Sunday, October 31, 2010

Polisi Wajifunze Nidhamu, Wazingatie Haki

Mara kadhaa, hasa wakati wa kampeni za kisiasa na uchaguzi, tumeshuhudia vitendo vya polisi na vyombo vingine vya dola ambavyo vimechangia kuleta hofu miongoni mwa wananchi na pia kuvuruga amani.

Katika uchaguzi wa mwaka huu, vitendo hivi vimejitokeza tena, kama inavyoonekana katika video hii



Kwanza namsifu na kumshukuru huyu dada anayeongea katika video hii kwa kutuelezea hayo anayoelezea, kwa uwazi na kwa dhati. Nafikiri ametoa somo la maana sana, na nategemea wahusika watajirekebisha. Kama wahenga walivyosema, kosa si kufanya kosa, bali kurudia kosa.

Kwa upande mwingine, ni lazima niseme kuwa, kwa ujumla, kazi ya polisi si rahisi. Katika mazingira kama haya ya kampeni za siasa na uchaguzi, hali inaweza kuwa ngumu pia, kwa sababu ya ushindani mkubwa na pengine uhasama unaoweza kuwepo katika jamii. Kwa hivi, naamini kuwa polisi wanaweza kufanya maamuzi au vitendo kwa lengo la kulinda amani, kumbe ikawa vitendo vyao vikachangia kuharibika kwa amani.

Hata hivi, naamini kuwa polisi wakipata mafunzo zaidi wataweza kukwepa makosa ambayo si ya lazima. Kwa mfano, mwaka 2001, polisi walikiuka maadili ya kazi yao kule Visiwani, kwa kufanya umachinga kwa CCM. Matokeo yake ni kuwa Taifa letu lilipata aibu kimataifa, kutokana na CCM kuitumia polisi kwa manufaa yake, na polisi kujidhalilisha kwa kukubali kutumiwa namna hii. Kwa taarifa, soma hapa. Kosa la aina hii halina utetezi, kwani tunategemea polisi wawe wanaongozwa na sheria tu, na wawe wanalinda haki za raia wote.

Saturday, October 30, 2010

Mahojiano: JK na Wanahabari

Jana tangu asubuhi hadi leo mchana nilikuwa Chicago, katika mkutano. JK alifanya mahojiano yake na wanahabari jana hiyo hiyo. Leo nimeona yamewekwa katika blogu maarufu ya wavuti. Nami nimeyaweka hapa kwangu, nikitanguliza shukrani kwa Da Subi.




Thursday, October 28, 2010

Mgombea wa CCM Kufanya Mahojiano

Zikiwa zimebaki siku tatu tu hadi uchaguzi ufanyike nchini Tanzania, tumepata habari kuwa mgombea urais kwa tiketi ya CCM atafanya mahojiano na vyombo vya habari. Hii ni tofauti na msimamo wa CCM katika kipindi chote cha kampeni, ambapo wagombea wake walikuwa hawashiriki midahalo.

Wengi wetu tunafahamu kuwa midahalo, mahojiano, na kadhalika, ni mambo muhimu katika jamii inayothamini elimu. Sasa kwa nini CCM haikutambua hilo kabla? Tena CCM ni chama chenye wanachama milioni kadhaa, wakiwemo "wasomi" wengi.

Ni lazima niulize: hao ni wasomi kweli au ni wababaishaji? Ni aibu kuwa hawakuweza kuchangamka kabla na kutambua umuhimu wa midahalo, hadi saa hii ya mwisho, na baada ya Dr. Slaa kuonyesha mfano.

Mimi kama mwalimu, na pia raia ambaye si mwanachama wa chama chochote cha siasa, nawajibika kuwashutumu CCM kwa kutoonyesha mfano bora, pale walipotamba kuwa mgombea wao hahitaji kushiriki midahalo. Na pamoja na hayo, wagombea wao wote wakawa hawashiriki midahalo. Sijui kama ilikuwa ni fikra zao au ndio nidhamu ya chama. Kama ndio nidhamu ya chama, ni heri nibaki bila chama, kuliko kuwa katika himaya ya udikteta.

