Saturday, April 24, 2010

Nimepita Tena Kwenye Duka la Vitabu

Leo nilikuwa Minneapolis nikihudhuria kikao cha kuandaa mkutano wa waAfrika, Wamarekani Weusi na wengine wenye asili ya Afrika ambao tutafanya Oktoba tarehe 9, 2010. Nilihudhuria pia kikao cha bodi ya Afrifest.

Nilipokuwa narudi, nilipita mjini Apple Valley, nikaingia kwenye duka la vitabu la Half Price Books. Duka hili nimelitembelea mara nyingi na nilishawahi kuandika habari zake katika blogu hii. Niliyoyaona leo ni yale ambayo nayaona daima ninapotembelea maduka ya vitabu hapa Marekani. Watu wengi walikuwemo, watoto, vijana, wazee, wake kwa waume. Wazazi wengine walikuwemo na watoto wadogo sana, na hata watoto wachanga.

Duka ni kubwa, lakini watu walikuwa wanapishana kila sehemu, wakiangalia vitabu, wakivisoma, na kuvinunua. Wengine walikuwa wanawasomea watoto wao hadithi. Watoto wadogo sana niliwasikia wakiongea na wazazi au kujibizana nao kuhusu vitabu. Ni jambo la kugusa sana moyoni unapomwona mama ameketi akijibizana na mtoto wake kuhusu kitabu ambacho mtoto anaangalia.

Ndivyo watoto wa ki-Marekani wanavyolelewa. Nimeshaandika kuhusu suala hili katika makala mbali mbali katika blogu hii na katika kitabu cha CHANGAMOTO: Insha za Jamii.

Muda wote niliokuwa katika duka lile nilikuwa na fikra zile zile za kila siku, nikiwazia malezi ya watoto hao na kufananisha na malezi ya watoto wetu Tanzania. Hatuna maduka ya vitabu kama Marekani, ingawa tunazo baa katika kila mji, hata miji midogo, na kila kona. Hatuna utamaduni wa kusoma vitabu na kuwapeleka watoto wetu kwenye maduka ya vitabu au maktaba.

Wakati wenzetu wanawajengea watoto wao msingi imara wa kutafuta elimu, sisi tunachezea maisha yetu na maisha ya watoto wetu. Je, katika dunia hii, inayohitaji elimu na maarifa, watoto wetu wataweza kushindana na hao watoto wa wenzetu?

24 comments:

Fadhy Mtanga said...

Kwa kuwa wazazi wengi hapa nyumbani hawana utamaduni wa kujisomea vitabu mbalimbali, hawawezi kuwajengea watoto wao tabia hiyo. Tazama hata majumba makubwa yanayojengwa na Watz....ni nadra kukuta pametengwa study room.
Hali hii inachangia sana upeo mdogo mno wa sisi vijana wa Kitz.

Katu said...

Sasa Profesa, inakuwa ngumu kwa watoto wa watanzania na wazazi wao kufikiria vitabu kwa sababu mahitaji ya msingi yenyewe hayapatikana...Mtoto wa marekani kichwani kwake hawazi kabisa kama kuna suala la kuchota maji kisimani maili tatu, kutumia koroboi kusoma, hana nguo ya kuvaa, hana pencil ama peni na daftari la kuandikia. Kutembea maili tatu ama zaidi kwenda shuleni, kukata kuni za kupikia chakula..nadhani tunaangalia haya mambo kwa watanzania milioni arobaini ambao ndiyo wanakabiliana na haya matatizo ya msingi na siyo hao milioni nne waliobaki...Kuna tatizo kubwa hapo nyumbani la ufisadi...Nadhani hili ndiyo kujengea mikakati kupambana kwa pamoja tena bila kuonea aibu na unafiki nalo ili liweza kuhamsha hizo ngazi nyingine za maendeleo

Mbele said...

Ndugu Mtanga, naona tunakubaliana kimtazamo. Labda niongelee tu kidogo hoja ya Ndugu Katu.

Nimefuatilia utamaduni wa waTanzania kwa miaka mingi, na nimekuwa nikilalamika kwa miaka mingi. Ingawa ni kweli kuwa wako waTanzania wengi ambao wana maisha ya dhiki na hata hela ya daftari na penseli inawaletea taabu, lakini ukweli mwingine ni kuwa kuna maelfu ya waTanzania katika kila mkoa na wilaya ambao wanaunguza mamilioni ya pesa kwenye bia, sherehe, na kadhalika.

Angalia hata kwenye blogu ya Michuzi, uone jinsi watu wanavyofurika kwenye minuso, meza zikiwa zimefurika vyupa na vikopo vya bia.

Bajeti ya bia ya waTanzania wengi ni maelfu kila wiki. Huwa nakutana nao huko Tanzania, maana ninafika kila mwaka. Ninalumbana nao kila mahali, maana huwa nasafiri sehemu mbali mbali za nchi. Hata mwezi Juni, Julai na Agosti mwaka huu nitakuwa huko huko, na nitakuwa nalumbana nao.

Hawana utamaduni wa kununua vitabu wala kusoma, hata kama wana fedha nyingi kiasi gani. Hawathamini elimu, maana wangethamini, hata michango ya sherehe wangepunguza na kuchangia angalau madawati ya shule kwenye mji wao au kuanzisha fungu la kuwanunulia daftari watoto wasiojiweza.

Watanzania wengi wana uwezo, ila hawana utamaduni wa kuthamini elimu.

Hapa Marekani, pamekuwa na matatizo makubwa ya uchumi kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa. Wengi wamepoteza ajira na maisha ni magumu. Wanao utamaduni wa kununua vitabu na kuvisoma, lakini kutokana na hali hii, uwezo wao wa kununua umepungua.

Lakini taarifa zinasema kuwa wakati huu mgumu, idadi ya watu wanaoenda maktaba kusoma imeongezeka sana. Maktaba za Marekani zinaripoti hivyo. Yaani kule kupungukiwa uwezo wa kununua vitabu wanaidhibiti kwa kwenda zaidi maktaba.

Lakini Tanzania hakuna kitu kama hicho. Huwa napita kwenye maktaba za mikoa, kila ninapokuwa nchini. Sana sana nawaona watoto wa shule. Watu wazima wanaweza kuwa hapo nje kwenye kijiwe, wakisogoa, lakini hawaingii maktabani.

Wanalalamika kuwa hawana ajira, lakini wazo la kuingia maktabani na kujielimisha, hata kama ni kwa kusoma tu vitabu vya kiIngereza, ili kujiweka sawa katika ulimwengu huu wa ushindani, haliko vichwani mwa waTanzania.

Matokeo yake ni kuwa hata vibarua vya kutandika vitanda mahotelini watakuwa wanachukua waKenya, kwa sababu waTanzania wanashinwa hata kuongea na mgeni atakayelala humo. Wangeingia maktaba na kujifunza angalau kiIngereza na kusoma hadithi za kiIngereza, wangejiongezea ujuzi fulani.

Kwa hivi, waTanzania tatizo kubwa ni uvivu, maana hata hivi vitabu vya bure maktabani hawaendi kusoma.

