Wednesday, April 7, 2010

Hospitali ya Ludewa/ Mambo ndio haya!!

Habari hii ameichapisha Dada Yasinta kwenye blogu yake, nami imenigusa kiasi cha kuamua kuiweka Hapa Kwetu, ili habari ienee zaidi kadiri iwezekanavyo. Inasikitisha kuwa katika nchi yetu, yenye mali nyingi, hali ya watu katika vijiji vingi na mijini ni mbaya kiasi hiki.

Wenye madaraka wanafuja utajiri wa Tanzania. Kwa mfano, hivi karibuni tu, CCM imeagiza magari 200 kwa ajili ya kampeni za uchaguzi. Fedha hizi zingeweza kutumiwa kuboreshea huduma za afya kwenye hospitali kama hii ya Ludewa, au kuwapa mitaji hao akina mama, wakabadilisha maisha yao.

Wako ambao wanachuma mishahara na marupurupu kwa mamilioni ya shilingi. Wako ambao wanatumia mamilioni kwenye sherehe na starehe. Wengine wamechota na labda bado wanachota, mamilioni ya shilingi na kuyahamishia nje, kwenye akaunti binafsi. Badala ya kutumia hela kuboresha huduma za afya sehemu kama hii ya Ludewa, Tanzania imetumia mabilioni ya shilingi, tangu miaka ya mwanzo ya Uhuru, kwa kuwapeleka waheshimiwa nje ya nchi, kwa matibabu au hata tu kuchekiwa afya, mambo ambayo yangeweza kufanywa katika hospitali za nchini, kama vile Muhimbili. Ninafahamu jinsi gharama ya matibabu ilivyo mbaya katika nchi kama Marekani. Fedha zilizotumika miaka yote hii zingekuwa zimeboresha huduma katika hospitali sehemu mbali mbali za nchi.

Hayo yote yananijia akili ninaposoma taarifa hii hapa chini, kutoka Ruhuwiko.

----------------------------------------------------------------

Thursday, April 8, 2010

Hospitali ya Ludewa/Mambo ndio haya!!













Akina mama ambao wanawauguza ndugu zao katika hosptali ya Wilaya ya Ludewe wakisonga Ugali nje ya wodi ya akina mama wanaosubiri kujifungua, kati ya akina mama 100,000.wajawaito 200 hupoteza maisha katika Wilaya hiyo kutokana na ukosekanaji wa miundombinu.












Wanawake wajawazito toka katika vijiji 76 vinavyo zunguka Wilaya ya Ludewa wakiwa wamelala na wengine wakila chakula huku wakiwa wamesubilia siku zao za kujifungua katika hospitali ya Wilaya ya Ludewa Mkoa wa Iringa kati ya akina mama 100,000 wajawazito 200 hufariki kutokana na ukosefu wa huduma.












Inasikitisha: Baadhi ya akina mama wajawazito wakiwa nje ya wodi ya wazazi katika hospitali ya Wilaya ya Ludewa ambapo jengo hilo lina vitanda 6 na kila kitanda hutumiwa na akina mama wajawazito wawili. Wengine hulazimika kulala chini.(Picha na Albart Jackson)

6 comments:

Yasinta Ngonyani said...

Nashukuru kama nawe imekugusa kwani ni mambo mahimu katika jamii. Ahsante

Mija Shija Sayi said...

Prof. Hivi hapa ni nani wa kulaumiwa?

Mbele said...

Da Mija, shukrani kwa suali lako. Nimelitafakari tangu pale ulipolileta na naona si rahisi kulijibu, maana kila jibu linazua masuali zaidi. Labda niseme tu machache.

Hao akina mama nadhani ni wakulima. Kama kuna vijihela wanavyopata kwa kuuza mahindi au maharage, inawezekana vihela hivyo haviwasaidii wao, bali waume zao wanavitumia kwenye ulanzi hapo hapo kijijini na pengine mara moja moja kwenye bia, maana uwezo wao si mkubwa.

Hapo kijijini, au mbali kidogo na hapo, unaweza kukuta baa na gesti ambazo zimejengwa vizuri. Baa zina makochi mazuri na gesti zina vitanda vizuri na magodoro na shuka, wakati hospitali hii ndio kama unavyoiona.

Kila mahali Tanzania utakuta baa, gesti, na kitimoto ziko katika hali nzuri, ingawa karibu na hapo utakuta shule yenye nyufa na inavuja mvua, na hospitali isiyo na vitanda vya kutosha, wala huduma za kutosha.

Watanzania wanataka baa ziwe nzuri. Potelea mbali shule na hospitali. Na kama una baa, halafu utumie mapato yako kukarabati shule ya hapo mtaani, badala ya kuboresha baa yako, wanywaji na walevi watahama baa yako kuhamia baa nzuri zaidi. Hawataki kunywa kwenye baa yenye nyufa na viti vya ovyo. Nyufa na paa zinazovuja ni mambo ya shuleni, sio baa au gesti.

