Sunday, January 30, 2011

TAMKO LA JUMUIA NA TAASISI ZA KIISLAM JIJINI MWANZA

Nimeona tamko hili nikaamua kuliweka katika blogu yangu, kwa vile ninaheshimu uhuru na haki ya watu kujieleza. Mimi ni m-Katoliki, na ingawa sikubaliani na kila kilichomo katika tamko hili, nimeona lina mengi ya kufikirisha, kwa manufaa ya Taifa letu. Hatuwezi kukwepa ukweli kwamba ni Taifa la watu wa imani mbali mbali na mitazamo mbali mbali, na kwa hivi, pamoja na tofauti zetu, lazima tutafute namna ya kuishi pamoja kwa maelewano. Hatua moja ni kusikiliza maoni ya kila mtu, kwa utulivu na kuheshimiana. Ndio maana nachangia kueneza tamko hili.

---------------------------------------------------------------------------------------

TAMKO LA JUMUIYA NA TAASISI ZA KIISLAMU JIJINI MWANZA KUHUSU HALI YA KISIASA, KAULI ZA MAASKOFU, NA MUSTAKBALI WA NCHI LILILOTOLEWA JUMAPILI TAREHE 23 JANUARI, 2011 KATIKA VIWANJA VYA SHULE YA MSINGI MBUGANI (MUSLIM SCHOOL), JIJINI MWANZA
UTANGUZI:

Mwaka 2010 ulikuwa mwaka wa Uchaguzi wa viongozi wa ngazi mbali mbali wakiwemo madiwani, wabunge, wawakilishi, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Zanzibar.

Kabla ya Uchaguzi huo, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), kupitia Idara yake ya Kichungaji ya Tume ya Haki na Amani, lilitoa Waraka wa Kichungaji lililouita "MPANGO WA KUHAMASISHA HUDUMA YA KICHUNGAJI KATIKA JAMII KUELEKEA UCHAGUZI MKUU 2010 na baada ya muda wakatoa walichokiita ILANI YA UCHAGUZI NA VIPAUMBELE VYA TAIFA. Huu ulikuwa mweleko mpya wa Kanisa kuingia katika siasa mia kwa mia kwani huko nyuma Kanisa halikuwahi kutoa Waraka wenye maudhui kama hiyo na halikuwahi kutoa Ilani ya Uchaguzi na Vipaumbele vya Taifa.

Kwa kuelewa hatari ya Waraka na Ilani hiyo ya Kanisa, waislamu walipinga kwa nguvu zote mwelekeo huu mpya wa Kanisa. Hata baadhi ya wanasiasa wenye upeo, akiwemo Mzee Kingunge Ngobale Mwiru, walikemea mweleko huo wa Kisiasa wa Kanisa Katoliki lakini wakabezwa kwa kuambiwa kuwa wamezeeka na kufilisika kisiasa na hata kutakiwa wanyamaze kimya.

Baada ya waislamu kuona kuwa wamepuuzwa, na kwa kuelewa nafasi yao kwa waislamu, Shuura ya Maimamu Tanzania, ikatoa maelekezo kwa waislamu kupitia "MWONGOZO KWA WAISLAMU" ili waislamu "Wasidhulumu wala wasikubali kudhulumiwa" kama Qur'an inavyoagiza (Qur'an 2:279).

Wakati wote wa Kampeni za Uchaguzi, msimamo wa Maaskofu kutoka takriban Makanisa yote ya Kikristo nchini ulikuwa ni kuunga mkono Mgombea Urais wa Chadema na wagombea wengine wa chama hicho nchi nzima. Makanisa yakatumika kumnadi mgombea huyo kama Waraka wao wa Kichungaji ulivyoelekeza wazi kwa kusema;-
"Mungu anakuhitaji, haya si maneno tu, bali ni uamuzi wa makusudi wa Mungu anayetukabidhi wajibu huu. Kutopokea mwaliko huu unaotoka kwa Mungu ni kushindwa kutimiza wajibu wetu, ni dhambi ya kutotimiza wajibu wa wito wetu wa kikristo. Wito wa kutimiza wajibu wa Kijamii, ambao ni kutia chachu ya tunu za Injili na Mafundisho ya Kristo katika masuala na shughuli za kijamii, kiuchumi na kisiasa ya taifa letu". (Tazama: Mpango wa Kuhamasisha Huduma ya Kichungaji Katika Jamii Kuelekea Uchaguzi Mkuu 2010, Uk. 2).

Kwa kuwa Padri Slaa aliamini kwamba yeye ni chaguo la Kanisa, alijiridhisha yeye binafsi, wafuasi wake, viongozi wenzake wa Chadema na Maaskofu kuwa lazima atashinda na akasema wazi kuwa hatokubali matokeo mengine yoyote kinyume na ushindi wake kwani wakristo walishaambiwa kuwa kutokutekeleza waraka wa Maaskofu ni dhambi. Ni muumini gani ataambiwa na viongozi wa dini yake kuwa kutokufanya jambo fulani ni dhambi kisha asilifanye?

Mfano hai, huko Sumbawanga, Kanisa Katoliki liliwatenga waumini wake kwa kile lilichodai kwenda kinyume na maelekezo ya Kanisa kuhusu wagombea wa chama gani wapigiwe kura. Hali hiyo imepelekea Waziri Mkuu wa Tanzania, Mhe. Mizengo Peter Kayanza Pinda kuwaomba radhi Maaskofu kwa niaba ya Serikali na Chama chake kwa kile alichodai "kuwaudhi Maaskofu hao wakati wa Kampeni za Uchaguzi"!

Hatimaye tarehe 31 Oktoba, 2010, taifa lilifanya Uchaguzi Mkuu na tarehe 5 Novemba, 2010, Tume ya Taifa ya Uchaguzi ikamtangaza Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete kuwa mshindi wa kiti cha Urais na akaapishwa tarehe 6 Novemba, 2010.

Wagombea wote wa kiti cha Urais walikubali matokeo yaliyotangazwa na Tume ya Taifa ya uchaguzi isipokuwa Padri Wilbrod Slaa wa Chadema na chama chake waliyakataa matokeo hayo na hata siku ya kutangazwa na siku ya kuapishwa Rais si yeye Padri Slaa wala viongozi wengine wa Chama chake cha Chadema aliyeshiriki. Hata siku ya Rais Kikwete kuzindua Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mjini Dodoma, wabunge wote wa Chadema walitoka nje ya Ukumbi wa Bunge kuonesha kuwa hawamtambui Rais aliyetangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi.

