Sunday, January 2, 2011

Mwongozo wa "Things Fall Apart"

Nimefundisha riwaya ya Things Fall Apart ya Chinua Achebe tangu yapata mwaka 1976, sehemu kama Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Chuo Kikuu cha Burundi, na vyuo vya Colorado na St. Olaf.

Kutokana na uzoefu huu, na mengi niliyojifunza, na kwa lengo la kuweka kimaandishi mawazo yangu juu ya riwaya hii, niliandika mwongozo. Nimeshaongelea kidogo kuhusu mwongozo huu katika blogu hii, lakini napenda kueleza zaidi habari zake.



Aliyenisukuma kuandika mwongozo huu kwa wakati niliofanya hivyo ni rafiki yangu A.S. Muwanga, aliyekuwa katika Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Yeye na mimi tulikubaliana kuwa niandike pia mwongozo kuhusu kitabu cha The African Child, kilichoandikwa na Camara Laye. Muwanga alifanya mpango na kitabu kilichapishwa mwaka 1988 na Nyanza Publications Agency kama inavyoonekana katika picha hapo juu. Lengo mahsusi lilikuwa ni hasa kuwasaidia wanafunzi wa sekondari waliokuwa wanasoma riwaya hizo.

Miaka hiyo, 1976 hadi 1991, nilikuwa mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Mwaka huo 1991, niliondoka pale mwaka 1991, nikaja kufundisha Chuo cha St. Olaf, katika idara ya kiIngereza.

Mwaka 1997, bodi ya South Dakota Humanities Council iliyokuwa ikiratibu mradi wa usomaji katika jimbo la South Dakota iliniomba kuandika mwongozo kuhusu Things Fall Apart. Katika utaratibu wao, walikuwa wanachagua kitabu ili kisomwe na vikundi mbali mbali katika jimbo zima.

Ili kuchangia zoezi hili, walikuwa wana utaratibu wa kutafuta mtu wa kuandika mwongozo kuhusu kitabu husika, na mwongozo huu ulikuwa unatumiwa sambamba na kitabu husika. Kila kikundi kilikuwa kinajadili kitabu kweye mji wao, au eneo lao, na kisha walikuwa wanajumuika na wenzao wa sehemu zingine katika mjadala kwa njia ya barua pepe.

Mwaka huo 1997 kitabu kimojawapo walichokuwa wamekichagua ni Things Fall Apart. Ndio maana nikaombwa kuandika mwongozo. Nilitumia fursa hii kurekebisha ule mwongozo niliouchapisha Dar es Salaam. Kwa vile ilikuwa imepita miaka mingi nami nilikuwa nimetafakari zaidi riwaya ya Things Fall Apart niliweza kuweka marekebisho na kuuboresha mwongozo ule.

Kitabu kingine kilichokuwa kinajadiliwa ni Crimes of Conscience cha Nadine Gordimer, na aliyeombwa kuandika mwongozo ni profesa Karen A. Kildahl. Kazi yake na yangu zilichapishwa katika kijitabu kimoja, kama inavyoonekana katika picha hapo juu. Yeye na mimi tulialikwa kwenda kuendesha warsha kuhusu hivi vitabu viwili, katika mji wa Brookings, warsha ambayo ilihudhuriwa na watu kutoka sehemu mbali mbali za jimbo la South Dakota.

Mpango huu wa kuhamasisha usomaji katika jimbo zima ulinivutia sana, nikaona kuwa kama tungeweza kufanya jambo kama hili Tanzania, kuwafanya watu wajadili kitabu kimoja baada ya kingine, katika mkoa mzima au nchi nzima, tungefika mbali sana. Hatimaye, wahusika katika bodi hii ya South Dakota Humanities Council waliuweka mwongozo wangu wa Things Fall Apart mtandaoni, ukatumiwa na watu kutoka sehemu mbali mbali duniani.

Nilianza kuwazia umuhimu wa kuufikisha huu mwongozo Tanzania, ukiwa umeboreshwa zaidi. Niliurekebisha, nikauchapisha Chuo Kikuu Dar es Salaam, mwaka 2003, kwa gharama ya dola 520 za Marekani.