Kwenye ngazi ya taifa akili ni hiyo hiyo. Vigogo wamekuwa wakikimbilia nje kwa matibabu au kuchekiwa afya, badala ya kutumia pesa hizi kukarabati hospitali na kuboresha huduma.

Badala ya kukarabati shule nchini, vigogo wanapeleka watoto wao Kenya na ughaibuni.

Utajiri wa nchi unateketezwa na wageni na mafisadi wananchi. Lakini wananchi tunajisikia raha pale tunapokaa baa na fisadi ambaye anaagiza bia "kama tulivyo."

Tunapokuwa kwenye vikao vya kupanga arusi au sherehe, tunapiga vigelegele na makofi wakati fisadi anaposimama na kuahidi kuchangia laki tatu. Ni furaha kubwa anapoahidi kuleta kreti kumi za ulabu.

Hatujiulizi kwa nini hii michango isiwe ya kununulia vitanda kwenye hospitali kama hii ya Ludewa. Kipaumbele chetu ni bia.

Ningeweza kuendelea sana na haya mazungumzo yangu, lakini nadhani ninachotaka kusema ni kuwa kwa hali hii ya hospitali ya Ludewa, wa kulaumiwa ni wengi, karibu kila mwananchi, maana hata hao akina mama tunawaona kwenye picha inawezekana ni CCM wa damu.

Mija Shija Sayi said...

Prof. Mbele baada ya kusoma maelezo yako nimegundua kwamba watanzania tuko katika hatari kubwa, ni malimbukeni, tuna macho lakini hatuoni. Haiwezekani tukawa tunatoa kipaumbele katika anasa badala ya mambo yajengayo. Labda nisiendelee sana ila naomba nikuulize swali moja tena, JE UNADHANI TUNAWEZA KUBADILISHA HALI HII? UNADHANI MBINU GANI ITUMIKE?

Binafsi huwa nadhani labda tuanze kuwajenga watoto sasa hivi ambao bado hawajaharibika kiakili kwa kuandaa mpango maalumu wa KUWALAZIMISHA kupenda kujisomea. Mpango huo usambazwe katika vyombo vyote vya habari badala ya habari za umbeya, kuandaliwe maigizo jukwaani yenye kuchochea watoto kusoma, badala ya mashindano ya urembo yaandaliwe mashindano ya kutunga insha, au ya kutunga njia rahisi ya kukokotoa hisabati halafu mshindi anapata ufadhili wa kusoma bure na vitu kama hivyo. Yaani kwa ufupi naongelea tuanze kujenga mazingira ya kuwafanya watoto waone kuna maana kubwa ya kuwa na ELIMU. Sijui kama nimeeleweka.

Prof. Wewe unadhani tufanyeje? Je una mbinu kali tuanze kuifanyia kazi?

Mbele said...

Dada Mija, shukrani sana kwa mawazo yako. Kwa kweli sina la kuongezea, kwani masikitiko uliyotoa ndio yangu pia, na pendekezo ulilotoa naliafiki moja kwa moja.

Nakubaliana nawe kabisa kuwa kizazi hiki chetu kimekwishatokomea. Ni kizazi cha makamuzi. Kilichobaki sasa labda sisi wachache tunaotambua tatizo hili tuanze mkakati huu wa kushughulika na watoto.

Dada Mija, na mwingine, na mwingine, na mimi, na wengine, wenye mawazo kama haya yetu tunaweza kuanza kuwaunganisha watoto kwenye mtaa moja au kijiji na kuanza kushughulika nao. Mnakuwa kikundi ambacho kinatumia muda wake kwa hii elimu unayosemea. Pole pole mbegu inakomaa na kuota. Pole pole mfano huu ukaanza kusambaa. Naamini hili linawezekana.

Miaka kadhaa iliyopita nilianza kutambua uwezekano wa kuanza kusambaza fikra mpya kwa mtindo huu. Nilianza uhusiano na kikundi cha vijana waliokuwa wamejiunga katika shughuli za utalii pale Mto wa Mbu. Kila ninapokuwa Tanzania naenda pale na kuongea nao. Tumejenga uhusiano ambao unaendelea, na nina hakika tutafanikiwa kuleta mapinduzi fulani, ikiwemo kujenga fikra mpya miongoni mwa vijana wa Tanzania, fikra ya kujiamini na kujishughulisha ili kujiletea maendeleo pale pale nchini, badala ya kuwazia kuzamia meli na kutokomea majuu.

Vijana hao ukiwakuta watakuelezea sana mambo yetu. Waliwahi kuelezea kidogo kwenye blogu yao. Bofya hapa.

o'Wambura Ng'wanambiti! said...

Hii inaonesha ni kwa jinsi gani kama nchi hatuna dira wala vipaumbele :-(

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...