Saturday, April 24, 2010

Nimepita Tena Kwenye Duka la Vitabu

Leo nilikuwa Minneapolis nikihudhuria kikao cha kuandaa mkutano wa waAfrika, Wamarekani Weusi na wengine wenye asili ya Afrika ambao tutafanya Oktoba tarehe 9, 2010. Nilihudhuria pia kikao cha bodi ya Afrifest.

Nilipokuwa narudi, nilipita mjini Apple Valley, nikaingia kwenye duka la vitabu la Half Price Books. Duka hili nimelitembelea mara nyingi na nilishawahi kuandika habari zake katika blogu hii. Niliyoyaona leo ni yale ambayo nayaona daima ninapotembelea maduka ya vitabu hapa Marekani. Watu wengi walikuwemo, watoto, vijana, wazee, wake kwa waume. Wazazi wengine walikuwemo na watoto wadogo sana, na hata watoto wachanga.

Duka ni kubwa, lakini watu walikuwa wanapishana kila sehemu, wakiangalia vitabu, wakivisoma, na kuvinunua. Wengine walikuwa wanawasomea watoto wao hadithi. Watoto wadogo sana niliwasikia wakiongea na wazazi au kujibizana nao kuhusu vitabu. Ni jambo la kugusa sana moyoni unapomwona mama ameketi akijibizana na mtoto wake kuhusu kitabu ambacho mtoto anaangalia.

Ndivyo watoto wa ki-Marekani wanavyolelewa. Nimeshaandika kuhusu suala hili katika makala mbali mbali katika blogu hii na katika kitabu cha CHANGAMOTO: Insha za Jamii.

Muda wote niliokuwa katika duka lile nilikuwa na fikra zile zile za kila siku, nikiwazia malezi ya watoto hao na kufananisha na malezi ya watoto wetu Tanzania. Hatuna maduka ya vitabu kama Marekani, ingawa tunazo baa katika kila mji, hata miji midogo, na kila kona. Hatuna utamaduni wa kusoma vitabu na kuwapeleka watoto wetu kwenye maduka ya vitabu au maktaba.

Wakati wenzetu wanawajengea watoto wao msingi imara wa kutafuta elimu, sisi tunachezea maisha yetu na maisha ya watoto wetu. Je, katika dunia hii, inayohitaji elimu na maarifa, watoto wetu wataweza kushindana na hao watoto wa wenzetu?

Thursday, April 22, 2010

Kenya Yaondoa Vibali vya Kazi

Kuna taarifa kuwa Kenya inaondoa vibali vya kazi kwa raia wa Afrika Mashariki wanaotaka kufanya kazi Kenya. Bofya hapa. Sijui wa-Tanzania wanaipokeaje habari hii, lakini binafsi sishangai, kwani naifahamu Kenya kiasi fulani, na nafahamu kuwa wa-Kenya sio tu wamejiandaa kwa ushindani bali wanajiamini.

Tatizo liko upande wa wa-Tanzania. Kwa miaka mingi sana, labda kuanzia miaka ya themanini na kitu, wa-Tanzania wamekuwa na tabia ya kupuuzia elimu. Shuleni wanatafuta njia za mkato badala ya kusoma sana, ndani na nje ya yale yanafundishwa.

Wakishamaliza shule (ambayo ni dhana ya kipuuzi, kwani shule haimaliziki), wanaona kusoma ni kero. Sijui kuna wa-Tanzania wangapi wanaonunua vitabu na kuvisoma, au wanaoenda maktaba na kujisomea tu, au wana vitabu majumbani na wanavisoma, au wanashirikiana na watoto wao katika kusoma vitabu.

Binafsi, nimeandika kwa miaka mingi nikiwalalamikia wa-Tanzania kwa tabia hizo, na nimeelezea sana nilivyoona tofauti baina ya Tanzania na Kenya, tangu nilipoanza kutembelea Kenya, mwaka 1989.

Nimeelezea mara kwa mara kuwa hata huku ughaibuni, wa-Tanzania hawafanani na wenzetu wa nchi zingine za Afrika. Siwaoni wa-Tanzania kwenye tamasha za vitabu au kwenye maduka ya vitabu. Siwaoni wa-Tanzania wanaomiliki maduka ya vitabu au magazeti. Lakini wenzetu, kama vile wa-Kenya au Wanigeria, wamo katika shughuli hizi.

