Wednesday, January 26, 2011

Kitimoto

Neno kitimoto ni maarufu Tanzania. Kitimoto ni nyama ya nguruwe; inapendwa sana katika mabaa na sehemu zingine. Ubora wa kitimoto ni kivutio kwa wateja na neema kubwa kibiashara kwa wenye baa. Hapa kushoto ni sahani ya kitimoto ambayo niliinunua kwenye baa moja Sinza, hatua chache kutoka Lion Hotel.

Ninapokuwa katika miji kama Dar es Salaam, napatikana mitaa ya u-Swazi, kama inavyoonekana katika picha hii, iliyopigwa Sinza, bondeni ukifuata barabara inayopita mbele ya Lion Hotel. Kwa wale wasiojua, neno u-Swazi linamaanisha sehemu wanazoishi wananchi wa kawaida.

Hapo kushoto kuna baa na sehemu ya kitimoto ambapo nimeshakuwa mteja mara kadhaa. Picha hii inaonyesha jinsi mwenye kitimoto anayotangaza biashara yake. Tofauti na zamani, anaweza kuagiza nyama kutoka bucha kwa kutumia simu, na anaweza kuchukua oda za wateja kwa simu pia.


Pamoja na umaarufu wake, kuna hisia tofauti, michapo, na utani kuhusu kitimoto, mambo ambayo yanaweza kufanyiwa utafiti kama sehemu muhimu ya utamaduni wa leo wa m-Tanzania.

13 comments:

Simon Kitururu said...

Naombe tu nyama zetu zisiingie magonjwa ya ajabu ajabu TANZANIA kwa maana tutapukutika sana tu!

Kwa maana kuna udhaifu sana katika kukagua usalama wake. Na kama magonjwa kama yale ya kichaa cha ng'ombe na mengineyo yakianza kutawala Tanzania cha moto tutakiona kwa kuwa sidhani kama kuna mzoga utatupwa na kuchomwa uteketee kama wafanyavyo wenzetu nchi tajiri.:-(

Na nasikia mpaka CHIPSI ni kawaida kabisa kutumia mafuta ya transformer za umeme kwenye vikao vingi tu.:-(

emuthree said...

We acha tu, na watu wanavypenda kuila hii nyama ya nguruwe...kwanza ina mafuta mengi...halafu ...oh, ...na wengine sasa wanaila kwa `ushabiki'..tuangalieni na afya zetu kwanza, mafuta mengi ni hatari!

Simon Kitururu said...

Nakubali kuwa kuna mapungufu katika vyakula UGHAIBUNI kutokana na makemikali na nakadhalika lakini angalau wenzetu wanajinsi ya kufuatilia. Sisi kwetu mpaka uoteshaji wa mazao unageuka siku hizi.

Makemikali hata Tanzania yamebobea, mbolea za chumvichumvi nk. Kwa hiyo unaweza kukuta unakula kitu ambacho unazania ni freshi na hakina kemikali lakini kinazo.

Nakumbuka kwa mfano shamba letu la mahindi Songea kabla Baba yangu hajaliuza ilifikia bila mbolea za chumvi chumvi hupati kitu na pia hata kulima nyanya ilikuwa madawa kwa kwenda mbele.


Nachojaribu kusema ni kwamba Tanzania haina usimamizi wa afya za watu katika mazao na vyakula viuzwavyo. Magharibi pamoja na makemikali yao angalau wana institutions zinazofanya kazi kila siku kujaribu kukabili hali!

Ila mengine nakubali kabisa ulicho sema.


Narespond hivyo kwa comment hii hapa chini ambayo niliidaka hapo kabla halafu sasa siioni ambayo ni :


``Napenda kuwamegea kidogo uzoefu wangu, nikiwa mzoefu wa u-Swazi na mteja wa kuaminika wa kitimoto :-)

Mkaanga kitimoto ana wateja wengi ambao ni wateja wa kudumu, watu wa karibu yake, kuanzia marafiki, na pengine ndugu. Anawafahamu; anawapenda na kuwajali sana. Ana uchungu nao. Hawezi kuwafanyia jambo la kudhuru afya zao, labda iwe bahati mbaya au kutojua.

Yawezekana akatumia mafuta ya transfoma, kwa kutojua madhara yake. Lakini akielimishwa, naamini ataacha, maana hawezi kufanya kitu kwa makusudi cha kumdhuru ndugu yake, rafiki yake, au shangazi yake anayekuja kula kitimoto hapo.

