Friday, October 22, 2010

Mazungumzo Mjini Faribault Kuhusu Tamaduni, Oktoba 21

Jana jioni, kama nilikuwa mjini Faribault, kuongelea kitabu changu cha Africans and Americans, kama nilivyoandika juzi katika blogu hii. Matangazo yalikuwa yamewekwa sehemu mbali mbali, kama vile gazeti la Faribault Daily New na ukumbi wa Facebook. Wahudhuriaji walikuja kutoka Faribault na miji ya karibu. Wengine, ambao tumefahamiana Facebook, walikuja kutoka Minneapolis.


Nilianza kwa kuelezea kifupi, nilivyokuja Marekani mara ya kwanza, kusomea shahada ya uzamifu katika chuo kikuu cha Wisconsin-Madison, 1980-86, ndipo nikapata uzoefu wa kuishi katika utamaduni tofauti na wangu, na nikaanza kupata ufahamu wa yale niliyokuja baadaye kuyaandika katika kitabu cha Africans and Americans na kadhalika. Niliongelea jinsi tunavyojengeka katika utamaduni wetu na kuona utamaduni wetu ndio sahihi na wenye mantiki bora.

Kumbe, tukienda kwenye utamaduni wa wengine, tunaona mambo tofauti, na hii inaweza kuwa chanzo cha matatizo katika mahusiano yetu na watu wa utamaduni ule. Nilitaja mifano mingi kutokana na maisha yangu, uzoefu wangu wa kuangalia na kuchunguza matatizo duniani. Nilitoa mifano ya matatizo yanayotokea baina ya wa-Marekani na wa-Afrika, kwani ufahamu wangu uko zaidi upande huo.

Nilisisitiza, kama ninavyofanya daima, umuhimu wa kujielimisha, ili tujitambue na kuwafahamu wengine. Jukumu hili halikwepeki, na hakuna pa kukimbilia, kwani dunia inazidi kuwa kijiji. Watu wanatapakaa duniani kutoka tamaduni mbali mbali. Si miji ya Marekani tu ambao inakumbana na suala la kuingiliwa na watu kutoka sehemu zingine za dunia, bali hata Afrika ni hivyo hivyo. Miji kama Dar es Salaam, kwa mfano, inaendelea kuwa na watu kutoka mbali, kama vile China, na hivi kuwa changamoto katika suala la kumudu tofauti za tamaduni. Bila juhudi ya kujielimisha na kuelimishana tunajitakia matatizo.
Baada ya mazungumzo yangu na kipindi cha masuali na majibu, watu walipata fursa ya kuviangalia au kuvinunua vitabu vyangu, kama ilivyopangwa kwenye ratiba.






Huyu mama mwenye shati jeupe alikuwa mfanyakazi katika chuo cha St. Olaf, ambapo nafundisha. Nilimkuta hapo ila alistaafu miaka kadhaa iliyopita. Ni mwenyeji wa Faribault na ni mmoja wa mashabiki wangu wakubwa.





Shughuli nzima ilikuwa ya mafanikio mazuri. Kila mtu alifurahi, na waandaaji waliwahimiza waliokuwepo kuandaa mazungumzo ya aina hii sehemu zao za kazi.

Mmoja wa waliohudhuria ni Bwana Milo Larson, mwenyekiti wa Faribault Diversity Coalition. Leo ameandika kwenye ukumbi wa Facebook kuhusu mazungumzo yangu:

Great Forum by Joseph Mbele last night at the Library, always learn something new about the different cultures whenever I hear him. Everybody should see him just once, would be a more harmonious place
.

7 comments:

Simon Kitururu said...

Asante kwa taarifa Mkuu!

Ila nanukuu``Kumbe, tukienda kwenye utamaduni wa wengine, tunaona mambo tofauti, na hii inaweza kuwa chanzo cha matatizo katika mahusiano yetu na watu wa utamaduni ule´´- mwisho wa nukuu.

Naaminimi kuwa :``Kumbe tukienda kwenye utamaduni wa wengine, tunaona mambo tofauti, na hii inaweza kuwa chanzo cha matatizo kaitak mahusiano yetu na watu wa utamaduni wetu´´ - ni moja ya kauzoefu kangu kadogo uchochoroni.:-(

Natamani mambo unayofanya huko MWALIMU,...
....yangekuwa rahisi kuyafanya BONGO.

Si unajua WASOMI BONGO wakishapasi mtihani vitabu havinogi?:-(

Simon Kitururu said...

Profesa samahani :``....chanzo cha matatizo kaitak...´´ kaitak ilikuwa niandike ``...katika ..´´ katika hiyo sentensi.

Na samahani PAMOJA NA KUSTUKIA MAPYA niko kwenye Blogu yako usiku huu ila niko ZAIDI katika atiko ulizoanzanazo zaidi au ulizoandika zamani.:-(

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Bravo kaka Mbele. Umekuwa balozi mzuri wa Afrika hapa Marekani. Wasomi wetu wengi wanakwepa jukumu hili na kujibebesha mizigo ya kujikana bila kujua madhara yatokanayo na ujuha huu.

Hata watawala wetu wanapokuja huku huwa hawajishughulishi na kueleza chanzo cha matatizo yetu hasa utamaduni badala yake huwa bize kufanya shopping na kuomba omba ili wakaibe kwa kuwatumia maskini waliowatengeneza kule nyumbani.

Diversity na jinsi ya kuihimili ni suala linalopasua vichwa kwa sasa kule Ulaya tokana na kuzaliwa upya chuki dhidi ya wageni. Sweden kwa sasa inazizima na mashambulizi dhidi ya wageni yanayofanywa na mlenga shabaha ambaye hajatiwa nguvuni. Juzi tu Kansela wa Ujerumani Angela Merkel alikiri kuwa Multicultural existance au Multikulti imeshindikana nchini mwake.
Uarabuni ndiyo usiseme. Waswahili na wafilipino wengi hasa wafanyakazi wa ndani wananyanyaswa hata kuuawa na hakuna anayechukua hatua!
Tunahitaji kuanzisha somo la Diversity kwenye mitaala yetu kutokana na utandawazi na utandawizi.

Simon Kitururu said...

Mkuu Mhango umemaliza. Nilimtafuta mpaka Yasinta mutoto ambaye yuko Sweden jana hasa inavyozidi kuwa kuna mtu anapiga risasi watu. CHa kushangaza wakati nimempata Yasinta kwenye simu yeye wala hakuwa anatishika na swala hata nilipo sema kuwa inasemekana kutakuwa na Makopikati.
Nilijifunza kitu lakini kwa hilo.:-(

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Hili si suala la kupuuzia ingawa baadhi ya watu wanaweza kujiona kama hawahusiki kiasi cha kutojishughulisha na tishio hili wala kuhofu. You nary know when and how this/these criminal/criminals will strike. Hata kama wao hawatishiki, wenzao (wageni) waliokwishaathirika huenda walidhani hivyo.

Mzee wa Changamoto said...

Mliotangulia ni WAALIMU TOSHA.
Nashukuru kwa maoni yenu hasa Mwl N.N Mhango.
Blessings

Mbele said...

Waandaaji wa mazungumzo yangu wameweka picha za mazungumzo hayo hapa.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...