Watanzania ni wapenda ulabu na starehe, wawe Tanzania au ughaibuni. Hayo nimesema sana kwenye kumbi mbali mbali, na kwenye blogu zangu, na hata kwenye kitabu ambacho nimechapisha mwaka jana, kiitwacho CHANGAMOTO: Insha za Jamii

Sasa basi, katika huu utandawazi, ni wazi wa-Kenya wanajiamini zaidi na hawatishiki kama wanavyotishika wa-Tanzania. Wa-Kenya wamejiandaa zaidi kielimu na wanaweza kujieleza. Watanzania wengi wanawapeleka watoto wao kusoma Kenya, na wa-Kenya wanazidi kuchukua ajira hata nchini Tanzania. Kwa hali ilivyo, wataendelea kuchukua ajira, iwe ni kwao au kwetu, au sehemu nyingine duniani. Wa-Kenya wamejiandaa kiasi kwamba hata fursa za kufundisha ki-Swahili huku ughaibuni wanazichukua zaidi wao.

Wahenga walisema kuwa asiyefunzwa na mama yake, hufunzwa na ulimwengu. Ndio yatakayowapata wa-Tanzania, katika ulimwengu huu wa utandawazi.

Siku za karibuni nitakuwa Tanzania nikiendesha warsha kuhusu masuala ya aina hiyo. Warsha mbili nitafanyia Arusha, tarehe 3 Julai, na nyingine tarehe 10 Julai. Nilishawahi kutangaza katika blogu hii. Lakini, sina hakika kama ni wa-Tanzania wangapi watakaohudhuria. Ila nina hakika wageni watahudhuria, ili mradi wapate taarifa.

Mimi kama mwalimu, siwezi kumezea au kuendekeza uzembe kama huu walio nao wa-Tanzania, ambao wanatumia pesa nyingi sana kwenye sherehe na bia, lakini kununua kitabu cha shilingi elfu saba hawakubali, wala kutumia saa mbili kwa wiki wakisoma maktabani hawawazii, uzembe ambao unawafanya wawe wanatoa visingizio kila siku, au lawama kwa wengine, hasa serikali, wakati wao wenyewe hawawajibiki.

Kama nilivyogusia, hakuna jipya ambalo nimesema hapa juu, bali ni marudio ya yale ambaye nimekuwa nasema kwa muda mrefu, katika blogu hii na kwingineko.

Monday, April 19, 2010

Fisadi Anapoingia Baa

Binafsi, siwaamini wa-Tanzania wanapojifanya kuwalalamikia mafisadi. Hapo nawaongelea wa-Tanzania kwa ujumla, ingawa bila shaka wako baadhi ambao kweli wanachukia ufisadi. Lakini jamii kwa ujumla, siamini kama inachukia.

Wa-Tanzania wanapenda sana starehe, au kwa maneno ya siku hizi, makamuzi na minuso. Shughuli muhimu katika maisha ya wa-Tanzania ni sherehe. Pamoja na kwamba yote hayo yanagharimu sana, michango ya sherehe haiishi.

Katika hali hii yeyote anayechangia sana sherehe hizi anaheshimiwa na kushangiliwa. Fisadi anayo nafasi kubwa ya kujijengea heshima katika jamii yetu, kama ni mchangiaji bora wa sherehe hizi.

Fisadi akiwa baa na kuwanunulia watu bia sana, anajijengea heshima kubwa. Wote wanamtetemekea na kumwita "mzee," na heshima yake inabaki juu.

Wa-Tanzania hawaulizi huyu mtu anapata wapi hela. Na hata wakijua, maadam anawanunulia bia na kuchangia sherehe kwa kiwango cha juu, wanafurahi na kumwenzi. Pamoja na kelele zote za kulalamikia ufisadi, sijawahi kuwasikia wa-Tanzania wakizisusia bia za fisadi. Kelele hizi kwa kiasi kikubwa ni usanii mtupu.

Saturday, April 10, 2010

Mpambano na Lonely Planet

Siku kadhaa zilizopita niliandika kuhusu msomaji wa kitabu changu cha Africans and Americans ambaye alisema kinafaa kuliko kile cha Lonely Planet. Bofya hapa. Nilitamka kiutani kuwa Lonely Planet wakae chonjo, maana wamepata mshindani.

