Thursday, August 28, 2014

Marekani Hata Wazee Wananunua na Wanasoma Vitabu

Kama nilivyoandika katika blogu hii, nilishiriki tamasha la tamaduni za kimataifa lililofanyika mjini Faribault tarehe 23 mwezi huu. Kati ya mambo niliyoelezea ni shughuli niliyofanya ya kusaini vitabu, na kati ya picha nilizoweka, ni hiyo inayoonekana hapa kushoto, ambayo inamwonesha mama mmoja mzee niliyekuwa namsainia nakala ya Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, aliyokuwa ameinunua hapo hapo.

Sijui kama jambo hili linaweza kutokea mahali kama Tanzania. Kule watu wanachojua ni kuwa vitabu ni kitu kinachowahusu wanafunzi, labda kiwe kitabu cha hadithi, hasa hadithi za kusisimua na za mapenzi. Vitabu vya maarifa ya aina yoyote vinachukuliwa kuwa ni kwa ajili ya wanafunzi, na hao wanafunzi wanatafuta vitabu vinavyotumika mashuleni.

Hapa Marekani, hali ni tofauti. Hata wazee hununua na husoma vitabu. Ukienda kwenye maduka ya vitabu, utawaona. Kwenye matamasha ya vitabu, utawaona. Nenda maktabani, utawaona.

Nasema hayo kutokana na uzoefu wangu. Nisiende mbali. Hapo hapo Faribault nimeshiriki matamasha, mwaka hadi mwaka, na baadhi ya watu waliofika kwenye meza yangu na kununua vitabu ni wazee.

Tarehe 11 Oktoba, kutakuwepo na maonesho makubwa ya vitabu mjini St. Paul. Nimeshiriki maonesho hayo mwaka hadi mwaka, na nimewaona wazee, sambamba na watu wazima, vijana, na watoto. Nina uhakika kuwa hiyo tarehe 11 Oktoba, wazee watakuwepo.

Kuna mambo ya kujifunza hapo. Jambo moja ni lile alilotufundisha Mwalimu Nyerere, kuwa elimu haina mwisho. Lakini, kwa ujumbe kama huu, sitegemei kuwa jamii yetu ya Tanzania itashtuka au kubadilika hima. Hali ni mbaya sana. Itachukua miaka mingi kutokea mabadiliko, ambayo yatabidi yaendane na malezi tofauti kwa watoto wetu. Itabidi wazazi kujijengea utamaduni wa kununua vitabu, kuvisoma, na kuwasomea watoto wao wanapokuwa wadogo kabisa, na kuwakuza katika utamaduni huo, ili hata watakapokuwa wazee, wawe na hamasa ya kununua na kusoma vitabu.

Tuesday, August 26, 2014

Tamasha la Tamaduni Faribault, Minnesota, Agosti 23Tamasha la tamaduni za kimataifa lilifanyika mjini Faribault tarehe 23 mwezi huu, kama ilivyopangwa. Nilihudhuria. Kati ya mambo yaliyonivutia ni bendera za nchi mbali mbali. Mwanzoni bendera hizi zilikuwa kwenye jukwaa kuu. Washiriki wa tamasha ambao nchi zao ziliwakilishwa na bendera hizi walikuja kwenye jukwaa kuu, wakasema machache kuhusu bendera hizi na nchi zao.Baada ya hapo, waliandamana katika mstari mmoja wakiwa na bendera zao, kisha bendera zilisimikwa uwanjani, ambapo zilipepea muda wote wa tamasha.

Kama nilivyosema katika blog hii, kabla ya siku ya tamasha, sikuwa na bendera ya Tanzania. Kwa hivi, sikushiriki shughuli hii ya bendera.
Yalikuwepo mabanda mengi ambamo vitu mbali mbali vilikuwa vinauzwa, kama vile vyakula, maji ya kunywa, soda, nguo, vipodozi na vitu kadha wa kadha vya urembo.

Vilikuwepo pia vikundi vya burudani, vikiwakilisha tamaduni mbali mbali.