Narudia kuushutumu uamuzi wa kutoshiriki midahalo. Na hao wagombea wote nawashutumu kwa kutii amri isiyo na busara kama hiyo. Je, sasa, kwa vile JK ameamua kufanya mahojiano, nao watakimbilia kwenye vyombo vya habari kufanya mahojiano? Akili gani hiyo? Mimi kama mwalimu, lazima niulize: tunawafundisha nini watoto wetu, ambao ni taifa la kesho?

Baada ya kusema hayo, mimi kama raia mwema, ambaye si mwanachama wa chama chochote cha siasa, nina masuali kwa mgombea wa CCM. Kwa vile hakuna muda wa kuuliza yote, nitauliza matatu tu.

La kwanza ni kwa nini wale ambao Dr. Slaa amewataja katika orodha yake ya mafisadi hawajampeleka mahakamani hadi leo?

La pili ni je, kwa nini CCM inadai kuwa amani Tanzania inatokana na uongozi wa CCM, wakati CCM inashiriki kikamilifu katika kuhujumu amani, hasa nyakati za kampeni na uchaguzi? Mifano ni mingi, kuanzia Visiwani hadi Bara, na hata ripoti za kimataifa zinathibitisha hilo. Kwa mfano, soma hapa na pia angalia video hizi hapa.

Ukweli ni kitu muhimu sana. Je, CCM haitambui kuwa wanaotunza amani Tanzania kikweli kweli ni sisi mamilioni ya raia ambao si wanachama wa chama chochote cha siasa? Hatuna rekodi yoyote ya kuvuruga amani kama wenzetu wenye vyama wanavyofanya. Kwa nini CCM inafunika ukweli huo?

Suali la tatu ni je, CCM ina maelezo gani kuhusu shutuma alizotoa Mwalimu Nyerere dhidi ya CCM katika kitabu chake cha Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania? Kuzifahamu kwa ufupi shutuma hizi, soma hapa.

Tuesday, October 26, 2010

Mbumbumbu Waache Kugombea Uongozi

Kitu kimoja kinachonikera ni jinsi wakati wa kugombea uongozi, mbumbumbu wengi wanavyojitokeza kuwania uongozi. Halafu, kwa jinsi wapiga kura wengine walivyo mbumbumbu, wanawapigia kura hao mbumbumbu wenzao na kuwawezesha kushinda.

Baada ya hapo, kunakuwa na matatizo mengi. Tatizo moja kubwa ni jinsi hao mbumbumbu wanaoitwa viongozi wanavyojifanya miungu. Hawakubali kukosolewa.

Kwa mfano, gazeti likiwakosoa, wanalitishia au wanazuia lisichapishwe. Kama kuna kitabu kimewakosoa, wanakipiga marufuku. Msimamo wangu ni kuwa watu wasiojiamini au wasioheshimu uhuru wa watu kutoa fikra, wasigombee uongozi.

Nchi inahitaji viongozi wa kweli, ambao wanatambua kuwa wao si miungu, na ambao hawatetereki kwa kukosolewa. Kibaya zaidi ni kuwa hao mbumbumbu wanadhani kuwa wao ndio nchi. Wakikosolewa, wanasema ni hatari kwa usalama wa taifa. Ni usalama wa taifa au ni usalama wa mbumbumbu? Ni taifa gani ambalo linatetereka kwa sababu ya mbumbumbu kukosolewa?

Haya ninayosema nayasema kwa dhati. Mimi mwenyewe ninakosolewa na hata kutukanwa. Kwa mfano, soma hapa, na hapa.

Sioni sababu ya kuwazuia watu wanaofanya hivyo, hata kama ningekuwa kiongozi. Ni muhimu watu wawe huru kutoa mawazo yao. Ingawa tunasema kuwa tutumie lugha ya kuheshimiana, na mimi nakubali hivyo, lakini hatimaye nasema kuwa hata anayetukana anakuwa amepata fursa ya kujieleza. Ni bora iwe hivyo kuliko kuwafunga watu mdomo, kwani madhara ya kuwanyima watu fursa ya kujieleza yanaweza kuwa mazito. Nimefafanua zaidi msimamo wangu huo katika kitabu cha CHANGAMOTO.