Baada ya kuona kuwa mpango wao wa kushika madaraka kupitia mgongo wa Chadema umeangukia patupu, Maaskofu na chama wanachokiunga mkono wakaamua kuhakikisha kuwa nchi haitawaliki. Tunachoshuhudia sasa ni kutolewa kauli mbali mbali dhidi ya Uongozi uliko madarakani hata kwa mambo ambayo hayakufanywa na uongozi huu uliopo sasa bali yalifanywa na awamu zilizotangulia.

Kwa mfano, mikataba mibovu ya migodi ya madini inayolalamikiwa ilifanywa wakati wa awamu ya Mkapa, Kuuzwa mashirika ya umma kwa bei za kutupwa kulifanywa wakati huo huo wa Mkapa, kuuzwa kwa nyumba za serikali katika maeneo ya serikali kwa bei ya kutupwa kiasi kwamba baadhi ya viongozi wa serikali hivi sasa wanaishi nyumba za wageni (guest house) kulifanywa wakati wa Mkapa. Aidha, uvunjaji mkubwa wa haki za binadamu, Kufukiwa wachimba dhahabu Bulyankulu, mauaji ya raia wasio na hatia – Mwembechai, Zanzibar, Pemba, Morogoro, ufisadi na rushwa, Kuvunjwa maadili ya Uongozi, Kashfa za EPA, Meremeta, Kagoda, Net Group Solutions yote hayo hayakufanyika katika awamu hii bali wakati wa awamu ya Mkapa.

Wakati wa awamu ya Mkapa, hatukusikia Maaskofu wakijitokeza kuyakemea haya wala kulaani mauaji ya raia wasio na hatia kama wafanyavyo hivi sasa ila wamekuwa mbogo wakati wa Uongozi huu kama walivyokuwa mbogo wakati wa awamu ya pili ya Mzee Mwinyi. Kinachowasukuma si kingine bali kuogopa ile waliyoiita "dhambi" ya kutokutekeleza wito wao wa Kichungaji wa kuhakikisha kuwa "Tunu za Injili na Mafundisho ya Kristo vinaonekana katika masuala na shughuli za kijamii, kiuchumi na kisiasa za taifa". Laiti isingekuwa hivyo, basi wangesimamia uadilifu wa kukemea maovu katika jamii wakati wote.

Aidha, kwa kuona kuwa mawakala wao wameshindwa kushika nafasi walizoamini kuwa ni haki yao, Maaskofu na chama wanachokiunga mkono hivi sasa wamehamishia juhudi zao zote kudai katiba mpya ya Tanzania kwa nguvu zote (By all means possible) ikiwemo hata kumwaga damu. Mmoja wa viongozi wa juu wa Chadema, Mabere Marando, amesikika akisema wazi katika Mdahalo wa Katiba Mpya Ukumbi wa Nkurumah Chuo Kikuu Dar es Salaam siku ya Jumamosi tarehe 15 Januari, 2011 kuwa "Damu iliyomwagika Arusha ndiyo wino wa kuandika dibaji ya Katiba Mpya Tanzania".
Watu waliotayari kumwaga damu za watanzania kwa malengo ya kisiasa na kudai katiba mpya ni hatari kwa amani na usalama wa nchi yetu kwa sababu katiba huandikwa kwa wino wa kalamu wala si kwa damu ya raia.

Hii inaonesha mwelekeo wa hatari wa kundi hili la Maaskofu na wanasiasa kwa amani na usalama wa Taifa letu. Katiba ya nchi haiwezi kuandikwa kwa damu ya watanzania. Aidha katiba ya nchi haiwezi kuundwa katika mazingira ya vurugu, fujo, uasi kwa viongozi, dharau, kibri, uchu wa madaraka na ubinafsi. Katiba itakayoundwa katika mazingira haya, haitokuwa kwa maslahi ya taifa bali kwa maslahi ya Kanisa.

Hatari nyingine kubwa inayolinyemelea taifa letu, ni ile ya viongozi wa Chama kilichopo madarakani na wale wa serikali kupingana kauli katika mambo ambayo wangepaswa kuwa na kauli moja (Collective responsibility). Mwenendo huu unatishia mustakbali wa nchi yetu kwa sababu utawala uliogawanyika hauwezi kutekeleza majukumu yake kwa raia wake, na ndivyo Maaskofu wanavyotaka iwe. Rais mmoja wa Marekani alipata kusema "A house divided can not stand by itself"-yaani nyumba iliyogawanyika haiwezi kusimama yenyewe. Tunaamini kwamba kugawanyika huku kwa Mawaziri wa serikali iliyopo madarakani ni kazi ya kundi hili hili la Maaskofu na mawakala wao katika Chama tawala na Serikali.

TAMKO LA JUMUIYA NA TAASISI ZA KIISLAMU
JIJINI MWANZA.

Kwa vile, Baadhi ya Maaskofu wamejitokeza wazi wazi kuupinga uongozi uliotangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi wakati walikuwa kimya kipindi chote cha awamu ya tatu,

Na kwa vile, mwelekeo na kauli za Maaskofu hao vinapelekea kuiyumbisha nchi ili isitawalike wapate kudai kuwa Rais aliye madarakani hafai bali chaguo lao Padri Slaa ndiye anayefaa,

Na kwa vile, tayari madhara ya mwelekeo huu yameshajitokeza huko Arusha kwa kuuawa watu katika vurugu zilizotokana na uchu wa madaraka ya Umeya wa Jiji hilo na kuchangiwa na kauli za Maaskofu kutomkubali Meya huyo,

Na kwa vile, waislamu ni watu wapenda amani, haki na usawa kwa watu wote bila kujali rangi, jinsia, kabila, dini wala itikadi za kisiasa,

Na kwa kuwa, kuna kila dalili ya kutoweka kwa amani kupitia kauli na vitendo vya Maaskofu kuunga mkono Chama maalum cha siasa,

Na kwa kuwa, baadhi ya Mawaziri wa Serikali ya Rais Kikwete wameonesha wazi kuipinga Serikali yake,

Sisi waislamu wa Jiji la Mwanza tunatamka yafuatayo;-

1. Tunaunga mkono mia kwa mia yote yaliyoandikwa katika tamko la Waislamu lililotolewa Diamond Jubilee Dar es Salaam siku ya Jumamosi tarehe 15 Januari, 2011.

2. Maaskofu kuunga mkono Chama kinachopinga matokeo ya Urais ni kitendo cha Uhaini, U-dini na ni hatari kwa mustakbali wa Taifa letu. Hali kadhalika ni kukiuka hata maandiko ya Biblia yao wenyewe yasemayo "Heri walio wapatanishi kwa maana wataitwa wana wa Mungu. ( Mathayo: 5 msitari wa 9 ).

