Katika hali ya kawaida, dini ni kitu cha manufaa kwa wanadamu, kwa maana kwamba inatufundisha kumtambua na kumcha Mungu, na kwa wale wanaoamini miungu wengi, ni hivyo hivyo. Dini inatufundisha maadili ya kumtendea binadamu mwingine kama tunavyopenda kutendewa. Kwa ufafanuzi zaidi maadili hayo ni kama kupendana, kusikilizana, kuheshimiana, kusameheana, na kutakiana mema.
Kwangu mimi m-Katoliki, maadili hayo yalielezwa kwa uwazi na Yesu katika mafundisho yake mengi, hasa pale aliposema kuwa amri kubwa kuliko zote ni kumpenda Mungu kwa moyo wetu wote, nguvu yetu yote na akili yetu yote, na kumpenda jirani kama tunavyojipenda wenyewe na pia kuwapenda adui zetu. Kwa lugha rahisi ni kuwa tunapowachokoza wengine au kuumiza hisia zao kwa makusudi, au tunapokosa uvumilivu na badala yake tunatunisha misuli na kujibu mapigo, tunaasi dini na kuwa makafiri.
Kwa kuzingatia hayo, niliandika makala kuwa penye dini hapana magomvi, na kwamba kuwepo kwa magomvi ni ushahidi wa kukosekana kwa dini. Dhana ya mgogoro wa kidini haina mantiki; ni sawa na kusema "usiku wa mchana," dhana ambayo haina mantiki. Soma hapa na hapa.
Hata kitu kizuri kinaweza kutumiwa vibaya. Na ndivyo ilivyo Tanzania, kwenye suala la dini. Dini imegeuzwa kuwa bangi. Dhana ya dini kuwa bangi ilielezwa na Karl Marx katika Critique of Hegel's Philosophy of Right, lakini naitafsiri kwa namna yangu.
Kadiri siku zinavyoenda, bangi hii inazidi kuenea katika Tanzania na kukolea vichwani. Imekuwa kichocheo cha malumbano, magomvi, uhasama, ubaguzi, majungu na chuki.
Sehemu za ibada zimegeuzwa kuwa majukwaa ya kueneza sumu hizo, kwa kutumia vipaaza sauti. Papo hapo, wahusika wanaamini kuwa ni wafuasi na watetezi wa dini. Wanaendelea kujenga nyumba wanazoziita za ibada, kumbe wanazitumia kuendeleza ukafiri. Hawakumbuki busara za wahenga kuwa kucha Mungu si kilemba cheupe.
Kilichonisukuma kuandika hayo niliyoandika ni wasi wasi wangu kuhusu hali ya nchi yangu. Dini yangu hainiruhusu kuwahukumu wengine. Kama nimekiuka angalizo hili, mwenye kujua ni Mungu.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault
Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...
-
Leo ni kumbukumbu ya siku ya kuzaliwa kwangu, ambayo ni tarehe 17 Agosti, 1951. Familia yangu, ndugu, na marafiki wamejumuika nami kushereh...
-
Leo napenda kukitambulisha kwako mdau kitabu muhimu cha ki-Swahili, Tenzi Tatu za Kale . Nilinunua nakala yangu miaka kadhaa iliyopita katik...
-
Kutafsiri kazi ya fasihi ni kazi ngumu ya kuchemsha bongo. Inahitaji ufahamu wa hali ya juu wa lugha husika, na pia hisia makini za kifasih...
4 comments:
Kama makala isemavyo, watanzania hatuna udini zaidi ya kupenyezwa na watawala wachovu walioishiwa hoja.
Watanzania wana ufisadi na umaskini vitu vilivyosababishwa na watawala wabaya wanaotaka kuepusha watanzania kuvikabili kwa kuwapandikizia udini.
Nenda pale Muhimbili unaumwa. Humuulizi daktari kama ni dini yako wala nini zaidi ya kuwa mgongjwa.
Kimsingi kinachoitwa udini ni usanii wa watawala mafisadi kutaka kuficha uovu wao kwa kuwapachikia wananchi kitu kingine ili kutengeneza hofu na kutoaminiana.
Katika kitabu changu cha SAA YA UKOMBOZI nimedurusu dhana hii kwa kumtumia mwenye nyumba anayejinakidi kuwa ni muislamu swaafi wakati anapandisha kodi ya pango kila uchao huku akitaka wapangaji wamuonjeshe kila mlo wapikao hasa wali na pilau.
Nia aibu na kashfa kusikia mtu kama rais akilalamika kuna udini wakati ukiangalia uteuzi wake kwa mfano wa balozi na majaji ni udini mtupu.