Napenda kurudia, mbumbumbu waache kugombea uongozi. Nafasi hizi zinahitaji viongozi, si watu ambao hawajiamini.

Sunday, October 24, 2010

Video za Mdahalo wa Dr Slaa, ITV

Zimepatikana video za mdahalo wa Dr. Slaa katika ITV. Ni wazi kuwa Dr. Slaa ni mtu anayejua anachoongea, anayeijua nchi, anayewaheshimu wananchi, na anaipenda sana nchi yetu. Anafahamu vizuri nini anachotaka kifanyike ili kuinusuru na kuiendeleza nchi yetu. Ni muhimu kuwa na mtu wa aina hii, hata kama mnapishana mawazo. Nyerere alikuwa mtu wa aina hii hata kama baadhi walipishana naye mawazo.

Mimi kama msomi nimevutiwa sana na jinsi Dr. Slaa anavyoongea kwa kujiamini. Kwa hilo nalo amenikumbusha ya Mwalimu Nyerere, ambaye wakati mwingine alikuwa anatumbukia pale Chuo Kikuu Dar es Salaam ili kujibizana na wasomi masuali ya papo kwa papo. Nami nilikuwepo, kwanza kama mwanafunzi, na kisha kama mhadhiri. Mtu wa namna hii ananivutia sana.

Saturday, October 23, 2010

Mdahalo, ITV, Dr. Slaa

Mgombea urais kwa tiketi ya CHADEMA, Dr. Slaa, amefanya mdahalo ITV, kama ilivyotangazwa kwa siku kadhaa. Mimi kama mwalimu naiheshimu sana midahalo, kwani ni njia madhubuti ya kuelimishana, na katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi, ni njia madhubuti ya kuwaelewa wagombea. Namsifu Dr. Slaa kwa kujitokeza mbele ya umma namna hii, na nawashutumu wale wote ambao wamekataa kushiriki midahalo. Sikiliza mdahalo huu wa ITV na Dr. Slaa hapa:



Check this out on Chirbit

Mdahalo huu unaweza kuufuatilia pia na kupata taarifa nyingi zaidi hapa.

Friday, October 22, 2010

Mazungumzo Mjini Faribault Kuhusu Tamaduni, Oktoba 21

Jana jioni, kama nilikuwa mjini Faribault, kuongelea kitabu changu cha Africans and Americans, kama nilivyoandika juzi katika blogu hii. Matangazo yalikuwa yamewekwa sehemu mbali mbali, kama vile gazeti la Faribault Daily New na ukumbi wa Facebook. Wahudhuriaji walikuja kutoka Faribault na miji ya karibu. Wengine, ambao tumefahamiana Facebook, walikuja kutoka Minneapolis.


Nilianza kwa kuelezea kifupi, nilivyokuja Marekani mara ya kwanza, kusomea shahada ya uzamifu katika chuo kikuu cha Wisconsin-Madison, 1980-86, ndipo nikapata uzoefu wa kuishi katika utamaduni tofauti na wangu, na nikaanza kupata ufahamu wa yale niliyokuja baadaye kuyaandika katika kitabu cha Africans and Americans na kadhalika. Niliongelea jinsi tunavyojengeka katika utamaduni wetu na kuona utamaduni wetu ndio sahihi na wenye mantiki bora.

Kumbe, tukienda kwenye utamaduni wa wengine, tunaona mambo tofauti, na hii inaweza kuwa chanzo cha matatizo katika mahusiano yetu na watu wa utamaduni ule. Nilitaja mifano mingi kutokana na maisha yangu, uzoefu wangu wa kuangalia na kuchunguza matatizo duniani. Nilitoa mifano ya matatizo yanayotokea baina ya wa-Marekani na wa-Afrika, kwani ufahamu wangu uko zaidi upande huo.