Wakati huo nilikuwa nimeanzisha kijikampuni, na kukisajili hapa Minnesota, kwa jina la Africonexion. Shughuli zake ni masuala ya elimu, kama vile kutoa ushauri, warsha, uandishi na uchapishaji. Nilivyochapisha mwongozo huu Dar e Salaam, nilitumia jina la Africonexion kama kampuni husika.

Hata hivi, lazima niseme ukweli. Pamoja na juhudi hizi zote, sikuona mwamko wa kuridhisha miongoni mwa wa-Tanzania, wa kutumia fursa niliyowaletea. Lakini, naridhika kwamba sina lawama. Kama vijana wa shule wa Rukwa, Pemba, Morogoro na Kondoa hawana kitabu kama hiki, kosa ni la wananchi na serikali. Mimi kama mwalimu nawajibika kusema kuwa serikali inapotosha ukweli inaposema haina hela, wakati kila mtu anaona jinsi inavyofuja hela, kwa magari ya fahari, na kadhalika. Tabia hiyo na wananchi wanayo pia, kama nilivyoeleza hapa.

Harakati za mwongozo huu ziliendelea. Mwaka 2005 nilikuwa nimechapisha kitabu mtandaoni, kiitwacho Africans and Americans: Embracing Cultural Differences. Baada ya kuvutiwa na uchapishaji wa aina hii, niliamua kuchapisha mwongozo wangu wa Things Fall Apart kwa njia hiyo hiyo. Niliufanyia marekebisho na kuuboresha, na hatimaye niliuchapisha, kama inavyoonekena katika picha kushoto.

Mwongozo wangu huu unawafaidia wengi. Nilifurahi, kwa mfano, nilipoona umechaguliwa na Chuo Kikuu cha Cornell kwa ajili ya wanafunzi wa mwaka wa kwanza waliokuwa wanatakiwa kusoma Things Fall Apart.

Huo ni utaratibu wao, kwamba wanafunzi wote wa mwaka wa kwanza wasome kitabu fulani, na vitabu hubadilika mwaka hadi mwaka. Kwa jinsi Chuo Kikuu cha Cornell kilivyo maarufu duniani, na kwa kuwa kuna vijitabu vingi na machapisho mengine kuhusu riwaya hii, kuchaguliwa mwongozo wangu ni heshima ya pekee. Soma hapa. Niliumiza kichwa kwa miaka mingi kuufikisha mwongozo huu kwenye kiwango hiki na nilijua ubora wake, kwani hilo ni somo langu, lakini inapendeza pia kuwasikia wataalam wengine wanaonaje.

Ninaendelea na shughuli ya kuandika miongozo kwa vitabu vingine. Kwa mfano, ninataka kurekebisha mwongozo wangu wa The African Child, ili niuchapishe kama kijitabu. Vile vile, kwa miaka kadhaa nimejishughulisha na uandishi wa mwongozo wa utungo maarufu wa Song of Lawino, uliandikwa na Okot p'Bitek. Nikijaliwa uzima, nitaandika sana siku za usoni. Kwani kazi na wajibu wa mwalimu ni nini?

9 comments:

Fadhy Mtanga said...

Prof Mbele nimefurahi sana kuyasoma maelezo hayo. Mie ni shabiki wa fasihi ya Kiafrika. Nimemsoma Chinua Achebe, Camara Laye, Meja Mwangi, na wengine walioandika na kuchapa na AWS (African Writers Series)...nakumbuka wakati nikikua nilipenda sana kuwa na vitabu vyenye nembo ya AWS ingawa Kingereza kilikuwa bado mgogoro kwangu.

Nina kitabu kimoja, The Black African Voices ambapo wataalamu wa fasihi ya Kiafrika wamezichambua riwaya, hadithi fupi, tamthiliya na ushairi wa kiafrika. Moja ya kazi zilizochambuliwa ni The African Child, Mine Boy, Facing Mount Kenya na nyingizo za waandishi mufti kutoka Afrika kusini hadi Senegal..

Kwa mpenzi yeyote wa Fasihi ya Kiafrika, ni raha sana kuwasoma waandishi hawa.

Ahsante sana Prof Mbele kwa kunipa hamasa kila nizurupo hapa blogini kwako.

emuthree said...

Ahsante sana Prof Mbele kwa msaada huu mkubwa, kwa wapenzi wa vitabu hivi tuna shauku sana ya kuuona mwongozo huo.

Mbele said...