Lakini baadaye, nililazimika kuandika tena kuhusu Lonely Planet, baada ya wao kuandika taarifa iliyoudhalilisha mji wetu wa Arusha. Bofya hapa. Hapo uzalendo ulinisukuma kusema kuwa hao sasa wanatuchokoza, na lazima tujizatiti kujibu mapigo.

Dada Subi, ambaye ni mfuatiliaji makini wa maandishi ya wanablogu wa Bongo na pia mshauri wetu tunayempenda na kumheshimu sana, kanibonyeza leo asubuhi kuwa kuna jambo limetokea Lonely Planet, yaani mteja anayepangia kwenda Tanzania anaulizia kitabu au vitabu vya kusoma, ambavyo si vya aina ya Lonely Planet.

Basi, hapo nimeona lazima niingie mzigoni na kuwachangamkia hao Lonely Planet. Sio kuwalazia damu; ni kuwavalia njuga tu. Nimefanya hivyo tayari, kwa kumpa yule mteja taarifa anazohitaji. Bofya hapa. Heshima na shukrani kwa Dada Subi, kama kawaida, na blogu yake maarufu hii hapa.

Wednesday, April 7, 2010

Hospitali ya Ludewa/ Mambo ndio haya!!

Habari hii ameichapisha Dada Yasinta kwenye blogu yake, nami imenigusa kiasi cha kuamua kuiweka Hapa Kwetu, ili habari ienee zaidi kadiri iwezekanavyo. Inasikitisha kuwa katika nchi yetu, yenye mali nyingi, hali ya watu katika vijiji vingi na mijini ni mbaya kiasi hiki.

Wenye madaraka wanafuja utajiri wa Tanzania. Kwa mfano, hivi karibuni tu, CCM imeagiza magari 200 kwa ajili ya kampeni za uchaguzi. Fedha hizi zingeweza kutumiwa kuboreshea huduma za afya kwenye hospitali kama hii ya Ludewa, au kuwapa mitaji hao akina mama, wakabadilisha maisha yao.

Wako ambao wanachuma mishahara na marupurupu kwa mamilioni ya shilingi. Wako ambao wanatumia mamilioni kwenye sherehe na starehe. Wengine wamechota na labda bado wanachota, mamilioni ya shilingi na kuyahamishia nje, kwenye akaunti binafsi. Badala ya kutumia hela kuboresha huduma za afya sehemu kama hii ya Ludewa, Tanzania imetumia mabilioni ya shilingi, tangu miaka ya mwanzo ya Uhuru, kwa kuwapeleka waheshimiwa nje ya nchi, kwa matibabu au hata tu kuchekiwa afya, mambo ambayo yangeweza kufanywa katika hospitali za nchini, kama vile Muhimbili. Ninafahamu jinsi gharama ya matibabu ilivyo mbaya katika nchi kama Marekani. Fedha zilizotumika miaka yote hii zingekuwa zimeboresha huduma katika hospitali sehemu mbali mbali za nchi.

Hayo yote yananijia akili ninaposoma taarifa hii hapa chini, kutoka Ruhuwiko.

----------------------------------------------------------------

Thursday, April 8, 2010

Hospitali ya Ludewa/Mambo ndio haya!!













Akina mama ambao wanawauguza ndugu zao katika hosptali ya Wilaya ya Ludewe wakisonga Ugali nje ya wodi ya akina mama wanaosubiri kujifungua, kati ya akina mama 100,000.wajawaito 200 hupoteza maisha katika Wilaya hiyo kutokana na ukosekanaji wa miundombinu.












Wanawake wajawazito toka katika vijiji 76 vinavyo zunguka Wilaya ya Ludewa wakiwa wamelala na wengine wakila chakula huku wakiwa wamesubilia siku zao za kujifungua katika hospitali ya Wilaya ya Ludewa Mkoa wa Iringa kati ya akina mama 100,000 wajawazito 200 hufariki kutokana na ukosefu wa huduma.