Nimeshahudhuria matamasha ya vitabu hapa Dar es Salaam. Utawakuta watoto wa shule, lakini watu wazima hawaonekani. Niliwahi kuwaona watoto wakiimba nyimbo kwenye tamasha mojawapo, wakiwaomba wazazi wawanunulie vitabu au wawe wanasoma nao vitabu majumbani. Ilisikitisha, kwa sababu wazazi wenyewe hawakuwepo.

Watoto wetu, kama walivyo watoto duniani kote, wana hamu ya kusoma vitabu. Watu wazima ndio wanaowaangusha. Kama Ndugu Mtanga anavyosema, hata wenye pesa wanapojenga nyumba, hawaweki sehemu ya kusomea. Na hao wenye pesa wana umeme majumbani, kwani wanamudu kununua mashine za umeme. Lakini wazo la kujenga sehemu ya kusomea halipo kichwani.

Katu said...

Hivi Tanzania unayosema wewe ni ipi Profesa!? Kama hii ninayoishi mimi ina maktaba moja kila mkoa wenye zaidi wilaya nne. Hiyo bia unayosema inanyweka na watanzania wangapi kwa takwimu.

Mimi naona kufananisha mtoto wa Tanzania na wamarekani ni sawa na mashindano mwendesha baiskeli na msukuma mkokoteni la mkaa hapa kijijini kwangu Lungongole hapa Ifakara.

Profesa naomba tujadili hili suala kwa takwimu na siyo kwa nadharia ambayo siyo maisha halisi yaliyopo kwa watanzania asilimia themanini(milioni arobaini)).

Kuna tatizona la msingi naona hautaki kuliongelea na kukimbilia matokeo tuu ya matatizo hayo yote...Wewe profesa jaribu kukaa bila ula chakula kwa siku moja halafu kama unaweza kupata kipande cha muhogo kimoja cha urefu 5cm, upanda 7 cm na unene 2 cm...halafu kaa bila ya kula kitu chochote tena kwa masaa sita halafu jaribu kuchukua kitabu kisome halfu jiulize kama umekielewa....!!!

Jinsi utakavyojisikia hapo ndiyo hali halisi ya mtoto na wazazi wa kitanzania wanavyoishi. Mimi na mashaka na sehemu unazotembelea hazikupi picha halisi ya mtanzania...Nenda tembelea sehemu moja inaitwa kisimaGuru Morogoro Vijijini, Tanganyika Masagati wilayani Kilombero, Wilayani nachingwea, Nenda na sehemu nyingi za kukueleza, ndiyo hupate picha kamili cha Tanzania na siyo Masaki na Makao makuu ya mikoa na wilaya. Unatakiwa kwenda kwenye maisha halisi ya watanzania walio wengi Tanzania....Siyo Dar, Arusha, Tanga na Mbeya hautapata picha kamili ya watanzania. Nimeona makala zako nyingi unalaumu watanzania bila kuangalia vikwazo vinavyowakabili watanzania kwa ujumla...

Mbele said...

Ndugu Katu

Mimi ni mtafiti na ninazunguka sana vijijini ambako naona dhiki hizi unazoongelea. Ninafika kwenye vijiji ambako gari haiwezi kufika, bali ni kwa miguu. Nimezunguka vijiji vya kisiwani Ukerewe na Ukara, vijiji vya Bariadi, Shinyanga, Magu, Mbulu, Lushoto, Tanga. Halafu mimi mwenyewe nilikulia kijijini, kule Mbinga, na huwa naenda mara kwa mara. Vijijini Tunduru nimepita, na vijiji vya Songea, Iringa, na kadhalika.

Nimeona maisha ya hao watu unaosemea, na nimeshinda na njaa kwenye baadhi ya vijiji hivi. Nimeona dhiki za kila aina.

Kwa hivi, naomba unielewe hivyo, kwamba hakuna unachokijua kuhusu ufukara katika Tanzania, ambacho sikijui.

Pamoja na hayo, ninachosema ni kuwa kuna maelfu ya waTanzania ambao wanatumia mamilioni katika bia na sherehe, kuanzia huko kwenye miji midogo hadi kwenye miji mikubwa. Michango ya arusi haiishi.

Kama ni takwimu, tunaweza kuzipata kiwanda cha bia. Humo mitaani tunaona kreti zinazopakuliwa. Na kwenye arusi na sherehe tunaona kreti zinazopakuliwa.

Nimeshaona kwenye baa watu wanakunywa kwa bili na kudaiwa malaki. Na wanazilipa, wanapopata hela.

Hayo yote ni ukweli kabisa. Lakini tunachosema sisi ni kuwa, hao waTanzania ambao hawana dhiki ya pesa, nao hawana utamaduni wa kununua na kusoma vitabu.

Cha zaidi ni kuwa, hata hao waTanzania wanaolia na umaskini, ikitokea wapate pesa hawatanunua vitabu, bali ulabu.

Ndoto ya maskini wa Tanzania ni kupata fursa ya kutanua kama wanavyotanua hao wenye pesa. Wazo la kununua vitabu halipo vichwani. Na hili ndilo tatizo la msingi.

Hata huku ughaibuni, waTanzania hawana utamaduni wa kununua na kusoma vitabu. Nimeongelea hilo kwa miaka na miaka, kwa sababu naishi huko na nathibitisha kwamba hali ndio hiyo. Watanzania wanafika ughaibuni wakiwa na utamaduni ule ule wa nyumbani: kwenye makamuzi na sherehe utawakuta, lakini kwenye vitabu huwakuti.

Katu said...

Hivi unafahamu kwamba pombe inanyweka na watanzania wengi za kienyejeji kuliko hizo bia unazosema wewe.........

Pia unatambua kuwa hao watanzania wanaopata hizo wengi wao wanazipata kwa nia zisizo halali na mfumo uliyopo wa utawala na sheria unatoa hizo fursa watu kufanya hivyo. Unatambua kuwa wastaafu wengi wanakufa mapema mara ya kutoka kazini..Je uafahamu kuwa kiwango cha uamasikini kimeongezeka kwa sababu nyingi tuu Mojawapo wasomi kama wewe kukimbia nchini kwetu na kwenda ng'ambo kwa sababu ya maslahi.

Mimi nadhani wewe haujakulia kijijini kwa sababu sisi tuliyopo huku ndiyo tunafahamu hayo siyo wewe unayekuja kutu-enjoy kwa kila baada ya blue moon maumivu ya kiatu anayajua anyevaaa hivyo wewe siyo mtu sahihi kuzungumza maisha ya mtanzania.

Unasema uvivu kwa lipi hasa!!!!!!!!...Unatambua watoto wa mkulima walisoma kipindi na kupata hiyo fursa kipindi cha Nyerere tuu na siyo vinginevyo na wewe ukiwa mmojawapo ambaye ulisomeshwa na fedha za walipa Kodi na kukimbilia huko marekani na hivi sasa unatudhiaki na wakati hatujapata matunda yoyote ya wewe kuoma kwa kodi zetu. Tunalokuja kusikia kejeli na dharau bila kujua matatizo ya kwa kina

Mbele said...