Ndugu Mtanga na emu-three, shukrani kwa mchango wenu. Ni faraja kuona tuko pamoja katika masuala haya muhimu ya elimu.

Ingawa wa-Tanzania kwa ujumla hawajishughulishi na vitabu na wengine wanaviona kama kero, wako wachache ambao wana moyo tofauti. Wazo langu ni kuwa sisi wachache tujipange, tuwe kikundi thabiti cha kuleta mapinduzi yatakiwayo katika jamii yetu.

Binafsi kama mwalimu nafarijika kuwa kuna angalau wachache kule nyumbani ambao nimefanikiwa kuwagusa kwa namna moja au nyingine, kwa mfano vijana wanaoshughulika na utalii pale Mto wa Mbu, kama wanavyojieleza hapa.

Anonymous said...

Shikamoo Profesa Mbele!

Asante kwa hili,ila mimi naona unatuonea Watanzania. Nilivyoona mimi,kwa kufuatilia mada na linki humu ndani, tatizo hapa sio kwamba Wabongo hawasomi bali hawasomi vitabu vyako.

Nasema hivi kwaajili naona hapa naona unazungumzia mwongozo wako tu wakati pengine kuna nyingine nyingi ambazo zinafaa. In other words, this is self serving as you are promoting your own work and,as you say,the profits (or losses - whatever the case maybe) will go to the kijikampuni ulichokianzisha huko marekani:vijisenti vyote citaishia huku. (I say this not as a criticism but an observation.In principle i believe it is fair and valid that you should profit from your hard work and effort:lazma ule jasho lako mwenyewe. Indeed you probably have incurred more costs than profits in this whole endearvour hence your changamoto).

Going back to the point,kama tatizo ni kwamba watanzania hawasomi na wanapendelea starehe naona ingebidi upanue hoja zaidi ya vitabu vyako tu. Ingawaje najua kwamba kwenye blogu hili huwa unazungumzia vitabu vya kiswahili vingine,lakini ukichunguza kwa makini utaona hoja huwa zinalalia kupigia debe kinyemela vitabu vyako kwa mbinu ya "soft marketing" or "product placement". (i repeat again,nothing wrong with this but you just need to make it clear that this is what your blog for and thus your gripe about lack of reading is about).

Binafsi naona kwamba,ukilinganisha na nchi jirani,Watanzania tupo mbele kwenye kusoma. Hata kama hatusomi vitabu vya wasomi waliobobea naona sekta yetu ya habari ina ushindani mkubwa na magazeti mengi ya Kiswahili yapo.Indeed, wageni wengi wakija Tanzania wanashangaa jinsi kila kona kuna kagenge cha gazeti na kwenye madaladala watu wapo na magazeti yao wakisoma. Offcourse we can argue about the depth of analysis in these newspapers but,for Africa, Watanzania lazma tujipongeze kwa kuwa na tabia yakutafuta habari na kusoma.

Upande wa vitabu kama hivyo unavyoouza wewe,hata huko ulaya tukubali kwamba desturi ya kusoma ilichukua kama miaka mia tano hivi kukolea katika jamii. Na sababu kubwa ya desturi hii kuingia katika "vichwa" vya watu ni pale mapinduzi ya protestantism yalivyowapa changamoto watu wajisomee wenye Neno la Mungu kuliko kuambiwa na Mapadre. This is the source of the great tradition and love of reading in the West. Before Luther and the critical doctrine of "Sola Scripture" most of the folk in Europe were illiterate. Kwahiyo kama mapinduzi yatafika kwetu naamini lazma yapitie njia hiyo hiyo: waumini kupewa motisha kujisomea wenyewe Biblia na sio kutengemea ya kuambiwa.

Naomba kutoa hoja.

Majaliwa

Mbele said...

Ndugu Wachumi, shukrani kwa ujumbe wako. Kwa vile mitazamo yangu na hisia zangu nazieleza katika hii blogu yangu, tangu zamani, na nitaendelea kufanya hivyo, naona nisirudie yale ambayo nimekuwa nayasema, na ambayo umekuwa ukiyafuatilia.

Niseme tu kuwa nashukuru kuwa unafuatilia maongezi yangu katika blogu hii.

Kuhusu suala la wa-Tanzania kutokuwa na utamaduni wa kusoma, ukweli ni kuwa huu ndio mtazamo wa wadau wanaohusika na vitabu Tanzaniau. Mimi ni mwanachama wa Umoja wa Waandishi wa Vitabu Tanzania (UWAVITA) tangu zamani, na ninajua tatizo.