Kama ni vyakula bomu, ughaibuni ndiko kwenyewe. Kuku wanalishwa kemikali wakue upesi. Matunda yanakaa "supermarket," hadi kupoteza thamani yake kwa afya ya binadamu. Lakini yanamwagiliwa maji ili yaonekane "fresh." Lakini ni matunda bomu. Na kadhalika.

Tofauti na kitimoto, wanaoandaa vyakula ughaibuni ni makampuni ya kibeparti ambayo lengo lao ni kuchuma pesa. Hawamjui mteja.

Na sasa hao mabepari wasiotujua wametua Bongo na "supermarket" zao zenye kuku kutoka Brazil, vikopo au vipaketi vya juisi ya machungwa vilivyofungashwa Dubai, na kadhalika.

Na wa-Tanzania walioenda shule sana utawakuta kwenye hizo "supermarket." Shule imewaharibu; wanaamini kuwa kwenda "supermarket" ndio maendeleo.

Mimi napendelea u-Swazi. Ukikatiza mtaa kama unavyoniona kwenye picha hapo juu, unakutana na mkokoteni umebeba maembe yaliyoteremka leo leo kutoka Morogoro, au unakumbana na genge panapouzwa machungwa yaliyoshuka asubuhi hii kutoka Msoga kwa Kikwete :-)´´

Mbele said...

Lo, ndugu Kitururu, kumbe makala yangu uliiwahi hivyo, maana niliiondoa ili kurekebisha pale nilipotaja kitabu, lakini nimerejea tena nikaona umeshaniwahi. Sasa basi, sitaiweka tena, maana itakuwa ni kurudia hicho kipande ulichokinukuu.

Simon Kitururu said...

@Prof.Mbele: Mtandao unatisha! Yani uki press tu send kitu mtandaoni jua kuna mtu labda kashakidaka!:-(

Mbele said...

Ndugu Kitururu, ni kweli unavyosema. Na wewe ni msomaji makini kuliko kawaida. Samahani kwa usumbufu niliosababisha kwa kuondoa makala na wewe ukakuta patupu :-(

Lakini mada yenyewe ni muhimu sana, na hayo unayosema, kwamba kemikali na matatizo mengine yameshaingia Bongo ni ukweli.

Inatisha, maana sasa suali linakuja: Je, kuku wa kienyeji ni wa kienyeji kweli? :-)

Yasinta Ngonyani said...

kitimoto we acha tu!

Simon Kitururu said...

Mie nakuelewa katika hii,...

.... ila kueleweka nimegundua sio kitu rahisi hapa duniani hata ukirahisisha vipi jambo kwa kuwa labda watu tunajaribu sana kila kitu kila mtu aelewe!

Na hapa najibu comment:




``Niligusia kuhusu nafasi ya kitimoto katika utamaduni wetu, na kati ya vipengele nilivyotaja ni utani. Mfano mmoja ni jinsi wa-Islam na wa-Kristu wanavyotaniana kuhusu kitimoto. ´´

Nje ya pointi!

Samahani Prof. MBELE- imetokea mara kadhaa niko hapa kijiweni kwako ,...

...na nikinasa kitu,...


.... wakati najibu ,...

... comment ASILIA inapotea.!:-(

Mbele said...

Ni kweli imetokea tena. Niliandika hayo maneno uliyoyanukuu, nikayaondoa baada ya sekunde chache kwa vile niliona yanafaa kuandikiwa makala ya peke yake.

Simon Kitururu said...

@Prof. MBELE: Samahani sijawahi kuwa darasani kwako ukaniona ila napenda ujue karibu kuna miaka KADHAA karibu kila usemacho mpaka vitabu mwako vyote nilidaka!:-(



Ila kwa kuwa sitaki kukutisha naacha ku -comment kwa muda hapa!:-(


Ila jua niko sensitivu sana na yoyote unayosema hata kama nitakaa kimya!:-(

Mbele said...


Kuna msomaji mmoja wa blogu hii, Makusaro Tesha, ambaye ameniletea ujumbe akijitambulisha kuwa anashughulika na "online marketing." Ameomba nimweke kiunganishi cha shughuli zake hapa, kutokana na kuwepo kwa neno "kitimoto." Kiunganishi chenyewe ni hiki hapa.

Anold T Malisa said...

Naombeni kujua asili ya neno "Kitimoto"

Mbele said...

Ndugu Anold T Malisa

Shukrani kwa ujumbe wako. Kwa bahati mbaya, sikufuatilia na sijafuatilia asili ya neno hili. Sijui, labda kuna wasomaji wa blogu hii wanaofahamu au wenye fununu. Nikifanikiwa kupata taarifa yoyote, nitaileta hapa. Nakutakia kila la heri.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...