingamizi kikubwa cha mafanikio; ni kama kuta ambazo tumejizungushia. Jukumu letu, ambalo halikwepeki, ni kuvunja hizo kuta, tuwe na uwanja na upeo usio na mipaka.
Wengi wa watunzi wa makala zilizomo kitabuni humu nilikuwa sijawahi hata kuwasikia, isipokuwa Joseph S. Nye, Jr., Stephen R. Covey, na Peter F. Drucker, ambaye niliwahi kusoma andiko lake mojawapo. Kati ya makala ambazo nilivutiwa nazo hata kabla ya kuzisoma ni "And the Walls Came Tumbling Down" (Jim Collins), "Dissolving Boundaries in the Era of Knowledge and Custom Work" (Sally Helgesen), "Culture is the Key" (Regina Herzlinger, "New Competencies for Tomorrow's Global Leader" (Marshall Goldsmith, Cathy Walt), na "Creating Success for Others" (Jim Belasco).
Kila makala ambayo nimesoma katika kitabu hiki imenipanua mawazo. Nimegundua mambo ya maana ambayo yataboresha mihadhara ninayotoa kwa jumuia, taasisi na makampuni. Nawazia, kwa mfano, mihadhara niliyotoa kwenye kampuni ya RBC Wealth Management.
Ninashukuru kuwa nilinunua kitabu hiki, ingawa sikumbuki ilikuwa lini. Nina ari kubwa ya kumaliza kusoma insha zote zilizomo, na nina hakika kuwa, Mungu akinijalia uzima, nitazisoma tena na tena.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault
Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...
-
Leo ni kumbukumbu ya siku ya kuzaliwa kwangu, ambayo ni tarehe 17 Agosti, 1951. Familia yangu, ndugu, na marafiki wamejumuika nami kushereh...
-
Leo napenda kukitambulisha kwako mdau kitabu muhimu cha ki-Swahili, Tenzi Tatu za Kale . Nilinunua nakala yangu miaka kadhaa iliyopita katik...
-
Kutafsiri kazi ya fasihi ni kazi ngumu ya kuchemsha bongo. Inahitaji ufahamu wa hali ya juu wa lugha husika, na pia hisia makini za kifasih...
No comments:
Post a Comment