Wadau mbali mbali Tanzania wanasema hayo ninayosema. Kwa mfano, soma taarifa hizi:

hii hapa

hii hapa

hii hapa

hii hapa

hii hapa

Kwa kumalizia, mimi kama mwalimu nawajibika kujielimisha na kuwaelimisha wengine. Kwa vile nimezama katika taaluma fulani, nina wajibu wa kuongelea sana taaluma hizo. Ninachozingatia tu ni kuwa ninapokuwa darasani ninaongea kwa namna fulani, ninapokuwa kwenye mikutano ya wanataaluma naongea kwa namna fulani, na ninapokuwa hapa kwenye blogu ninaongea kwa namna fulani. Lakini somo ni lile lile, nami nitaendelea na harakati ninazofanya. Kunisikiliza au kutonisikiliza ni uhuru wa kila mtu.

Anonymous said...

Asante Profesa kwa majibu na viambatanisho ambavyo nimevisoma

Pia nakuomba uendelee na mikakati hapa kwenye blogu. Nashukuru kwa kutuelimisha na kuelewa nilichisema.

Lakini nimeona katika makala hapo juu (ya kwanza)kwamba usomaji vitabu kumeshuka kutoka 90% mpaka 72%.Hii data naona kama inasapoti kwamba,kwa Africa,Tanzania tunajitahidi kusoma. Maana hata hiyo 72% ni ya juu na poromoko sio kubwa sana kwavile bado tupo juu ya 50%. Ukilinganisha na nchi nyingine (hata za ulaya) utaona kwamba wao wameporomoka kwa spidi ya kinoma kweli kweli! Pia,kushuka huko kunaweza kuendana sambamba na watu kusoma media tofauti sio vitabu tu(yaani its simply a mirrow effect of a substitution thats going on between "old" and "new" media kadri watu wanavyohamia kutoka kule kuja karne ya 21): so it need not all be bad news.

Kwakunalizia niseme tu, hata hivyo, mimi naona pengine kwamba tukiilenga Tz na wabongo peke yao tunaweza kuwa tunaoneana na kutunyima credit where it is due. Navyosikia na kusoma mimi ni kwamba,kwa ujumla swala hili ni la dunia nzima. Yaani hata huko Ulaya wadau wengi wanalalamikia na swala hilo,hilo kuhusu usomaji wa vitabu. Nadhani utakua familiar na mada na makala nyingi zilizoandikwa na wasomi kujaribu kutoa changamoto ku ughaibuni kuwavutia vijana wa sasa kujijengea utamaduni wakusoma. Indeed,wengine wakiri kwamba inaelekea ulimwegu wa vitabu na kusoma umefikia njia panda miaka hii...especially with the onset of new social media and e-learning etc. Sijui wewe Profesa unaonaje?

basi asante kwa mara nyingine,nashukuru majibu hayo. Aluta Kontinua!
(p.s. nimetoa maoni hapo juu kwani nilikosea kuingiza na yalijirudiarudia).

Mbele said...

Huwa nasimama upande wa kuhimiza ufanisi zaidi na zaidi, hata kama tunaonekana sisi ni afadhali kuliko wengine. Kwa suala hili la elimu, msimamo wangu ni kusema glasi ni nusu tupu, badala ya kusema imejaa nusu.

Ndio maana, nikirudi kwenye hiki kijimwongozo changu, nimeelezea jinsi nilivyokirekebisha, tena na tena, ingawa kilikuwa kizuri tangu mwanzo. Na hata katika hali yake hii ya sasa, bado naangalia namna ya kukiboresha.

Kwa mimi mwalimu, naona hatari kuwaambia wanafunzi kuwa wamehitimu. Elimu haina mwisho, na kwa hivi muda wote nawaambia kuwa bado kuna kazi kubwa mbele.

Ndio maana, hata tunapoongelea utamaduni wa kusoma Tanzania, mimi nasisitiza jinsi tulivyopungukiwa, iwe changamoto ya watu kufanya bidii zaidi na zaidi. Kama Mwalimu Nyerere alivyosema, tusipime afya zetu kwa kujifananisha na wagonjwa wenzetu.