Nilisisitiza, kama ninavyofanya daima, umuhimu wa kujielimisha, ili tujitambue na kuwafahamu wengine. Jukumu hili halikwepeki, na hakuna pa kukimbilia, kwani dunia inazidi kuwa kijiji. Watu wanatapakaa duniani kutoka tamaduni mbali mbali. Si miji ya Marekani tu ambao inakumbana na suala la kuingiliwa na watu kutoka sehemu zingine za dunia, bali hata Afrika ni hivyo hivyo. Miji kama Dar es Salaam, kwa mfano, inaendelea kuwa na watu kutoka mbali, kama vile China, na hivi kuwa changamoto katika suala la kumudu tofauti za tamaduni. Bila juhudi ya kujielimisha na kuelimishana tunajitakia matatizo.
Baada ya mazungumzo yangu na kipindi cha masuali na majibu, watu walipata fursa ya kuviangalia au kuvinunua vitabu vyangu, kama ilivyopangwa kwenye ratiba.






Huyu mama mwenye shati jeupe alikuwa mfanyakazi katika chuo cha St. Olaf, ambapo nafundisha. Nilimkuta hapo ila alistaafu miaka kadhaa iliyopita. Ni mwenyeji wa Faribault na ni mmoja wa mashabiki wangu wakubwa.





Shughuli nzima ilikuwa ya mafanikio mazuri. Kila mtu alifurahi, na waandaaji waliwahimiza waliokuwepo kuandaa mazungumzo ya aina hii sehemu zao za kazi.

Mmoja wa waliohudhuria ni Bwana Milo Larson, mwenyekiti wa Faribault Diversity Coalition. Leo ameandika kwenye ukumbi wa Facebook kuhusu mazungumzo yangu:

Great Forum by Joseph Mbele last night at the Library, always learn something new about the different cultures whenever I hear him. Everybody should see him just once, would be a more harmonious place
.

Monday, October 18, 2010

Nataongelea Kitabu Changu Faribault, Minnesota, Oktoba 21

Tarehe 21 Oktoba nitakwenda Faribault, Minnesota, kuongelea kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences. Nimealikwa na uongozi wa Maktaba ya Faribault kwa kushirikiana na mji wa Faribault.

Nimeshatembelea Faribault mara kadhaa, kutoa mihadhara na kushiriki shughuli zinazohusu elimu kwa jamii na hata kusuluhisha migogoro inayotokana na tofauti ya tamaduni, kama inavyoelezwa hapa na hapa.

Kwa hapa Marekani, ni jambo la kawaida kuwaita waandishi kuongelea vitabu vyao. Huwa ni fursa ya kukutana ana kwa ana na mwandishi, kuuliza masuali, na kununua vitabu.

Kitu kimoja kinachowavutia sana wa-Marekani ni kununua kitabu wakati huo na kumpa mwandishi aandike jina lake na pia ujumbe kwenye nakala ya kitabu hicho.

Wengine wananunua vitabu kadhaa, halafu wanapokuja kuwekewa sahihi, inabidi wakuambie uandike jina la nani, kwani wanawanunulia pia marafiki, watoto, au ndugu wengine. Ni mila ambayo iko ndani kabisa ya mioyo ya wa-Marekani. Wanaona furaha, kama inavyoonekana kwenye picha hii hapa, ambayo ilipigwa karibu na Grantsburg, Wisconsin, nikiwa naweka hizo sahihi vitabuni.

Kuhusu shughuli ya hiyo tarehe 21 Oktoba mjini Faribault, Mama Delane James, mkurugenzi wa maktaba ya Faribault, ameandika mwaliko huu katika ukumbi wa Facebook:


Dear Friends:

I hope you will be able to join us in the Great Hall at 6:30 p.m. as St. Olaf Professor Mbele speaks about his book, Africans and American: Embracing Cultural Differences.

Professor Mbele visited with our library staff last spring and we all agree... he is incredible! We are thrilled to be hosting this event and hope you can make it!

--Delane


Saturday, October 16, 2010

Maonesho ya Vitabu Minneapolis, Oktoba 16

Nimerejea jioni hii kutoka Minneapolis, kushiriki maonesho ya vitabu ambayo huandaliwa na jarida la Rain Taxi na kufanyika mara moja kwa mwaka.