Tulitaraji viongozi wa dini, Maaskofu wakiwepo, wawe wapatanishi pale wanasiasa wanapogombana. Inapokuwa wao ndiyo sehemu ya ugomvi huo ni nani atawapatanisha wana siasa? Kama Maaskofu wamekuwa wagomvi, watakuwa wana wa nani kama si wa Shetani?

3. Tunawaonya Maaskofu waache kuivuruga Serikali kwa matamshi yao yaliyojaa chuki za U-dini kwani watapelekea amani ya nchi hii kuvurugika kama walivyochangia mauaji ya Kimbari ya Rwanda mwaka 1994.

4. Kwa kuwa Kauli za Maaskofu huko Arusha kutomtambua Meya aliyechaguliwa kwa kufuata taratibu zote za kisheria, zilichangia kuuawa kwa watanzania wasio na hatia, tunaitaka Serikali kuwafikisha Mahakamani Maaskofu wote waliotoa kauli hizo za uchochezi.

Hakuna mtu aliye juu ya sheria. Kama Masheikh hufukishwa Mahakamani na wengine hata kuswekwa kizuizini bila kupelekwa mahakamani, Mfano Al Marhum Sheikh Al Amin Abdallah wa hapa Mwanza na Masheikh wengine mwaka 1964 na wengine kuswekwa ndani kwa kesi za kubumba, Maaskofu wametenda kosa hili la uchochezi wazi wazi hivyo kwa nini sheria isichukue mkondo wake dhidi yao?

5. Kama uchu wa madaraka ya Umeya wa Jiji la Arusha tu umesababisha maisha ya watanzania watatu kupotea, damu za wengi kumwagika na mali kuharibiwa pamoja na kusimamisha shughuli za kiuchumi katika Jiji hilo la kitalii, hali itakuwaje kwa uchu wa kutaka kiti cha Urais? Ni watanzania wangapi watapoteza maisha yao na damu za watanzania wangapi zitamwagika ili Padri Slaa aingie Ikulu?

6. Wakati wa ziara ya Papa Yohana Paulo wa Pili nchini Tanzania mwaka 1990, Kanisa Katoliki lilimtaarifu kuwa linayo Tume ya Majeshi. Hivi jeuri hii ya Maaskofu ni kwa kuwa wanayo hiyo tume ya majeshi? Hata kama wanayo hiyo tume ya majeshi, sisi waislamu kamwe hatuiogopi kwa sababu Mwenyezi Mungu anasema:

"Je, mnawaogopa? Basi Allah anastahiki zaidi ninyi kumuogopa ikiwa mu-waumini wa kweli" (Qur'an 9 : 13).
Pamoja na hayo, tunarudia kuitaka Serikali kuueleza umma wa watanzania tume ya majeshi ya Kanisa ni ya nini? Au hawayaamini majeshi yetu ya ulinzi na usalama?

7. Waislamu tunamtaka Rais Kikwete awawajibishe mara moja Mawaziri wote wanaoipinga Serikali yake kama Mwalimu Nyerere alivyomfanya Kambona alipopinga sera ya Utaifishaji ya serikali yake mwaka 1967. Tunamtaka Rais asiwaonee haya hata kidogo Mawaziri hawa wanaoipinga Serikali yake kwani waswahili husema "Mchelea mwana kulia, hulia mwenyewe" na "Mchelea mwiba, mguu huota tende".

8. Baadhi ya vyombo vya habari vimechangia sana kuzorotesha hali ya amani nchini kwa kuandika au kutangaza habari za uchochezi na hivyo kupelekea kuvunjika kwa amani. Tunavitaka vyombo hivyo vya habari kuacha mara moja kushabikia U-dini na vitende haki. Vinginevyo waislamu tutavitangaza hadharani na kuwahimiza waislamu wasivinunue, kusikiliza au kuvipa matangazo. Tukumbuke pia kuwa mauaji ya kimbari nchini Rwanda yalichangiwa sana na vyombo vya habari.

9. Vyombo vya dola navyo, Jeshi la Polisi, Usalama wa Taifa, Jeshi la Wananchi vitende haki kwa kufanya kazi zao kwa uadilifu, kwa ukweli na uzalendo na kutokupendelea Chama au kundi jamii fulani kwani kwa kufanya hivyo vitasababisha kutoweka kwa amani nchini. Kwa mfano, inapokuwa jambo linahusu Masheikh au waislamu, vyombo hivyo, husuusan Jeshi la Polisi, huwa na ujasiri wa kuwapiga na kuwasweka ndani waislamu lakini ujasiri huo hatuuoni kwa Maaskofu na viongozi wengine wa Kikristo wanapovunja sheria.

10. Kwa wanasiasa na wanaharakati wa mashirika ya kijamii, tunawataka waache kutoa kauli za uchochezi na vurugu kwani amani itakapotoweka hakutakuwa na wanachama wa kuwaongoza. Tumieni busara zenu kujadili mambo kwa hoja na msiporidhika pelekeni malalamiko yenu Mahakamani ili sheria ichukue mkondo wake.

11. Waislamu tunaunga mkono tamko la Rais Jakaya Kikwete kuhusu kuundwa kwa Katiba mpya. Pamoja na hayo, kwa mwenendo wa Maaskofu na Chama chao wanachokiunga mkono, tunamtahadharisha Rais kwamba amebeba dhamana kubwa ya usalama wa watanzania wote hivyo asisite kuwachukulia hatua wale wote watakaotaka kutumia mjadala wa katiba mpya kwa njia zitakazohatarisha amani au kudhoofisha Serikali.

12. Kwa kuwa mchakato wa Katiba mpya ndiyo kwanza unaanza, waislamu tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwani sasa kupitia Katiba mpya tutadai haki zetu zote ikiwemo ya Mahakama ya Kadhi kuwepo katika katiba kama ilivyo nchini Kenya, Nigeria, Ethiopia, Gambia, Zanzibar na hata Uganda.

13. Tunataka Katiba mpya itamke wazi kuwa Tanzania inaamini kuwepo kwa Mungu Muumba, serikali haina dini ila wananchi wake ndio wana dini mbali mbali. Katiba ya sasa haitambui kuwepo kwa Mwenyezi Mungu jambo ambalo linaifanya Tanzania kuwa nchi ya Kikafiri. Katiba za nchi nyingi duniani zimetamka kuamini kuwepo kwa Mwenyezi Mungu na hata baadhi kusema wazi "In God We Trust" – Tunategemea kwa Mungu.

