Sunday, October 24, 2010

Video za Mdahalo wa Dr Slaa, ITV

Zimepatikana video za mdahalo wa Dr. Slaa katika ITV. Ni wazi kuwa Dr. Slaa ni mtu anayejua anachoongea, anayeijua nchi, anayewaheshimu wananchi, na anaipenda sana nchi yetu. Anafahamu vizuri nini anachotaka kifanyike ili kuinusuru na kuiendeleza nchi yetu. Ni muhimu kuwa na mtu wa aina hii, hata kama mnapishana mawazo. Nyerere alikuwa mtu wa aina hii hata kama baadhi walipishana naye mawazo.

Mimi kama msomi nimevutiwa sana na jinsi Dr. Slaa anavyoongea kwa kujiamini. Kwa hilo nalo amenikumbusha ya Mwalimu Nyerere, ambaye wakati mwingine alikuwa anatumbukia pale Chuo Kikuu Dar es Salaam ili kujibizana na wasomi masuali ya papo kwa papo. Nami nilikuwepo, kwanza kama mwanafunzi, na kisha kama mhadhiri. Mtu wa namna hii ananivutia sana.

5 comments:

malkiory said...

Asante sana Prof. Mbele kwa video na audio ulizotuwekea kweny blogu yako.

Mbele said...

Mheshimiwa Matiya, shukrani. Kwa kweli huyu mgombea amenivutia sana, kwani mimi naheshimu sana midahalo na elimu kwa ujumla.

Nikitoa mfano moja tu, ni kwamba anavyoongelea hali duni ya elimu nchini na jinsi hali hii inavyoiangamiza nchi, ni sawa kabisa na ninavyoongea tena na tena kwenye blogu zangu. Amenigusa sana.

Huyu Dr. Slaa ni hazina kubwa kwa Taifa. Na nasema hivi nikiwa ni raia ambaye si mwanachama wa chama chochote cha siasa.

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Kama si uzembe, ujinga hata ushabiki wa kibubusa, hapakuwa na haja ya kutomchagua Dk Slaa. Tofauti na Kikwete, anajua anachopaswa kufanya na kwa namna gani. Si msanii wala fisadi wala kihiyo kama hao wengine.
Si mtoa rushwa wala hayuko mikononi mwa mafisadi ingawa wachache kama Sabodo wameanza kuinyemelea CHADEMA.
CCM imeisha na kuishiwa kiasi cha kuhitajika kuzikwa na si kupumzishwa. Imeporwa na mafisadi mchana kweupe na Kikwete kwa kibri na urushi anazidi kuwapigia hata debe. Hata hivyo tusimlaumu kwa hili kwa vile naye alitajwa kwenye list of shame ya Slaa na hakukanusha. Hii maana yake ni kweli na ndiyo maana Slaa amekuwa akimkumbusha kumkamata au kumfikisha mahakamani na asifanye hivyo.

emuthree said...

Twashukuru kwa taarifa na video hizo! Kwani siasa pamoja na matendo, lakini `talatala' ni muhimu sana. Kuonyesha `nini dhamira yako' na jinsi gani utakavyopambana na changamoto za watu! Sasa kumbukumbu hizi ni muhimu sana kwa wanataaluma, wachambuzi nk

Mbele said...

Mimi nangojea hao wanaompinga Dr. Slaa wajitokeze nao wajieleze, sio kupiga kelele wakati wamejificha msituni.

Kama ni mgombea wa CCM, nataka wafafanue masuala ya ufisadi, na pia waongelee shutuma alizotoa Mwalimu Nyerere dhidi ya CCM, kama nilivyogusia hapa.

Mimi kama raia ambaye si mwanachama wa chama chochote cha siasa nitaziweka video zao kwenye hii blogu, kwani naamini umuhimu wa midahalo. Kama nilivyokwishasema, nawashutumu vikali wote wanaotoroka midahalo.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...