Ndugu Katu, shukrani tena kwa mchango wako. Pamoja na yote, nimekuja huku ughaibuni kutafuta maarifa, na nimefanikiwa kuifahamu dunia.

Nina mkakati, kuanzia miaka michache iliyopita wa kuja kuwamegea waTanzania, ili kuwasaidia kuondokana na haya matatizo na kuweza kuwa kwenye upeo wa kushindana katika dunia ya leo.

Ndio ajenda ninayoitekeleza katika miaka hii, kabla ya kuja kabisa Tanzania. Wakati huu ninaandaa safari ya kuja na nitakuwa naendesha warsha Arusha, Tanga, Dar es Salaam, na labda Zanzibar.

Kuhusu habari zangu binafsi, kifupi ni kuwa mimi nikiwa mwajiriwa Tanzania, nilikuja na kusoma Marekani, 1980-86. Nilipomaliza, nilirudi Tanzania kujenga Taifa. Baada ya miaka mitano niliondoka, kutokana na mizengwe na ukosefu wa haki. Labda kuna siku utakuja kuwasikia walioshuhudia.

Ila tu napenda kusititiza shukrani zangu kwa changamoto uliyotoa katika mjadala huu. Ni muhimu sana kwa sisi tunaopenda mijadala.

Fadhy Mtanga said...

Nimekuja kwa mara nyingine kuchangia mawazo yangu maana jambo hili lanigusa sana.

Awali ya yote naomba kupingana na ndugu Katu. Amesema kila mkoa una maktaba moja. Natoa mfano, mwaka 2004 wakati nikifanya kazi kama mwelimisha rika wilayani Njombe, wilaya hiyo peke yake ilikuwa na maktaba nne za serikali. Moja ilikuwapo pale Njombe mjini, moja kijiji cha Ilembula, moja kijiji cha Kifanya na moja kijiji cha Lupembe. Ukiachilia hizo, palikuwa na maktaba moja binafsi pale Njombe mjini, palikuwa na maktaba ya Walei wa kanisa Katoliki, palikuwa na maktaba mbili za shule za sekondar za Njombe na Mpechi. Sambamba na hizo kila shule ya sekondari wilayania hapo (kabla ya shule za kata kuja) ilikuwa na maktaba iliyosheheni vitabu na machapisho mbalimbali. Shule za serikali, taasisi za dini na NDDT(Njombe Dist Devpmt Trust fund). Lakini utamaduni wa kujisomea haukuwa utamaduni wa wananchi wahusika.

Mimi na rafiki yangu Elisante tulifanya kazi katika tarafa ya Lupembe mwezi Januari hadi Agosti 2004. Kijijini Lupembe palikuwa na maktaba ya TLS na ya shule. Lakini tulikuta vitabu vyaliwa na mchwa. Tena kuna vitabu vingi ambavyo leo ni nadra kuvikuta madukani. Wahudumu wa maktaba ya umma walilalamika hakuna wahudhuriaji kabisa katika maktaba. Wahudumu walikwenda pale kutimiza tu wajibu. Walishinda wakifuma vitambaa.
Tukamshawishi mkuu wa shule ya sekondari Lupembe, akatukubalia kuanzisha klabu ya wasomaji. Tulipata mafanikio kiasi cha kurishisha, tulipata wanachama zaidi ya sitini katika jumla ya wanafunzi mia nne na ushee. Wakaanza kupeana hata zamu za kusafisha maktaba na wakawa wanasoma kwelikweli. Alama B ya kwanza ya historia ktk shule hiyo ilitoka kwa wanafunzi wale. Jambo lililonisikitisha, mwaka uliofuata nilipofuatilia, klabu ilikuwa imekufa, sababu imekosa msukumo. Hii ndiyo jamii yetu ya watanzania iliyo wabunifu wa kutoa sababu kwa nini wanashindwa kufanya jambo wakati kuna sababu dhahiri kwanini wangeweza kulifanya jambo hilo.

Jambo la pili, mimi si mtaalamu wa kiuchumi, lakini nitasema hili kwa upeo wangu. Mimi ni shabiki mkubwa wa futiboli. Jumapili iliyopita nilikuwa uwanja wa taifa kuishangilia Simba ikicheza na Yanga. Jana tena nikaenda Simba ikicheza na Al Hadood ya Misri.
Mechi ya Simba na Yanga ilihudhuriwa na watazamaji zaidi ya 37,000 na kutengeneza mapato zaidi ya shilingi milioni 230/=. Kiingilio cha chini kilikuwa sh 7,000/=, mtu akajipigapiga wee hata akaipata hiyo pesa. Tungesema kuna tamasha la vitabu navyo vyauzwa kwa bei ya chini ya sh 2,000/= wala watu wasingejali.
Ukiwa pale nje ya uwanja wa taifa utakuta watu wakila gambe (ndo lugha ya siku hizi mjini hapa, wakinywa pombe) kwa kufuru. Natembea sana jijini hapa nyakati za wikendi. Maeneo yote ya starehe watu pomoni. Watu hao hao ukiwaambia juu ya vitabu, watakujibu unajua watanzania wengi ni masikini hatumudu kununua vitabu.
Tuje hata kwenye magazeti. Magazeti yanayoandika habari makini zenye kujenga ufahamu mkubwa wa mambo ya msingi, hapa nchi yanauzwa sh 400/= lakini yale yanayoandika habari za fulani kafumaniwa na fulani gest hausi nayo bei ni sh 400/= ile ile. Watz wamechagua kuwa wanunuzi wazuri sana wa haya ya fulani anatembea na fulani. Yanagombaniwa kama njugu, yanaisha mapema sana. Mama wa nyumbani anajinyima pesa ya mboga kila siku ili apate magazeti haya. Lakini hawezi nunua Mwananchi Jumapili ambalo ndani yake linafundisha namna ya kupamba nyumba zetu, namna nzuri ya mapishi na namna nzuri ya kuboresha mahusiano kwenye ndoa. Sisi ndiyo Watz.

Nimesema sana, naomba nimalize kwa kusema, ukiachilia mbali hali zetu duni kimaisha, pia Watz tumechagua kipaumbele kwenye starehe na siyo kwenye kukuza ufahamu.

Huu ni mtazamo wangu.

Ahsanteni.

Katu said...

iwapo lugha itakayotumika tuu Nashukuru Profesa Mbele kukubaliana na mtazamo wangu kuhusiana na mjadala huu.

Na pia ni habari njema kusikia kwamba unataka kurudi kutusaidia pamoja kwa maarifa uliyojifunza. Mimi nataka nikukumbuhe tuu kuwa Tanzania uliyoiacha wakati huo wa miaka tisini ilikuwa bado ya mtazamo wa mfumo wa maisha ya kijamaa. Na hivi sasa tunafuata mfumo ambao haueleweki hupi ingawa inasemekana kuwa ni wa kibepari. Sasa hii ni kukuthibitishia hiyo Tanzania ambao wewe huwa unaiangalia unapokuja kwa siku chache siyo ambayo sisi tunaishi miaka nenda miaka rudi.