Kama hatuamini kuwepo kwa Mwenyezi Mungu kwa nini watu huapishwa Mahakamani? Kwa viongozi, kwa nini waapishwe kwa kutumia vitabu vya dini, Ikulu na Bungeni na kwa nini kuwepo dua ya kuliombea Bunge? Ni Mungu gani huyo anayeombwa hapo?

14. Tunataka Katiba mpya ya Tanzania iweke mgawanyo wa madaraka kwa uadilifu kwa kutamka wazi kuwa Rais akiwa Muislamu, Waziri Mkuu awe Mkristo na Rais akiwa Mkristo, Waziri Mkuu awe Muislamu kama ilivyo Nigeria na Lebanon ili kuepuka U-dini. Na vivyo hivyo kwa ngazi zote za madaraka mgawanyo uwe nusu kwa nusu.

15. Tunataka iundwe Wizara Maalumu ya Mambo ya dini ili ishughulikie masuala ya dini kuliko kuyaacha kama yalivyo sasa hayana Wizara inayoyashughulikia. Kama mambo ya kipuuzi tu kama vile muziki na maagizo yana Wizara maalum, vipi dini zisiwe na Wizara yao?

16. Tunataka Katiba mpya isiruhusu Serikali kuingia Mkataba wa upendeleo na kundi jamii moja kama ilivyofanya kupitia Makubaliano ya Maridhiano na Makanisa ya Kikristo mwaka 1992, makubaliano ambayo yanatekeleza andiko la Bibilia "Mwenye nacho ataongezewa na asiyekuwa nacho atanyang'anywa hata kile kidogo alicho nacho"(Luka 8 msitari wa 18). Wakristo walikuwa na shule, hospitali, Vyuo vya Ualimu, Vyuo Vikuu n.k huku waislamu wakiwa hawana kitu. Badala ya kupewa Waislamu wasiokuwa na rasilimali hizo wakapewa Wakristo na hivi sasa wanaongezewa kupitia Makubaliano ya Maridhiano kati yao na Serikali.

17. Kwa kuzingatia tamko namba 16 hapo juu, tunaitaka Serikali iache mara moja kutekeleza Maridhiano hayo batili kati ya Serikali na Makanisa na pia ituambie hadi sasa imeshayapa Makanisa ya Kikristo Mabilioni mangapi tangu mwaka 1992? Aidha tunataka watendaji wote wa serikali waliohusika kuandaa na kupitisha Maridhiano hayo ya U-dini wachukuliwe hatua za kisheria kwani huu nao ni ufisadi kama ule wa EPA, Kagoda, Meremeta, Dowans n.k.

18. Sambamba na hilo, tunaitaka Halmashauri ya Jiji la Mwanza ikabidhi kwa waislamu Shule ya Msingi Mbugani (Muslim School) mara moja kama alivyoagiza Rais Mkapa miaka kumi na tano iliyopita. Hali kadhalika tunaitaka Serikali irejeshe shule zote zilizokuwa Muslim Schools ambazo zilitaifishwa wakati waislamu walikuwa na shule chache kulinganisha na Wakristo waliokuwa wakipata misaada kutoka serikali ya Kikoloni na sasa kupitia Makubaliano ya Maridhiano na Serikali tuliyoyaeleza hapo juu.

19. Tunataka Katiba Mpya itamke wazi kuwa Siku ya Ijumaa nayo ni siku ya mapumziko ili waislamu nao waweze kwenda kusali sala ya Ijumaa kwa utulivu pasina kuhofia kufukuzwa kazi au kukosa masomo kama ilivyo sasa ambapo kwenda kusali ijumaa ni fadhila tu. Kama hilo halikubaliki, basi siku zote tatu Ijumaa, Jumamosi na Jumapili ziwe siku za kufanya kazi nusu siku ili sote tuwe sawa. Mkao wa sasa wa mapumziko Jumamosi na Jumapili unaonesha kuwa nchi hii ni ya Kikristo.

20. Tunataka wimbo wa Taifa uliopo ufutiliwe kwa mbali kwani unaonesha wazi Tanzania ni nchi ya Kikristo kwa sababu hakuna asiyejua historia ya wimbo huo kuwa ulianzia Kanisani huko Soweto Afrika ya Kusini. Kwa Kizulu wimbo huo unaitwa "Nkosi Sikeleli Afrika". Pia hakuna asiyejua kuwa upo katika kitabu kiitwacho "Chuo Kidogo cha sala na Maombi cha Kanisa Katoliki". Hata Mashahidi wa Yehova huko Mbeya waliwahi kuukataa.

21. Tunataka Katiba Mpya itamke wazi kuwa Rais akitoka Bara, Raisi wa awamu nyingine atoke Zanzibar ili kuwatendea haki Wazanzibari. Tayari hivi sasa, Tanzania bara imeshatoa Marais mara tatu, Mwalimu Nyerere, Rais Mkapa na Rais Kikwete. Ni Rais Mwinyi tu ndiye aliyetoka Zanzibar kwa hiyo Rais ajaye lazima atoke Zanzibar kutoka chama chochote kile kiwacho.

22. Tunamtaka Rais Kikwete aongoze mchakato wa kuleta Katiba mpya kwa amani, haki, ujasiri, bila woga wala upendeleo wowote. Katu asiruhusu dharau kutoka kwa kiongozi yeyote awe wa kisiasa ndani au nje ya Serikali yake au hata kiongozi wa kidini. Na pale atakapoona mazingira ya nchi hayapo katika utulivu na amani, ni kheri ausitishe mchakato wa Katiba mpya kwani Katiba haiandaliwi katika mazingira ya vurugu, chuki na uhasama kama tuliyo nayo hivi sasa.

HITIMISHO:

Nchi hii ni ya Watanzania wote. Hakuna aliye na haki zaidi ya mwingine. Kama taifa, watanzania tunafanana na watu walio katika merikebu. Hivyo tunapomuona mmoja wetu anataka kuitoboa merikebu yetu, hatupaswi kumwangalia tu atimize azma yake kwani akifanikiwa tutaangamia sote.

Tunawataka watanzania wote kwa makundi jamii yao, vyama vyao, dini zao na tabaka zao mbali mbali kutanguliza mbele maslahi ya taifa kwanza. Aidha tunawataka Maaskofu kuheshimu imani za dini nyingine katika kutekeleza wito wao wa kichungaji. Si lazima umkandamize mwingine asiendelee ili wewe uendelee.

Tukumbuke kuwa hakuna mahali pengine ambapo watanzania wanapategemea kuishi wao na vizazi vyao hivyo tuilinde nchi yetu kwa faida yetu na vizazi vijavyo.