Nilipata fursa ya kukutana na kuongea na watu ambao hatukuwa tunafahamiana kabla. Hapa kushoto, naonekana na mama kutoka Ireland, ambaye yuko kulia kabisa, akifuatiwa na bwana mmoja kutoka Somalia, na huyu mama mwenye nguo nyeusi ni m-Marekani. Tulipiga picha hii baada ya wote watatu kununua vitabu vyangu.


Akina mama wanaoonekana pichani hapo juu wako tena hapa kushoto, na bwana mmoja kutoka Nigeria. Tuliongea sana kuhusu masuala ya tofauti za tamaduni, na mazungumzo yalikuwa ya kufikirisha na kutajirisha akili, hasa ukizingatia kuwa tulikuwa watu wa kutoka nchi mbali mbali kabisa.

Hapa naonekana na msichana mmoja kutoka Sudan. Aliniambia kuwa ananifahamu tangu miaka kadhaa iliyopita, alipokuwa mdogo.

Baadhi ya watu wanaonunua vitabu huomba kusainiwa vitabu hivyo. Shughuli hii ina maana ya pekee kwa mteja na mwandishi pia, kama tunavyojaribu kuelezea katika maongezi baina ya mwanablogu na msomaji makini wa vitabu Christian Bwaya na mimi.Na kama inavyotokea tena na tena, kuna wateja ambao, baada ya kununua kitabu au vitabu, hupenda kupiga picha na mwandishi. Bahati mbaya ni kuwa huyu dada hapa kushoto hakuniachia anwani. Ningependa kumpelekea picha hii, kwa kumbukumbu.

Friday, August 22, 2014

Kesho Naenda Faribault, Kwenye Tamasha la Tamaduni

Kesho asubuhi naenda mjini Faribault, kushiriki katika tamasha la tamaduni za kimataifa. Nimeshajiandaa. Vitabu vyangu na machapisho mengine nimeshafungasha. Meza nimeshatayarishiwa. Nitailipia kesho hiyo hiyo.

Kitakachokosekana in bendera ya Tanzania, kama nilivyosema katika ujumbe wangu wa tarehe 19 Agosti. Wakati wengine watakapokuwa wanapeperusha bendera za nchi zao na kusema machache kuhusu bendera na nchi hizo, mimi nitabaki naangalia tu.

Wakati wa tamasha, nitakuwa napeperusha picha na taarifa kwenye mtandao wa "twitter," Insh' Allah.

Tuesday, August 19, 2014

Laiti Ningekuwa na Bendera ya Tanzania

Jana nimeona taarifa mtandaoni kuwa Jumamosi hii, tarehe 23, mjini Faribault, Minnesota, kutakuwepo na tamasha la kimataifa la tamaduni. Hapo hapo nilipiga simu kwa waandaaji, ili kuona kama bado kuna nafasi ya mimi kushiriki.

Leo mratibu mkuu wa tamasha, amenipigia simu. Tumeongea kwa muda, nami nikamwulizia kama bado kuna nafasi ya kushiriki katika tamasha. Hapo hapo aliniambia kuwa nafasi bado iko, na kwamba tukimaliza maongezi atanitumia fomu ya kujisajili.

Tuliongelea shughuli nifanyazo katika jamii, ikiwemo kushiriki matamasha ya aina hii kama mwandishi na mwelimishaji, hasa kuhusu masuala ya tofauti za tamaduni na athari zake. Tuligusia pia ushiriki wangu katika masuala ya Faribault, kama ilivyotamkwa katika taarifa hii hapa.

Wakati tunaendelea na mazungumzo, aliniuliza kama nina bendera ya nchi yangu, yaani Tanzania. Alifafanua kwamba kwenye jukwaa kuu, zitakuwepo bendera za nchi wanakotoka washiriki wa tamasha, na kuna kipindi ambapo wawakilishi wa nchi hizo watakuwepo jukwaani wakiwa na bendera zao. Watapata dakika kadhaa za kuongelea mbele ya kadamnasi kuhusu nchi zao na hizo bendera. Hapo nilijisikia vibaya, kwani sina bendera ya Tanzania ya ukubwa utakiwao, ambao ni angalau futi  tatu kwa tano. Nilikiri kuwa sina, ila nikasema nitajitahidi katika siku hizi mbili tatu kutafuta.