Tena nimefurahi kusikia kilichokuondoa awali kwenda ughaibuni ilikuwa kuto kutendewa haki....nafikiri hivi sasa imekuwa maradufu au tatu hiyo hali...kama unakawaida ya kukimbia mazingira nafikiri safari hii hautarudi tena kwenye ardhi ya yetu sisi wanyonge daima. Maana haki yako hapa inatapatikana kwa kununua ama kukubali kudhulumiwa kwa kukaa kimya na kufa na tai shingoni.

Wewe Fadhili Mtanga...nadhani hauifahamu vizuri Tanzania...Nchi ya Tanzania ina mikoa ishirini na sita na wakristo, waislamu na wapagani. Hivyo kila kitu ukiongelea unatakiwa kuweka takwimu ili kuona uiwiano. Mfano unasema hiyo mechi Simba na yanga. Kwa hesabu za asilimia ni sawa na watanzania wangapi hao mashabiki katika asilimia mia moja ya idadi wa watu wa Tanzania...

Kwa nini husijiulize Wabunge na Posho tena wengine hawaongei chochote kwa kipindi ya miaka mitano yote lakini posho wanakinga kama kawaida, Kashfa za ufisadi...Mfano ya Richmond ni pesa kiasi gani...Zinaweza kujenga maktaba ngapi?

Naona Bwana fadhili Mtanga mtazamo wako unaegemea zaidi katika kwenye matoke ya siyo chanzo cha matatizo. Muhimili wa maendeleo ya nchi na watu wake ni uchumi imara na unajengwa na siasa bora na viongozi ambao siyo wala rushwa.

Hivi sasa unasikia kuhusiana na visa vya ufisadi kila kikicha kutoka magazetini ya ndani ya nchi na nje ya nchi na vyombo vingine vya habari. Na huu uisadi tunauongelea ni mfumo ambao siyo ulianza jana ni kipindi kirefu tangu hujijenge pengine ni zaidi ya miongo minne iliyopita...Kwa sababu kumbuka kuwa adui wa maendeleo ya nchi ni RUSHWA...Na hivi sasa kwa maisha yetu sisi watanzania imekuwa sehemu ya maisha yetu kutoka ngazi kiongozi wa kijiji/kitongoji mpaka wa juu kabisa kila mahala ni pesa(RUSHWA).

MUHIMU MIMI NA WEWE TUSHIRIKIANE KATIKA KUONDOA HUO MFUMO DUME WA RUSHWA ILI TUWE NA UTAWALA WA SHERIA...AMBAO ITALETA UCHUMI IMARA NA MAENDELEO YA MTANZANIA ILI VITU VINGINE KAMA HIVYO UNAYOONGEA VYA WATU KWENYE UTAMADUNI WA KUJISOMEA VITAKUJA VYENYEWE.

Naona umeongelea suala la Magazeti ya udaku kwamba watanzania wanapenda kusoma hayo zaidi kuliko hard stories. Sasa unafikiri ukiwa una matatizo mengi kichwani nini kinaweza kukuliwaza kwa mtu maskini ni pombe na ngono na dniyo sababu unaoan watanzania wengi wasoma hizo habari hizo. Na nchi yenye walevi wengi maana yake ni watu waliokata tamaa hivyo unatakiwa kujua kwa nini wamekata tamaa nadhni hili pia Profesa Mbele ndiyo unatakiwa kuweka skills zako za kufanya utafiti hili tutambue siyo kutoa majibu kwa kuangalia tuu watu wanakunywa pombe...la asha ni kwa kuwauliza kwa nini wanakunywa pobe hata kwa
kipato kidogo wanachopata...Pia hata hizo nyumba chahe zinazojengwa jee haoa wataalamu wa michoro wanatoa huo ushari...Mambo mengi sana Bwana Mtanga na Profesa ya kujadili kuhusu.Profesa umesema utakuja Tanzania kuendesha mijadala lakini kumbuka uliandika kuwa itaendeshwa kwa kiingereza.

Na sisi watanzania(milioni arobaini) ambao ndiyo tuna tunaitumia kiswahili kma lugha yetu. Je tutawezaje kushiriki imeisha tuondoa

Fadhy Mtanga said...

Nimerudi tena.

Ahsante sana ndugu Katu kwa kuchangia maoni yangu. Umesema siifahamu vizuri Tanzania. Nakubaliana nawe. Maana eneo nililotolea mfano si sehemu ya Tanzania. Ngoja niseme hivi, kuifahamu Tanzania si kufika kila pahala pa nchi. Sehemu moja ama mbili tu zaweza kukupa mwanga wa upande mmoja wa nchi na sehemu nyingine kukupa mwanga wa upande mwingine.

Hoja ya msingi tunayoijadili hapa ni utamaduni wa kujisomea na kununua vitabu. Tukijadili ufisadi, nao una mjadala wake mpana maana siyo watu wote wanautazama kama litazamavyo jicho lako ama jicho langu.

Nimesema katika maoni yangu yaliyotangulia haya, Watanzania tu mafundi wa kutengeneza sababu lukuki za kwa nini hatuwezi kufanya jambo. Tukisema tunasoma magazeti ya udaku kwa kuwa tuna misongo ya mawazo vichwani mwetu kwa sababu ya mifumo mibovu ya utawala, tunajidanganya wenyewe. Hatuwezi kuwa na fikra pevu ati kwa sababu mafisadi wanakula tu pesa. Tunalewa na busara ya kale ya aliye juu mngoje chini.

Ndugu yangu Katu, nimeizungumzia Tanzania kwa kutoa mifano. Mi si mjuvi wa takwimu, ndiyo sababu nikasema najadili kutokana na upeo wangu. Nimesema jambo la dhahiri kabisa. Kama watanzania zaidi ya elfu thelathini na saba (sijui hawa ni asilimia ngapi ya Watz) wanao uwezo wa kutafuta kiingilio mpirani, basi naamini wanao uwezo wa kutafuta pesa ya kununulia vitabu.

Tanzania ninayoifahamu mimi, si vijijini, wala si mijini, kuna kundi kubwa la watu wanaotumia vipato vyao kwenye pombe na anasa zingine. Suala hili halihitaji takwimu za ukristu, uislamu ama upagani. Linahitaji mazingira halisi tunayoyaishi. Nadhani ni jambo lisilopendeza kama tutakuwa na utamaduni wa kuchangia harusi pesa nyingi sana, pombe na kuhonga wanawake, lakini tukija kwenye maendeleo ya usomaji vitabu tukasema, tunakatishwa tamaa na serikali na mafisadi hivyo wacha tuponde raha.

Tanzania nayoijua mimi, mtu anaweza kulipa kiingilio shilingi laki moja ya kwake na laki moja nyingine ya mpenzi wake ili kuingia Mlimani City Hall kutazama mashindano ya ulimbwende. Huyu ukitaka kujadili kuhusu vitabu, atasema wewe huijui Tanzania, Tanzania ina watu masikini sana (sijui lini Yesu atashuka kutuondolea huu umasikini ulio kiteteo cha kila jambo). Atasema tujadili ufisadi kwanza ndo kisha tuyatazame mambo hayo.