Kama ambavyo waislamu walimlinda Mwalimu Nyerere dhidi ya wakoloni na tukavumilia madhila yote tuliyofanyiwa ili kulinda na kudumisha amani, sasa tunasema wazi wazi kuwa hatutakuwa mhanga wa agenda za Maaskofu na Mfumo Kristo bali tutakuwa tayari kuitetea dini yetu kwa hali na mali.

Waislamu kamwe si wachokozi. Lakini hapa tulipofikishwa na Mfumo Kristo, tunapenda Maaskofu na mwingine yeyote yule aelewe wazi kuwa waislamu nchini Tanzania hivi sasa tuko tayari kufa kuliko kuishi huku tukiiona dini yetu ikidhalilishwa kwani hatuna cha kupoteza- Kwetu ni mawili tu, ima Ushindi Dhidi ya Dhulma au Kuuwawa Tupate Pepo.

Na Mwenyezi Mungu Ndiye Mjuzi na Muweza wa Yote.

Wabillaahi Tawfiiq.

Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi.

Saturday, January 29, 2011

Mikataba Bomu Itaendelea Kutumaliza

Wa-Tanzania wanalalamika sana kuhusu mikataba bomu ambayo inalisababishia Taifa hasara kubwa. Tafsiri yao, kwa ujumla, ni kwamba tunaingizwa katika janga hili na mafisadi ambao wanasaini kwa makusudi mikataba hii, kwamba hao ni wa-Tanzania wenye ubinafsi na uroho, na hawana uchungu na nchi, bali wanatafuta namna ya kunufaika wao. Mafisadi wetu hao wanashirikiana na mafisadi wa nje kuitafuna nchi yetu.

Kwa ujumla, nami nina hisia hizo. Kwanza kuna ukweli usiopingika kuwa maadili katika nchi yetu yanazidi kuporomoka. Vile vile nazingatia usemi wa wahenga kuwa lisemwalo lipo, na kama halipo laja. Pia tunaona taarifa kutoka sehemu mbali mbali za dunia kuhusu uozo wa rushwa katika masuala ya mikataba, zabuni, na kadhalika.

Lakini msimamo wangu hauishii hapa. Naamini kuwa hata kama tukiondoa kabisa rushwa na ufisadi, tukawa na watu wanaojali maslahi ya nchi na hao ndio wakawa wanaosaini mikataba yetu, bado tutaendelea kulizwa na mikataba bomu.

Kitakachosababisha janga hili ni kuanguka kwa elimu katika Tanzania. Kama ninavyosema daima katika blogu hii na sehemu zingine, wa-Tanzania tumejichimbia kaburi kwa kutothamini elimu ipasavyo. Ushahidi ni ufahamu wa lugha ulivyo duni, na utamaduni wa kununua na kusoma vitabu ulivyofifia au kutoweka miongoni mwetu.

Nikifafanua suala la lugha na kulihusisha na suala la mikataba, napenda kusema kuwa tupende tusipende, mikataba ya kimataifa itaendelea kuandikwa kwa ki-Ingereza, nasi tutajikuta tunasaini bila kuelewa vizuri kilichomo. Kuna matapeli wengi duniani, ikiwamo katika uwanja wa biashara na uwekezaji.

Wajanja, kwa kutambua umbumbumbu wetu, watachukulia mwanya huu kama mbinu ya kutukomoa. Laiti tungekumbuka msisitizo wa Mwalimu Nyerere pale tulipopata Uhuru, kuhusu maadui watatu tuliopaswa kupambana nao: umaskini, maradhi na ujinga.

Mwaka jana, serikali ya CCM ilitamka mara kwa mara kwamba imefanya marekebisho katika mikataba ya madini, ili kuziba mianya iliyokuwepo, iliyokuwa inatukosesha mapato tunayostahili. Sasa hapo nina suali. Ni nini kilichotufanya tusione hizo dosari tangu mwanzo? Kama si ufisadi, labda ni huu ujinga ninaoongelea. Binafsi, nakerwa kwamba serikali haijatuelezea undani wa suala hilo.

Wednesday, January 26, 2011

Kitimoto

Neno kitimoto ni maarufu Tanzania. Kitimoto ni nyama ya nguruwe; inapendwa sana katika mabaa na sehemu zingine. Ubora wa kitimoto ni kivutio kwa wateja na neema kubwa kibiashara kwa wenye baa. Hapa kushoto ni sahani ya kitimoto ambayo niliinunua kwenye baa moja Sinza, hatua chache kutoka Lion Hotel.

Ninapokuwa katika miji kama Dar es Salaam, napatikana mitaa ya u-Swazi, kama inavyoonekana katika picha hii, iliyopigwa Sinza, bondeni ukifuata barabara inayopita mbele ya Lion Hotel. Kwa wale wasiojua, neno u-Swazi linamaanisha sehemu wanazoishi wananchi wa kawaida.

Hapo kushoto kuna baa na sehemu ya kitimoto ambapo nimeshakuwa mteja mara kadhaa. Picha hii inaonyesha jinsi mwenye kitimoto anayotangaza biashara yake. Tofauti na zamani, anaweza kuagiza nyama kutoka bucha kwa kutumia simu, na anaweza kuchukua oda za wateja kwa simu pia.


Pamoja na umaarufu wake, kuna hisia tofauti, michapo, na utani kuhusu kitimoto, mambo ambayo yanaweza kufanyiwa utafiti kama sehemu muhimu ya utamaduni wa leo wa m-Tanzania.

Saturday, January 22, 2011

Kwa wa-Tanzania, Dini Imekuwa Bangi

Katika hali ya kawaida, dini ni kitu cha manufaa kwa wanadamu, kwa maana kwamba inatufundisha kumtambua na kumcha Mungu, na kwa wale wanaoamini miungu wengi, ni hivyo hivyo. Dini inatufundisha maadili ya kumtendea binadamu mwingine kama tunavyopenda kutendewa. Kwa ufafanuzi zaidi maadili hayo ni kama kupendana, kusikilizana, kuheshimiana, kusameheana, na kutakiana mema.

Kwangu mimi m-Katoliki, maadili hayo yalielezwa kwa uwazi na Yesu katika mafundisho yake mengi, hasa pale aliposema kuwa amri kubwa kuliko zote ni kumpenda Mungu kwa moyo wetu wote, nguvu yetu yote na akili yetu yote, na kumpenda jirani kama tunavyojipenda wenyewe na pia kuwapenda adui zetu. Kwa lugha rahisi ni kuwa tunapowachokoza wengine au kuumiza hisia zao kwa makusudi, au tunapokosa uvumilivu na badala yake tunatunisha misuli na kujibu mapigo, tunaasi dini na kuwa makafiri.