Baada ya maongezi, nimeangalia mtandaoni nione wapi naweza kuipata bendera ya aina hiyo. Nimeona sehemu kadhaa, ambapo naweza kuagiza bendera hiyo. Nimepiga simu sehemu tatu, nikaambiwa kuwa hatawezekana kuipata kabla ya tamasha.

Kwa maana hiyo, nimekwama. Nimekosa fursa ya kuelezea habari za Tanzania na bendera yetu, mbele ya wote watakaohudhuria tamasha. Nimejifunza. Niko mbioni kuagiza bendera, niweze kuitumia siku za usoni.

Mji wa Faribault uko umbali wa maili kama 25 tu kutoka hapa ninapoishi. Nami si mgeni katika mji ule, kwani, kwa miaka iliyopita, nimeshafanya shughuli nyingi za jamii katika mji ule, kama ilivyoelezwa hapa, hapa, na hapa.

Lakini, pamoja na yote, hili suala la kutokuwa na bendera limenikera na papo hapo limenigutua. Mimi kama m-Tanzania, tena sio m-Tanzania wa uraia pacha, ningejisikia vizuri sana kuwepo kwenye jukwaa kuu na bendera yangu, nikasema mawili matatu kuhusu nchi yangu na bendera yake. Dosari hii ni lazima irekebishwe hima.

Saturday, August 16, 2014

Tenzi Tatu za Kale

Leo napenda kukitambulisha kwako mdau kitabu muhimu cha ki-Swahili, Tenzi Tatu za Kale. Nilinunua nakala yangu miaka kadhaa iliyopita katika duka la vitabu la Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Kitabu hiki ni mkusanyo wa tenzi tatu za kale maarufu: Fumo Liyongo, uliotungwa na Muhamadi Kijumwa; Al Inkishafi, uliotungwa na Sayyid Abdalla bin Ali; na Mwanakupona, uliotungwa na Mwana Kupona binti Mshamu. Kitabu kimehaririwa na M.M. Mulokozi, profesa mstaafu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Kilichapishwa na Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili mwaka 1999.

Hizi ni kati ya tenzi maarufu kabisa katika ki-Swahili. Kwa msingi wa sanaa na maudhui, tenzi hizi zina hadhi kamili ya kuwemo katika orodha ambayo kwa ki-Ingereza huitwa "classics."

Fumo Liyongo ni hadithi inayomhusu shujaa Fumo Liongo, ambaye mimi, kutokana na utafiti wangu wa miaka mingi, napendelea kumwita Liongo Fumo. Huyu ni shujaa wa kale, labda miaka elfu moja iliyopita, na ndiye anayesifika kuliko wote tangu zamani katika jamii ya wa-Swahili.

Alikuwa pandikizi la mtu, mwenye vipaji kadhaa: kuwashinda maadui, shabaha katika kutumia upinde na mshale, ufundi wa kutunga nyimbo na mashairi. Juu ya yote, alikuwa muungwana sana, mfano wa kuigwa. Lakini alifanyiwa visa na ndugu yake ambaye alikuwa mfalme, hadi hatimaye akauawa na kijana mdogo, ambaye alikuwa mpwa wake.

Al Inkishafi ni utenzi wa tafakuri na falsafa kuhusu maisha, ambao umejikita katika kuuliza maana ya maisha ni nini. Mtunzi alilishughulikia suali hili kwa kuzingatia jinsi ustawi na utukufu wa wa-Swahili, hasa wa mji wa Pate, ulivyoanguka. Pate ulikuwa mji maarufu, wenye hadhi na mali, lakini kutokana na masaibu mbali mbali, ullipoteza hadhi hiyo na kuishia kuwa magofu.