Kuhusu hizi mbinu mpya za mawasiliano, ambazo zinaweza kuchukua nafasi ya vitabu, ninafuatilia vizuri maendeleo yake na malumbano juu yake.

Ingawa wako wanaohisi kuwa kitabu, kama tunavyokielewa, kitakufa, wengi wanasema kuwa kitabu kitaendelea kuwepo.

Na kwa kweli, hizi nchi kama Marekani, ambako tekinolojia hizi mpya za mawasiliano zimeenea zaidi, bado vitabu vinachapishwa na kuuzwa kwa wingi na watu wanavisoma. Wanablogu tumekuwa tukiongelea masuala hayo sana.

Kwa upande wa nchi kama Tanzania, hizi tekinolojia zenyewe hazitawafikia wananchi wa vijijini Newala au Kasulu kiurahisi. Ni muhimu tuzingatie suala la vitabu kama vitabu, ili vikafike kule. Ni rahisi zaidi kuliko kutegemea hizi tekinolojia mpya, ambazo zinahitaji kompyuta, na vikorombwezo vingine.

Kuhusu magazeti, ni kweli wa-Tanzania wanasoma sana magazeti. Nimeshuhudia hivyo hata kijijini kwangu, wakati gazeti la "Kwanza Jamii" lilipofika kule. Lakini taaluma nyingi bado ziko vitabuni, na vinaendelea kuchapishwa muda wote.

Kwa mfano, kila ninapopita kwenye maduka ya vitabu hapa Marekani, au ninapopita katika viwanja vya ndege hapa au Ulaya, nakuta vitabu vingi vipya, katika nyanja mbali mbali. Hivi vitabu havipo Tanzania, na hapo naona wazi kuwa tunaachwa nyuma. Kwa mfano, suala la biashara na ujasiriamali linaandikiwa vitabu vingi sana, muda wote. Tanzania hakuna hivyo.

Wa-Tanzania wanaopata fursa ya kutembea huku nje, kwa vigogo wanaokuja katika misafara ya serikali, wangeweza kabisa kununua hivi vitabu na kurudi navyo Tanzania. Lakini nahisi wananunua zaidi mizinga ya "whisky" na "brandy." Vile vile, nahisi wananunua sana vipodozi, maana mkorogo ni kipaumbele kikubwa katika nchi yetu.

Anonymous said...

Asante kwa Mara nyingine Pro. Mbele.

Mengi uliyosema Mimi naitikia,ila unaposema majuu,kwenye airport nktk,wanavitabu vine etc,ningependa kuuliza kama hii ni ishara ya uwezo wao kifedha tu?Yaani soko la vitabu lina kin a sambamba na utajiri wao(higher levels of discretionary income). Nauliza hili kwakujua mad a ya uwezo na tabia/utamaduni wa kusoma mmeshaijadili kwa kina,lakini naona ulivyojadili mlisahau kugusia kwamba hata kule majuu watu wengi wanapenda starehe.

Indeed,soko la vitabu via ngono nchi za Ulaya/magharibi ni maradufu ya total gdp ya chi ndogo ya kiafrika.Kwa namna nyingine niseme usomaji wao ni wajuujuu na soko la vitabu,hat a uwanja wa ndege,mara nyingi ni vijitabu via raha mustarehe.Hata magazeti yao nayo yanaelekea huko,huko. Lakini,kimsingi changamoto yako ni poa na utapendeza Kama watz tungeashisha mpango wakujinga maktaba,kwa nguvu binafsi,vijijini nktk,ili watoto wetu wapate access ya huduma hiyo.Pengine kaNGO fulani kitaweza kazi hii.

Mwisho,kuhusu hoja ya "watanzania hawapendi kusoma",naomba muangalie anachosema dada Chimamanda Adichie hap,on the dangers of a single narrative ":
http://www.ted.com/talks/chimamanda_adichie_the_danger_of_a_single_story.html

Mbele said...

Ndugu Wachumi, shukrani. Angalizo lako, ulilolitoa kwenye hotuba ya Chimamanda Adichie, ni muhimu. Tunapaswa kuzingatia, ili tuwatendee watu haki, wakiwemo hao wa-Tanzania ambao baadhi yetu tunadai hawapendi kusoma. Nakubaliana na mtazamo wako. Tunapaswa kutumia uyakinifu zaidi ili tuwatendee haki.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...