Kwa kuzingatia hayo, niliandika makala kuwa penye dini hapana magomvi, na kwamba kuwepo kwa magomvi ni ushahidi wa kukosekana kwa dini. Dhana ya mgogoro wa kidini haina mantiki; ni sawa na kusema "usiku wa mchana," dhana ambayo haina mantiki. Soma hapa na hapa.

Hata kitu kizuri kinaweza kutumiwa vibaya. Na ndivyo ilivyo Tanzania, kwenye suala la dini. Dini imegeuzwa kuwa bangi. Dhana ya dini kuwa bangi ilielezwa na Karl Marx katika Critique of Hegel's Philosophy of Right, lakini naitafsiri kwa namna yangu.

Kadiri siku zinavyoenda, bangi hii inazidi kuenea katika Tanzania na kukolea vichwani. Imekuwa kichocheo cha malumbano, magomvi, uhasama, ubaguzi, majungu na chuki.

Sehemu za ibada zimegeuzwa kuwa majukwaa ya kueneza sumu hizo, kwa kutumia vipaaza sauti. Papo hapo, wahusika wanaamini kuwa ni wafuasi na watetezi wa dini. Wanaendelea kujenga nyumba wanazoziita za ibada, kumbe wanazitumia kuendeleza ukafiri. Hawakumbuki busara za wahenga kuwa kucha Mungu si kilemba cheupe.

Kilichonisukuma kuandika hayo niliyoandika ni wasi wasi wangu kuhusu hali ya nchi yangu. Dini yangu hainiruhusu kuwahukumu wengine. Kama nimekiuka angalizo hili, mwenye kujua ni Mungu.

Thursday, January 20, 2011

Tamko Kuhusu Matamko ya Wa-Tanzania

Tanzania sasa imekuwa nchi ya matamko. Kila kukicha linatolewa tamko kutoka kikundi au jumuia fulani. Katika siku za karibuni, kwa mfano, tumeshasikia matamko kutoka vyama vya siasa, jumuia za kidini, na taasisi mbali mbali, za serikali na zisizo za serikali.

Matamko ya wa-Tanzania yanahusu zaidi masuala tata ya jamii, au migogoro. Yanahusu mambo kama sera za serikali au vitendo vya watendaji mbali mbali, kama vile polisi, au taasisi zingine. Mara kwa mara, matamko yanakuwa na hisia za kulalamika, kuonya, au kutangaza msimamo.

Kila mtu anaweza kuwa na mtazamo wake kuhusu jambo hilo. Binafsi, naliona ni jambo zuri, kwa maana kwamba watu wanatumia uhuru wao wa kuelezea hisia, mawazo na mitazamo yao. Kwa hivi, sishangai kuyasikia matamko hayo. Kila mtu ana haki ya kutoa tamko lake, ili mradi havunji sheria au kuingilia uhuru wa wengine wa kutoa matamko.

Utamaduni wa matamko ni mzuri. Ni bora kuliko tunayoyaona au kuyasikia yakitokea katika jamii za wenzetu, ambao migogoro yao inawapeleka katika kupigana na kuvunjika kwa amani.

Kwa watu wasiopendezwa na jambo, au wenye hasira, fursa ya kujieleza kwa namna yoyote, kama hii ya matamko, ni njia nzuri ya kupooza hisia za kusumbua. Ni aina ya tiba kisaikolojia, hata kama wanayosema katika haya matamko ni upuuzi. Kuzuia uhuru na fursa ya kujieleza ni jambo lenye athari mbaya.

Kwa upande mwingine, utamaduni wa wa-Tanzania wa matamko unanichekesha, kwa jinsi matamko yanavyofumuka kama uyoga au kumiminika kama mvua.

Tungeweza kuendeleza utamaduni wa kufanya mazungumzo ya ana kwa ana au kuwatumia wawakilishi wetu. Tungeweza hata kufuata utamaduni wa zamani wa mabibi na mababu, kama alivyouelezea Mwalimu Nyerere, kwamba wahenga walikuwa wanakaa chini ya mti na kujadili masuala hadi kukubaliana. Lakini nafurahi nami nimetoa tamko langu.

Wednesday, January 19, 2011

Andika ki-Swahili; ki-Ingereza Hatuelewi

Kuna tabia katika jamii ya wa-Tanzania ya kulalamika pale mtu anapoandika ki-Ingereza. Malalamiko haya yanaonekana mara kwa mara katika blogu ya Michuzi, kwa mfano, ambayo inasomwa sana na wa-Tanzania, pale inapotokea makala iliyoandikwa kwa ki-Ingereza.

Walalamikaaji wanakumbushia kuwa wa-Tanzania wengi hawajui ki-Ingereza, na kwa hivi wanataka mwandishi awafikirie hao kwa kuandika kwa ki-Swahili, lugha wanayoifahamu. Ujumbe unaojitokeza katika malalamiko hayo ni kwamba ni jambo la uzalendo kwa mwandishi kuwafikiria hao wa-Tanzania walio wengi, ili nao wapate kufaidika na yale yanayoandikwa.

Sijawahi kuona malalamiko hayo yakipingwa. Inaonekana kuwa hoja inayotolewa katika malalamiko hayo inakubalika miongoni mwa wa-Tanzania.

Katika kulitafakari suala hili, naona kuna haja ya kuwakosoa hao walalamikaji. Ingawa ni kweli kuwa mtu akiandika kwa ki-Swahili anawafikia wananchi wasiojua ki-Ingereza, kuna pia tatizo la uvivu katika jamii yetu.

Malalamiko hayo ni sehemu ya tatizo hili la uvivu ambalo naliongelea tena na tena katika blogu hii na zingine, na pia katika maandishi mengine. Wa-Tanzania wanapenda kutafuta visingizio na kuwalaumu wengine. Kwa nini wa-Tanzania waridhike na hali yao, ya kujua ki-Swahili tu, badala ya kujifunza lugha zingine?

Kama wa-Tanzania wanataka kudekezwa, ni bora wajue kuwa dunia hii ya ushindani haidekezi mtu. Wasipojituma katika masuala ya elimu, ikiwemo elimu ya lugha mbali mbali, sio tu watabaki nyuma, bali wataumia. Mawasiliano ya kimataifa yatakuwa mtihani mkubwa ambao watashindwa. Mikataba ya nje watashindwa kuielewa.

Wakati huu tunanyoosheana vidole kutokana na mikataba tunayohisi waTanzania wenzetu wanaisaini kifisadi. Lakini, kwa jinsi tunavyoendekeza uvivu ninaoongelea, tutaendelea kusaini mikataba mibovu kwa kutojua lugha. Nchi itaendelea kuumia.

