Wednesday, January 19, 2011

Andika ki-Swahili; ki-Ingereza Hatuelewi

Kuna tabia katika jamii ya wa-Tanzania ya kulalamika pale mtu anapoandika ki-Ingereza. Malalamiko haya yanaonekana mara kwa mara katika blogu ya Michuzi, kwa mfano, ambayo inasomwa sana na wa-Tanzania, pale inapotokea makala iliyoandikwa kwa ki-Ingereza.

Walalamikaaji wanakumbushia kuwa wa-Tanzania wengi hawajui ki-Ingereza, na kwa hivi wanataka mwandishi awafikirie hao kwa kuandika kwa ki-Swahili, lugha wanayoifahamu. Ujumbe unaojitokeza katika malalamiko hayo ni kwamba ni jambo la uzalendo kwa mwandishi kuwafikiria hao wa-Tanzania walio wengi, ili nao wapate kufaidika na yale yanayoandikwa.

Sijawahi kuona malalamiko hayo yakipingwa. Inaonekana kuwa hoja inayotolewa katika malalamiko hayo inakubalika miongoni mwa wa-Tanzania.

Katika kulitafakari suala hili, naona kuna haja ya kuwakosoa hao walalamikaji. Ingawa ni kweli kuwa mtu akiandika kwa ki-Swahili anawafikia wananchi wasiojua ki-Ingereza, kuna pia tatizo la uvivu katika jamii yetu.

Malalamiko hayo ni sehemu ya tatizo hili la uvivu ambalo naliongelea tena na tena katika blogu hii na zingine, na pia katika maandishi mengine. Wa-Tanzania wanapenda kutafuta visingizio na kuwalaumu wengine. Kwa nini wa-Tanzania waridhike na hali yao, ya kujua ki-Swahili tu, badala ya kujifunza lugha zingine?

Kama wa-Tanzania wanataka kudekezwa, ni bora wajue kuwa dunia hii ya ushindani haidekezi mtu. Wasipojituma katika masuala ya elimu, ikiwemo elimu ya lugha mbali mbali, sio tu watabaki nyuma, bali wataumia. Mawasiliano ya kimataifa yatakuwa mtihani mkubwa ambao watashindwa. Mikataba ya nje watashindwa kuielewa.

Wakati huu tunanyoosheana vidole kutokana na mikataba tunayohisi waTanzania wenzetu wanaisaini kifisadi. Lakini, kwa jinsi tunavyoendekeza uvivu ninaoongelea, tutaendelea kusaini mikataba mibovu kwa kutojua lugha. Nchi itaendelea kuumia.

Hata kama watu hawana vitabu, kuna maktaba katika miji mbali mbali. Mtu yeyote anaweza kujipangia utaratibu wa kwenda kusoma vitabu vilivyomo, akajiongezea angalau ufahamu wa ki-Ingereza. Lakini wa-Tanzania wako radhi kukaa kwenye kijiwe nje ya maktaba, siku hadi siku, wiki hadi wiki, mwezi hadi mwezi, mwaka hadi mwaka, bila kuingia humo maktabani. Hili ni tatizo kubwa katika nchi yetu.

3 comments:

Yasinta Ngonyani said...

Afadhali umeandika hii mada ProF. nakuunga mkona au niseme mikono. Kusoma kitabu au habari kwa kiingereza sio kazi lakini kama ulivyosema UVIVU. Halafu jingine la kushangaza Wa-Tanzania tunajifanya sana kujua wakati hatujui kitu. Fikiria katika hizi shule, sijui kweli wanafunzi wanaelewa kitu au. kKuna wakati unaweza ukaanza kufikiri afadhali kila kabila lingekuwa likifundisha kwa kabila lile lakini unarudi tena na kusema haingekuwa bora. Na kiswahili chenyewe utakuta mtoto/mtu hakimudu kabisa kwa kweli kuna umuhimu wa kuanza kulifikiria hili jambo.... naacha naona kama kichwani kuna (mabungu vile yananisumbua)= kizunguzungu

Simon Kitururu said...

Najiuliza tu wakati huu kila mtu anakiri baada ya miaka ishirini atakaye tawala kiuchumi atakuwa ni MCHINA itakuwaje wakati hata ``yesiyesi YO mzungungu kala MAFENESI siku hizi bado kwa wengi ni ngumu!´´:-(

Mbele said...

Dada Yasinta una bahati unakijua ki-Swidi, ambacho sisi wengine tunakisikiaga tu :-)

Kuhusu lugha za makabila, wengi wetu ambao tumo katika taaluma hizi za lugha tunasema ni hazina kubwa ambayo hatupaswi kuipoteza.

Ndugu Kitururu, hapo ulipomtaja m-Mchina umenikumbusha kitu kimoja nilichowahi kusoma, kwamba wenzetu Zimbabwe wanajifunza lugha ya ki-China.

Hapo utaona wazi kuwa hao wanaona mbali, wakati sisi tumezamisha akili zetu kwenye udaku na ulabu, bila kusahau "send-off" na "kitchen party" :-)

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...