Hii dhamira imeshughulikiwa tangu zamani na waandishi wengi wa pande za Arabuni, Uajemi, Ulaya na sehemu zingine duniani. Wanafalsafa pia wamehoji maana ya maisha, hasa wanafalsafa wa mkondo wa "existentialism."

Mwana Kupona ni utenzi uliotungwa na mama kumuusia binti yake kuhusu maisha ya ndoa, wajibu wake katika maisha hayo, na wajibu wake kwa watu kwa ujumla. Huu ni utenzi maarufu sana, ambao ni chimbuko la tungo za waandishi wengine, kama vile Shaaban Robert.

Mhariri amefanya kazi nzuri ya kuweka maelezo juu ya historia ya tenzi hizi, kuhusu watunzi, na kuhusu tafiti zilizofanywa juu ya tenzi hizi. Ametoa orodha ya maandishi ya wataalam mbali mbali, kumwezesha msomaji kufuatilia zaidi masuala hayo.

Kwa bahati nzuri, katika utafiti niliofanya kwa miaka mingi kuhusu tungo za kale za ki-Swahili, nimezitafiti tenzi hizi tatu, hasa Utenzi wa Fumo Liongo, ambao nimeutafiti kwa kina na kujipatia umaarufu kama mtafiti anayeongoza katika utafiti wa utenzi huu na masimulizi husika.

Watafiti bado wana majukumu makubwa ya kutafiti tenzi hizi na tenzi zingine. Kazi moja muhimu inayohitaji kufanyiwa bidii sana ni kuangalia miswada mbali mbali ya kila utenzi. Inahitajika juhudi na umakini kuangalia maneno yaliyotumika katika miswada hiyo, sentensi na lahaja, na kubaini tofauti zinazojitokeza.

Kuna tofauti za kila aina baina ya mswada na mswada, na ni juu ya watafiti kuzitambua na kuzitolea maelezo. Miswada ya tenzi zote za zamani za ki-Swahili inatofautiana katika vipengele mbali mbali.

Jukumu jingine ni kuzunguka katika maeneo ya wa-Swahili, kama vile mwambao wa Kenya, ambako nilifanya utafiti miaka ya 1989 hadi 1991. Huko nilikutana na mabingwa wa lugha na tungo za ki-Swahili, kama vile Mzee Ahmed Sheikh Nabhani wa Mombasa, na wazee wengine wa miji kama Witu na Lamu. Ni muhimu watafiti waende Pate, Siu, na kadhalika. Pia tunahitaji kufanya utafiti zaidi katika hifadhi za miswada ya ki-Swahili iliyopo katika maktaba ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Chuo Kikuu cha London, Berlin, na sehemu zingine.

Tenzi Tatu za Kale ni hazina kubwa kwa wasomaji wa kawaida, watafiti, na wanafunzi, hadi kiwango cha chuo kikuu. Kwa bahati nzuri kitabu hiki kinapatikana kirahisi Tanzania. Ninakipendekeza kwa yeyote anayetaka kujiongezea ufahamu wa lugha na fasihi ya ki-Swahili.

Thursday, August 14, 2014

Nimezawadiwa Kitabu: "Picturing Hemingway's Michigan"

Leo nimepata zawadi ya kitabu, Picturing Hemingway's Michigan kilichotungwa na Michael R. Federspiel. Kinahusu sehemu ya kaskazini ya jimbo la Michigan, ambapo familia ya Ernest Hemingway ilikuwa inakwenda kwa mapumziko.

Kitabu kina picha na maelezo kuhusu sehemu hiyo, ambapo Hemingway alitembelea tena na tena wakati wa utoto na ujana wake. Hapa ni chimbuko la matukio ya riwaya ya mwanzo ya Hemingway, The Torrents of Spring na hadithi zake ziitwazo Nick Adams Stories.Nimeletewa kitabu hiki na Bwana David Cooper wa Ohio na mwanae Clay ambaye ni mwanafunzi wangu aliyekuja Tanzania mwezi Januari, 2013 katika kozi yangu ya "Hemingway in East Africa."