Kama kawaida, nilipeleka vitabu vyangu. Nilikuwa nimelipia meza ndogo. Lakini hii ilitosha kwa vitabu tu, bila maandishi mengine. Kwa vile idadi ya vitabu vyangu si ile ile ya mwaka jana au mwaka juzi, siku zijazo itanilazimu kulipia meza kubwa ili niweze kuweka maandishi mengine pia.








Leo ninaleta hapa picha mbali mbali nilizopiga, kama mfano wa namna wa-Marekani wanavyojali suala la vitabu.








Kama nilivyosema siku zilizopita, wa-Marekani wanafurika kwenye maonesho ya vitabu. Wanafika tangu asubuhi, milango ya ukumbi inapofunguliwa. Na siku nzima watu wanakuwa wengi katika ukumbi, wakienda na kuja.







Wanafika watu wa kila rika: watoto, vijana, watu wazima, na waze, wanawake kwa wanaume.







Pamoja na hali ya uchumi wa Marekani kuwa mbaya miaka hii, watu wanavichambua vitabu na kuvinunua.







Wana dukuduku na hamu ya kusoma. Ukisikiliza maongezi yao, utawasikia wakiongelea sifa walizosikia kwa wenzao kuhusu kitabu hiki au kile. Au utawasikia wale waliosoma kitabu fulani wakiwaeleza wenzao na kuwahamasisha wanunue.



Mimi kama m-Tanzania ninashinda kwenye shughuli hizi nikiwa na masikitiko makubwa, kwani hali kama hii haiko Tanzania. Ninajua, kwa sababu ninashiriki maonesho ya vitabu kule, kama ninavyoripoti mara kwa mara katika blogu hii.






Ni wazi kuwa wa-Tanzania tumeshajichimbia kaburi katika dunia hii inayoendeshwa na elimu, ujuzi na maarifa. Tusijidanganye.







Kwa mtazamo wangu, dalili ya kuelimika ni kuwa na duku duku na hamu ya kudumu ya kujitafutia elimu. Shule inapaswa iwe ni chanzo tu na kichocheo cha duku duku na hamu hii ya kujitafutia elimu.






Kupata digirii, kwa mfano, si mwisho wa elimu, bali hatua moja au chachu katika safari ya kutafuta elimu. Hayo niliyaelezea pia katika mahojiano katika Kombolela Show.


Kama ninavyosema mara kwa mara, napenda sana kushirikia maonesho ya aina hii, kwani ni fursa ya kukutana na watu walio katika fani za uandishi, uchapishaji, uhariri na uuzaji wa vitabu. Kila mmoja wao ana jambo la kunichangamsha akili au kunipanua mawazo.




Kukutana na watu wanaotaka kununua vitabu ni jambo jingine linalonigusa. Wakati mwingi natumia kujibu maulizo ya watu wanaotaka kujua maandishi yangu yanahusu nini.



Watu wengi wanapoona kuwa natoka Afrika, wanapenda kuelezea vipengele vya maisha yao. Kama walishafika Tanzania au sehemu yoyote ya Afrika, wanaelezea. Kwa maana hiyo, kushiriki tamasha la vitabu ni kweli fursa ya kuonana na kufahamiana na watu wa aina mbali mbali.

Wednesday, October 6, 2010

Vitabu Vyangu Kwa Bei Nafuu

Lulu.com, ambako nachapisha vitabu vyangu, kumetokea tangazo linalotoa fursa kwa mwandishi kupunguza bei ya vitabu vyake akipenda.

Kwa heshima ya wasomaji wangu, nimeamua kutumia fursa hiyo. Nimepunguza bei ya vitabu vyangu vyote kwa mwezi huu Oktoba.

Vitabu hivi vimetajwa hapo kulia na pia hapa. Bofya sehemu ya kununulia, ili kuona punguzo hilo.

Wale ambao hawanunui vitu mtandaoni na wanavihitaji vitabu hivi wanaweza kuwasiliana nami kwa barua pepe: info@africonexion.com.

Siku ya mwisho ya punguzo hili ni Oktoba 31.