Kuamka kwa jamii ili iweze kupambana na ukandamizaji kunategemea maarifa kwa jamii hiyo. Kama tutajitanganya kwa kuona ni aheri tusome udaku kwa kuwa tunakatishwa tamaa na Richmond, Ticts na binamu zake, tutakuwa watu wa kubaki nyuma daima.

Tanzania ninayoifahamu mimi ugumu wa maisha hautokani na ukristu, uislamu ama upagani wa mtu. Kama tutaketi chini kusubiri malaika ama kina Zito waje watusemee kila siku nasi tuishie kuwapigia makofi, shauri letu. Kujisomea haimaanishi usome ili uajiriwe. Ina maanisha kupata uwezo wa kuyatawala mazingira yako.

Ndugu yangu, nimejadili pia namna maktaba zisivyotumika. Nimetoa mifano ya Tanzania ambayo bado wewe unaona siifahamu. Ngoja niseme hili, sasa naishi Dar es Salaam, marafiki wengi ninaowatembelea wana majumba makubwa, magari ya kifahari, samani kutoka Dubai, simu za gharama, manukato na vikorombezo hivyo vya bei ghali. Wana baa ndogo za nyumbani zikiwa zimejaa mvinyo wa kuanzia Dodoma hadi Utaliano. Lakini hawana hata kashelfu kadogo ka vitabu. Hawa ni Watz ambao nawafahamu ingawa mwenzangu wadhani siwafahamu.

Hawa pekee, ukijumlisha na wale wajazao uwanja wa taifa, (ndo uwezo wangu kitakwimu) wangeweza kutenga pesa kidogo tu kujinunulia vitabu, basi wangefaidisha kizazi hiki na kijacho. Hili suala la utamaduni wa vitabu nitalisema siku zote kwa sababu ninakerwa nalo sana.

Ndugu yangu Katu, tutasema mengi sana. Mimi naomba nisimamie hoja yangu hii, Watanzania tuna ubingwa wa kutengeneza sababu lukuki za kwanini hatuwezi kufanya jambo fulani, wakati tungehitaji sababu moja tu, ya kwanini tunaweza.

Ahsante sana kwa kunisoma.

Siku njema.

Katu said...

Fadhy Mtanga!

Kama umeelewa nilichosema kuhusiana na hizo chache unazozingumzia...Kumbuka nyumba yenyewe kabla ya kujengwa mjengaji anafuata wataalamu ili kujenga nyumba na michoro inatolewa...sasa tatizo hilo lina mlolongo mrefu sana siyo tu kwa wajengaji hata wachoraji pia. Na hao wanaojenga hizo nyumba pesa wamepataje...kama utafanya utafiti wa kina utakuja kugundua shule ama vyeti vya shule havichangii kupata hizo hivyo msingi ni huo huo...fedha za njia za mkato.....Kumbuka hiyo nchi unayozungumzia watu wake wanaishi chini dola moja Marekani kwa siku.

Kama unatumia Dar ndiyo chanzo chako maisha ya Watanzania basi utakuwa unapotoka katika mstari wa utafiti. Husikiri kila kinachotokea Mijini ndiyo maisha ya mjini yalivyo hata hapo Dar watu wanatofoutiana sana maisha..Mtu vingunguti na masaki ni tofauti kabisa...Manzese kwa mfuga mbwa na Mikocheni haya yote ni tofauti mzee....Mimi ndiyo naihi uswahilini nafahamu kwamba tunanunua suka kwa kijiko ili kunywa chai siyo sawa na hao unaosema wa Msasani tupo tofauti sana

Fadhy Mtanga said...

Ndugu Katu,
Mfano wangu kwenye maoni yangu ya pili ulikuwa ukizungumzia eneo la kijijini. Huko Lupembe ni kijijini kweli. Ambako nimesema kuna maktaba lakini hazina wahudhuriaji. Nikatoa mfano wa klabu tuliyoianzisha ambayo nayo haikudumu baada ya kuondoka kwetu.
Sijui unahitaji reference ya ukijijini kwa kiwango kipi kitakachokuridhisha.

Kwenye mfano wa pili nimezungumzia maisha ya Dar es Salaam. Tena hapa sijawazungumzia wenye umasikini bali wale wenye uwezo wa kumudu kuingia mpirani, na wale wenye majumba mazuri lakini hawana mwamko wa kununua wala kusoma vitabu.

Labda nifupishe hii mifano miwili kama ifuatavyo.

Moja, kijijini Lupembe ambako watu wake ni masikini, kuna maktaba mbili ambazo wala hawahudhurii kusoma vitabu vilivyomo. Hawa hawawezi kujitetea kwa kusema hawana uwezo wa kununua vitabu. Vitabu vipo, wao hawana mwamko wa kujisomea.

Mbili, jijini Dar es Salaam, kuna kundi la watu wanaomudu kwenda uwanjani kucheki mpira, kula gambe, kuhudhuria mashindano ya ulimbwende, kumiliki vitu vya kifahari. Hawa nao hawanunui vitabu. Nao hawawezi kujitetea kuwa hawana uwezo wa kununua vitabu. Uwezo wanao, ila hawana mwamko wa kujinunulia vitabu na machapisho.

Sidhani kama napaswa kusema zaidi ya nilivyosema kutetea hoja yangu.

Assalam Aleykum.

Katu said...

Fadhy Mtanga

unatakiwa kufahamu maisha ya watanzania yanaowakabili kwa undani na siyo kuangalia tuu nje. Starehe ni sehemu ya maisha kujipongeza hata kunguru wanafanya hivyo kwa kukuasanyika na kufurahia pamoja.

Matatizo ya mtanzania yapo kila kona, na tafdhali husiangalia kona moja tuu...hivi sasa hivi wewe unatumia computer kuwasialiana mimi natumia mobile phone kujibu hizo hoja zako.....

Nini kikifanyike ndiyo msingi wa kumkomboa mtanzania na siyo kualaumu tuu bila kujua kwamba watu kwa nini wanashindwa hayo unayona wewe ni tatizo.

Kwanza tunakiwa tupate viongozi wenye uzalendo na nchi yao, mtu ama taasisi inayojishughulisha na rushwa basi sheria ichukuhe mkondo wake na siyo kulindana na wale walioshiriki rushwa wawajibishwe bila kuzingatia nafasi yao ktk jamii....Imani ya wananchi itarudi na pia wananchi watweza kushiriki maendeleo hivi sasa nchi imesimama dede katika maendeleo....Kukosekana maji ya uahakika , na umeme ni seheu ya maisha mtanzania wakawaida...hivi karibuni Gazeti Nipashe lilotoa picha wanafunzi 200 na mwalimu mmoja darasani hipo KImara Temboni Dar es salaam tena cha kusikitisha zaidi hao wanafunzi wote walikuwa wamekti chini sakafuni kwa kukosa madawati....unafikiri hapo unamfanya mwanafunzi ambaye jioni yake hiyo anweza kuona wanafunzi wengine kutoka ktk luninga wakisoma na kukekti ktk viti vya uhakika....Shule inatakiwa iwe na mazingira ya shule na siyo mahala pa kunyonga watu.