Baba huyu ndiye aliyetupeleka Montana kwa ndege yake mwaka jana, kuonana na Mzee Patrick Hemingway. Hapa kushoto ni picha tuliyopiga mjini Lakeville, Minnesota, kabla ya kuruka kwenda Montana. Bwana Cooper anaonekana kulia kabisa, halafu anafuata mwanae, halafu mwanafunzi wangu mwingine aliyekuwemo katika kozi ya "Hemingway in East Africa," na mimi naonekana kushoto kabisa.


Mwanafunzi aliyeniletea kitabu anaonekana nami pichani hapa kushoto, tukiwa kwenye mpaka baina ya hifadhi za Ngorongoro na Serengeti.

Nilipokipata kitabu hiki, yapata saa saba mchana, nilijawa na furaha, nikaanza kukisoma mara, lakini nikaona nipige kwanza simu kwa walioniletea. Nilimpata Bwana Cooper, nikamshukuru sana. Ameniambia kuwa yeye na mwanae walikiona kitabu hiki katika duka kule sehemu ya Michigan Kaskazini, wakaniwazia. Baada ya maongezi nimeendelea kukisoma, nikamaliza baada ya masaa mawili hivi..

Wameninunulia nakala yenye sahihi ya mwandishi, kama inavyoonekana hapa kushoto. (Ninaposema hivi, mawazo yangu yameshakwenda kwenye mazungumzo baina yangu na Ndugu Christian Bwaya kuhusu suala hili la kusainiwa vitabu).

Nilifahamu kuwa sehemu hii ya Michigan Kaskazini ni muhimu katika utoto na ujana wa Hemingway, lakini kitabu hiki kimenifungua macho zaidi kwa kuonyesha sehemu mbali kwa picha na maelezo. Picha nyingi ni za mtoto Hemingway na watoto wengine katika familia yao, picha za wanaukoo, na sehemu mbali mbali. Nyingi katika ya picha hizo sikuwa nimeziona kabla. Kwa yote hayo, nimefurahi sana.

Tuesday, August 12, 2014

Nimemaliza Kusoma "The Pearl," Kitabu cha John Steinbeck

Leo asubuhi, nimemaliza kusoma The Pearl, kitabu cha John Steinbeck. Kitabu hiki kimeyagubika mawazo yangu siku nzima. Nilipomaliza kukisoma, nilibaki nimeduwaa, wala sikuweza kuandika ujumbe katika blogu yangu, ingawa nilitamani kufanya hivyo. Ni jioni hii, saa moja na kitu, ndipo nimeweza kuanza kuandika ujumbe huu.

Nirudi nyuma kidogo. Wiki kadhaa zilizopita, kitabu hiki nilikitaja katika blogu hii kuwa kimoja kati ya vitabu nilivyokuwa navisoma kwa mpigo. Sikuwa na haraka, bali niliamua mwenyewe muda gani nisome, na katika kusoma, niliamua mwenyewe niishie wapi, siku hadi siku. Mtindo huu naendelea nao kwa vitabu vingine.

Haiwezekani kuelezea nilivyojisikia wakati nasoma The Pearl. Ni kama kumwelezea mtu ambaye hajawahi kuumwa na jino au kula embe, jinsi jino linavyouma, au utamu wa embe. Hata hivi, naona nigusie tu kuhusu kitabu hiki,

Ni hadithi yenye mvuto wa pekee. Inasisimua, inasikitisha, na inatisha pia. Ni hadithi iliyoniteka, kama vile ndoto ya ajabu au jinamizi. Kisa chenyewe kinamhusu Kino, mvuvi anayebahatika kuokota lulu baharini, lulu kubwa, ya thamani isiyoelezeka. Jamii yake yote inapata habari hima, kuanzia walalahoi ambao ni majirani zake, mabepari wachuuzi wa lulu, padri, daktari, omba omba, kila mtu. Habari ya lulu hii inawasisimua wote hao kwa namna tofauti, wengi kwa wivu na tama ya kumwibia maskini mvuvi huyu. Kwa kutumia habari ya hii lulu, Steinbeck amefanikiwa kuanika tabia na hisia za binadamu.