Hata kama watu hawana vitabu, kuna maktaba katika miji mbali mbali. Mtu yeyote anaweza kujipangia utaratibu wa kwenda kusoma vitabu vilivyomo, akajiongezea angalau ufahamu wa ki-Ingereza. Lakini wa-Tanzania wako radhi kukaa kwenye kijiwe nje ya maktaba, siku hadi siku, wiki hadi wiki, mwezi hadi mwezi, mwaka hadi mwaka, bila kuingia humo maktabani. Hili ni tatizo kubwa katika nchi yetu.

Thursday, January 13, 2011

Nimejiunga na Bodi ya Operation Bootstrap Africa

Nimerejea jioni hii kutoka Minneapolis, kuhudhuria mkutano wa bodi ya Operation Bootstrap Africa (OBA). Mimi ni mwanabodi wapya. Niliteuliwa mwishoni mwa mwaka jana, na mkutano wa leo ulikuwa ni wa kwanza kwangu.

Nilifahamu habari za OBA tangu nilipokuwa nasoma Chuo Kikuu cha Wisconsin-Madison, 1980-86, kwamba ilikuwa inajishughulisha sana na masuala ya elimu Tanzania. Mwaka jana, nilipopendekezwa kuwa mwanabodi, nilifanya juhudi za kuifahamu zaidi OBA.

OBA, imefanya mengi ya manufaa kwa nchi ya Tanzania, kwa kuhamasisha michango miongoni mwa wa-Marekani. Yeyote anayewafahamu vizuri wa-Marekani, anatambua jinsi wanavyojituma katika shughuli za kujitolea. Ni jambo ambalo wanafundishwa tangu utotoni, na linasisitizwa mashuleni, kuanzia madarasa ya mwanzo kabisa hadi chuo kikuu.

Nilikaa katika mkutano wa leo nikisikiliza taarifa za michango inayotolewa na watu mbali mbali kwa manufaa ya Tanzania, watu wenye hela nyingi na wasio na hela nyingi, nikawa najiuliza kwa nini sisi wenyewe tusiwe na moyo wa namna hiyo, wa kuchangia masuala ya elimu, afya na kadhalika.

Nilifarijika kusikia kuwa mfanyabiashara maarufu Reginald Mengi amechangia shilingi milioni nyingi kuendesha mradi maalum wa OBA, ambao ni shule ya wasichana wa Maasae. Ilikuwa faraja kusikia juhudi za angalau huyu m-Tanzania mmoja.

Uanabodi katika OBA ni shughuli ya kujitolea. Wajibu mojawapo muhimu wa mwanabodi ni kuchangia au kuchangisha hela kwa ajili ya OBA. Napangia kufanya kila niwezalo kutekeleza jukumu hili, pamoja na kuwahamasisha wa-Tanzania wafuate nyayo za Mengi. Hatuna sababu za msingi za kushindwa kuchangia mambo kama elimu na afya, wakati daima tunachanga michango ya sherehe na mambo mengine.

Tuesday, January 11, 2011

Wauza Vitabu wa Mitaani Dar es Salaam

Kitu kimojawapo kinachonivutia ninapokuwa Dar es Salaam ni wauza vitabu wa mitaani. Wako wa aina mbili. Wako wenye sehemu maalum ya kuuzia vitabu, iwe ni meza tu au kibanda. Hao wanaonekana sehemu mbali mbali za mjini Dar es Salaam, kuanzia katikati ya mji, kama vile barabara ya Samora, hadi sehemu za pembeni, kama vile Mwenge na Ubungo. Picha iliyoko hapa kushoto niliipiga Ubungo, mwaka jana, karibu na kituo kikuu cha mabasi. Pembeni ya mwuza vitabu kuna kibanda cha muuza machungwa.

Wako wauza vitabu wengine ambao hutembeza vitabu mitaani, sawa na wale vijana ambao wanatembeza bidhaa mbali mbali, ambao tunawaita machinga. Hapo kushoto kuna picha niliyopiga Sinza Kijiweni, mwaka jana, kwenye hoteli ya Deluxe.



Nilikuwa hapo, na hao vijana wawili wakaja, mmoja akiuza vitabu na mwingine peni za kuandikia. Nilivutiwa, nikaanza kuongea nao. Nilimwuliza huyu muuza vitabu kuhusu wateja, na kama wa-Tanzania wananunua vitabu, akanielezea uzoefu wake. Nilinunua vitabu viwili. Kimoja ni tafsiri ya maneno ya ki-Ingereza kwenda ki-Swahili, na kingine ni tafsiri ya maneno ya ki-Swahili kwenda ki-Ingereza. Vyote vimechapishwa Kenya, na walengwa ni wageni wanaotembelea Afrika Mashariki. Ni vijitabu vidogo vidogo sana, kimoja cha kurasa 30 na kingine kurasa 32.

Karibu na lango la kituo cha mabasi Ubungo nilipiga picha iliyo hapa kushoto, mwaka jana, baada ya kumwomba kijana mwenye kibanda hicho. Tuliongea kuhusu biashara yake, naye alinieleza kuwa biashara inaenda vizuri, ila ingekuwa nzuri zaidi kama angekuwa na mtaji wa kutosha ili kuwa na meza kubwa zaidi na vitabu vingi zaidi. Nilifurahi kusikia hivyo, ushahidi kuwa wako watu wanaonunua vitabu. Kinachobaki ni kufuatilia zaidi kuona ni watu wa aina gani. Yule kijana niliyeongea naye Sinza alisema kuwa wanaonunua vitabu zaidi ni watu wa Zambia. Nitafuatilia zaidi suala hili siku zijazo, panapo majaliwa.

Katika pitapita yangu na kuangalia nimeona kuwa kuna vitabu vya aina nyingi humo mitaani, kuanzia hadithi za waandishi maarufu wa sehemu mbali mbali za dunia, hadi taaluma mbali mbali. Kuna vitabu vilivyotumika na vipya pia. Mtu makini anaweza kujipatia vitabu vingi vya manufaa kutoka kwa hao wauzaji wa mitaani akawa na maktaba binafsi ya kueleweka.

Sunday, January 2, 2011

Mwongozo wa "Things Fall Apart"

Nimefundisha riwaya ya Things Fall Apart ya Chinua Achebe tangu yapata mwaka 1976, sehemu kama Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Chuo Kikuu cha Burundi, na vyuo vya Colorado na St. Olaf.

Kutokana na uzoefu huu, na mengi niliyojifunza, na kwa lengo la kuweka kimaandishi mawazo yangu juu ya riwaya hii, niliandika mwongozo. Nimeshaongelea kidogo kuhusu mwongozo huu katika blogu hii, lakini napenda kueleza zaidi habari zake.