Labda nikujulishe tuu, Mimi ni mkazi wa Kijiji cha Lungongole hapa Kikwawila- Ifakra...hivyo nafahamu maisha ya kijijini vizuri na hvi punde nitakwenda kuchota umbali wa maili moja ili niweze kutumia hapa nyumbani tena kutoka kwenye kisima kisischo salama..Je na wewe hupo wapi hivi sasa...ili niweze kujua kama naongea mwenzangu ama na mtu anayenikejeli!!!?

Fadhy Mtanga said...

Ndugu Katu,

Daima naitazama jamii kwa undani kabla sijaamua kuizungumzia. Niliitazama jamii ya kijijini kwa undani. Jamii zetu zina matatizo chungu mbovu yanayohitaji mijadala mirefu sana. Lakini kwa kuwa hoja inahusiana na vitabu, niliijadili kutokana na mada iliyopo mezani.

Mwenzangu una bahati sana, kwani pamoja na kuishi kijijini lakini umeweza kumudu kuwa na simu yenye intaneti. Hongera sana kwa hilo. Unanipa imani kuwa pengine kijiji chako ni moja ya vile vijiji wilayani Kilombero (yenye makao makuu kwenu Ifakara) vyenye kujivunia utajiri wa zao la mpunga. Ambapo baada ya mavuno vijana hulimbuka na mamilioni wayapatayo na kuyamalizia kwenye starehe kama pombe, wanawake, simu zenye memory card na bluetooth na pikipiki za kuweza kuwafikisha vijiji vingine kufuata nyamachoma, pombe na wanawake. Lakini mwisho wa siku tunaungana kulalamika 'sisi ni watu masikini.'

Niseme ukweli, nipo jijini Dar es Salaam. Nimeishi kijijini Kisaki, Morogoro vijijini kwa miaka miwili. Kwa muda huo, nimeweza kutembelea vijiji vingi vya wilaya ya Moro vijijini, Kilosa na kwenu Kilombero. Napafahamu Ifakara, na ukanda wake wote. Tena katika watu wanaopaswa kutopiga kelele kuwa ni masikini, basi ni watu wa Ifakara, na Kisaki na Mang'ula.

Pale Kisaki kwa mfano, kunalimwa mpunga na ufuta kwa kiwango kikubwa sana. Miezi ya Mei hadi Novemba ni miezi ya kufuru za vijana. Vijana wanashindana kuhonga, wanashindana kununua simu kali na mambo mengine. Ukifanya jambo la maendeleo kama kujenga nyumba nzuri unaonekana 'wa wapi huyu'

Mwaka 2008, nilipojifunza vijana wengi wanapoteza muda na pesa kwenye anasa, niliushauri uongozi wa kijiji, tushirikiane tuanzishe walau ligi ya futiboli na netiboli ya kata nzima ili vijana wawe mobilized wajifunze stadi za maisha. Matokeo yake nilipigwa majungu kuwa najifanya msomi niwaache wao 'boni hia hia' na maisha yao kwakuwa mimi ni 'wakuja'

Ndugu Katu, watu kama hawa watazidi kuilalamikia serikali kwa kila umasikini wao. Mwisho watasema hata malaria na typhoid vinaletwa na serikali. Mimi si shabiki wa serikali, lakini penye ukweli nitasema kwa yakini.

Ndugu Katu, nimeishi sana vijijini katika umri wangu huu mdogo, nilipenda daima kujifunza changamoto za watu wale. Nasema tena watu kama wa Kisaki ama Ifakara hawapaswi kulalamika, wana utajiri lakini hawataki kuutumia kwa matumizi chanya.

Fikiria mfano huu, mwaka juzi kijana mmoja kijijini Dakawa, Moro vijijini alishinda tuzo ya mkulima bora wa pamba Tanzania. Akaletewa wataalamu wamwendeleze na kumpa misaada. Lakini viongozi wa kijiji na wanakijiji wenzake ndiyo walikuwa watu wa kwanza kumfitini. Mwezi Machi nilikutana naye pale Msamvu stendi, Moro, amekata tamaa na kilimo cha pamba. Anataka kufanya mambo mengine.

Jaribu kufikiria, kama watu wale wangekuwa na utamaduni wa kujisomea, huoni kuwa baadhi ya tabia za kipuuzi wangekuwa wameondokana nazo kutokana na kukuza uelewa wao?

Ndugu Katu, ninayo mifano mingi sana ya vijijini. Nimefanya kazi vijijini kabisa mkoani Mbeya, Iringa, Moro na Pwani. Lakini nimesoma kijijini kabisa Kigonsera mkoani Ruvuma. Tunapozungumzia vijijini, nina uzoefu wa kutosha. Ngoja nikufahamishe, ninapenda sana kuandika mambo yote ninayojifunza katika jamii kwenye diaries zangu. Hivyo nina kumbukumbu za kimaandishi kuhusiana na mambo haya tunayoyajadili.

Ukweli utabaki kuwa ukweli. Watz hatupendi kujisomea. Hivyo ni wepesi wa kutengeneza sababu chungu mbovu za kwa nini hatupendi kujisomea. Tungehitaji sababu moja tu, ya kwa nini ni muhimu kujisomea.

Nadhani tunakwenda sawa ndugu yangu Katu.

Assalam aleykum.

Mbele said...

Ndugu Katu, ni kweli nilisema kuwa warsha zangu nitaziendesha kwa kiIngereza. Bofya hapa. Hii ni kwa sababu wahudhuriaji ni wa mataifa mbali mbali.

Kuna wa-Tanzania wengi wanaojua ki-Ingereza, na katika warsha zilizopita, wa-Tanzania wamekuwepo. Kwa hivi, nikisema nitaendesha warsha kwa ki-Ingereza haimaanishi kuwa ni kipingamizi kwa wa-Tanzania wote.

Halafu, masuala ninayotegemea kuongelea katika warsha hizi nimeyaandika kwa kiasi fulani katika kitabu nilichochapisha mwaka jana, kiitwacho CHANGAMOTO, ambacho kinapatikana mtandaoni. Bofya hapa.

Nitachukua nakala na kwenda nazo Tanzania, ili wale watakaohudhuria warsha waweze kununua, kwa ajili yao au kwa ajili ya wenzao ambao hawajui ki-Ingereza. Warsha zitafanyika kwa ki-Ingereza. Lakini je, hao wa-Tanzania wanaojua ki-Ingereza, hawawezi kuwaeleza wenzao baadaye kwa ki-Swahili?

Kama kweli wa-Tanzania wana uchungu na wenzao ambao hawajui ki-Ingereza, basi wanayo fursa ya kuthibitisha kama kweli wana uchungu huo au kama wanapiga siasa tu. Hili ni tatizo kubwa la wa-Tanzania.