Chukua Chako Mapema

Pale CCM ilipoanzishwa, baadhi ya wa-Tanzania walianzisha minong'ono wakitafsiri CCM kama "Chukua Chako Mapema."

Nilitaja jambo hilo katika makala fupi, "Jokes Play Social Role," ambayo ilichapishwa katika gazeti la Daily News (Tanzania) (Juni 16, 1987) ukurasa 4.

Ni miaka mingi imepita, na ushahidi wa nini hasa maana ya CCM umeendelea kujitokeza. Tumsikilize katibu mkuu wa CCM:

Monday, October 4, 2010

Mahojiano Yangu "Kombolela Show"

Tarehe 2 Oktoba, nilihojiwa katika "Kombolela Show." Hiki ni kipindi cha redio kinachoendeshwa na Jaduong Metty, ambaye pia ni mmiliki wa blog ya Metty's Reflections. Kusikiliza mahojiano, bofya hapa au hapa

Friday, October 1, 2010

Mwalimu Nyerere Aliongelea Uozo Katika CCM

Mwalimu Nyerere aliongelea uozo katika CCM. Kwa mfano, wakati alipokuwa anajiandaa kung'atuka uenyekiti wa CCM, alizunguka nchi nzima akikagua uhai wa CCM. Wakati wa ziara hiyo, inaonekana Mwalimu alitatizwa na yale aliyoyaona. Aliwahi kusema kuwa kuna watu ndani ya CCM ambao hata mtihani juu ya Azimio la Arusha hawawezi kupasi.

Mwaka 1993 Mwalimu alichapisha kitabu kiitwacho Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania (Harare: Zimbabwe Publishing House, 1993). Pamoja na mambo mengine katika kitabu hiki, Mwalimu alisema kuwa kuna kansa katika uongozi wa CCM. Nanukuu baadhi ya maneno yake:

Chama cha Mapinduzi, kwa sababu ya uzito wa historia yake, hadhi ya jina lake, mfumo wa wavu wake, mazoea ya watu, na ubovu wa Vyama vya Upinzani, kinaweza kuchaguliwa na Watanzania, pamoja na kansa ya uongozi wake. Au watu wanaweza wakachoka, wakasema, "potelea mbali:" wakachagua Chama cho chote, ilimradi tu watokane na kansa ya uongozi wa CCM. Hainifurahishi kuyasema haya, lakini uhai wa Nchi yetu unataka yasemwe
. (Ukurasa 61)

Mwalimu hakuishia hapo, bali aliongezea namna hii:

Nilisema awali kwamba kansa ya uongozi ndani ya Chama cha Mapinduzi isingekuwa ni jambo la kutisha sana kama tungekuwa tumeanza kuona Chama kizuri cha upinzani kinachoweza kuiongoza Nchi yetu badala ya CCM. Ubovu wa uongozi ndani ya CCM ndio uliofanya nikapendekeza tuanzishe mfumo wa Vyama Vingi. Nilitumaini kuwa tunaweza kupata Chama kingine kizuri ambacho kingeweza kuiongoza Nchi yetu badala ya CCM; au ambacho kingekilazimisha Chama cha Mapinduzi kusafisha uongozi wake, kwa kuhofia kuwa bila kufanya hivyo kitashindwa katika uchaguzi ujao. Lakini bado sijakiona Chama makini cha upinzani; na wala dalili zo zote za kuondoa kansa ya uongozi ndani ya CCM. Bila upinzani mzuri wa nje, na bila demokrasia halisi ndani ya Chama cha Mapinduzi, Chama hiki kitazidi kudidimia chini ya uzito wa uongozi mbovu. Kwa hali yetu ya kisiasa ilivyo nchini hili si jambo la kutarajia bila hofu na wasi wasi! (Ukurasa 66)

Mwalimu Nyerere aliongelea hayo miaka yapata ishirini iliyopita. Leo hali ikoje? Kwa mtazamo wangu, uozo aliosemea Mwalimu umeongezeka. Hayo yamekuwa mawazo yangu tangu zamani. Kwa mfano, soma hapa.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...