Inasikitisha: Baadhi ya akina mama wajawazito wakiwa nje ya wodi ya wazazi katika hospitali ya Wilaya ya Ludewa ambapo jengo hilo lina vitanda 6 na kila kitanda hutumiwa na akina mama wajawazito wawili. Wengine hulazimika kulala chini.(Picha na Albart Jackson)

Tuesday, April 6, 2010

Huduma kwa Wateja: Nathan Mpangala

Suala la huduma bora kwa wateja ni muhimu katika biashara au sekta yoyote inayotoa huduma. Mchora katuni maarufu Nathan Mpangala amechora katuni nzuri, ambayo imenikumbusha makala niliyowahi kuandika kuhusu suala hilo, "Ubora wa Huduma, Msingi wa Mafanikio." Bofya hapa.

Friday, April 2, 2010

Wenzetu Wanazindua iPad, Sisi Tunazindua Bia

Mapema leo niliandika ujumbe mdogo kwenye ukumbi wa Tanzanet, ambao ni ukumbi wa mijadala, taarifa, na michapo unaowajumuisha waTanzania na marafiki wa Tanzania duniani kote. Ujumbe wangu unahusu mambo mawili tofauti, ambayo yanatokea wiki hii: moja ni uzinduzi wa kifaa kiitwacho iPad, na jingine ni uzinduzi wa bia kule Tanzania.

Muda mfupi baada ya kutokea ujumbe wangu kule Tanzanet, nimeandikiwa na wahusika wa blogu ya Watanzania waishio Oslo kuwa wanapenda kuiweka makala yangu kwenye blogu yao. Nami sikuwa na kipingamizi. Bofya hapa.

Thursday, April 1, 2010

Warsha Zangu Tanzania, 2010

Niko katika maandalizi ya kuendesha warsha Tanzania, kama nilivyofanya mwaka jana na mwaka juzi. Kwa taarifa fupi, bofya hapa na hapa. Maandalizi yanakwenda vizuri, na hadi leo, kwa kutumia mawasiliano ya barua pepe, nimeshapanga ratiba hii:

Juni 12, 2010, warsha kuhusu, "Culture and Globalization," Meeting Point Tanga.

Julai 3, 2010, warsha kuhusu, "Culture and Globalization," Arusha Community Church.

Julai 10, 2010, warsha kuhusu, "Cultural Tourism," Arusha Community Church.

Niko katika mawasiliano na wadau wa Zanzibar, ili kuandaa warsha Visiwani. Taarifa nitaleta baadaye. Nafanya mpango wa warsha Dar es Salaam pia.

Warsha hizi zitaendeshwa kwa ki=Ingereza, kama siku zilizopita, kwa sababu wahudhuriaji huwa wa mataifa mbali mbali. Yeyote anakaribishwa.

Nina mengi yanayonisukuma kuja kuendesha warsha hizi Tanzania. Kadiri ninavyotoa mihadhara huku ughaibuni, katika vyuo, taasisi, makampuni, na mashirika kuhusu athari za tofauti za tamaduni duniani, nazidi kutambua kuwa waTanzania tutapata shida katika dunia hii ya utandawazi kama hatufanyi juhudi ya kujielimisha na kujiandaa.

Haijalishi kama wewe ni mwanadiplomasia, mfanyabiashara, mwanafunzi, mmiliki wa shule, mfanya kazi katika kampuni, au mtafiti. Katika dunia ya leo, hatuwezi kukwepa kukumbana na watu wa tamaduni tofauti, na bila kuelewana, tutaishia katika migogoro na kuyumba au kuharibika kwa yale tunayotegemea kuyafanikisha. Mifano ni mingi duniani kote, na nchi mwetu pia.

Warsha hizi ni fursa si tu ya kunisikiliza mimi na kuniuliza masuali, bali pia fursa ya washiriki kufahamiana. Kwa hivi, nawahimiza wahudhuriaji kuja na taarifa za shughuli zao, iwe ni biashara, au shughuli nyingine yoyote. Ni njia nzuri ya kujitangaza na kujijengea mtandao. Nami nitaleta taarifa zangu, pamoja na vitabu vyangu.

Ninafanyia warsha hizi Tanzania, kama kianzio tu, lakini mkakati wangu ni kuzipeleka katika nchi zingine za jirani, nikianzia na Kenya. Hatimaye nataka kufanya warsha hizi katika nchi mbali mbali za Afrika na kwingineko, kwani elimu haijui mipaka ya nchi.

Kwa taarifa zaidi, na pia kujisajili kwa warsha, andika ujumbe: info@africonexion.com. Kama unataka kununua vitabu vyangu Tanzania, piga simu 0717 413 073 au 0754 888 647.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...