Vile vile, wa-Tanzania wasiojua ki-Ingereza wanaweza kuwasiliana nami hata leo, kama wanataka kuletewa kitabu hiki, nami nitaleta. Wale wanaofurika kwenye minuso na mashindano ya urembo wakipunguza ulabu kidogo tu, watamudu kabisa gharama ya kitabu hiki.

Hayo nasema ingawa nafahamu fika kuwa tatizo la wa-Tanzania ni lile lile ambalo Ndugu Mtanga na mimi tunaelezea, kwamba hawana utamaduni wa kununua vitabu na kuvisoma.

Vitabu vyangu vimechapishwa mtandaoni, na vinaweza kununuliwa kwa kutumia "credit card." Siku chache zilizopita tumepata taarifa kuwa Exim Bank Tanzania imezindua hizo kadi. Hii inamaanisha kuwa walioko Tanzania na kadi hizi wanaweza kununua wenyewe kama vile wanavyoweza kununua bidhaa zingine. Hakuna kisingizio.

Vile vile, wa-Tanzania wa ughaibuni, huku Marekani, wanazo kadi hizi. Ingekuwa wana utamaduni wa kununua vitabu, wangeweza kuvinunua na kuwapelekea ndugu zao Tanzania.

Hakuna visingizio, lakini, kama Ndugu Mtanga anavyosema, wa-Tanzania ni wabunifu wakubwa wa visingizio.

Katu said...

Tena nimefurahi kusikia hiyo kitu credit card...nini hiyo ni pesa ama kitu gani.. Maana mimi hata amana ya benki sina sasa hivi vingine naona kama miujiza unaongea...Hicho kitabu cha changamoto kinagharimu kiasi gani!?.

Kumbuka kasoro mojawpo iliyotufanya tufikie hapa tulipo na matatizo haya mojawapo ni kusoma shule kwa kitabu kimoja tuu cha kiada ambacho mwalimu pekee ndiyo alikuwa anakitumia na sisi kusubiri kusimuliwa...

Sasa unaposema suala watanzania wanaongea hicho kiengereza wawasimulia wenzao siyo ndiyo pale pale Profesa Mbele kuendeleza kutokuwa wabunifu.!!!!!!!!

Mtanga sasa naona unasahau kwamba kilimo chetu kinategemea rehema za mwenyezi Mungu kama mvua itanyesha kwa jinsi tunavyotaka...Mfano msimu huu mimi katika ekari zangu 100 za mpunga nategemea kuvuna gunia mia mbili tuu. Hii ni sawa kutumia shilingi 5000 na kupata shilingi 100 kama pesa kamili na kuwa na hasara ya shilingi 4900....sasa sijui unachoengea kinaenda na duni hii ya sasa na hali ya hewa...Unategemea uongozi wa kijiji ndiyo uwezo kuleta kilimo cha umwagiliaji ni serikali kuu ndiyo ifanye!!

Fadhy Mtanga said...

Ndugu Katu,

Unajua unapojadili jambo na mtu yeyote ni vema kuwa na hakika na maelezo yako.

Nasikitika umesema uwongo juu ya ulimaji. Labda kama wewe utaniambia kuwa u mkulima wa aina ya peke yako. Unaponiambia kwa ekari zako 100 unategemea gunia 200 tu we si mkweli.

Zingatia nimekwambia nina uzoefu na maeneo unayodai unaishi. Kwa wastani, ekari moja inayotunzwa vizuri hutoa gunia kumi za mpunga. Lakini kama mvua itasumbua, zinaweza kupungua hadi sita ama tano. Jambo la kushangaza, mwaka huu ukanda wenu umepata mvua ya kuridhisha kabisa na maeneo ya Kilosa imeleta hadi mafuriko.

Nilikuwa huko hivi karibuni kufanya utafiti wa riwaya ninayotaka kuandika.

Halafu jambo jingine, kama una uwezo wa kuwa na ekari 100, wewe si mtu masikini hata kidogo. Kwani utalazimika kukodi trekta kulima. Utakodi vibarua wa kuhudumia ekari zako 100. Kumbe ndiyo sababu unamudu kuwa na simu ya kisasa yenye intaneti wakati wakazi wengi wa huko wanapenda simu za kichina zisizo na intaneti bali zenye muziki mnene.

Ndugu yangu, tunapojadili hoja, tunapaswa kuwa wakweli na wenye takwimu za kweli ili kutetea hoja zetu.

Nimesikitika kwa hilo, kuutumia muda wangu kujadili mada na mtu asiye na hakika na mambo yake.

Jioni njema.

Katu said...

Ndugu Mtanga wa jiji la Dar es salaam

Kilichotekea mvua nyingi na mafuriko zimeharibu mavuno yangu...wewe Mtanga hupo dar....angalia lugha unayotumia bila ku-abuse watu wanaoshriki mjadala.

Mimi kutoka kijijini Lungongole-Kikwawila -Ifakara

Fadhy Mtanga said...

Ndugu Katu,

Sikufikira kuwa naku-abuse wakati najieleza.

Tafadhali niwie radhi kwa hilo.

John Mwaipopo said...

fadhy mtanga pole na kazi ya kumpigia gitaa mbuzi. sikupitia hapa kwa profesa na nilipobahatika kupitia leo nimekuta kumbe kuna mjadala mnene, unene ambao sio wa lazima asilani. nimechukua zaidi ya saa moja kuyasoma maoni yoote nukta-kwa-nukta. kweli unaweza kumlazimisha punda kwenda mtoni lakini huwezi kumlazimisha kunywa maji.

pengine umetumia nguvu nyingi sana kumuelimisha ndugu katu. takwimu mlizozikosa ni mimi. huko sekondari nilikuwa mchawi wa kujisomea hasa novels. niliweza hata kujipatia vitabu kwa njia za hila ili nisome.

chuoni nikaendeleza wimbi hili la kusoma. sasa nikawa natakiwa nisome vitabu vinavyohusu shule yangu lakini pasi na kuacha hobi yangu ya kujisomea novels. hapa nikajifunza kununua vitabu pasi na kuacha njia zangu za kupatavitabu kwa hila. kwa hiyo unaona kuwa pamoja na kutokuwa na kipato chuoni, niliweza kusevu hizo hizo 2500 kununua vitabu (na vingine kukwapua kwa marafiki zangu na ndugu zangu waliokuwa hawavihitaji tena - ndio hila yenyewe hiyo)

njoo sasa maisha ya mimi mtaani. nikapata kazi na 'kazi ikanipata' nikaingia kweny jamii ya harusi, fasheni, ulabu, na vitu kama hivyo. kama haitoshi hamasa ya kusoma ikapungua sana. sasa nasoma kidogo sana ingawaje nina muda kuliko nilipokuwa sina muda huko shuleni na vyuoni. sasa sinunui vitabu kama ambavyo nilijitahidi kujinyima ili ninunue kitabu huko zamani, ingawaje sasa naweza kununua vitabu hata 10 kwa mwezi.