Aliyenisukuma kuandika mwongozo huu kwa wakati niliofanya hivyo ni rafiki yangu A.S. Muwanga, aliyekuwa katika Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Yeye na mimi tulikubaliana kuwa niandike pia mwongozo kuhusu kitabu cha The African Child, kilichoandikwa na Camara Laye. Muwanga alifanya mpango na kitabu kilichapishwa mwaka 1988 na Nyanza Publications Agency kama inavyoonekana katika picha hapo juu. Lengo mahsusi lilikuwa ni hasa kuwasaidia wanafunzi wa sekondari waliokuwa wanasoma riwaya hizo.

Miaka hiyo, 1976 hadi 1991, nilikuwa mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Mwaka huo 1991, niliondoka pale mwaka 1991, nikaja kufundisha Chuo cha St. Olaf, katika idara ya kiIngereza.

Mwaka 1997, bodi ya South Dakota Humanities Council iliyokuwa ikiratibu mradi wa usomaji katika jimbo la South Dakota iliniomba kuandika mwongozo kuhusu Things Fall Apart. Katika utaratibu wao, walikuwa wanachagua kitabu ili kisomwe na vikundi mbali mbali katika jimbo zima.

Ili kuchangia zoezi hili, walikuwa wana utaratibu wa kutafuta mtu wa kuandika mwongozo kuhusu kitabu husika, na mwongozo huu ulikuwa unatumiwa sambamba na kitabu husika. Kila kikundi kilikuwa kinajadili kitabu kweye mji wao, au eneo lao, na kisha walikuwa wanajumuika na wenzao wa sehemu zingine katika mjadala kwa njia ya barua pepe.

Mwaka huo 1997 kitabu kimojawapo walichokuwa wamekichagua ni Things Fall Apart. Ndio maana nikaombwa kuandika mwongozo. Nilitumia fursa hii kurekebisha ule mwongozo niliouchapisha Dar es Salaam. Kwa vile ilikuwa imepita miaka mingi nami nilikuwa nimetafakari zaidi riwaya ya Things Fall Apart niliweza kuweka marekebisho na kuuboresha mwongozo ule.

Kitabu kingine kilichokuwa kinajadiliwa ni Crimes of Conscience cha Nadine Gordimer, na aliyeombwa kuandika mwongozo ni profesa Karen A. Kildahl. Kazi yake na yangu zilichapishwa katika kijitabu kimoja, kama inavyoonekana katika picha hapo juu. Yeye na mimi tulialikwa kwenda kuendesha warsha kuhusu hivi vitabu viwili, katika mji wa Brookings, warsha ambayo ilihudhuriwa na watu kutoka sehemu mbali mbali za jimbo la South Dakota.

Mpango huu wa kuhamasisha usomaji katika jimbo zima ulinivutia sana, nikaona kuwa kama tungeweza kufanya jambo kama hili Tanzania, kuwafanya watu wajadili kitabu kimoja baada ya kingine, katika mkoa mzima au nchi nzima, tungefika mbali sana. Hatimaye, wahusika katika bodi hii ya South Dakota Humanities Council waliuweka mwongozo wangu wa Things Fall Apart mtandaoni, ukatumiwa na watu kutoka sehemu mbali mbali duniani.

Nilianza kuwazia umuhimu wa kuufikisha huu mwongozo Tanzania, ukiwa umeboreshwa zaidi. Niliurekebisha, nikauchapisha Chuo Kikuu Dar es Salaam, mwaka 2003, kwa gharama ya dola 520 za Marekani.

Wakati huo nilikuwa nimeanzisha kijikampuni, na kukisajili hapa Minnesota, kwa jina la Africonexion. Shughuli zake ni masuala ya elimu, kama vile kutoa ushauri, warsha, uandishi na uchapishaji. Nilivyochapisha mwongozo huu Dar e Salaam, nilitumia jina la Africonexion kama kampuni husika.

Hata hivi, lazima niseme ukweli. Pamoja na juhudi hizi zote, sikuona mwamko wa kuridhisha miongoni mwa wa-Tanzania, wa kutumia fursa niliyowaletea. Lakini, naridhika kwamba sina lawama. Kama vijana wa shule wa Rukwa, Pemba, Morogoro na Kondoa hawana kitabu kama hiki, kosa ni la wananchi na serikali. Mimi kama mwalimu nawajibika kusema kuwa serikali inapotosha ukweli inaposema haina hela, wakati kila mtu anaona jinsi inavyofuja hela, kwa magari ya fahari, na kadhalika. Tabia hiyo na wananchi wanayo pia, kama nilivyoeleza hapa.

Harakati za mwongozo huu ziliendelea. Mwaka 2005 nilikuwa nimechapisha kitabu mtandaoni, kiitwacho Africans and Americans: Embracing Cultural Differences. Baada ya kuvutiwa na uchapishaji wa aina hii, niliamua kuchapisha mwongozo wangu wa Things Fall Apart kwa njia hiyo hiyo. Niliufanyia marekebisho na kuuboresha, na hatimaye niliuchapisha, kama inavyoonekena katika picha kushoto.

Mwongozo wangu huu unawafaidia wengi. Nilifurahi, kwa mfano, nilipoona umechaguliwa na Chuo Kikuu cha Cornell kwa ajili ya wanafunzi wa mwaka wa kwanza waliokuwa wanatakiwa kusoma Things Fall Apart.

Huo ni utaratibu wao, kwamba wanafunzi wote wa mwaka wa kwanza wasome kitabu fulani, na vitabu hubadilika mwaka hadi mwaka. Kwa jinsi Chuo Kikuu cha Cornell kilivyo maarufu duniani, na kwa kuwa kuna vijitabu vingi na machapisho mengine kuhusu riwaya hii, kuchaguliwa mwongozo wangu ni heshima ya pekee. Soma hapa. Niliumiza kichwa kwa miaka mingi kuufikisha mwongozo huu kwenye kiwango hiki na nilijua ubora wake, kwani hilo ni somo langu, lakini inapendeza pia kuwasikia wataalam wengine wanaonaje.

Ninaendelea na shughuli ya kuandika miongozo kwa vitabu vingine. Kwa mfano, ninataka kurekebisha mwongozo wangu wa The African Child, ili niuchapishe kama kijitabu. Vile vile, kwa miaka kadhaa nimejishughulisha na uandishi wa mwongozo wa utungo maarufu wa Song of Lawino, uliandikwa na Okot p'Bitek. Nikijaliwa uzima, nitaandika sana siku za usoni. Kwani kazi na wajibu wa mwalimu ni nini?

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...