Kino mwenyewe anajawa na ndoto za kuiwezesha familia yake kuondokana na maisha duni na kumpa fursa mtoto wake mdogo ya kusoma. Lakini pole pole, wasi wasi unaanza kumnyemelea Kino, na hofu pia, kuhusu usalama wa lulu yake na hata maisha yake, hasa pale watu wasiofahamika wanapomnyemelea usiku.

Hapo hadithi inaanza kutisha. Steinbeck ni mbunifu wa kiwango cha juu sana. Hadithi inaendelea hadi mwishoni Kino, mkewe, na mtoto wao wanahama mji usiku, kuinusuru lulu na maisha pia. Ajabu juu ya ajabu, baada ya kutembea kwa mwendo wa mbali usiku, na hatimaye kujificha porini, asubuhi Kino anawaona watu watatu wakija pole pole katika barabara ile ile aliyopitia. Ni wapelelezi makini, ambao wanaweza kutambua hata njia aliyopita mnyama kwenye miamba, ambako alama za nyayo hazionekani kwa binadamu wa kawaida.

Hapo nilijikuta nimeelemewa na hofu, ambayo iliongezeka kadiri nilivyoendelea kusoma kisa hiki. Naona nisiendelee, bali niseme tu kuwa hadithi inapoisha, watu kadhaa wamepoteza maisha, akiwemo mtoto wa Kino, na kwa jinsi lulu ilivyoandamana na mikosi, Kino na mkewe wanaenda ufukweni na kuitupilia mbali baharini.

Nina hakika nilikifahamu kitabu hiki tangu nilipokuwa nasoma sekondari, Seminari ya Likonde. Nilipomaliza kukisoma kitabu hiki, wazo moja kubwa lililokuwa akilini mwangu ni kuwa mara nitakapopata wasaa, nisome The Grapes of Wrath, kitabu kingine maarufu cha Steinbeck, ambacho nimetamani kukisoma kwa miaka mingi. Nimemaliza kusoma The Pearl nikiwa na masononeko, nikiwafikiria wa-Tanzania ambao hawajui ki-Ingereza, na mengi ya thamani yanawapitia mbali. Bado nimesononeka.

Monday, August 4, 2014

Furaha ya Kusainiwa Kitabu

Wapenzi wa vitabu wakishajipatia nakala ya kitabu cha mwandishi fulani, huguswa pale mwandishi anaposaini kitabu hicho. Aghalabu mwandishi huandika ujumbe mfupi kwa mteja huyu na kasha kuweka sahihi. Ni jambo linalowagusa sana wasomaji. Mimi mwenyewe, kama mwandishi, nimeshasaini vitabu vyangu vingi. Ninazo baadhi ya picha za matukio haya kutoka miaka iliyopita.

Msomaji makini na mwanablogu Christian Bwaya hivi karibuni ameelezea vizuri katika blogu yake, hisia zake baada ya kujipatia kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differencesambacho nilikuwa nimekisaini:

Namshukuru kwa dhati mwandishi wa kitabu hiki, Prof. Mbele kwa kunitumia kitabu hiki bila malipo, tena kwa gharama zake. Si jambo linalowatokea wengi. Ni furaha iliyoje hatimaye nimekipokea leo asubuhi. Naanza kukisoma kitabu hiki kwa mara nyingine, safari hii kikiwa na saini ya mwandishi. Ni upendeleo na muujiza wa pekee kunitokea katika siku za hivi karibuni. Ni lazima nimshukuru kwa dhati. Asante sana Profesa.

Utamaduni wa kusaini na kusainiwa vitabu nimeuzoea. Hata juzi tarehe 2 Agosti, niliposhiriki tamasha la Afrifest kule Brooklyn Park, Minnesota, nikiwa na vitabu vyangu, wadau kadhaa walionunua vitabu vyangu waliomba kusainiwa.

