Thursday, April 22, 2010

Kenya Yaondoa Vibali vya Kazi

Kuna taarifa kuwa Kenya inaondoa vibali vya kazi kwa raia wa Afrika Mashariki wanaotaka kufanya kazi Kenya. Bofya hapa. Sijui wa-Tanzania wanaipokeaje habari hii, lakini binafsi sishangai, kwani naifahamu Kenya kiasi fulani, na nafahamu kuwa wa-Kenya sio tu wamejiandaa kwa ushindani bali wanajiamini.

Tatizo liko upande wa wa-Tanzania. Kwa miaka mingi sana, labda kuanzia miaka ya themanini na kitu, wa-Tanzania wamekuwa na tabia ya kupuuzia elimu. Shuleni wanatafuta njia za mkato badala ya kusoma sana, ndani na nje ya yale yanafundishwa.

Wakishamaliza shule (ambayo ni dhana ya kipuuzi, kwani shule haimaliziki), wanaona kusoma ni kero. Sijui kuna wa-Tanzania wangapi wanaonunua vitabu na kuvisoma, au wanaoenda maktaba na kujisomea tu, au wana vitabu majumbani na wanavisoma, au wanashirikiana na watoto wao katika kusoma vitabu.

Binafsi, nimeandika kwa miaka mingi nikiwalalamikia wa-Tanzania kwa tabia hizo, na nimeelezea sana nilivyoona tofauti baina ya Tanzania na Kenya, tangu nilipoanza kutembelea Kenya, mwaka 1989.

Nimeelezea mara kwa mara kuwa hata huku ughaibuni, wa-Tanzania hawafanani na wenzetu wa nchi zingine za Afrika. Siwaoni wa-Tanzania kwenye tamasha za vitabu au kwenye maduka ya vitabu. Siwaoni wa-Tanzania wanaomiliki maduka ya vitabu au magazeti. Lakini wenzetu, kama vile wa-Kenya au Wanigeria, wamo katika shughuli hizi.

Watanzania ni wapenda ulabu na starehe, wawe Tanzania au ughaibuni. Hayo nimesema sana kwenye kumbi mbali mbali, na kwenye blogu zangu, na hata kwenye kitabu ambacho nimechapisha mwaka jana, kiitwacho CHANGAMOTO: Insha za Jamii

Sasa basi, katika huu utandawazi, ni wazi wa-Kenya wanajiamini zaidi na hawatishiki kama wanavyotishika wa-Tanzania. Wa-Kenya wamejiandaa zaidi kielimu na wanaweza kujieleza. Watanzania wengi wanawapeleka watoto wao kusoma Kenya, na wa-Kenya wanazidi kuchukua ajira hata nchini Tanzania. Kwa hali ilivyo, wataendelea kuchukua ajira, iwe ni kwao au kwetu, au sehemu nyingine duniani. Wa-Kenya wamejiandaa kiasi kwamba hata fursa za kufundisha ki-Swahili huku ughaibuni wanazichukua zaidi wao.

Wahenga walisema kuwa asiyefunzwa na mama yake, hufunzwa na ulimwengu. Ndio yatakayowapata wa-Tanzania, katika ulimwengu huu wa utandawazi.

Siku za karibuni nitakuwa Tanzania nikiendesha warsha kuhusu masuala ya aina hiyo. Warsha mbili nitafanyia Arusha, tarehe 3 Julai, na nyingine tarehe 10 Julai. Nilishawahi kutangaza katika blogu hii. Lakini, sina hakika kama ni wa-Tanzania wangapi watakaohudhuria. Ila nina hakika wageni watahudhuria, ili mradi wapate taarifa.

Mimi kama mwalimu, siwezi kumezea au kuendekeza uzembe kama huu walio nao wa-Tanzania, ambao wanatumia pesa nyingi sana kwenye sherehe na bia, lakini kununua kitabu cha shilingi elfu saba hawakubali, wala kutumia saa mbili kwa wiki wakisoma maktabani hawawazii, uzembe ambao unawafanya wawe wanatoa visingizio kila siku, au lawama kwa wengine, hasa serikali, wakati wao wenyewe hawawajibiki.

Kama nilivyogusia, hakuna jipya ambalo nimesema hapa juu, bali ni marudio ya yale ambaye nimekuwa nasema kwa muda mrefu, katika blogu hii na kwingineko.

2 comments:

Unknown said...

Asante mkuu. This is a nice article.

Tanzanians we need to change for the better. Kama sisi tumeshindwa, basi tufundishe au tuwezeshe watoto wetu. Kinyume na hapo, we are doomed for life.

Nawakilisha...

Mbele said...

Ndugu Ahmed, shukrani kwa ujumbe wako. Hayo ninayosema hayapendezi kabisa, lakini ukweli lazima usemwe, hata kama unaumiza.

Nikiwa ni m-Tanzania ambaye ninazunguka duniani, nina upeo mzuri wa kuona jinsi wa-Tanzania wanavyojichimbia kaburi na kujifunga kitanzi. Ni wajibu kuwaambia ukweli, ili waamke, wakitaka.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...