Kama Tanzania kuna udini basi wanao watawala wanaoutenda na kujifanya haupo. Kwanini udini unaibuka pale viongozi wa kidini wanapotaka watawala wawajibike kwa makosa na maovu yao?
Kwanini siku anapoapishwa rais maaskofu na mashehe wanamuombea usiwe udini ila udini uwe ni kuwakumbusha watawala juu ya uovu wao?
KWanini rais anapochangia msikiti aua kanisa usiwe udini ila udini uibuke viongozi wa kidini wanapompinga au kumkaripia?
Ukiipigia debe CCM kanisani ua msikitini si udini ila ukifanya hivyo kwa CUF ni udini. Huu kimsingi ni uhuni wa kawaida utokanao na ombwe la uongozi na ufinyu wa kufikiri wa watawala wetu.
Katika hili ninakuunga Prof. binafsi katika uchanga wangu ninawashangaa hawa wanaojifanya kutoa matamko ya kuwa kuna udini wakati ni wao wenyewe wanaoongoza kusambaza huo udini. Hiingii akili kusikia watu wanasema wakristu wamheshimu rais mwislam kwani wao wamefanya hivo sana na kuanza kuzungumzia suala la wakatoliki kuwa na balozi Tz. Jamani Vatican ni nchi kama chi yeyote ile. Hata hii tuwafundishe kuwa sio udini ila utaratibu tu jamani
Binadami ni mbinafsi kwa asili na anachokipenda yeye au imani yake inavyomtuma hasa pale imani hiyo inapolenga matakwa yake ndiyo `dini halali'
Dini kama dini zipo wazi, na zipo kwa ajili ya amani na upendo...asije akaja mtu akazungumza yake kuhusu dini yake au ya mwingine kuweka kinyume na haya kuwa dini zinafundisha fujo na uadui, hiyo haipo. Soma kwa makini dini zote ni amani na upendo!
Sasa kutokana na hulka ya ubinfasi, basi watu wanapenyeza imani za dini katika matamanio yao. Na utaona mtu anaongea vizuri lakini anapofikia katika `imani' anaanza ubinfsi...anajipinga mwenyewe ...kwanini..kwasababu dini zipo wazi, amani na upendo.
Hata ukitafuta yale yanayokupendezesha wewe, lakini kama yana ulakini, utajikuta mwisho wa siku unajisuta mwenyewe.
Mimi kitu kinachonishangaza ni kuwa watu wanasoma hata kuapata udakitari uprofesa, lakini hawataki kusoma `nini dini, nini kilichopo kwenye vitabu vya dini..' hivi vitabu havigusiki, havisomeki, mapaka tunaangalia matendo ya watu ndio tunaita dini ya hawo watu, hapana dini ni dini na misngi yake ni amani na upendo, na matendo ya watu ni watu ambao asilimia kubwa tumejaa ubinafsi, na tunaogopa kusoma hivi vitabu ...kwasababu tunaogopa ukweli...
Ni hayo tu prof
Mimi nafikiri tatizo tulilonalo ni dini zenyewe. Kwamba dini ndiyo inayoleta matatizo tunayoyaona. Na dini haijawahi kuwa kitu kizuri. Kwanza ni kwa sababu dini hazitusaidii kumfahamu Mungu. Sana sana zinatuchorea mipaka ya kumjua Mungu na mara nyingi zikifanya majaribio ya kumbinafsisha Mungu (aonekane ni wa dini fulani kuliko alivyo wa wanadamu). Dini zinasaidia kujenga utengano badala ya upendano. Watu wa dini moja hujisikia kuwa katika njia sahihi kuliko wengine na hivyo kujiona wamoja na kupendana wenyewe kwa wenyewe ilihali wakiwapuuza wenzao! Dini hutufanya tujione kama watu tulio sahihi kupitiliza kiasi cha kupuuzia tabia ya kuyasaili mambo kwa mtazamo unaovuka mipaka ya dini zetu.
Katika mazingira kama haya (ya kupendana na kupuuzana) si rahisi kuwa wamoja.
Katika mazingira haya penye dini magomvi ni hali ya kawaida. Migogoro ya kidini (inayotokana na ile hali ya kushindwa kuyatazama mambo nje ya mipaka ya dini yangu), inajiotea mizizi.
Kwa hiyo tunachokishuhudia sasa hivi, ni matokeo ya mizizi ya dini kushika kasi katika mioyo ya waumini.
Na salama yetu ni kuzisaili upya dini zetu na kuzitafuta imani zilizo nje ya dini hizi zilizojaa ugomvi na mafarakano.
Post a Comment