Hapa kushoto anaonekana mdau akiniangalia wakati nasaini nakala ya Matengo Folktales, ambayo alikuwa amenunua hapo.
Baada ya kusainiwa nakala yake, aliona furaha ya ziada kupiga picha nami huku akiwa ameshika kitabu hicho. Hiyo nayo ni kawaida hapa Marekani; wadau wakishanunua kitabu na kusainiwa, wanapenda kupiga picha na mwandishi, ikiwezekana.

Mdau huyu, aitwaye Adrian, m-Marekani Mweusi, alinifahamu tangu miaka kadhaa iliyopita. Alikuwa anasoma katika chuo fulani mjini Minneapolis. Kulikuwa na mkutano wa kitaaluma, nami nilikuwa mmoja wa wanajopo, nikitoa mada. Adrian alivutiwa sana. Halafu, alinisikiliza tena mwaka jana, nilipokuwa naongea katika jopo la watu wawili, nikiwa na Profesa Mahmud el-Khati, m-Marekani Mweusi, tukiongelea mbele ya umati, mahusiano baina ya wa-Afrika na wa-Marekani Weusi.

Adrian ni msomi kijana makini. Tayari naona nyota yake imeanza kung'ara katika medani ya uongozi katika jamii. Nina imani atafika mbali katika jamii ya wa-Marekani weusi na Marekani kwa ujumla.
Hapa kushoto ni picha nyingine, kutoka hiyo hiyo juzi katika tamasha la Afrifest, nikiwa na mdau kutoka Liberia, ambaye alikuwa amenunua kitabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, nami nikiwa nimekisaini. Inaonekana aliguswa sana, na hakuweza kujizuia kuniwekea mkono wake begani pangu.

Suala hili la kusaini au kusainiwa vitabu linastahili  kutafakariwa. Naamini lina vipengele kadhaa muhimu, kama vile kiutamaduni, kisoshiolojia, kisaikolojia, na kifalsafa. hata katika maduka ya vitabu hapa Marekani, aghalabu utaona vimepangwa vitabu vya mwandishi vikiwa na ujumbe "Signed copy." Jambo hili linaisukuma akili yangu kutaka kulielewa zaidi. Ningependa kujifunza zaidi kuhusu suala hili, kwa kusoma maandishi mbali mbali na kufanya tafakari mwenyewe.

Sunday, August 3, 2014

Watoto Katika Tamasha la Afrifest 2014

Kati ya watu waliotembelea meza yangu jana kwenye tamasha la Afrifest, alikuwepo mto anayeonaka katika picha hapa kushoto.

Ninawapenda watoto, Kila nikipata fursa ya kutembelea darasa la watoto, napenda kuwasimulia hadithi na mambo mengine. Nimefanya hivyo sehemu mbali mbali hapa Marekani, kama vile Colorado, Minnesota, na Pennsylvania.

Mtoto huyu alifika hapa mezani pangu ghafla, wakati namalizia kutafuna vipande vya kuku, Nilikuwa nimesalimiana na wazazi wake, kama nakumbuka sawa sawa, nao walikuwa pemdeni wakiangalia vitabu. Binti yangu Zawadi alipoona naongea na mtoto, alifanya uamuzi wa haraka wa kupiga hii picha, hata kabla sijasafisha meza, kwani mtu huwezi kujua mtoto atakuwepo hapo dakika au sekunde ngapi.

Unapoongea na motto, unakuwa katika mtihani mzito, wa kujua sio tu mambo ya kumwambia, bali namna ya kuongea naye ili avutiwe na aendelee kukusikiliza. Unapaswa kumweleza mambo yanayomgusa.

Binafsi, nikishauliza jina na mtoto, napenda kujua kama yuko shuleni. Na kama jibu ni ndio, natumia fursa hii kumhimiza mtoto kufanya bidii shuleni. Namsisitizia kuwa mimi nilipokuwa mtoto nilifanya bidii shuleni, na leo ninafundisha.