nilidhani lililokuwa linaongelewa hapa ni 'hamasa ya kusoma vitabu'. kumbe limegeuzwa na kuwa watanzania tu masikini. nikiwa 'masikini' shuleni nilinunua na kusoma vitabu.

maarifa huanzia kwenye kusoma. mathalaini ukitaka kukwamuka na huo umasikini unaweza kuamua kuwa mpishi. ili uwe mpishi uhahitaji kuwa na ujuzi. hapa utahitaji kufundishwa KWA KUTUMIA VITABU ama kujisomea KWA KUTUMIA VITABU.

ukitaka kuwa mkulima mzuri wa mpunga shurti ujiongezee elimu ambayo inapatikaka kwa kusoma na kjujisomea. ama umlipe mtaalamu akufundishe yale ALIYOJISOMEA KWENYE VITABU.

nadhani ifike wakati tuache kumtafuta mchawi wa matatizo hata madogomadogo. tuache kutafuta visingizio vya dini na umuhimu wa vitu visivyo muhimu kama pombe, harusi za diamond jubilee, maprado, simu za internet.

niliwahi kuwa na simu ya laki 3, bahati njema nilikaa nayo mwezi mmoja tu ikapotea. kuanzia hapo nina simu ya elfu 50 na nawasiliana na watu 'kama kawa'. kumbe ningeweza kununua simu sema ya laki moja na laki mbili nikanunua VITABU na kuwapelekea ndugu zangu kijijiji kajunjumele, kyela ili wajue kujikinga na mbu, ukimwi, nk. au wajue dunia inakwendaje. hawa ndio wengi wao hawawezi kumudu kununua vitabu. sidhani inafaa kuwatetea watu wenye uwezo wa kununua vitabu eti kwa kuwa wao wako 'katika nchi masikini' hivyo wanastahili kushauriwa kunywa pombe zaidi eti wausahau umasikini 'wa nchi yao' hapana.

Fadhy Mtanga said...

Kaka John nashukuru umeona kuwa tumetumia muda na nguvu nyingi isivyostahili.

Hakika nililazimika kukonsetreiti hapa baada ya kuona ndugu yangu anatumia hisia na si uhalisia kujadili hili jambo. Ndugu yangu akawa mwepesi wa kusema wenzake hawatumii takwimu ilhali yeye anatumia zisizo sahihi.

Lililonisikitisha zaidi, mwishoni alipoona anaelemewa akakimbilia kusema namu-abuse. Akasahau hata yeye alimu-abuse Prof Mbele kwa kutuhumu kuwa amesomea kodi za wananchi na kukimbilia Ulaya. Akani-abuse pia mimi mara kadhaa.

Ndiyo raha ya blog. Tunapata uwanja mpana wa majadiliano.

Nakushukuru sana Prof Mbele kwa kuleta mada kabambe kama hii.

Nakushukuru sana ndugu yangu Katu kwa kuutumia muda wako kubadilishana mawazo nami.

Wacha nami nijishukuru kwa kupata changamoto.

Kaka John, ndaga mwee!

Katu said...

Bwana Mtanga

Nilitegemea umeelewa na pia umeomba sahamani lakini naona unaendelea kusisitiza na kunihakikishia dharau yako juu yangu. Mimi naishi hapa kijijini. Na wewe wa Dar hivyo unafahamu vizuri kukutwa na majanga asilia hasa mafuriko mashambani

Mimi ndiye niliyepata hasara ya mavuno...wewe unaongea nadharia. Madhara ya mafuriko siyo lazima yafike kwenye makazi ya watu na ia hata pia mashamba na mazao yanaweza kuathiri na kupunguza mavuno.

Kuhusu kusomeswa kwa Profesa Mbele na kodi za watanzania yeye ameelewa ndiyo sababu ulimsikia nini alijibu kuhusu hili.

Wewe maneno yako ndani yake yanamajivuno kwa kumdharau mchangiaji mjadala ndiyo sababu nimeandika ni abuse.

Hivyo basi kila unapoandika angalia maneno na sentenso zako vizuri. Kutukana ama kumdharau mtu siyo lazima mpaka kumtemea mate ama kutamka matusi ya nguoni.

Mija Shija Sayi said...

Tabia ya kujisomea si rahisi hata kidogo. Ni ngumu kwa vile ni kitu kinachoupa ubongo challenge, na siku zote challenge huwa ni aina fulani ya usumbufu. Na ili uwe na uwezo wa kukabiliana na usumbufu au challenge za maisha ni lazima tangu utoto wako ujengwe hivyo, tabia ya mtu inatokana na msingi alioupata akiwa mtoto. Unapokuwa na msingi imara hali ya maisha haitakaa ikubadilishe hulka yako, utateteleka kidogo lakini bado hali ikiwa sawa unarudia katika tabia yako.

Ninachosema ni kwamba, Watanzania wa sasa hivi hatukulelewa katika msingi wa kupenda kujisomea na ndiyo maana inakuwa ngumu kuanza kuiingiza tabia hii sasa hivi wakati tumeshakomaa. Kama tungekuwa na msingi huu wa kujisomea hata umasikini wa aina gani ungekuja usingeweza kuibadili tabia, kwani tabia ni tabia.

Mimi huwa nasema ili tuweze kuibadili hali hii ni lazima tuanze kuwajenga watoto wetu leo ili wakue hivyo, halafu tutaona hata kama huo umasikini utakuwepo maana katika kujisomea huko, ndiko watakakogundua mbinu na maarifa mapya ya kuepukana na umasikini.

Naomba kuwasilisha.

Katu said...

Naomba sisi wachangiaji wachache tuwe-realistic katika kushiriki mjadala. Nikiwa na maana kwamba kwanza tutambue watumiaji wa hii huduma ya intanet ni wachache sana hasa africa na Tanzania kwa ujumla.

Mimi naona tunaposema kwamba watanzania ni wavivu wa kusoma vitabu. Naona kwa mfano tutakuwa tunahangaika kushughulikia na kukauka kwa jani moja katika mti wa Mninga ambao una matawi mengi tuu. Natarajai tuangalia haya mambo kwa kina sana jamani.

Maisha ya Watanzania walio wengi(milioni Arobaini) ni sawa na Mtu aliyeathirka na ugonjwa wa Ukimwi na kinga kupungua mwilini hivyo kupelekea kwa kila ugonjwa kinachomwandama kinatakiwa kutibiwa haraka iwezekanavyo ili isije kuwa sugu na kuhatarisha maisha ya muathiarika. Kifupi nachotaka kusema utamauni wa kusoama vitabu haupo walio wengi sisi watanzania ni kama ishara ndogo tuu ya chanzo kikuu cha matatizo.

Profesa Mbele na wachangiaji wengine, Naomba tuwe wawazi katika kujadili haya mambo bila kificho wala kuogopa kusema ukweli wa kiini cha matatizo.

Hii itakuwa sawa kumhudumia mgonjwa wa ukimwi kwa kila ugonjwa unaomshambulia bila kukubali na kuwajulisha watu wanamzunuka kiini cha huyu anayeumwa kuwa dhaifu kiafya.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...