Sunday, October 31, 2010

Polisi Wajifunze Nidhamu, Wazingatie Haki

Mara kadhaa, hasa wakati wa kampeni za kisiasa na uchaguzi, tumeshuhudia vitendo vya polisi na vyombo vingine vya dola ambavyo vimechangia kuleta hofu miongoni mwa wananchi na pia kuvuruga amani.

Katika uchaguzi wa mwaka huu, vitendo hivi vimejitokeza tena, kama inavyoonekana katika video hii



Kwanza namsifu na kumshukuru huyu dada anayeongea katika video hii kwa kutuelezea hayo anayoelezea, kwa uwazi na kwa dhati. Nafikiri ametoa somo la maana sana, na nategemea wahusika watajirekebisha. Kama wahenga walivyosema, kosa si kufanya kosa, bali kurudia kosa.

Kwa upande mwingine, ni lazima niseme kuwa, kwa ujumla, kazi ya polisi si rahisi. Katika mazingira kama haya ya kampeni za siasa na uchaguzi, hali inaweza kuwa ngumu pia, kwa sababu ya ushindani mkubwa na pengine uhasama unaoweza kuwepo katika jamii. Kwa hivi, naamini kuwa polisi wanaweza kufanya maamuzi au vitendo kwa lengo la kulinda amani, kumbe ikawa vitendo vyao vikachangia kuharibika kwa amani.

Hata hivi, naamini kuwa polisi wakipata mafunzo zaidi wataweza kukwepa makosa ambayo si ya lazima. Kwa mfano, mwaka 2001, polisi walikiuka maadili ya kazi yao kule Visiwani, kwa kufanya umachinga kwa CCM. Matokeo yake ni kuwa Taifa letu lilipata aibu kimataifa, kutokana na CCM kuitumia polisi kwa manufaa yake, na polisi kujidhalilisha kwa kukubali kutumiwa namna hii. Kwa taarifa, soma hapa. Kosa la aina hii halina utetezi, kwani tunategemea polisi wawe wanaongozwa na sheria tu, na wawe wanalinda haki za raia wote.

2 comments:

emuthree said...

Kuna jamaa yangu alisema yeye hatamruhusu mtoto wake afanye kazi ya upolisi, kwani itafika muda wanadai haki zao , na mwanae ni polisi, sasa wakipewa amri ya piga, atampiga na yeye hata kama ni mzazi wake...`nitamwachia laana bure' sikubali kabisa kazi hii!
Ajabu. lakini sio kweli kuwa kazi ya polisi ni mbaya kiasi hicho, hii ni kazi kama kazi nyingine, tofauti hapa kwetu elimu ya uraia haipo. askari wetu wamachukuliwa kindugu naizesheni, elimu ya usalama wa raia kwake ni hadithi za elifu-lela ulela!

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Jeshi letu la polisi linasumbuliwa na ujinga na usaliti. Mbona wao wana maisha mabaya ukiachia mbali kutegemea jinai ya rushwa? Wakati wa kuwa na jeshi lenye nidhamu ya mbwa umepita.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...