Napenda pia kuwatania watoto hao, kwa kuwaambia,  kwamba baadaye waje wasome kwenye darasa langu, na kwamba wawaambie wazazi  kuwa darasa langu litawafaa sana. Huwa nawaambia pia kuwa mimi ni msimuliaji mzuri wa hadithi, na hiyo habari ilionekana kumvutia mtoto huyu. Mtoto huyu hakuwa na haraka ya kuachana nami. Nilijisikia vizuri.

Nawapongeza wazazi wanaowaleta watoto wao kwenye shughuli kama haya matamasha, ambapo wanapafa fursa ya kuona mambo mbali mbali na kupanua ufahamu wao wa dunia kwa kiwango chao. Ni msingi bora katika maisha yao.

Saturday, August 2, 2014

Tamasha la Afrifest Limefana

Tamasha la Afrifest 2014 lilifanyika jana na leo hapa Minnesota. Jana jioni, shughuli ikuwa ni maonesho ya mavazi na muziki, kama inavyoonekana katika tangazo hapa kushoto.

Sikuweza kuhudhuria shughuli za jana, kutokana na masuala ya matibabu, lakini leo nimejikongoja hadi Brooklyn Park, ambako shughuli ya leo ilifanyika. Kule nilipata taarifa za mambo ya jana, kwamba yalifanikiwa vizuri kabisa.

Leo niliweza kwenda kuhudhuria Brooklyn Park ambako shughuli ziliendelea, kama ilivyopangwa. Nilikuwa pamoja na binti zangu, Assumpta na Zawadi.
Kama kawaida, watu kutoka nchi mbali mbali za Afrrika, Marekani, na kwingineko walihudhuria.

Kulikuwa na maonesho ya vitu  mbali mbali, kuanzia mavazi, vitu vya urembo, vitabu na machapisho mengine. Vile vile vile walikuwepo wauza vyakula.

Benki ya Wells Fargo. ambayo sasa huhudhuria Afrifest kila mwaka, ilikuwa na banda lake, ambapo paliwekwa taarifa za huduma za benki hiyo, na watu walikuwa na fursa ya kujiunga kama wateja.

Ilipokaribia jioni, kulikuwa na shindano la soka baina ya Afrika Mashariki na Magharibi, ambalo lilileta msisimko. Kama ilivyokuwa miaka iliyopita, tamasha la Afrifest la leo lilitoa fursa kwa watu kuja na kuondoka walivyopenda. Wengine walikuja hiyo jioni, kuangalia hayo mashindano ya soka. Sikukaa sana kiasi cha kuweza kuangalia mashindano hayo, ila niliona wachezaji walipokusanyika uwanjani.

Kitu kimoja cha pekee mwaka huu ni banda ambalo lilikuwa sehemu ya kukusanyia michango ya vitu mbali mbali kwa ajili ya waathirika wa ugonjwa wa ebola nchini Liberia na sehemu zingine za Afrika Magharibi.

Kwa upande wangu, niliweza kuongea na watu wengi waliofika kwenye meza yangu. Walitaka kujua mambo ya aina mbali mbali. Kwa mfano baadhi walitaka kujua mtazamo wangu kuhusu mahusiano baina ya wa-Afrika na wa-Marekani Weusi. Nilitamka wazi kuwa kuna changamoto nyingi na inahitajika elimu ya dhati na endelevu  kwa pande zote, kama tuna nia ya kujenga maelewano sahihi na mshikamano. 

Wengi, kama ilivyo kawaida, walitaka kufahamu kuhusu shughuli zangu, na hasa maandishi yangu. Nilipata fursa ya kujieleza kwa hao watu mbali mbali. Baadhi walinunua vitabu. Vile vile, nilihojiwa na kituo kimoja cha televisheni.

Hapa naleta picha kadhaa, zinazohusiana na  yale niliyosema hapa juu.